KITUO cha kuendeleza vipaji Africa Talent Forum-TZ (ATFT) cha Mkoani Pwani imewakutanisha wasanii wa fani mbalimbali ili kujadili namna ya kuendeleza vipaji vya wasanii ili viweze kutoa ajira.
Akizungumza kwenye kikao maalumu kujadili masuala mbalimbali ya namna ya wasanii wanavyoweza kupata fursa za kuinua vipaji vyao Mkurugenzi mtendaji wa kituo hicho Rosemary Bujash amesema kuwa vipaji hivyo bila ya kuendelezwa havitaweza kufika mbali
Bujash amesema kuwa lengo la kuanzisha kituo hicho ni kusaidia wasanii na watu wenye vipaji au ndoto mbalimbali waweze kuzifikia ili kujiletea maendeleo kupitia vipaji vyao.
"Katika kuhakikisha vipaji vinaendelea na ndoto za watu zinatimia tumekuja na mradi wa Kipaji bila Mpaka ambapo tutahakikisha Tunaibua, Kukuza na Kuvitangaza ili wafikie malengo na kujiajiajiri kwani kipaji ni ajira,"amesema Bujash.
Kwa upande wake ofisa utamaduni wa Halmashauri ya Mji Kibaha Evarista Kisaka amesema kuwa moja ya changamoto kwa wasanii wachanga ni kutojitangaza hivyo kituo hicho wakitumie ili kutangaza kazi zao.
Kisaka amesema kuwa wasanii hao wanapaswa kujisajili na kutumia fursa mbalimbali zilizopo zinazotokana na sanaa na utamaduni na sanaa siyo uhuni bali ajira kama ajira nyingine na wao ni kioo cha jamii.
Naye mwenyekiti wa Wasanii Kibaha Jimanne Kambi amesema kuwa wasanii wako wengi lakini hawapati fursa kuonyesha vipaji vyao hivyo watashirikiana na kituo hicho kuinua wasanii.
Kambi amesema moja ya njia wanazotumia kutangaza kazi za wasanii ni kuwashirikisha kwenye matamasha mbalimbali ili kazi zao zionekane ambapo katika usajili wameandikisha wasanii zaidi ya 700.
Awali Ofisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Mkuza Victoria Andrea amesema kuwa wasanii wanapaswa kuwa wabunifu ili kuboresha kazi zao ziweze kuvutia watu.
Andrea amesema sekta ya sanaa ina ajira kubwa endapo itatumika ipasavyo kwani ina fursa nyingi zikiwemo za mikopo kwa ajili ya wasanii hivyo ni wao kujisajili ili watambulike kisheria.
No comments:
Post a Comment