Na John Gagarini,Kibaha
HALMASHAURI ya Kibaha mjini Mkoani Pwani imeanza mchakato wa
tathmini ya kutekeleza miradi ya soko pamoja na stendi ya kisasa zitakazojengwa
kwenye eneo la kitovu cha Mji huo kilichopo mkabara na barabara kuu ya
Morogoro.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Kibaha
Adhudadi Mkomambo alisema kuwa huo ni utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo
iliwekewa mkakati mwaka wa fedha wa 2010-2011 ambapo upembuzi upembuzi yakinifu unatarajia
kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Mkomambo alisema kuwa wameshaingia ubia na banki ya rasilimali
(TDB) ambayo ndio itakayosaidia kufanikisha gharama za ujenzi kwa ushirikiano
na halmashauri hiyo.
“Taratibu zilizopo sasa ni kufanya tathmini ya uhakika ya
gharama za miradi hiyo kabla ya Desemba mwaka huu kisha zoezi la ujenzi
litaanza mara moja baada ya tathmini kupatikana,” alisema Mkomambo.
Alibainisha kuwa stendi hiyo itakuwa na uwezo wa kuegesha
magari 50 kwa wakati mmoja na upande wa soko la
kisasa litakalokuwa na eneo la soko la kawaida litakalohusisha wakulima
wadogowadogo,na soko la kisasa litakalovutia wageni mbalimbali kutoka nje ya nchi.
Mwenyekiti huyo wa halmashauri amebainisha kuwa ujenzi huo
unatarajiwa kuanza mapema mwakani na kutarajiwa kukamilika mwaka 2015-2016 na
litatumia heka Tisa.
Mwisho.
Na John Gagarini, Kibaha
KAMANDA wa Jumuiya ya vijana
(UVCCM) wilaya ya kibaha Mjini Mkoani Pwani Silvestry Koka amesema kuna kila
sababu ya kuendelea kuimarisha chipukizi ndani ya chama ili kuwajenga vijana na
watoto wakue kwa misingi ya kizalendo.
Akifungua
mkutano wa uchaguzi wa viongozi wa Chipukizi wilayani humo, alisema tangu enzi
za waasisi wetu walitambua kwa kuweka taratibu ya kuwa na chipukizi kutokana na
kuwa nguzo kwa maslahi ya chama na Taifa.
Koka alisema kuanzia
sasa atahakikisha anakuwa mlezi wa kutatua changamoto za chipukizi wilayani
humo ikiwa ni sanjali na kuwawezesha kwenye mafunzo mbalimbali, michezo ili
kuwalinda na kuwapa motisha .
matokeo ya
uchaguzi huo Katibu wa UVCCM kibaha mjini Khalid King alisema viongozi hao
wapya wataongoza kwa kipindi kingine cha mika mitatu.
King alimtaja Shadya
Ibrahim kuwa ni Mwenyekiti wa chipukizi aliyepata kura 74 baada ya kumshinda
mpinzani wake Imran Mohamed aliyepata kura 58.
Katika nafasi ya
Mjumbe wa mkutano mkuu wa chipukizi ngazi ya mkoa amechaguliwa Jesca
Mkenda , mwakilishi wa mkutano mkuu wa Wilaya ikishikiliwa na Zainabu Mpemba
,na nafasi ya kamati ya uendeshaji ya Chipukizi ngazi ya Wilaya ni Joseph
Ernest,Marwa Mwise na Neema Ahmed .
Mwisho
Na John Gagarini, Kibaha
VIONGOZI wa Skauti nchini wametakiwa wametakiwa kuzingatia
uadilifu na weledi katika kutimiza majukumu yao ya kikazi ili kuiletea nchi
maendeleo na endapo watakwenda kinyume na taratibu watachukuliwa hatua kali
ikiwa ni pamoja na kuondolewa kwenye nyadhifa zao.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Skauti mkuu wa Tanzania
Mwantumu Mahiza alipokuwa akimwapisha kamishna mkuu wa Skauti Abulkarim Shah na
kusema kuwa sifa kuu ya skauti ni uadilifu.
Mahiza alisema kuwa ili kiongozi
aaminike na jamii ni lazima aonyeshe juhudi, weledi uamnifu na
ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yake.
“Kiongozi anapaswa kuwa mfano kwa jamii na anapaswa
kuhakikisha chama kinarudi kwenye mstari na sitasita kumwondoa kiongozi
anayeshindwa kutimiza majukumu yake kama katiba inavyosema ili kujenga heshima
ya chama hicho ndani na nje ya nchi,” alisema Mahiza.
Aidha alibainisha kuwa hatutakuwa tayari kufanyakazi
na baadhi ya viongozi walioonekana kupoteza sifa ya chama hicho na badala yake
wale wote waliohusika kukipunguzia sifa watabaki kuwa wanachama na kazi ya
uongozi tutaendelea na wachache wanaokidhi vigezo.
MWISHO.
Na John Gagarini, Kibaha
MAHAKAMA ya hakimu Mkazi Kibaha Mkoa wa Pwani
imemuhukumu mkazi wa Miembe Saba
wilayani Kibaha Amosi Chacha (40) kwenda
jela miaka 6 baada ya kukutwa na hatia katika kesi ya Wizi wa vocha za mtandao
wa simu za Tigo pamoja na kukutwa na mihuri bandia.
Mtuhumiwa huyo alikutwa na hatia kwa makosa yote mawili
yaliyokuwa yakimkabili Katika kesi iliyokuwa ikisikilizawa na Hakimu Mkazi, Aziza Mbadyo.
Mwendesha mashitaka wa Serikali Emmanuel Maleko ameieleza mahakama kuwa
mtuhumiwa huyo alikutwa akiwa na Mihuri
ya Afisa Mtendaji Mtaa wa Kwesimu pamoja na wa Kituo cha Ukaguzi wa Maliasili
cha Soni kilichopo Wilaya ya Lushoto Mkoa wa Tanga mnamo tarehe 03 Juni 2013
huko eneo la Sinza Wilaya ya Kinondoni Mkoa wa Dar es Salaam.
Imeelezwa kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa akitumia mihuri hiyo
katika usafirishaji wa mali asili kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam kwa lengo
la kuweza kuvuka vizuizi vya mali asili vilivyopo kwenye barabara kuu.
Aidha Maleko alieeleza mahakama kuwa mtuhumiwa huyo
alikamatwa eneo la Kibaha Mkoa wa Pwani akiwa na vocha za muda wa hewani za
kampuni ya simu ya Tigo zenye thamani ya Tsh. 5,000,000/= akizisafirisha kwenda
Tanga akitokea Dar es Salaam.
Mwendesha Mashitaka huyo wa Serikali aliongeza kuwa makosa
yote hayo mawili aliyokutwa na hatiya dhidi yake, Chacha anadaiwa
kuyatenda kwa nyakati tofauti.
Akisoma hukumu hiyo kwa muda wa saa moja na nusu, Mbadyo
alisema kuwa Mahakama imeridhika na maelezo ya upande wa Jamhuri hivyo imemtia
hatiani Amosi Mwita Chacha kwenda Jela miaka sita ambapo katika kosa la Wizi wa
vocha za Tigo alihukumiwa miaka minne na kosa la Kukutwa na Mihuri bandia
alihukumiwa miaka miwili hivyo adhabu
zote mbili zitakwenda pamoja na atatakiwa kwenda Jela miaka sita.
Na John Gagarini, Kibaha
MKAZI wa kijiji cha Nyanduturu
Wilaya ya Mkuranga Mkoa wa Pwani, Ally Makakatau (46) amepoteza maisha baada ya
kuvamiwa nyumbani kwake na kukatwa na mapanga na watu wanaodhaniwa kuwa ni
majambazi.
Kwa mujibu wa kaimu kamanda wa Polisi mkoani Pwani Kamishana
Msaidizi wa Jeshi la Polisi Juma Ally alisema kuwa tukio hilo lilitokea Julai 19 majira ya saa 7:30
usiku baada ya watu wapatao sita kuvamia nyumbani kwa Makakatua na kuvunja
mlango wa nyumba aliyokuwemo kisha kumshambulia kwa kutumia mapanga kichwani,
mkononi na miguuni.
Ally alisema kuwa watu hao walivamia katika nyumba hiyo na
kumtaka marehemu kuwapatia pesa ambazo alikuwa amepata baada ya mauzo ya mafuta
aliyokuwa amefanya jioni ya siku hiyo na alipokataa kutoa ndipo waliamua
kumkata kwa mapanga sehemu mbalimbali za mwili.
“Watu hao mbali ya kuvunja nyumba ya mfanyabiashara
huyo, pia walivunja duka na kuchukua pesa taslimu shilingi m 2,800,000 ambazo
zilikuwa ni za mauzo ya mafuta,” alisema Ally.
Aliongeza kuwa Jeshi la linawasaka watu hao na kuwataka
wanachi kuwapatia taarifa zitakazo saidia kuweza kuwapata waliohusika na tukio
hilo.
Aidha alisema kuwa mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa
Daktari na tayari umekabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za
mazishi.
Katika tukio lingine,
JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani linawashikilia watu ishirini (20) raia wa
Ethiopia kwa kosa la kuingia nchi bila kibali.
Alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 7:30 usiku
eneo la Mkuranga Mjini Wilaya ya Mkuranga.
Kaimu Kamanda huyo alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza
kuwa watu hao walikamatwa na askari waliokuwa doria wakiwa wanatembea makundi
makundi katika eneo la Mkuranga Mjini.
Alifafanua kuwa watu hao baada ya kuwahoji walibaini kuwa
walishushwa kwa gari na kuamua kutembea ili kuweza kuvuka kwenye eneo
lililokuwa na kizuizi cha Polisi.
Aliwataja raia hao wa Ethiopia waliokamatwa kuwa ni Habtamu
Ambesi (21), Yesak Mishamo (19), Biuk Moltumo (20), Apepe Eshetu, (20), Mesfin
Taddes, (20), Debero Shenke, (20), Teamat Kesse, (18), Gerenu Debere, (20),
Tofek Anshabo, (25), Lomabebo Gahtchowo, (20) na Asle Mugoro, (20).
Wengine ni Chakiso Eriso, (20), Wondimu Birhanu, (18),
Mulatu Menuru, (22), Gezahegn Lire, (21), Tileahnu Desta (20), Muly Geta (21),
Abdi Mohamed (22), Ali Lonsako (25), Johann Bincebo (20), Degnat Tesema (16),
Femasene Fitamo (17) na Temaggne Kebeda (25).
Aidha Ally alisema pia Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata
John Kataraya (50) mkazi wa Mbezi Beach Dar es Salaam ambaye alikuwa
akiwasafirisha Waethiopia hao.
“Rai hawa waliingia nchini kwa kutumia njia ya usafiri wa
gari kutoka Dar es Salaam kwenda Mikoa ya Kusini ili kuweza kwenda nchi jirani
ya Msumbiji na watakabidhiwa kwa idara ya uhamiaji kwa ajili ya taratibu
zingine za kisheria,” alisema Ally
Aidha, aliwataka wanachi waendelee kutoa taarifa kwa Jeshi
la Polisi pindi wanapowatilia mashaka wageni wanaoingia kwenye maeneo yao.
Mwisho