Na John Gagarini, Kibaha
MAKAMU wa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Mohamed
Gharib Bilali ameuchangia mfuko wa elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani
Pwani kiasi cha shilingi milioni 10.
Alichangia fedha hizo jana wakati wa uzinduzi wa mfuko wa
elimu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha uliofanyika kwenye uwanja wa Bwawani
Maili Moja wilayani hapa.
Alisema kuwa katika kufikia malengo ya Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) kwenye sekta ya elimu lazima kuwe mikakati maalumu ya kuweza kufikia
malengo kwa kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.
“Nawapongeza kwa kuanzisha mfuko huu na serikali itawaunga
mkono kwa hali na mali na mimi nawachangia milioni 10 kwa ajili ya kukabiliana
na changamoto kwenye sekta ya elimu katika mji wa Kibaha wilaya na mkoa mzima
wa Pwani.
“Ningependa suala la choo kuwa historia kwani hii ni aibu na
si changamoto ya kudumu na inapaswa kufanyiwa kazi mara moja na kuiondoa kabisa
kwani ni jambo lisilo pendeza na changamoto nyingine zilizopo kama vile za
upungufu wa madawati kwa shule za msingi, ukosefu wa maabara kwa shule za
sekondari, upungufu wa nyumba za walimu, matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa
na maktaba kupitia mfuko huo utasaidia kukabiliana na hali hiyo,” alisema Dk
Bilali.
Aidha alisema kuwa amefurahi kusikia kuwa fedha hizo
zitatumika kujenga maabara tatu katika sekondari za Pangani, Visiga na Miembe
Saba na kununua madawati 1,500 kwa ajili ya shule za msingi za Tandau, Lulanzi,
Misugusugu, Zogowale, Msangani, Viziwaziwa, Vikawe, Mwanalugali, Mkuza na
Kidimu.
Alizitaka halmahauri hapa nchini kuiga mfano wa Halmashauri
hiyo ya Mji wa Kibaha kwa kuanzisha mifuko kama hii kwa ajili ya kutatua
changamoto za elimu badala ya kuisubiri serikali kwani ni mgao inaoutoa ni
mdogo na elimu na mafunzo bora ni mkakati wa kipaumbele katika kufikia malengo
ya mipango ya maendeleo ya Taifa ya 2025 na kutumia Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza umaskini MKUKUTA na malengo ya milenia.
Awali Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Kasimu
Majaliwa alisema kuwa ubunifu wa kupata fedha kwa ajili ya Halmashauri 167 hapa
nchini ni mzuri kwnai utasaidia kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta
ya elimu.
Majaliwa alisema kuwa uboreshaji wa elimu unapaswa kusimamiwa
na watu wote wakiongozwa na madiwani na wananchi wote wanapaswa kujitokeza
kuuchangia na wizara yake itachangia kiasi cha shilingi milioni tano.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry
Koka alisema kuwa amefurahishwa na uzinduzi huo ambapo alisema kuwa moja ya
ndoto zake za kukabiliana na changamoto za elimu.
“Ili kuwa na elimu bora ni pamoja na kuwa na miundombinu
mizuri na watu wa kuiboresha ni wazazi pamoja na wadau wote ndani ya
Halmashauri licha ya kuwa wananchi wanachangamoto kubwa ya kuchangia hata hivyo
wameonyesha nia ya kuchangia kwa kujitolea na mimi nawaunga mkono kwa kutoa
kiasi cha shilingi milioni 16,” alisema Koka.
Awali mwenyekiti wa mfuko huo Anna Bayi alisema kuwa lengo la
kuanzishwa mfuko huo ni kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambapo
hadi sasa mfuko huo una kiasi cha shilingi milioni 210 na ahadi ni shilingi
milioni 34 huku malengo yakiwa ni kukusanya kiasi cha shilingi milioni 300.
“Tunatarajia kati ya fedha hizo zitajenga maabara tatu katika
shule ya sekondari Nyumbu, Miembe Saba na shule ya wasichana Kibaha ambapo
tumejiwekea mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiunga na mfuko wa elimu
nchini kwa lengo la kupata ruzuku ya miundombinu, samani, vifaa vya kufundishia
na kujifunzia,” alisema Bayi.
Mwisho.