HALMASHAURI ya Mji Kibaha imepongezwa kwa kutekeleza kwa vitendo uhawalishaji wa fedha kwa kaya maskini kiasi kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) cha shilingi bilioni 3.1 kwa kaya 2,583.
Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejmenti ya Utumishi wa Umma Ridhiwani Kikwete kwenye mtaa wa Miwaleni kata ya Visiga alipokea akipokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Kikwete alisema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya Rais wa awamu ya Sita Dk Samia Suluhu Hassan serikali imetoa bilioni 51 kwa ajili ya mpango huo wa kusaidia wananchi.
Alisema kuwa wakati Rais wa awamu ya tano Dk John Magufuli aliacha mpango huo ukiwa kwenye awamu ya pili na ulikuwa ukitekelezwa kwa asilimia 75 lakini sasa wananchi wote wanafikiwa.
"Hadi sasa watu milioni 1.3 wananufaika na mpango huu wa kunusuru kaya maskini hali ambayo inaonyesha jinsi gani serikali inavyohakikisha wananchi wananufaika na miradi mbalimbali,"alisema Kikwete.
Alisema kata hiyo ulipo mtaa huo miaka tisa ilikuwa ni moja ya maeneo ysliyofanyiwa majaribio lakini leo watu wamenufaika na kuboresha maisha yao.
"Niwapongeze Halmashauri kwani hapa naona mabadiliko ni makubwa fedha zilizotolewa zinaonyesha matunda kwani zimebadili maisha ya watu kwani wamejikomboa kiuchumi,"alisema Kikwete
Aidha alisema kuwa kulikuwa na changamoto ya ucheleweshaji malipo lakini kwa sasa hilo halipo na mambo yanakwenda vizuri ili kila mwananchi anayelengwa na mpango afikiwe.
Akielezea kuhusu mpango huo mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde alisema kuwa katika malipo ya dirishani kwa mwezi Januari na Februari mwaka 2023 kiasi cha shilingi milioni 12.7 kililipwa kwa kaya 312 huku kiasi cha shilingi milioni 91 zililipwa kwa njia ya mitandao ya simu na benki kwa kaya 2,168.
Munde alisema kuwa kwenye miradi ya uendelezaji miundombinu kumefanyika ujenzi wa nyumba ya watumishi zahanati ya Vikawe na ujenzi zahanati ya Mwanalugali zote zikiwa zimepatiwa milioni 91.9 kila moja.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John alisema kuwa viashiria bora vya wanufaika ni uundaji wa vikundi ambavyo havina upotevu wa fedha.
John alisema kuwa walengwa wanaunda vikundi ambavyo vinajikopesha na kujikwamua kiuchumi kupitia Tasaf ni mkombozi kwa watu ambao walikuwa na hali mbaya ya kimaisha.
Naye Ester Mlinge ambaye ni mnufaika alisema kuwa ameweza kuboresha maisha yake kutoka kwenye kupanga nyumba hadi kumiliki nyumba ambayo anaishi na familia yake.
Mlinge alisema mbali ya kujenga nyumba pia wameanzisha vikundi vya kukopeshana ambapo hadi sasa wana akiba ya shilingi milioni 1.1.