Wednesday, August 14, 2024

SERIKALI YATAKIWA KUWA NA VITUO VYA KULEA VIPAJI VYA WACHEZAJI WA UMISSETA NA UMITASHUMTA ILI KUINUA MICHEZO NCHINI

SERIKALI imetakiwa kuwa na vituo vya kuwaandaa wachezaji wenye vipaji wanaoshinda kwenye michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA ili viweze kushindana kwenye mashindano ya kimataifa.

Aidha imetakiwa kuwezesha shule au vituo vya watu binafsi ambavyo vinakuza vipaji vya wanafunzi ili kuja kupata wanamichezo wenye uwezo na kuliletea sifa Taifa.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya ushiriki wa Tanzania kwenye mashindano ya Kimataifa hususani ya Olimpiki.

Bayi alisema kuwa ili kuwa na timu bora ambazo zitashindana kwenye mashindano za kimataifa lazima kuwe na vituo ambavyo vitawaandaa vijana mahiri ambapo wataandaliwa.

"Siri ya kufanya vizuri ni kuwa na vituo maalum au shule ambazo zitawachukua vijana hao ambao wanafanya vizuri kwenye mashindano hayo na kuwaandaa kwa muda mrefu ili waweze kufanya vizuri kwenye mashindano mbalimbali ikiwa ni pamoja na Olimpiki,"alisema Bayi.

Alisema kuwa kuwe na uwekezaji kwenye kambi maalum siyo kwa ajili ya kushiriki mashindano makubwa bali kuwaandaa wale wenye vipaji ambapo kwa sasa hao wanaofanya vizuri haijulikani wanaenda wapi.

"Tuliambiwa kutakuwa na vituo au shule 56 lakini jatujui imeishia wapi kwani kwa sasa michezo inakwenda kisayansi ambapo wenzetu wamewekeza kwa vijana wao wenye vipaji ambap ndiyo wanaleta mafanikio,"alisema Nyambui.

Alibainisha kuwa fedha zinazorudishwa kwa wananchi kupitia uwekezaji zipelekwe kwenye masuala ya michezo ambapo asilimia tano ya michezo ya kubahatisha inapelekwa Baraza la Michezo BMT lakini ni ndogo inapaswa kuongezwa ili ilete matokeo.

"Kuna shule au vituo kama vile Allince, Kipingu, Makongo, Bagamoyo na Filbert Bayi ni sehemu ambazo zinafanya jitihada kuandaa vijana ni vema vikawezeshwa na serikali ili viweze kuandaa vizuri vijana kwani wanawagharamia vijana hao kwani wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha,"alisema Bayi.

 Akizungumzia timu iliyoshiriki mashindano ya Olimpiki yaliyomalizika huko Ufaransa alisema wachezaji waliokwenda walikuwa na viwango vizuri lakini ilitokea tu bahati mbaya lakini waliandaliwa vizuri na kushinda au kushindwa ni matokeo tu.

WANANCHI PWANI WATAKIWA KUJITOKEZA KUJIANDIKISHA KUHAKIKI TAARIFA ZAO KWENYE DAFTARI LA MPIGAPICHA

 

WANANCHI Mkoani Pwani wametakiwa kujitokeza kwenye hatua za awali za kujiandikisha au kuboresha taarifa zao kwenye daftari la mpiga kura ili waweze kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Vijana (YPC) Kibaha Israel Ilunde alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha.

Ilunde alisema kuwa Ypc imepeta mradi wa michakato ya uchaguzi (K-VOTE) ambao unawahamasisha uwepo wa vijana kwenye masuala ya umma, elimu ya mpiga kura, uraia, kuwapatia elimu vijana wanaotaka kuwania nafasi za uongozi.

"Usipojiandikisha hutaruhusiwa kupiga kura na viongozi wabaya huwekwa madarakani na raia wema wasiojitokeza kupiga kura hivyo kuna haja ya wananchi kutumia fursa hiyo ya kujiandikisha au kuboresha taarifa zao mara zoezi hilo litakapofanyika Mkoani Pwani,"alisema Ilunde.

Alisema kuwa vijana milioni tano wataandikishwa kwenye daftari la kudumu la mpiga kura ambapo Tume Huru ya ya Uchaguzi iko kwenye uandikishaji na uboreshaji wa daftari la wapiga kura kwa ajili ya wapiga kura.

"Tutakuwa tukitoa elimu juu ya elimu ya mpiga kura kwa kushirikiana na mitandao mbalimbali lengo ni kuwahamasisha wananchi kushiriki uchaguzi kwani ni haki yao ya msingi ya kuchagua au kuchaguliwa,"alisema Ilunde.

Aidha alisema pia elimu hiyo wataitoa ndani na nje ya shule na vyuo ambapo watawahamasisha hata wale ambao walijiandikisha lakini hawapigi kura kwani wasipopiga kura watachaguliwa viongozi ambao watawaamulia na watu wengine.

"Ushiriki wa vijana kwa mwaka 2004 uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka 2005 vijana walikuwa ni asilimia nane na uchaguzi wa 2015 waliongezeka na kufikia asilimia 50 na tunatarajia mwaka huu na mwakani wataongezeka,"alisema Ilunde.

Aliongeza kuwa vijana hao waligombea nafasi mbalimbali kuanzia serikali za mitaa, udiwani na ubunge na baadhi walichaguliwa kuwa Manaibu Mawaziri wakiwemo Dk Zainab Katimba, Salome Makamba ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum.

"Vijana wapambane kugombea nafasi husika lakini wasinunue kura kwani zinavunja heshima ya nchi na zinaliaibisha taifa kwani wakiingia kwa njia hiyo uongozi wao utakuwa wa kulipa madeni hivyo wafanye siasa safi za heshima na siyo za matusi,"alisema Ilunde.

Aliwataka watoe hoja kwa kuweka utu mbele kwa kuijali jamii na wajue kuwa kuna kushinda na kushindwa na wakubali matokeo kwa kutokufanya fujo ambapo TAMISEMI na Tume Huru ya Uchaguzi watasimamia vyema vyema uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.


Tuesday, August 13, 2024

WIZARA YA MAJI IMEJIPANGA MABWAWA YA MAJI NA TOPE SUMU YANAKIDHI VIGEZO.

 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Wizara ya Maji kupitia Idara ya Rasilimali za Maji ina jukumu la kuhakikisha mabwawa ya maji na tope sumu yanakidhi vigezo vya usalama wa mabwawa kwa mujibu wa Sheria ya Rasilimali za Maji ili kuepusha madhara yatakayojitokeza katika jamii.

Hayo yamesemwa leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Wizara ya Maji uliopo Mtumba Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri, amesema Wizara ya Maji imeandaa mafunzo ya siku mbili katika kuhakikisha usalama wa mabwawa ya maji na tope sumu unaimarishwa.

Aidha Mhandisi Waziri amesema kuwa mafunzo yatahusisha watalaam kutoka wamiliki wa migodi kwa ajili ya usalama wa mabwawa ya tope sumu, wamiliki wa mabwawa makubwa ya maji, wataalam wa mabwawa waliosajiliwa na wataalam kutoka Serikalini.

Sambamba na hayo Mhandisi Waziri ameongeza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa kushirikiana na Tanzania Chamber of Mines na yatafanyika mkoani Mwanza .

TAKUKURU PWANI YAOKOA BILIONI 1.6

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 1.6 kutoka vyanzo mbalimbali vya Halmashauri ya Mji Kibaha.

Hayo yamesemwa na Naibu Kamanda wa Takukuru Mkoa huo Ally Haji wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha juu ya kipindi cha Aprili hadi Juni mwaka huu.

Haji amesema kuwa walibaini hayo wakati wa ufuatiliaji wa ukusanyaji wa ushuru wa huduma kama mbalimbali kuna viashiria vya uvunjifu wa maadili kwa kushindwa kuwajibika.

"Katika ufuatiliaji tuligundua kuwa baadhi ya watumishi wa Halmashauri kwenye kitengo cha ukusanyaji wa mapato watumishi kushindwa kufuata sheria, kanuni, na taratibu za ukusanyaji na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 1.6 zilizokuwa zinapotea,"amesema Haji.


Monday, August 12, 2024

VIJANA WAJA NA SERA MPYA

SERIKALI imezindua Sera mpya ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 toleo la 2024, ambayo inakwenda kujibu changamoto mbalimbali za vijana na kutoa mwongozo wa kuanzishwa rasmi kwa Baraza la Taifa la Vijana.

Hayo yamebainishwa leo Agosti 12,2024 Jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu,Mhe. Ridiwani Kikwete, wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya vijana kimataifa.

“Serikali imekwisha kamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Vijana ya mwaka 2007 na marekebisho yake imefanyiwa mwaka 2024 na leo hii tunakwenda kuizindua muda mfupi ujao.

“Ndugu washiriki changamoto nyingi zinazoelezwa kwa vijana zinatokana na ukweli kwamba yako baadhi ya maeneo hayana miongozo yake kupitia sera hii ya vijana ambayo tutaizundua leo nina hakika kabisa vilio vya vijana wengi vinakwenda kupataiwa ufumbuzi baada ya kupitishwa kwa sera hii”ameeleza.

Aidha, amesema kuwa sera hiyo inaeleza uelekeo na njia ambazo wanakwenda kuzitumia kwa pamoja ili kufikia malengo ambayo yanatatua matatizo waliyonayo vijana.

“Sera hii inakwenda kuanzisha baraza la taifa la vijana uanzishaji wa baraza hili la vijana unakwenda kuwa muarobani wa kutambua na kutatua changamoto nyingi za vijana.

“Vijana wamekosa maeneo ya kueleza changamoto zao vijana walikosa watu wa kuwasikiliza, vijana walikosa msukumo wa kufikisha changamoto zao na kuzitafutia majawabu kwa pamoja”amesema Mhe.Ridhiwan.

Amesema, ujio wa sera hiyo ya vijana na uudwaji wa baraza la taifa la vijana unaonesha wazi azma ya Rais Samia kujidhatiti na changamoto zote zinazo wakabili vijana zinapatiwa majibu.

Hata hivyo amesema kuwa sera hiyo pia inakwenda kutambua vijana katika sekta zote wanaofanya kazi katika maeneo hatarishi ikiwemo ya madini, maeneo ya uzalishaji mali ikiwemo mashambani na kwenye mifugo.

“Wapo vijana wanaofanya kazi za sanaa ikiwemo wabunifu, muziki, michezo, ubunifu na utungaji wa sanaa mbalimbali sera hii inakwenda katika maeneo hayo.

Pia  ametoa  wito kwa maafisa kazi kutambua kuwa nafasi zao siyo za kukaa ofisini wakisubiri vijana waje kulia na kueleza changamoto zao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu(Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Bi. Mary Maganga,amesema katika kuadhimisha siku ya vijana, wameendesha kongamano la siku mbili lililokutanisha vijana zaidi ya 3,000 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania.

“Katika kongamano hilo, vijana wamechangia juu ya mada za Sera ya Maendeleo ya 2050, fursa za kidigitali, vijana na uchumi, afya ya akili na saikolojia ya vijana na kusisitiza kuwa serikali imechukua maoni ya vijana katika eneo la elimu, afya, ajira na uwezeshaji.”amesema Bi.Maganga

Naye Mwakilishi wa Vijana, Charles Ruben amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake kuwainua na kuwasaidia vijana wa kitanzania na kuwa vijana wamepata elimu na ujuzi wa kazi unaofanya vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi na kuwapo ongezeko la vijana kwenye uongozi.

 “Ajira za vijana zimeongezeka ambapo kuanzia mwaka 2023 hadi 2024 ajira 607675 zimezalishwa huku ajira 204,000 zikitokana na miradi ya kimkakati inayotekelezwa hapa nchini huku akitenga Sh bilioni 1.1 kwa ajili ya miradi ya jenga kesho iliyobora BBT ambayo inawalenga vijana.”amesema Ruben

Friday, August 9, 2024

SELF MICROFINANCE WATAKA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Katika kuadhimisha kilele cha siku ya wakulima na wafugaji Nane Nane, Mfuko wa Fedha wa (SELF MICROFINANCE) ulio chini ya Wizara ya Fedha umewataka  wananchi wote wanaojishughulisha na shuguli za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kuchangamkia fursa za mikopo zinazotolewa na mfuko huo ili kukuza na kuongeza uzalishaji.

Wito huo umetolewa na Bi. Linda Mshana ambaye ni meneja masoko na uhamasishaji kutoka mfuko wa SELF wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la SELF lililopo katika maonesho ya Kitaifa ya Nanenane Jijini Dodoma.

Bi. Linda amesema, Mfuko huo una vifurushi mbalimbali kwaajili ya Wakulima, Wavuvi na wafugaji hivyo amewahimiza kujitokeza kwa wingi na kukopa mikopo hiyo ambayo imewekwa maalumu kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi.

Aidha,  Linda ameongeza kuwa mbali na Mikopo hiyo pia Mfuko wa Self unatoa Mikopo kwa taasisi ndogondogo za kifedha kwaajili ya kuwakopesha wakulima, wafugaji na wavuvi sambamba na mikopo mingine inayolenga kukuza uchumi wa watu mbalimbali.

"Self ina mikopo ya aina mbalimbali, tuna mkopo kwa ajili ya taasisi zinazokopesha, hivyo tunawakaribisha wakope na baadaye wawakopeshe wakulima, wafugaji na wavuvi,"amesema.

Linda amewakaribisha wananchi wote kutembelea banda lao lililopo katika maonesho hayo ili kupata elimu na kujua namna gani wanaweza kunufaika na Mikopo mbalimbali inayotolewa na Mfuko wa SELF.

Thursday, August 8, 2024

OFISI MAKAMU WA RAIS YAPONGEZWA UBUNIFU UTENGANISHAJI TAKA

Na Wellu Mtaki, Dodoma

MWENYEKITI wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu ameipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa utoaji wa elimu ya ubunifu wa mifumo ya utenganishaji taka ambao ni fursa ya ajira.

Mhe. Jaji Mwaimu ametoa pongezi hizo leo Jumatano Julai 7, 2024) wakati alipotembelea banda la Ofisi ya Makamu wa Rais katika maonesho ya Kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma.

Ameeleza kuwa taka zinazozalishwa nchini kwa sasa zimekuwa ni fursa kutokana na malighafi hiyo kutumika katika shughuli za uzalishaji mali na hivyo kuchangia katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya kaya, familia na jamii kwa ujumla.

“Taka ni fursa na pia ni vyanzo vya malighafi muhimu katika shughuli za uzalishaji kutoka. Nawapongeza kwa ubunifu wa utoaji wa elimu kuhusu fursa zilizopo katika taka kwani mbinu mbadala ya kukuza kipato cha jamii na kuhamasisha utunzaji wa mazingira” amesema Mhe. Jaji Mwaimu.

Aidha Jaji Mwaimu amewataka wananchi kutumia fursa ya maonesho hayo kutembelea Banda la Ofisi ya Makamu wa Rais na kujifunza teknolojia na bunifu mbalimbali zinazosaidia masuala ya uhifadhi wa mazingira kwani zipo fursa zinazoweza kusaidia ukuaji wa kipato katika ngazi ya kaya na jamii kwa ujumla.

Ameongeza kuwa taka ni fursa iliyojificha na hivyo elimu kuhusu fursa na manufaa yake wananchi wanapaswa kuitambua kwani sio kila kitu kinachotambulika kama takataka kinatakiwa kutupwa kwenye madampo, bali taka hizo zinaweza kutumika na kuwa fursa kujipatia kipato.

“Taka zinaweza kuwa fursa endapo zitachambuliwa kuanzia sehemu ya uzalishaji mpaka mtu wa mwisho anayetumia bidhaa husika, ili kuweza kuchangamkia fursa hiyo tunatakiwa kujua taka ambazo tunazalisha majumbani na namna zinavyotakiwa kutenganishwa” amesema Jaji Mwaimu.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Sarah Kibonde amesema Ofisi hiyo imekuwa ikitumia mbinu mbalimbali za kuemilisha umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira ikiwemo maonesho, mikutano ya wadau na vyombo vya habari.

Ameongeza kuwa katika kupanua wigo wa elimu kwa umma kuhusu masuala ya Muungano na Mazingira kupitia maonesho hayo, Ofisi ya Makamu wa Rais imeanisha maeneo matano ya kimkakati kwa ajili ya kuwafikia wananchi na wadau mbalimbali wanaotembelea banda la ofisi hiyo.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni pamoja na masuala ya nishati safi ya kupikia, mabadiliko tabianchi, uchumi wa buluu, fursa zitokanazo na taka, biashara ya kaboni na elimu kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

“Kupitia maonesho tuna nyaraka mbalimbali ambazo ni vitabu ikiwemo Kitabu cha Miaka 60 ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2032), vipeperushi, majarida ambayo ni mahsusi kwa ajili ya kutoa elimu kwa wananchi na wadau nk” amesema Kibonde.

Ofisi ya Makamu wa Rais imeungana na Wizara, Idara, Taasisi na Wakala za Serikali na sekta binafsi kushiriki maonesho ya kitaifa ya Sikukuu ya Wakulima Duniani (Nanenane) yanayofanyika kitaifa katika Viwanja vya Nanenane, Nzuguni Jijini Dodoma kuanzia tarehe 1-8 Agosti, 2024.

Maonesho hayo yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Chagua Viongozi Bora wa Serikali za Mitaa kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi”.