Na John Gagarini, Chalinze
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete amekanusha kumtuma mgombea wa Chama Cha (SAU) Shaban Maulid kugombea Udiwani Kata ya Talawanda.
Akizungumza kwenye mikutano ya kampeni iliyofanyika kwenye Vijiji vya Kisanga, Vundumu na Talawanda kwenye kata hiyo alisema kuwa yeye hajamtuma mtu huyo wala hajawahi kukutana naye.
Ridhiwani alisema kuwa yeye hawezi kumtuma mtu kwenda kugombea na kama ni kumtaka mtu basi angependekeza kutoka chama chake na si chama kingine kwani hakuna ushirikiano na vyama vingine.
“Huyo mtu kwanza na mshangaa kwani sijawahi kumuona wala sijawahi kukutana naye wala sijawahi kumtuma mtu namshangaa unajua wagombea wengine hawana sera hivyo wanatumia majina ya watu kujipatia umaarufu,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa huo ni uzushi na wananchi hawapaswi kumsikiliza mtu huyo kwani chama chake hakina uhusiano na CCM wala na yeye na hajawahi hata kukutana naye.
“Achaneni na maneno ya kutuvuruga kwani kwa sasa sisi tunafanya kampeni ili kuhakikisha chama cehtu kinashinda kwenye nafasi zote ikiwemo Urais, Ubunge na Udiwani hivyo wasituvurge wakati huu wa kampeni kama hawana sera wakae pembeni,” alisema Ridhiwani.
Kwa upande wake meneja wa kampeni Jimbo la Chalinze Alhaj Amir Mkangata alisema kuwa anamshangaa mgombea huyo kwani hakuna muungano baina ya CCM na SAU kama ilivyo kwa muungano wa vyama vya upinzani vinavyounda UKAWA.
Alhaj Mkangata alisema kuwa wagombea kama hao hawana uwezo hivyo wanatafuta njia ya kujipenedekeza ili kuonyesha kuwa wametumwa kugombea.
“CCM haijaungana na chama kingine sasa mgombea huyo anavyojitapa kuwa ametumwa na CCM atuambie umoja huo unaitwaje atuambie hapa na tunamshangaa aache kabisa kutengeneza maneno ya uongo,” alisema Mkangata.
Kwa upande wake mgombea udiwani kata ya Talawanda Said Zikatimu alisema kuwa endapo atachaguliwa atahakikisha kuwa changamoto zilizopo kwenye kata hiyo zikiwemo za Afya, Elimu na Maji.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WAKULIMA na Wafugaji kwenye Kijiji cha Lulenge Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wametakiwa kuheshimiana ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza na kusababisha vurugu zinazopelekea kuvunja amani baina ya wananchi.
Hayo yalisemwa na mgombea Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete wakati wa mkutano wa kampeni kwenye kijiji cha Lulenge kata ya Ubena.
Ridhiwani alisema kuwa tatizo kubwa la migogoro linatokana na pande mbili hizo kutoheshimu mipaka yao kwani kuna baadhi ya maeneo yametengwa kwa jamii hizo mbili.
“Mnaweza kuepusha migogoro kwa kuheshimiana na kuheshimu mipaka iliyopo kwani kila mmoja akimweshimu mwenzake migogoro haitakuwepo na watu wataishi kwa Amani na upendo,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa serikali inajitahidi kuhakikisha inaondoa migogoro ikiwa ni pamoja na kutenga maoeneo kwa ajili ya mipango ya matumizi bora ya ardhi wakulima na wafugaji kwa baadhi ya maeneo huku mengine yakiwa yanaandaliwa kufanywa hivyo.
“Nyie ni ndugu hakuna sababu ya kugombana na kuingia kwenye migogoro isiyokuwa ya lazima kwani mtashindwa kufanya shughuli za maendeleo kutokana na migogoro hiyo,” alisema Ridhiwani.
Naye mgombea udiwani kupitia chama hicho Nicholaus Myuwa alisema kuwa atatumia taaluma yake ya kuwa Mwanasheria kuikabili migogoro hiyo kwa kuziweka pamoja jamii hizo.
Myuwa alisema kuwa endapo atachaguliwa kuwa diwani watahakikisha changamoto za maji, zahanati na barabara zinatatuliwa kwa kuwashirikisha wananchi.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
WANANCHI wa Jimbo la Chalinze wametakiwa kutowachagua wagombea wa vyama vya upinzani kwani wengi wao ni viongozi wa msimu ambao wanajitokeza nyakati za uchaguzi.
Hayo yalisemwa na meneja wa kampeni wa Jimbo hilo Alhaj Amir Mkangata wakati wa mikutano ya kampeni ya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete kwenye kata ya Miono.
Alhaj Mkangata alisema kuwa chama chenye uwezo wa kuwaletea maendeleo wananchi ni CCM na vyama vingine viongozi wao hawana uwezo hivyo ni vema wakaendelea kukiamini chama.
“Msiwachague wapinzani kwani wengi wao wanajitokeza wakati wa uchaguzi lakini uchaguzi ukishaisha hawaonekani hivyo mkiwachagua hamtawapata kwani wengine hawajulikani hata wanapoishi lakini wa CCM wanafahamika na wanatambulika,” alisema Alhaj Mkangata.
Alisema kuwa CCM imechagua wagombea wenye uwezo na wanasifa za kuongoza lakini wagombea wa upinzani hawana uwezo wa kuongoza hivyo hakuna sababu ya kuwachagua.
“CCM imefanya kazi kubwa ya kuwaletea wananchi maendeleo hivyo hakuna sababu ya kuchagua chama kingine kutawala hivyo msihadaike na wapinzani ambao wanaongopa kuwa wataleta maendeleo msikubali kudanganyika,” alisema Alhaj Mkangata.
Aidha alisema kuwa kwa mwaka huu chama kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi wa kishindo ili kiweze kuongoza na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Aliwataka wananchi kuichagua CCM kwani ina uwezo wa kuongoza na wagombea walioingia kwenye kinyanganyiro cha ugombea kwenye ngazi mbalimbali wana uwezo kwani wamechaguliwa kwa uwezo wao.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
KIJIJI cha Lulenge kata ya Ubena Jimbo la Chalinze wilayani Bagamoyo kinatarajia kuanza ujenzi wa zahanati Desemba mwaka huu ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa huduma za afya.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwenyekiti wa Kijiji hicho Lucas Sultan alisema kuwa ujenzi huo utaanza baada ya kukamilika michango ya kila kaya.
Sultan alisema kuwa walikubaliana kwenye mkutano wa Kijiji kila kaya itoe kiasi cha shilingi 20,000 kwa ajili ya kujenga zahanati kwa ajili ya kuwapatia huduma ya afya.
“Tayari tuna eneo la ukubwa wa hekari tano kwa ajili ya kufanya ujenzi huo kwani ndani ya miezi michache ijayo tutakuwa tumekamilisha michango hiyo ili kuanza ujenzi,” alisema Sultan.
Alisema kuwa kwa kaya itakayoshindwa kutoa mchango huo atapaswa kufanya shughuli za kijamii kama sehemu ya mchango wake ili kila mtu atoe jasho lake kwenye kijiji.
Alisema kuwa kwa sasa wanapata huduma ya afya kwenye zahanati binafsi ambako ni mbali kwani usafiri uliopo ni wa pikipiki ambapo gharama yake ni shilingi 8,000 kwenda na kurudi.
“Gharama za kwenda kupata matibabu ni kubwa sana hivyo ndiyo maana tuliona kuwa kuna haja ya kweza kuanzisha ujenzi wa zahanati ili kukabiliana na changamoto hiyo,” alisema Sultan.
Aidha alisema kuwa changamoto nyingine ni kwamba sehemu kubwa ya kijiji iko kwenye hifadhi ya Wami Mbiki hivyo kushindwa kufanya shughuli za kimaendeleo.
“Suala la Kijiji kuwa kwenye hifadhi linafanyiwa kazi na tunaamini tutapata majibu mazuri na tunaamini mipaka itatengenezwa na tutaishi kwa utaratibu mzuri,” alisema Sultan.
Alisema kuwa Kijiji hicho kina jumla ya wakazi wapatao 2,700 huku kukiwa na mifugo mbalimbali ngombe wakiwa 17,000, mbuzi 4,000 na mbuzi 2,000 ambapo wakazi wake ni wakulima na wafugaji.
Mwisho.
Na John Gagarini, Chalinze
MGOMBEA Ubunge Jimbo la Chalinze kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwani Kikwete amesema kuwa endapo atafanikiwa kuwa mbunge atahakikisha anasimamia upelekwaji wa fedha pensheni za wazee kwa wakati.
Aliyasema hayo katika kijiji cha Tukamisasa kata ya Ubena na kusema kuwa wazee wanapaswa kuheshimiwa na kupewa stahiki zao kwani wamefanya kazi kubwa ya kuifanya nchi ifikie hapa ilipo.
Ridhiwani alisema kuwa kwa kuwa sera ya chama inaonyesha kuwa kuanzia mwaka 2016 wazee watakuwa wanapata pensheni zao kwa ajili ya kuwasaidia katika maisha yao.
“Wazee wetu wamefanya kazi kubwa hivyo kuna haja ya kuhakikisha wanapata stahiki zao kwani walifanya kazi kubwa kuikomboa nchi na kuifanya iwe kama ilivyo sasa moja ya vitu nitakavyovisimamia ni kuhakikisha fedha zao zinakuja kwa wakati,” alisema Ridhiwani.
Alisema kuwa wazee wanakabiliwa na changamoto nyingi hivyo wakipata pensheni zao zitawasaidia kuweza kujikimu na kumudu mambo madogomadogo tofauti na ilivyo sasa.
“Wazee wakilipwa pensheni zao zitawasaidia kumudu maisha yao kwani walikuwa wakiishi kwenye hali ngumu kutokana na kukosa fedha hata za kununua vitu vidogovidogo ambavyo vingewasaidia kumudu maisha,” alisema Ridhiwani.
Aidha wazee wamehudumia nchi ya Tanzania na kutumia nguvu zao na jasho lao hivyo ni haki yao sasa kupata pensheni ambayo itawafanya wajisaidie kwenye maisha yao.
“Mbali ya kusimamia malipo hayo pia nitahakikisha wanapata huduma mbalimbali ambao ni fursa kwao ikiwa ni pamoja na matibabu pamoja na mikopo ambayo itawasaidia kwenye ujasiriamali,” alisema Ridhiwani.
Mwisho.