Jumaa ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini ameyasema hayo Mjini Kibaha wakati akifungua kikao cha Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Pwani.
Amesema kazi ya Jumuiya hiyo ni kuhakikisha jamii hususani vijana wanakuwa na malezi bora ili kutojiingiza kwenye makundi ambayo hayana maadili mema.
"Tuwape elimu na malezi mazuri vijana wetu na tuzungumze nao juu ya amani kwani amani pia huleta afya njema na amani ndiyo kila jambo hivyo tuhubiri amani,"amesema Jumaa.
Aidha amesema vijana nchini wanapaswa kudumisha amani na kutokubali kurubuniwa ili wasivunje amani iliyopo kwani bila amani hatutaweza kufanya mambo ya maendeleo.
"Vijana wanapaswa kulinda amani kwani ndiyo msingi wa Taifa la Tanzania na wasukubali kushawishiwa na watu kuharibu amani iliyopo kwani ikipotea ni gharama kuirudisha,"amesema Jumaa.
Amewataka viongozi wa Jumuiya hiyo kuanza maandalizi ya uchaguzi wa Jumuiya utakaofanyika mwakani kwani uchaguzi ndani ya chama ni mgumu kuliko uchaguzi wa vyama.
"Muanze maandalizi na kama kuna kiongozi anaona anauwezo ajiandae kugombea kwenye chama wakati ukifika kwani Jumuiya hii ndiyo inayobeba jumuiya zote za chama,"amesema Jumaa.
Aliongeza kuwa viongozi wanapaswa kuacha alama kwa kuwa na miradi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kununua ardhi pamoja na ofisi za makatibu wa jumuiya kwa kila wilaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Mkoa wa Pwani Josiah Jackson amesema kuwa uchaguzi umekwisha kilichobaki ni kujenga jumuiya na chama.
Jackson amesema kuwa wanachama waache makandokando kwa kuwaacha waliochaguliwa wafanye kazi zao na kuwaunga mkono ambapo kwa mkoa walipata madiwani 17 kutoka jumuiya.
Naye katibu wa CCM Mkoa wa Pwani Kitte Mfilinge amesema kuwa anaipongeza jumuiya kwa kufanya vizuri kwenye uchaguzi mkuu kwani mkoa umeshika nafasi tatu za juu hapa nchini.
Mfilinge amesema kuwa Jumuiya hiyo iko vizuri kwani ina mshikamano na imetulia hivyo kwa sasa wajiandae na uchaguzi wa jumuiya mwakani lengo ni kujenga chama ili kiwe imara.






