Saturday, September 9, 2023

MTANZANIA ALICE GYUNDA AOMBA APIGIWE KURA MRS/MISS AFRICA UK 2023

MSHIRIKI wa shindano la Miss/Mrs Africa UK 2023 kutoka Tanania Alice Gyunda amesema kuwa endapo atafanikiwa kushinda taji hilo atajenga studio kwenye baadhi ya shule a msingi a Jijini Dar es Salaam ili kuzalisha vipaji vingi vya waimbaji waweze kuitangaa nchi kupitia muziki.

Aidha alisema kuwa ndoto yake nyingine ni kusaidia jamii ya watu wenye ulemavu hususani wanawake na watoto ili waweze kupata haki zao za msingi ili nao waweze kufikia malengo waliojiwekea katika maisha yao.

Gyunda ambaye ni mwalimu na mwimbaji akizungumza kwa njia ya simu kutokea nchini Uingereza anakoishi alisema kuwa endapo Watanania watampigia kura kwa wingi atakuwa na uwezo wa kushinda kwani hadi sasa bado yuko kwenye nafasi nzuri ya kufanya vema.

“Namewaomba Watanzania wanipigie kura ili nishinde ambapo vigezo ni kuonyesha utashi jinsi unavyo ongea na watu na namna unavyofanya mambo yako uwe mtu mwenye ushawishi na nikiwa mshindi nitakuwa balozi wa Kiswahili duniani na malengo yangu kuacha alama kwenye jamii kwa kusaidia watu wasiojiweza huko nyumbani japo niko mbali,”alisema Gyunda.

Alisema kuwa endapo atashinda atahakikisha anajenga studio kwenye baadhi ya shule za Msingi Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya wanafunzi ambao wana vipaji lakini hawana uwezo wa kurekodi itakuwa bure bure au kama kutakuwa na malipo yatakuwa ni madogo sana kwani muziki Tanzania uko chini sana licha ya kuwa na vipaji vingi kwani wengi hawawezi kurekodi kutokana na gharama kuwa kubwa.

“Nia ni kuinua muziki ambapo tutawekea kwa wanafunzi na vijana ambao wana vipaji vikubwa lakini kutokana na mazingira magumu ya uwezo wanashindwa kutimiza ndoto zao na wakipatikana vijana wenye vipaji wataenda kwenye matamasha ya American Good Talent au UK Good Talent ambapo vijana wa nchi za Uganda na Kenya huwa wanakwenda kwenye matamasha hayo ambapo atashirikiana na serikali ili nao washiriki wakirudi wawe chachu kwa wengine,”alisema Gyunda.

Aliongeza kuwa aliingia kwenye shindano hilo baada ya kuona tangazo na walipewa maswali 10 kuchujwa ambapo walikuwa 30 wakachujwa tena wakabaki 20 wakachujwa na kubaki 15 na baadaye mchujo mwingine ulifanyika na kubaki 13 ambapo wanatoka nchi za Afrika na Asia na kuwaomba Watanania wampigie kura ambapo hadi wakati anaongea alikuwa ameshapigiwa kura 1,800 kupitia https://africaukpageants.co.uk/poll/mrs-miss-africa-finalist-2023/

Friday, September 8, 2023

WAFANYABIASHARA WATAKA UBORESHWAJI WA HUDUMA SOKONI HAPO


WAFANYABIASHARA wa soko la Uhindini Wilaya ya Chunya wameomba uboreshwaji wa huduma  zikiwemo za miundombinu ya barabara maji na umeme ili waweze kutoa huduma kwa ubora kwa wateja wao.

Hayo yamebainishwa na wafanyabiashara wa wilaya hiyo wakati wa mkutano wa wafanyabiashara ulioongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Bw. Hamis Livembe September 7 wenye lengo la kupokea changamoto kero na maoni ya biashara ili kupatiwa ufumbuzi.

Mmoja wa wafanyabiashara wilayani hapo Qeen Mwasakela  amesema kuwa changamoto ya umeme ina takribani miaka 10 tangu soko hilo kuanzishwa na kuiomba serikali kutatua kero hiyo.

Naye katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga Ismail Masoud amewataka wafanyabiashara kueleza changamoto kwa mamlaka husika bila ya kuogopa ili zipatiwe ufumbuzi.

Katika hatua nyingine Masoud amewataka  wafanyabiashara hao kutoungana na baadhi ya maofisa wa mamlaka mbalimbali ambao wanahujumu mipango ya serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hasan ya ukusanyaji wa mapato.

Amesema kuwa wasikubali kudanganywa kuwa watapunguziwa au kufutiwa kodi kwa kutakiwa kutoa rushwa ambapo mamlaka zinazohusika zikifuatilia hujikuta akiwa na deni kubwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Bw. Hamis  Livembe amesema kuwa ukosefu wa huduma bora za msingi za kibiashara zinasababisha kushuka kwa biashara na ulipaji kodi kutofanyika vizuri na  atahakikisha changamoto hizo zinafikishwa kwenye mamlaka husika ili kupatiwa ufumbuzi.

WATAKA HATUA ZAIDI KUONGEZA MATUMIZI YA GESI

IMEELEZWA kuwa matumizi ya nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia ni asilimia moja tu huku matumizi ya kuni na mkaa ikiwa ni asilimia 98.9 hapa nchini huku ikihitajika hatua za makusudi za kuzuia matumizi hayo ya miti ili kupunguza athari kubwa za kimazingira.

Aidha serikali imeombwa kuweka bei ya juu ya
upatikanaji wa vibali vya ukataji wa miti ili kupunguza matumizi ya mkaa na kuhamasisha matumizi ya gesi majumbani.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na ofisa Mahusiano wa kampuni ya Taifa Gesi Ambwene Mwakalinga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali waliotembelea eneo la ujazaji wa gesi ya (LPG) kwenye ghala lililopo Kigamboni.

Mwakalinga amesema kuwa matumizi ya kuni na mkaa ni makubwa sana hivyo kuna haja ya serikali kuweka jitihada za makusudi za kukabiliana na hali hiyo ili kusitokee mabadiliko ya Tabianchi ambayo yanasababisha athari ikiwemo ukosefu wa mvua na uharibifu wa mazingira.

Naye meneja wa ghala hilo la Kigamboni Juma Masese amesema kuwa Taifa Gesi ndiyo kampuni ya hifadhi kubwa ya gesi hapa nchini ambayo inamilikiwa na mzawa ambapo kwa sasa inahifadhi ujazo wa metriki tani 7,400 ambapo inatarajia kuwa kampuni ya kwanza Afrika kwa kuwa na hifadhi kubwa ya nishati hiyo ambayo huletwa na meli kutoka nchi zinazozalisha gesi duniani.

Kwa upande wake ofisa usalama wa kampuni hiyo Albert Bungayela amesema kuwa wanatoa elimu kwa mawakala ili nao watoe elimu kwa watumiaji kuwa makini katika matumizi ili kuepuka madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya gesi.


Thursday, September 7, 2023

JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA TANZANIA WACHARUKA MKOANI MBEYA

 



WAFANYABIASHARA mkoani Mbeya waiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Mbeya kufanya marekebisho ya baadhi ya mifumo na Sheria za Kodi zinachochea rushwa .


Hayo yamesemwa na wafanyabiashara wa mkoani hapo wakati wa kupokea kero, maoni na changamoto za wafanyabiashara katika mkutano uliofanyika eneo la soko jipya la Mwanjelwa chini ya Rais wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe.

Wamesema kuwa TRA mkoani hapo imekuwa ikitumia mifumo hiyo kama chanzo cha mapato binafsi na si kuwasaidia kukuza biashara  za wafanyabiashara hao.

Aidha wameitaka serikali kutambua kuwa uchumi wa Watanzania wengi unajengwa kupitia biashara hivyo wanaiomba serikali ipunguze ututiri wa kodi .

Awali Mwenyekiti wa  Jumuiya wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe amesema kuwa moja ya sababu ya kufanya ziara mkoani hapo ni kukusanya changamoto , kero na maoni ili kuyatafutia ufumbuzi kwa mamlaka husika.

Livembe amesema kuwa zipo changamoto zinazowakumba wafanyabiashara hivyo kama kiongozi wa Jumuiya ya wafanyabiashara atahakikisha kero  zote zimetafutiwa ufumbuzi.

Naye katibu wa Jumuiya ya wafanyabiashara Tanzania Abdall Salim amesema kuwa wafanyabiashara wote Tanzania wanatakiwa kuungana kwa pamoja ili kukomboa biashara zao hivyo wanapaswa kujisajili na Jumuiya hiyo.

Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania ni Taasisi inayosimamiwa na wafanyabiashara wenyewe wenye lengo la kuhakikisha wanatatua changamoto za kibiashara.

Wednesday, September 6, 2023

JAMII YAFUNDISHWA USAWA WA KIJINSIA KULETA MAENDELEO JUMUISHI


HALMASHAURI ya Mji Kibaha imedhamiria kuhakikisha inafikia asilimia 50 ya usawa wa kijinsia ili kuleta maendeleo jumuishi kwa wananchi.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na ofisa maendeleo ya jamii kitengo cha jinsia wa Halmashauri ya Mji Kibaha Maria Nkangali wakati wa mafunzo kwa watu maarufu kwenye jamii kupitia mradi wa uongozi wa wanawake na haki za kiuchumi (WLER).

Nkangali alisema kuwa hadi sasa wamefikia asilimia 20 kwenye mradi huo wa miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026 ambapo hadi sasa wako kwenye kata tatu za Visiga, Mkuza na Pangani.

"Lengo la mradi huu ni kuwa na usawa wa kijinsia kwenye masuala mbalimbali ikiwemo uongozi, uchumi, umiliki wa ardhi na kupata huduma za kijamii,"alisema Nkangali.

Kwa upande wake wakili wa serikali kutoka Halmashauri ya Mji Kibaha Elizabeth Lukumay  alisema kuwa baadhi ya ndoa zinakuwa ni batili kutokana na kutofuata taratibu za kisheria hivyo inapotokea zinavunjika mwanamke na watoto wanakosa haki.

Naye mwenyekiti wa wazee kata ya Mkuza Anangisye Mwakapande alisema kuwa changamoto za ndoa na ardhi ni kubwa sana kutokana na kutokuwa usawa wa kijinsia.



Tuesday, September 5, 2023

MBUNGE MUHARAMI MKENGE AKUTANA NA NAIBU WAZIRI MKUU DK DOTTO BITEKO NA WAZIRI MSTAAFU WA MALIASILI WA KENYA NAJIB BALALA

MBUNGE wa Jimbo la Bagamoyo Muharami Shabani Mkenge, Leo tarehe 5 mwezi wa 9 alipata  wasaa wa kuwa na mazungumzo na Naibu waziri mkuu na waziri wa Nishati  Mhe Dotto Biteko,  pamoja na waziri wa maliasili mstaafu wa Kenya Mhe Najib Balala  ofisini kwa Naibu  waziri  mkuu 

Wakijadili uwekezaji  katika sekta ya chumvi, pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika katika Jimbo la Bagamoyo.

IMETOLEWA NA OFISI YA MBUNGE JIMBO LA BAGAMOYO🇹🇿

WAFANYABIASHARA WA PEMBEJEO NJOMBE WAMSHUKURU RAIS KWA RUZUKU YA MBOLEA

Na Mwandishi Wetu, Makambako

WAFANYABIASHARA wa pembejeo Soko Kuu la Mji wa Makambako, mkoani Njombe, wamemshukuru na kumpongeza Rais Samia kwa kuweka ruzuku ya mbolea iliyorahisisha shughuli za kilimo na upatikanaji mazao ya kutosha kwa wakulima mkoani humo.

Wizara ya Kilimo mwaka 2023/24, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), inaendelea kuratibu upatikanaji wa mbolea nchini  kutoa ruzuku kwa wakulima hadi mwaka 2025/26 ili kuongeza matumizi ya mbolea kutoka kilo 19 hadi kilo 50 kwa hekta, kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza upatikanaji wa mazao.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Pembejeo za Kilimo mkoani Njombe, Abdusalim Mangoma alitoa pongezi hizo kwa niaba ya wenzake wakati akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabishara Tanzania (JWT), katika ofisi za jumuiya hiyo zilizopo Mji Mdogo wa Makambako.

Vìongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wake Hamis Luvembe, wanafanya ziara ya kutembelea wafanyabishara wa mikoa ya Njombe, Mbeya na Songwe kwa ajili ya kusikiliza kero zinazowakabili ili kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu na kusajili wanachama  wake.

 Sanga alisema hatua ya serikali kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima imeonesha matokeo chanya kwenye uzalishaji mazao katika mkoa huo.

"Wakulima sasa wananunua mbolea kwa utaratibu maalum, tofauti na awali hawakuwa wanaunua mbolea kwa sababu bei zilikuwa siyo rafiki kwao hivyo kushindwa kupata mazao ya kutosha," alisema.

Naye Katibu wa wafanyabiashara hao, Mhema Wakala, alisema mfumo wa usajili wakulima umesaidia kutambulika maeneo walipo na mashamba yao.

"Hii imetusaidia wasambazaji wa mbolea kuwatambua wakulima na kuwafikia kwa urahisi hadi waliopo vijijini," alisema Wakala.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Mkoa wa Njombe na Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Sifael Msigala, alisema wafanyabiashara wa mikoa hiyo wanatekeleza majukumu yao kikamilifu kutokana na kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi wa serikali ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katibu wa JWT, Abdallah Salim, aliwasihi wafanyabishara kutekeleza vyema majukumu yao kwa kufuata taratibu na kanuni za serikali kwa sababu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anasikiliza na kuzifanyia kazi kero zinazowakabili.

"Endeleeni kufanyabiashara huku mkitembea kifua mbele kwa sababu Rais Dkt. Samia tunaendelea kumfikishia kero zenu na kuzifanyia ufumbuzi, lengo ni wafanyabishara kuwa na ustawi kwenye taifa latu," alisema.

Naye Katibu wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Mkoa wa Tanga na Mjumbe wa JWT, Ismail Masoud,  alisema Rais Dkt. Samia ni kiongozi wa mfano kwa sababu amegusa moja kwa moja matatizo ya wafanyabiashara nchini.

Kwa mujibu wa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akizungumza Agosti 8, 2023 kwenye kilele cha Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane, jijini Mbeya, alisema eneo la uzalishaji kabla ya ruzuku ya mbolea lilikuwa ekari 10,440,000  mwaka 2021/2022 hadi kufikia hekta 11,137,874.

Aidha, matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka hekta 363,599 mwaka 2021/22 hadi tani 580,529 5085,590 mwaka 2022/23

Uzalishaji wa chakula umeongezeka kutoka tani. 17,148,290 mwaka 2021/22 hadi tani 20,42,014 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la tani 3,000,000.

Aidha, mbolea zitakazohusika kwenye ruzuku ni mbolea za kupandia na kukuzia ambapo DAP kwaajili ya kupandia na Urea kwaajili ya kukuzia ambazo ni takribani asilimia 50 ya matumizi ya mbolea nchini.

Mbolea za kupandia na kukuzia za aina zingine zinahusika kwenye ruzuku kulingana na mahitaji ya soko.