Friday, August 25, 2023

𝗖𝗕𝗪𝗦𝗢𝘀 𝗦𝗔𝗦𝗔 𝗞𝗨𝗧𝗨𝗠𝗜𝗔 𝗠𝗙𝗨𝗠𝗢 𝗪𝗔 𝗠𝗔𝗝𝗜𝗜𝗦

Vyombo vya Watumia Maji vya jamii (CBWSOs) vinavyosimamiwa na Wakala ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), vimetakiwa kutumia Mfumo wa pamoja wa Ankara za Maji (MAJIIS), ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi.

Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Moshi Mhe. Kisare Makori, wakati akifunga mafunzo ya siku saba kwa Maafisa wa CBWSOs wa mkoa wa Kilimanjaro yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha USHIRIKA mjini Moshi .

Alisema, Serikali imedhamiria kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma ili  kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa urahisi, haraka na kwa gharama nafuu mahali walipo.

“Serikali ya awamu ya sita inachukua jitihada mbalimbali katika kuhakikisha TEHAMA inarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi, ambapo kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa kushirikiana na Wizara ya Maji, imetengeneza mfumo wa MAJIIS ili kutatua changamoto mbalimbali zilizokua zinaikabili Sekta ya Maji”, alisema.

Alifafanua kuwa, Serikali imewekeza katika mfumo huo hivyo ni jukumu la watumishi wa sekta ya Maji kufanya kazi ili kuhakikisha mfumo huo unakua mkombozi kwa wananchi.

Kwa upande wake mtaalamu wa TEHAMA kutoka Wizara ya Maji Mha. Masoud Almas alisema, mfumo wa MAJIIS umeboreshwa ili uweze kutumiwa na Vyombo vya Watumia Maji vya jamii (CBWSOs) vinavyotoa huduma vijijini ili kuhakikisha TEHAMA inarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi mahali walipo.

“Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa ni mkoa wa kwanza kuanza kutumia mfumo huu wa MAJIIS kwa CBSWOs na Wizara itaendelea kuhakikisha CBSWOs zote katika mikoa mingine zinatumia mfumo huu ili kurahisisha utendaji kazi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi waishio vijijini” alisema.

Aliongeza kuwa, hadi sasa mfumo huo umeleta mafanikio makubwa kwa Wizara ya Maji ikiwa ni pamoja na kuongeza ukusanyaji wa mapato na kurahisiha upatikanaji wa taarifa za Mamlaka zote za Maji nchini.

“Hadi sasa, Mamlaka za Majisafi na Usafi wa Mazingiara za miji mikuu ya mikoa, miradi ya kitaifa, miji ya Wilaya na miji Midogo 87 Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na Bodi za Maji za Mabonde 9 zinatumia Mfumo huu wa Pamoja”, alifafanua Almas.

Aidha, alibainisha kuwa ili kuongeza ufanisi katika utendaji kazi, mfumo wa MAJIIS umeunganishwa na mifumo mingine ya Serikali ikiwa ni pamoja na mfumo wa GePG, Mfumo wa Barua Pepe Serikalini (GMS), Mfumo wa Ujumbe Mfupi wa Simu za mkononi ambao hutumika kutoa taarifa za huduma kwa Wateja ikiwemo kutuma bili, mfumo wa NIDA na mfumo wa BRELA.

Jumla ya washiriki 72 kutoka Vyombo vya Watumia Maji vya jamii (CBWSOs) 39 vya mkoa wa Kilimanjaro walihudhuria mafunzo hayo.

JWT LATOA SIKU 7 WENYE MAVAZI YA JESHI KUYASALIMISHA

Jeshi la Ulinzi la  Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limetoa siku 7 za kusalimisha mavazi ya Jeshi kwa yeyote ambaye ana mavazi hayo iwe anavaa,kuuza au kwa wasanii kupanda nayo katika majukwaa ya utumbuizaji.

Hayo yametolewa na Luten Kanali Gaudentius Ilonda ambaye ni Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano makao makuu ya Jeshi (JWTZ) wakati akizungumza na wanahabari kuhusu katazo hilo na ukikwajji wa Sheria ya uvaaji wa mavazi hayo Jijini Dodoma

Aidha Luteni Kanali Ilonda amesema kuwa mavazi yanayokatazwa na Jeshi ni pamoja na kombati (vazi la mabaka), Makoti,Tisheti, Kofia,Viatu kwa mujibu wa sheria mbalimbali kama anavyoelezea.

Kwa upande wake msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa idara ya habari maelezo Bwana Gerson Msigwa amewaomba wazazi na walezi kuwakagua watoto wao ili kama Wana sale za Jeshi wazizuie na kusalimisha.

BILIONI 858.5 ZAIDHINISHWA BARABARA ZA WILAYA NCHINI

Katika mwaka wa fedha 2023/24, jumla ya barabara zenye urefu wa km 21,057.06 zitafanyiwa matengenezo, km 427 zitajengwa kwa kiwango cha lami, km 8,775.62 zitajengwa kwa kiwango cha changarawe, madaraja na makalavati 855 yatajengwa pamoja na mifereji ya mvua km 70.

Aidha, Jumla ya Shilingi Bilioni 858.517 zimeidhinishwa kwa ajili ya ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya barabara za Wilaya.

Taarifa hiyo imetolewa leo 24.8.2023 Jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Mhandisi Victor Seif wakati akizungumza ba waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa Majukumu na mwelekeo wake katika mwaka wa fedha 2023/24.

Mhandisi Victor,amesema Kati ya fedha hizo, shilingi Bilioni 710.31 ni fedha za ndani na shilingi Bilioni 148.207 ni fedha za nje kupitia miradi ya RISE, TACTIC, Bonde la mto Msimbazi na Mradi wa Agri connect.

Pia amebainisha Madaraja hayo yamejengwa katika mikoa ya Kigoma 92, Singida 24, Tabora 5, Kilimanjaro 10, Mbeya 2, Arusha 6, Morogoro 2, Rukwa 3, Pwani 1, Ruvuma 3 na Iringa 15.

Kwa Upande wake  Msemaji Mkuu wa Serikali,  Gerson Msigwa amesema TARURA imeanzishwa mwaka 2017 lengo likiwa ni kupanua mawanda ya namna ambavyo tutawahudumia Watanzania kwa kuwaboreshea barabara.

KPC YAWAASA WANAFUNZI KIBAHA KUZINGATIA MAADILI



WANAFUNZI Wilayani Kibaha Mkoani Pwani wametakiwa kuzingatia maadili wanayofundishwa shuleni na kutojiingiza kwenye vitendo viovu vya utovu wa nidhamu.

Hayo yamesemwa na msaidizi wa sheria kutoka Kituo cha Msaada wa Sheria Kibaha (KPC) Dominika Ndumbaro alipokuwa akifundisha somo la sheria ya mtoto kwenye shule ya sekondari ya Mwambisi.

Ndumbaro amesema kuwa ili kuepukana na vitendo vya ukatili ambavyo wanafanyiwa wanafunzi wanapaswa kutojiingiza kwenye vitendo viovu vinavyosababisha ukatili.

Amesema baadhi ya wanafunzi wamekuwa wakishiriki vitendo vya matumizi ya dawa za kulevya kama uvutaji bhangi, unywaji wa pombe, kwenda disko au sehemu za starehe.

Aidha alisema kuwa huko wanakutana na watu waliowazidi umri hivyo kuwafanyia vitendo vikiwemo vya ubakaji, ulawiti na hata vipigo endapo hawata sikiliza matakwa yao.

Aliongeza kuwa wanafunzi wanapojiingiza kwenye hali hiyo hushindwa kusoma na kujikuta wakiwa watoto wa mitaani na kujifunza wizi na kujiuza hivyo kutomaliza masomo yao.

Aliitaka jamii kwa kushirikiana na walimu na viongozi kukabili vitendo viovu kwa kuwahimiza wanafunzi kuwa na maadili mema na kumtanguliza Mungu ili kuepukana na vitendo hivyo.

Kituo cha Msaada wa Sheria kinanajihusisha na utoaji wa elimu ya sheria kwa masuala yote ya kisheria pia kinatoa msaada wa sheria kwa watu wenye changamoto za kisheria. 

Thursday, August 24, 2023

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU JULIUS NYERERE YATOA MSAADA WA WHEEL CHAIRS NA VITI.






TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani imetoa viti mwendo kwa wanafunzi wawili wenye ulemavu wanaosoma Shule ya Msingi Muungano iliyopo Wilayani Kibaha.

Aidha imetoa viti vitatu vya ofisini kwa ajili ya walimu wa shule hiyo ili kuwaondolea kero ya upungufu wa viti vya walimu kwenye shule hiyo.

Akikabidhi vifaa hivyo wakati wa mahafali ya 6 ya shule hiyo ya darasa la saba mratibu wa idara ya afya na mahitaji maalumu kutoka Taasisi hiyo Wilson Fungameza alisema kuwa wametoa viti mwendo hivyo baada ya kuona changamoto za wanafunzi hao wanazozipata wakati wa kwenda shule na kurudi nyumbani.

Fungameza ambaye ni muuguzi namba moja Tanzania na namba tano duniani alisema kuwa wamewapatia wanafunzi hao ili kiwarahisishia wazazi kwani walikuwa wakiwabeba kuwapeleka shuleni na kuwarudisha.

"Baada ya mwalimu mkuu kutoa ombi kwetu tuliona kuna umuhimu wa kuwasaidia watoto hao na wazazi kwani ilikuwa ni changamoto kubwa kwao hivyo kuwa na mazingira magumu ya kupata elimu,"alisema Fungameza.

Kwa upande wake katibu wa Taasisi hiyo Omary Punzi alisema kuwa jamii inapaswa kusaidia wanafunzi na watu wenye uhitaji ili waweze kufikia malengo yao kwa kuwapatia vifaa saidizi.

Punzi alisema kuwa kwakuwa taasisi yao inasaidia jitihada za serikali kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya elimu ili kuhakisha wanafunzi wanapata elimu bora.

Naye Mwalimu mkuu wa shule hiyo Faith Tawe alisema kuwa wanaishukuru taasisi hiyo kwa msaada walioutoa kwani utawapungizia mzigo wanafunzi na wazazi hao na pia viti vitasaidia walimu wakiwa ofisini.

Tawe aliomba wadau wengine wajitokeze kuwasaidia wanafunzi wanaotoka mazingira magumu pia shule ambayo nayo ina changamoto nyingi ikiwemo upungufu wa majengo.

Akisoma risala ya wahitimu wa shule hiyo Johnson Ernest alisema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya upungufu wa madawati ambapo yaliyopo ni 188 kati ya madawati 588 yanayotakiwa.

Ernest alisema kuwa kutokana na changamoto hiyo wanafunzi wengi wanakaa chini ambapo shule hiyo ina wanafunzi 1,175 na ilianzishwa mwaka 2021 na ina walimu 22.

WAENEZI WATAKIWA KUSEMEA MIRADI UTEKELEZAJI ILANI YA CCM

WAENEZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya za Mkoa wa Pwani wametakiwa kuisemea miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya chama.

Hayo yalisemwa Wilayani Bagamoyo na Katibu wa Siasa Itikadi na Uenezi wa CCM Mkoa wa Pwani David Mramba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa semina elekezi kwa waenezi wa wilaya za mkoa huo.

Mramba alisema kuwa semina hiyo ililenga waenezi hao kujua majukumu yao kwa wanachama na kwa wananchi ambapo wanapaswa kuielezea miradi ya maendeleo ambayo imetekelezwa kupitia ilani ya chama ya miaka mitano.

"Waenezi wanapaswa kusemea shughuli mbalimbali za chama pamoja na utekelezaji wa ilani kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ambayo inaongozwa na CCM,"alisema Mramba.

Alisema kuwa kuelezea miradi inayotekelezwa kwanza ni kumsaidia Rais Dk Samia Suluhu Hassan kumsemea jitihada anazozifanya kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

"Mambo mengi yanafanywa na serikali ya awamu ya sita lakini baadhi hayasemwi lakini mafunzo haya yawe sehemu ya kukitangaza chama na uzuri wa sera zake ili kuwavutia watu kujiunga nacho,"alisema Mramba.

Aidha alisema kuwa waenezi hao kupitia mafunzo hayo kubadilika na kwenda kisasa na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani nyakati za sasa zimebadilika lazima wajitume.

Kwa upande wake Mwenezi wa Kibaha Mjini Clemence Kagaruki alisema kuwa mafunzo jayo watayashusha ngazi ya kata na matawi ili kuboresha utendaji kazi.

Kagaruki alisema kuwa pia yamewajengea uwezo wa kujiandaa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji utakaofanyika mwakani na uchaguzi mkuu wa 2025.

Naye Mwenezi wa Wilaya ya Kibiti Juakali Kuanya alisema kuwa atakuwa kiungo muhimu katika kutoa taarifa mbalimbali kwa wananchi na umma kwa ujumla.

Kuanya alisema kuwa atatumia mafunzo hayo kuleta mabadiliko ambayo yataleta maendeleo kwa wananchi kupitia sera za chama na mipango mbalimbali ya kiwilaya na kitaifa.

Moja ya wakufunzi wa mafunzo hayo Khadija Juma alisema somo alilofundisha ni kuhusu uzalendo ambalo ni muhimu kwa kila Mtanzania kulijua ili kuitetea nchi yake.

Juma alisema kuwa ili watu waweze kutekeleza majukumu yao lazima wawe wazalendo kama ilivyokuwa kwa waasisi wa nchi ambao walitanguliza uzalendo kwanza.

Wednesday, August 23, 2023

KPC WAJADILI MAREKEBISHO YA BAADHI YA SHERIA

KITUO cha Msaada wa Sheria Kibaha (KPC) kimefurahishwa na marekebisho ya baadhi ya sheria yaliyofanyika kati ya mwaka 2019-2023 ikiwemo ya uendeshaji wa mirathi ambapo imeongeza adhabu kwa msimamizi wa mirathi anaposhindwa kutimiza wajibu wake kutoka shilingi 2,000 hadi milioni 2.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa kituo hicho Catherine Mlenga mara baada ya kufanya kikao kupitia marekebisho hayo yaliyofanyika kupitia bunge kwa mujibu wa sheria.

Mlenga alisema kuwa kwa mujibu wa sheria kifungu cha 107 (3) cha sheria ya usimamizi wa mirathi sura 352 ni kuwa msimamizi wa mirathi endapo atashindwa kupeleka taarifa za ukusanywaji na ugawaji wa mali ndani ya muda uliopangwa anaweza kuondolewa na kushtakiwa.

"Kabla ya mabadiliko adhabu ilikuwa ni kulipa shilingi 2,000 au kifungo cha miezi sita ambapo sheria hiyo imefanyiwa marekebisho ambapo faini isiyopungua milioni mbili au kifungo kisichopungua miaka miwili,"alisema Mlenga.