MTANZANIA ambaye alipata Tuzo ya Malkia Elizabeth || wa Uingereza, Prudence Kimiti amesema kuwapa hadhi maalum Diaspora itasaidia waweze kuwekeza nchini.
Kimiti aliyasema hayo Jijini Dar es Salaam alipotua nchini akitokea Uingereza anapoishi ambapo hadhi hiyo ikitolewa itasaidia sana kwa Diaspora kufanya uwekezaji ili kuleta maendeleo.
Prudence ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere ambaye pia aliwahi kuwa Mkuu wa baadhi ya Mikoa hapa nchini alisema kuwa yeye anaipenda Tanzania hivyo anatamani kutoa mchango wake wa maendeleo kwa nchi.
"Tunamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa jinsi anavyopambana kuwaletea Watanzania maendeleo hivyo watoe hadhi hiyo maalum kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi na ikiwa hivyo itasaidia kuwekeza ndani ya nchi yao,"alisema Kimiti.
Alisema kuwa suala kupewa hadhi maalumu kwa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni zuri kwani litasaidia kuleta maendeleo kwenye nchi yao.
Akizungumzia kuhusu tuzo aliyoipata ya Malkia wa Uingereza ya (MBE) aliipata kutokana na kutetea haki za watu weusi hasa wafanyakazi ambapo kuna baadhi ya changamoto wanazipata kutokana na rangi zao.
"Tuzo hii inafaida kubwa kwani inanipa moyo kuendelea kupigania haki za watu dunia nzima siyo Uingereza hata sehemu nyingine kwani napenda kila mtu apate haki yake,"alisema Kimiti.
Aidha alisema kuwa anatarajia kuanzisha shirika kwa ajili ya kusaidia makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanawake, watoto na wale waishio kwenye mazingira magumu.
"Tunaendeleza falsafa za mwasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Nyerere ambaye Waingereza wanampenda hivyo najivunia kuwa Mtanzania na tutaendeleza mazuri aliyoyaacha Nyerere,"alisema Kimiti.
Kwa upande wake Mzee Paul Kimiti alisema kuwa wanajivunia tuzo aliyoipata mtoto wao kwani imeiheshimisha familia na nchi kwa ujumla.
Kimiti alisema kuwa tangu mwanae akiwa mdogo alikuwa hapendi kuona mtu anaonewa na hilo amekwenda nalo hadi kufikia kupata tuzo hiyo na si bahati bali ni kitu kiko kwenye damu yake.
Alisema kuwa hata babu yake aliwahi kupata tuzo mwaka 1950 na sasa mwanae naye anapata tuzo hiyo hivyo ni jambo la kujivunia sana kwa nchi kutokana na tuzo hiyo.
Prudencia Kimiti alipata tuzo hiyo ya malkia hiyo wakati wa malkia kutimiza miaka 70 ya uongozi wa Malkia ambapo hutolewa kila mwaka.
No comments:
Post a Comment