 |
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lukenge kwenye mkutano maalumu |
 |
Mke wa mtuhumiwa Zena Manoza |
 |
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Lukenge waliohudhuria mkutano mkuu maalumu wakimsikiliza mkuu wa wilaya ya Kibaha hayupo pichani |
 |
Mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter Mshama akiangalia nyumba lilipotokea tukio la mtoto kuuwawa kwa kupigwa risasi,kushoto ni matundu ya risasi |
Na John
Gagarini, Magindu
WAKAZI wa
Kijiji cha Lukenge kata ya Magindu wilayani Kibaha wametakiwa kuendelea na
shughuli zao na kuishi kwa amani huku serikali ikiendelea na uchunguzi juu ya
tukio la mtoto kuuwawa kwa kupigwa na bunduki na baba yake mdogo Ally Sakalawe
(43) wakati akijibizana na polisi walipokwenda kukagua silaha.
Akizungumza
kwenye mkutano mkuu maalumu wa Kijiji hicho mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumter
Mshama alisema kuwa serikali inaendelea na uchunguzi na itatoa taarifa ili
kuondoa utata ambao umegubika tukio hilo kwa baadhi ya ndugu na wakazi wa
kijiji hicho kudai kuwa polisi ndiyo walimwua mtoto huyo aitwaye Mark Joel
Modest (15).
Mshama
alisema kuwa anajua kuwa tukio hilo limewaumiza sana wakazi hao pamoja na
familia husika lakini hawana budi kuwa na subira juu ya uchunguzi ili kubaini
ukweili juu ya tukio hilo.
“Nawaomba
muishi kwa amani na msiwe na wasiwasi serikali inaendelea na uchunguzi na
mtapewa majibu mara uchunguzi huo utakapokamilika watu wanaosema kuwa hawaishi
majumbani kuhofia kukamatwa wasiogope kama si wahalifu hawana haja ya kuogopa,”
alisema Mshama.
Alisema kuwa
vyombo vyote vya ulinzi na usalama vinafanya kazi zake na haki itatolewa kwani
jambo hili linasikitisha sana kwani mtoto kapoteza uhai na alikuwa hausiki kwa
lolote.
“Tunamasikitiko
makubwa ya kumpotez amtoto huyu ambaye hakuwa na hatia lakini ninachowaomba
muwe na imani na serikali kwani inalifanyia kazi suala hili ili kuweza kujua
ukweli hivyo nanyi mnapaswa kuwa na imani na endeleeni na shughuli zenu za
uzalishaji mali msiishi kwa hofu,” alisema Mshama.
Aidha alisema
kuwa wananchi hao pia wawe makini katika kumiliki silaha ambapo mtuhumiwa licha
ya kutokea kwa tukio hilo la mauaji pia alibainika kuwa alikuwa akimiliki gobore
bila ya kibali pia alikutwa na vitu mbalimbali ambavyo vinaleta maswali mengi
juu ya matumizi ya silaha hiyo.
“Lazima
tujiulize licha ya kifo cha mtoto huyo lakini mtuhumiwa ambaye anashikiliwa na
polisi alikutwa na bunduki mbili aina ya gobore, risasi ya mark 4, vipande vya
nondo na gololi vyote vikitumika kama risasi hivyo lazima tujiulize matumizi ya
silaha hizi,” alisema Mshama.
Awali
akielezea juu ya tukio hilo mke wa mtuhumiwa Zaina Manoza alisema kuwa siku ya
tukio hilo walikuwa wamelala ndani majira ya saa 8 kwenda saa 9 usiku askari
walifika na kuanza kupiga bunduki na wao kuanza kupiga kelele wakiomba msaada
kwa majirani.
Manoza
alisema kuwa walitakiwa kutoka nje na kuambiwa watoke nje na kujitambulisha kwa
majina lakini yeye akawaambia katika hao mtoto mmoja hayupo wakamwambia
akamwangalie chumba kingine ambapo alipokwenda alimkuta mtoto huyo akiwa
anavuja damu ubavuni.
“Baada ya
hapo walinitaka nikamwite mwenyekiti wa kitongoji na alipofika wakawaambia
wampeleke mtoto akapate tiba na kunitaka niongozane na huyo mtoto na mwanangu
mwingine tukiwa tumembeba nikaona kama hali ni mbaya nikajua tayari kafa,”
alisema Manoza.
Kwa upande
wake kamanda wa Polisi wa wilaya Caster Ngonyani alisema kuwa wananchi
wanapaswa kuishi kwa amani na hawatakiwi kuwa na woga na hawakwenda kwa ajili
ya kuwatisha wananchi na wanafanya kazi kwa kufuata sheria.
Ngonyani
alisema kuwa ripoti aliyopewa juu ya tukio hilo ilisema kuwa polisi walikwenda
kwenye nyumba hiyo baada ya kupata taarifa kuwa kuna silaha aina ya gobore bila
ya kibali ambapo taarifa hizo walizipata kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho
ndipo walipokwenda kwa ajili ya kuzikamata.
“Kulikuwa na
wamiliki wawili wa hizo silaha ambao ni Ally Sakalawe na Robinus Almas na
hawakutoa taarifa kwa uongozi kwa hofu taarifa kuvuja na walipofika waligonga
na kushindwa kuingia ndani baada ya mtuhumiwa kukataa kufungua mlango na kuanza
kurusha hewani,” alisema Ngonyani.
Alisema kuwa
mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa ya
Tumbi mbele ya baba Mzazi Modest na Anna Raphael mama mzazi
“Ndani ya
tumbo walikuta kipande cha chuma ambacho ni kipande cha nondo kwenye tumbo la
marehemu hali ambayo inaonyesh silaha iliyotumika ni gobore na silaha ya polisi
haitumii chuma inatumia risasi na zingekutwa tungejua kuwa polisi walihusika,”
alisema Ngonyani.
Aidha alisema
kwa mujibu wa ripoti hiyo ni dhahiri kuwa mtoto huyo alipigwa na mtuhumiwa
kwani tumboni kilikutwa kipande cha nondo ambazo zimekatwa na hutumika kama
risasi kwenye magobore hayo ambapo vipande vingine 10 vilikutwa nyumbani kwa
mtuhumiwa.
Tukio hilo
lilitokea Oktoba 28 mwaka huu wakati polisi walipokwenda kufanya upekuzi juu ya
uwepo wa silaha hizo aina ya magobore ambaye yalikuwa yakitumika kwa uhalifu na
uwindaji haramu ambapo licha ya mtuhumiwa wa kwanza kukutwa na silaha hizo pia
walimkamata Robson Almas naye akiwa na magobore mawili yakiwa hayana vibali vya
umiliki.
Mwisho.