Wednesday, February 15, 2023

TBA YAENDELEA NA MIPANGO YA UJENZI KWA NYUMBA WATUMISHI



Na Mwandishi Wetu Dodoma

WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) wamefanikiwa kuendelea kutekeleza Malengo waliyojiwekea kwenye mpango mkakati wa mwaka 2021/22 hadi 2025/2026 pamoja na kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 ikiwa ni pamoja na kusimamia na kuhakikisha utengenezaji wa makazi bora kwa watumishi.

Hayo yamebainishwa na katibu mkuu mtendaji (TBA) Daudi Kondoro wakati akizungumza na wandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu wa wakala huo katika kipindi cha miaka miwili ya serikali ya awamu ya sita.

Kondoro amesema wakala wameendelea kutoa huduma ya uhakika ya makazi kwa serikali na kwa watumishi wa umma kwa kutoa huduma ya uhakika ya makazi na nyumba ambapo mpaka sasa kuna nyumba 1,622 zilizopangishwa kwa watumishi wa umma na pamoja na nyumba 7,700 zilizouzwa kwa watumishi wa umma Tanzania Bara Bara.

"TBA imetengeneza fursa za ajira na kutoa mafunzo kwa vitendo ambapo imetengeneza ajira takribani 100,000 kwa vijana walio na ujuzi na ambao hawana ujuzi kupitia miradi ambayo imekua ikitekelezwa,"alisema Kondoro.

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeishukuru serikali ya Rais Dkt. Samia kwa kukuendelea kuwawezesha kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ikiwemo kupewa fedha bilioni 54.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi.

WANANCHI WATAKIWA KUKOPA KWA MALENGO

Na Mwandishi Wetu Dodoma

KATIBU Mtendaji Mkuu wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Beng'i Issa amewataka wananchi kuacha kukopa fedha bila malengo badala yake watumie mikopo kama fursa kujiletea maendeleo.

Issa ameyasema  hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya baraza la uwezeshaji wananchi kiuchumi Katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita.

Amesema kupitia Baraza la Uwezeshaji kiuchumi wameunda njia mbalimbali ambazo zitawasaidia wananch kunufaika na Baraza hilo la kuwezesha wananchi kiuchumi ikiwemo mifuko ya mikopo ya jamii ambayo kwa sasa kuna jumla ya mifuko 72 ili kuwanufaisha wanchi wote walio katika mifuko hiyo ya jamii.

"Hadi sasa imewezesha kuwapatia ya zaidi ya shilingi bilioni 3.5 wafanyabiashara wenye viwanda vya kati na vidogo katika miradi 62 kwenye mikoa 12 nchini na inasimamia majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi katika mikoa yote 26 na Halmashauri zote nchini.

Aidha amesema kuwa  Watanzania zaidi ya 83,000 wamepata ajira za kimkakati na Baraza huandaa makongamano kwa ajili ya maonesho kwa lengo la kuendelea kutoa elimu kwa wananchi.

Tuesday, February 14, 2023

MFUKO WA MAWASILIANO KWA WOTE KUPELEKA VIFAA VYA TEHAMA SHULE MAHITAJI MAALUM



Na Mwandishi Wetu Dodoma

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unatarajia kutumia shilingi milioni 575 kwa ajili ya mradi wa kupeleka vifaa maalum vya TEHAMA vya kujifunzia kwa Shule 16 zenye watoto wenye mahitaji maalum hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Mtendaji mkuu wa mfuko wa mawasiliano kwa wote ( UCSAF) Justina Mashimba leo Februari 13,2023 Jijini Dodoma, wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mfuko huo.

Mashimba amesema kuwa vifaa vitakavyopelekwa katika shule hizo ni pamoja na TV, mashine ya (Nukta Nundu) Orbit reader (Machine za Kisasa), Laptops, (Printa ya nukta nundu).

"Jumla ya shule 811 zimefikishiwa vifaa vya TEHAMA ambapo kwa wastani kila shule imepewa Kompyuta 5, Printa 1 na Projekta 1 kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 ambapo Shule 150 zitafikishiwa vifaa vya TEHAMA bajeti yake ikiwa ni shilingi 1.9 na vifaa hivyo vitasaidia wanafunzi kusoma katika shule hizo,"amesema Mashimba

Amezitaka Shule hizo zitakazonufaika ni pamoja na Shule ya Sekondari ya Mpwapwa (Mpwapwa-Dodoma), Sekondari ya Mkolani (Mwanza), Sekondari ya Kashaulili (Mpanda-Katavi), Sekondari ya Morogoro (Morogoro), Sekondari ya Shinyanga (Kishapu-Shinyanga), Sekondari ya Wavulana Songea (Songea), Sekondari ya Kazima (Tabora) na Sekondari ya Haile Selassie (Mjini Magharibi)

Aidha akizungumzia hali ya mawasiliano nchini amesema kuwa mwaka 2009 Huduma za Simu ilikuwa asilimia 45 wakati kwa sasa imeongezeka hadi kufikia asilimia 96,Teknolojia ya 2G ni asilimia 96,3G ni asilimia 72,4G ni asilimia 55 na Geographical Coverage ya 2G ni asilimia 69; 3G ni asilimia 55 na 4G ni asilimia 36.

Amesema kuwa upande wa ujenzi wa minara Vijiji UCSAF imeingia mikataba kufikisha huduma katika kata 1,242 zenye Vijiji 3,654, Wakazi 15,130,250 ambapo Minara 1,087 yenye Vijiji 3,378 na wakazi 13,320,750 na Utekelezaji unaendelea katika Minara 155 yenye Vijiji 276 na wakazi 1.8 kwa ruzuku iliyotolewa ya shilingi bilioni 199 ikiwemo pia mradi wa kimkakati wa Zanzibar Minara 42, Shehia 38 ruzuku bilioni 6.9


BARAZA LA TAIFA LA UJENZI LATATUA MIGOGORO YA MIRADÍ YA UJENZI



Na Mwandishi Wetu Dodoma

BARAZA la Taifa la ujenzi limeendesha mafunzo ya kusimamia mikataba ya ujenzi na utatuzi wa migogoro katika miradi ya ujenzi kwa wadau 155 kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Hayo yasemwa Mtendaji Mkuu wa baraza la taifa la ujenzi Dkt.Matiko Mturi wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa baraza hilo katika serikali ya awamu ya sita.

Dkt Mturi amesema wameandaa rasimu ya mapendekezo ya gharama za msingi za ujenzi wa barabara kwa kila mkoa wa Tanzania Bara na kuwakilisha katika kikao cha wadau wa ndani ya serikali ili kupata maoni na ushauri wao.

"Baraza limefanikiwa kuratibu ,kuandaa na kuwasilisha Wizara ya ujenzi na uchukuzi(sekta ya ujenzi) andiko dhana lenye mapendekezo ya kuboreshwa kwa mfumo wa sheria zinazosimamia ujenzi wa nyumba na majengo nchini,"amesema Mturi.

Amesema mwelekeo wa taasisi katika kutekeleza majukumu ni pamoja na kufuatilia utekelezaji wa sera ya ujenzi nchini,kuandaa na kutekeleza mpango mkakati wa maendeleo wa sekta ya ujenzi,kutoa miongozo mbalimbali ya kitaalam ya maeneo mbalimbali ya ujenzi.

Aidha amesema Taasisi inaendelea kutoa mafunzo kwa wadau wa ujenzi kuhusu maadili na utekelezaji wa miradi ya ujenzi, sanifu jenga na usimamizi wa mikataba ya ujenzi kwa wadau mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo yanayolenga kukuza na kujenga wataalam mahiri katika sekta ya ujenzi.

Monday, February 13, 2023

REDIO ZITANGAZE HABARI ZA VIJIJINI

Na Mwandishi Wetu Dodoma

NAIBU Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew amevitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinaendelea kutangaza na kuanda makala na vipindi vinavyolenga Maeneo ya Vijijini ambako kumekuwa na usikivu mkubwa wa Redio.

Methew amesema hayo Jijini Dodoma katika Maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani ambapo kumefanyika Mkutano Mkuu wa mwaka wa watoa huduma wa sekta ya utangazaji Tanzania.

Amesema kuwa mchango wa vyombo vya habari ni mkubwa sana hasa Redio vimekuwa vikitoa taarifa nzuri hivyo kwa sasa Redio za FM zihakikishe zinakuwa na vipindi na makala nyingi zinazogusa Jamii na Utekelezaji wa Miradi ya serikali ya awamu ya sita.

"Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt  Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuhakikisha inasimamia na kuboresha upatikanaji wa habari serikalini na Taasisi zake kwa umakini na haraka hivyo vyombo vya habari vina haki ya kutumia fursa hiyo viweze kuitangaza nchi iliko toka na ilipo sasa ambapo kuna Utekelezaji wa miradi mingi inayowagusa Wananchi ikiwemo afya, Elimu,maji,nishati na miundonbinu,"amesema Methew.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amepongeza vyombo vya Habari hasa Redio za Dodoma kwa kuendelea kuitangaza Dodoma ambako ndio Makao Makuu ya nchi huku akiwataka wamiliki, wahariri na Waandishi wa habari katika siku mbili wapate fursa ya kuizunguka Dodoma kuona ujenzi unaoendelea kwenye mji wa kiserikali Mtumba kunaendelea ujenzi wa majengo ya wizara na Taasisi mbalimbali za serikali ambapo watakuwa wamefanya utalii wa ndani  ambako serikali imetoa fedha nyingi katika Ujenzi huo.

Kwa Upande wake Mkurugenzi wa kituo cha Redio cha Wapo Fm Edina Malisa ameishauri mamlaka ya Mawasiliano TCRA kuhakikisha inakuwa inavitembelea vyombo vya habari na kujadiliana changamoto mbalimbali ambazo wanazipata ili kuweza kushirikiana na serikali ili kuweza kupatia ufumbuzi na kuendana na sheria na kanuni za vyombo vya habari.

Mkutano Mkuu wa mwaka wa watoa huduma wa sekta ya utangazaji Tanzania umewashirikisha wamiliki wa vyombo vya habari, wakurugenzi, wahariri na Waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali hapa nchini ambapo Mkutano huo ni wa siku mbili.

Friday, February 10, 2023

12 WAFA 63 WAJERUHIWA AJALINI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

WATU 12 wamefariki dunia na wengine 63 kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa kuamkia Alhamisi Februari 9, 2023 Wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na kusababisha vifo vya watu 12 (wanaume nane , wanawake wanne) na majeruhi 63 (wanaume 40 wanawake 23).

Senyamule amesema ajali hiyo imetokea usiku Kata ya Pandambili Kijiji cha Silwa wilayani Kongwa, barabara ya Dodoma - Morogoro.

"Majeruhi wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo na miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkoa wa Morogoro na majeruhi wawili wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,"amesema Senyamule.

Amesema ajali hiyo imetokea majira ya saa  6 usiku na imehusisha lori la mizigo lenye namba za usajili T 677 DVX na basi la abiria  la Kampuni ya Frester lenye namba za usajili T 415 DPP lililokuwa likitokea Bukoba kwenda Dar es Salaam.

Akizungumza na wakazi wa Pandambili eneo ambapo ajali ilipotokea Senyamule ametoa rai kwa jamii kutii sheria bila shuruti ili kuepuka ajali. 

"Serikali ilikuwa na nia njema ya kuruhusu vyombo vya usafiri kutembea usiku, lakini sasa baadhi ya madereva wanaanza kutozingatia Sheria za usalama barabarani, tutaendelea kuwachukulia hatua kali,"amesema Senyamule.a

Pia mewatembelea majeruhi katika Hospitali ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo na kutoa pole na kuwatakia uponyaji wa haraka.

Naye Mkuu wa Operesheni na Mafunzo  wa Jeshi la Polisi Kamishna Awadh Haji ametaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa basi kutaka kulipita gari la mbele yake bila ya kuchukua tahadhari na kugongana na lori hilo  lililokuwa limebeba saruji.


WATUMISHI HOUSING A YAJENGA NYUMBA KWA WATUMISHI

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WATUMISHI Housing Investment (WHI) imeweza kujenga nyumba 983 kwa ajili ya watumishi wa umma katika mikoa mbalimbali nchini.

Aidha kupitia kampuni yake ya ujenzi imeshiriki katika ujenzi wa mji wa serikali Jijini Dodoma pomoja na majengo ya taasisi za serikali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa chuo Cha utumishi wa umma katika mkoa wa Singida.

Hayo yamesemwa na Mkurugezi mtendaji wa WHI Dkt Fred Msemwa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu mwenendo wa taasisi hiyo ambapo kumekuwa na ongezeko la kushuka kwa bei ya nyumba kutoka asilimia 10 hadi asilimia 30.

Amesema kuwa wanategemea kuwa na miradi mipya ya ujenzi katika mwaka wa fedha 2022/2023 ambayo ni Kawe, Dodoma, Gezaulole, mradi wa viwanda Arusha pamoja na nyumba za watumishi Halmashauri mpya.

"Yapo baadhi ya mafanikio ambayo taasisi imefanikiwa ikiwa ni pamoja na kupata vifaa vya upimaji wa ardhi vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 kutoka serikalini kupitia mkopo wa benki ya dunia unaoratibiwa na benki kuu ya Tanzania,"amesema Msemwa.

Watumishi Housing Investment ni taasisi ya umma iliyo chini ya ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora (OR-MUUUB) iliyoanzishwa Mwaka 2014 na ilianzishwa na serikali kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii ikiwemo mfuko wa pensheni kwa watumishi wa umma (PSSSF), mfuko wa hifadhi ya jamii ( NSSF) pamoja na shirika la nyumba la Taifa na mfuko wa bima ya Afya (NHIF)