Thursday, May 16, 2024

TUMEPANGA, TUMETEKELEZA, KUTEKELEZA: JAJI MKUU

 

Na Mwandishi Wetu , Dodoma 

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza watumishi wote wa Mahakama kwa kuendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano awamu ya pili pamoja na programu ya Maboresho ya Miaka Mitano, ambazo zinalenga pia kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.

Mhe. Prof. Juma ametoa pongezi hizo kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Jaji Amidi wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, leo tarehe 16 Mei, 2024 kwenye Baraza Kuu la Wafanyakazi linalofanyika kwenye Ukumbi wa PSSSF jijini hapa.

“Nina kila sababu ya kuwapongeza wafanyakazi wa Mahakama kutokana na kujituma kwenu kuhakikisha kuwa tunatekeleza kwa ufanisi mipango tuliyojiwekea. Tufahamu kuwa kupanga ni jambo moja na utekelezaji wa mipango ni jambo lingine, kwetu sisi tumepanga, tumetekeleza na tunaendelea kutekeleza,” amesema.

Jaji Mkuu ametoa rai kwa wafanyakazi wote kutokurudi nyuma katika jitihada za kimaboresho kwani Viongozi wa Mahakama wanatambua na kuheshimu mchango wa kila mmoja ambao ndiyo uliowezesha utekelezaji wa programu mbalimbali za kimaboresho.

Ametumia fursa hiyo kuwahimiza watumishi wote kuipokea mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayotumiwa na Mahakama ya Tanzania ambayo siyo tu inawalenga wananchi na watumiaji wa huduma za Mahakama kwa kuwapa huduma kwa weledi, ufanisi, uwazi na kwa haraka lakini pia inalenga kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi za utoaji wa huduma.

Jaji Mkuu ametaja mfano wa Mfumo Mpya wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) ambao una faida lukuki zinazolenga kurahisha utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania. 

Amesema kuwa, badala ya kupitia malundo ya majalada na karatasi kukusanya takwimu, Mfumo huu utakusanya takwimu na taarifa mbalimbali kwa njia ya elektroniki kwa usahihi. 

Jaji Mkuu amesema kuwa takwimu zitasaidia kuona yaliyojificha, hivyo kusaidia katika utekelezaji wa mipango mbalimbali na kuboresha jukumu la utoaji haki. 

“Mfumo huu utasaidia kupima utendaji wa kila mmoja wetu bila ubaguzi au uonevu kwa watumishi. Utaongeza tija, ufanisi na uono wa viwango vya utoaji wa huduma wa kila mtumiaji wa mfumo huu, kwa mfano Majaji, Wasajili, Mahakimu, Masjala za Mahakama, wadau wote wa Mahakama,” amesema.

Jaji Mkuu ametaja faida nyingine ni kupungua kwa watumishi kukutana na wadaawa uso kwa uso na kuondoa lawama za kimaadili kwa vile wadaawa na wananchi watapata fursa ya kuingia katika mfumo kutafuta taarifa bila kumuona mtumishi wa Mahakama. 

“Hakutakuwa na nafasi ya mtumishi kudhaniwa kuwa kapokea rushwa ili atoe huduma. Mfumo huu pia utaboresha usimamizi na ukaguzi. Kwa mfano, Jaji au Hakimu Mfawidhi na Wasajili, wataweza kuona kila hatua ambayo shauri lolote linapitia na kufikia mbele ya Jaji au Hakimu, bila kuliita jalada au kuomba taarifa ya mashauri kutoka kwa aliye na jalada,” amesema.

Jaji Mkuu ametaja Mfumo mwingine wa Tafsiri na Unukuzi (Transcription and Translation Software -TTS) ambao umelenga kuwapunguzia watumishi, hususan Majaji na Mahakimu, mzigo mzito wa kuandika mienendo ya mashauri kwa kalamu ya mkono. 

Ameeleza kuwa Mfumo huo unapokea sauti, uinakili hiyo sauti na kuiweka katika maandishi ya kiswahili na unao uwezo wa kutafsiri hayo maandishi kutoka lugha ya kiswahili hadi kiingereza na pia kutoka lugha ya kiingereza hadi kiswahili.

“Mfumo wa TTS tayari umefungwa na kuanza kutumika katika Mahakama 11, ikiwemo baadhi ya Mahakama Kuu (ambazo pia ni Masjala Ndogo za Mahakama ya Rufani),” Mhe. Prof. Juma amesma. 

Amesisitiza kuwa, mfumo huo wa TTS utaongeza ufanisi katika uchukuaji wa mwenendo wa shauri kwa kumpunguzia Jaji au Hakimu mzigo wa kusikiliza na kuandika kwa wakati mmoja na kuharakisha kupatikana kwa mienendo ya mashauri kwa ajili ya kukata rufani.

TANZANIA YAADHIMISHA MIAKA 60 YA KIDIPLOMASIA KATI YAKE NA CHINA

 

- Filamu ya " Amazing Tanzania " yazinduliwa China

Na Mwandishi Wetu - Beijing 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeadhimisha Miaka 60 ya Kidiplomasia kati yake na China sambamba na uzinduzi wa mwaka wa Utalii na Utamaduni ulioambatana na  uzinduzi rasmi wa filamu ya “Amazing Tanzania” Mei 15, 2024 jijini Beijing China.

Akizungumza katika Maadhimisho hayo Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema uhusiano kati ya China na Tanzania ulianza tangu kipindi cha Hayati Mwalimu Julius  Kambarage Nyerere.

Aidha,amesema mahusiano kati ya China na Tanzania  ni thabiti chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping.

"Tunapoadhimisha miaka 60 ya uhusiano wetu  na pia tunasherehekea mwaka wa utamaduni na utalii kama ilivyotangazwa na viongozi wetu mwaka 2022 katika ziara ya Kiserikali ya Rais Samia Suluhu alipotembelea nchini China" Mhe. Kairuki amesisitiza.

Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ally Mwinyi pamoja na mwigizaji maarufu wa filamu kutoka China, Jin Dong kwa kushiriki katika uandaaji wa filamu hiyo.

Kufuatia uzinduzi wa filamu ya " Amazing Tanzania " Mhe. Kairuki amesema kuwa filamu hiyo itaonyesha vivutio vya utalii wa Tanzania kwa soko la utalii la China na kwamba Tanzania inatarajia kupokea watalii wengi kutoka nchini China baada ya uzinduzi huo.

Naye,Waziri wa Utamaduni na Utalii wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Sun Yeli amesema kuwa urafiki wa jadi kati ya China na Tanzania ulijengwa na viongozi wa kizazi cha zamani wa nchi hizo mbili na kwamba 

tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia miaka 60 iliyopita China Tanzania imestahimili jaribio la mabadiliko ya mazingira ya kimataifa na kuimarika zaidi.

"Leo tunapokutana hapa kuzindua mwaka wa Utalii na Utamaduni wa Tanzania China natumai tutaifanya kuwa mwanzo mpya wa kuendeleza mabadilishano ya kitamaduni na ushirikiano wa Utalii ili kurahisisha ziara zetu za pande mbili,  mabadilishano kati ya taasisi za kiutamaduni na sanaa na vile vile kampuni za utalii kuongeza usambazaji wa bidhaa za utalii." amesisitiza.

Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, wajumbe wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania akiwemo Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro,Waziri wa Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita  pamoja na maafisa wa taasisi mbalimbali za sekta za umma na binafsi.

Wednesday, May 15, 2024

MAKUMBUSHO YA CHINA NA TANZANIA KUSHIRIKIANA




Na Mwandishi Wetu-Beijing 

Makumbusho ya Taifa  ya China na Tanzania zimekubaliana  kushirikiana katika kubadilishana uzoefu, teknolojia na kuwa na maonesho ya pamoja  kwa lengo  la kuhakikisha kuwa huduma za makumbusho zinakuwa na faida kwa pande zote mbili za nchi hizo.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la China, Gazo Zheng yaliyofanyika kwenye Makumbusho ya China jijini Beijing Mei 14,2024.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema kwa kuwa Makumbusho ya Taifa la China ina uzoefu wa miaka mingi, ni vyema ikashirikiana na Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika dijitali ,kufanya tafiti, kuwa na Maonesho ya pamoja, kuonesha utamaduni na historia ya nchi zote mbili pamoja na kubadilishana uzoefu wa utaalamu katika kutunza na kuhifadhi mikusanyo.
Aidha, Mhe. Kairuki amesema kuwa Tanzania ingependa kujifunza namna ya  kuvutia kizazi cha vijana kinachokua ili kiwe na utamaduni wa kutembelea Makumbusho mbalimbali zilizopo nchini Tanzania.

Amesema  Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake ulipo jijini Beijing nchini China utahakikisha unafuata taratibu zote za kuwepo kwa  Mkataba wa Makubaliano kati ya makumbusho hizo ili kurasimisha ushirikiano huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Zheng amesema Makumbusho ya Taifa la China iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo yote yaliyopendekezwa.

“Makumbusho ya Taifa la China ina uzoefu mkubwa na ina wataalamu zaidi ya mia moja hivyo ina furaha kushirikiana na Makumbusho ya Taifa la Tanzania hasa katika kuhifadhi mikusanyo, kufanya tafiti, kubadilishana uzoefu na namna ya kuvutia  vijana kuwa na utamaduni wa kutembelea makumbusho” amesema.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, wajumbe wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania akiwemo Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa pamoja na maafisa wa taasisi mbalimbali za sekta za umma.

Waziri Kairuki yuko nchini China kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Kidiplomasia kati ya Tanzania na China pamoja na uzinduzi wa mwaka wa Utalii na Utamaduni na pia uzinduzi rasmi wa filamu ya “Amazing Tanzania” utakaofanyika Mei 15, 2024 jijini Beijing

Wednesday, May 8, 2024

KUSIMAMA VIVUKONI NI AMRI SIO HIARI

Mkuu wa Dawati la elimu ya usalama barabarani Tanzania Kamishina Msaidizi wa Polisi, Michael Deceli amewataka madereva wa vyombo vya moto kuzingatia alama za barabarani ili kupunguza ajali kwa watumiaji wengine wa barabara.

Akizungumza Leo Mei, 08 baada ya kuhitimisha utoaji wa elimu ya uvukaji wa barabara kwenye vivuko vya waenda kwa miguu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani Deceli amesema kumekuwepo na baadhi ya madereva wa vyombo vya moto wakiwemo madereva wa serikali kutokusimama kwenye  vivuko vya waenda kwa miguu na kupelekea ajali katika baadhi ya maeneo.

"Suala la kuheshimu alama za barabarani ni la kila dereva anayeendesha  chombo cha moto, Sheria haijabagua madereva wa kuziheshimu alama hizo na wengine kutokuheshimu".

Kadhalika, Deceli amewataka madereva walioweka magari yao ving'ora pasipo kuwa na kibali cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuondoa mara moja na wale watakao kamatwa wakiwa hawana vibali hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Friday, May 3, 2024

KPC YAWATAKA WANANCHI KUTUMIA KITUO CHAO KUTATUA CHANGAMOTO ZA KISHERIA.

 

WANANCHI wa Halmashauri ya Mji Kibaha wametakiwa kukitumia Kituo cha cha Msaada wa Kisheria (KPC) ili kutatua changamoto zinazohusiana na masuala ya kisheria ili kuokoa muda wa kwenda Mahakamani.


kimeendelea na utoaji elimu na msaada wa kisheria kwa makundi mbalimbali ili kuwajengea ufahamu wa sheria wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Akizingumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Mkurugenzi wa KPC Catherine Mlenga amesema kuwa baadhi ya masuala ya kisheria yanaweza kutatuliwa kituoni hapo kabla hawajayafikisha Mahakamani.

Mlenga amesema kuwa wananchi wanaweza kutatuliwa changamoto za kisheria na kuokoa muda ambao wangeutumia kwenda mahakamani na kufanya shughuli zao za maendeleo.

Aidha amesema kuwa wanatoa elimu pamoja na msaada kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali kupitia ustawi wa jamii pamoja na mahakama.

Amewataka wananchi wa Kibaha kukitumia kituo hicho ili waweze kusaidiwa pale wanapopata changamoto za kisheria na wasifumbie vitendo vya ukatili ndani ya jamii kwa kutoa taarifa.

Mwisho.

KPC YAENDELEA KUTOA MSAADA NA ELIMU YA KISHERIA KWA WANANCHI WA KIBAHA

KITUO cha Msaada wa Kisheria (KPC) kimeendelea na utoaji elimu na msaada wa kisheria kwa makundi mbalimbali ili kuwajengea ufahamu wa sheria wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Akizingumza na waandishi wa habari baada ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa Shule mbalimbali Mkurugenzi wa KPC Catherine Mlenga amesema kuwa elimu hiyo ni kwa wananchi wote.

Mlenga amesema kuwa wanatoa elimu pamoja na msaada kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali.

"Tunaishukuru serikali kwa kutupatia vibali ambavyo vinatuwezesha kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi lengo likiwa ni kuwapa uelewa wa kujua sheria mbalimbali,"amesema Mlenga.

Amesema kuwa elimu ya sheria imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi ambapo baadhi wamepata uelewa na kuweza kutoa taarifa pale wanapoona kuna uvunjwaji wa sheria.

"Elimu tunayoitoa ni kuanzia kwa wanafunzi mashuleni, majumbani, masokoni, kwenye nyumba za ibada, kwenye mikutano na mikusanyiko mbalimbali ta kijamii,"amesema Mlenga.

Aidha amesema kuwa wanatoa msaada wa kisheria bure kwa watu wasiokuwa na uwezo hususani wanawake na watoto na kuwapigania hadi kupata haki zao.

"Sheria tunazowafundisha ni zote ikiwa ni pamoja na mirathi, ndoa, ardhi, matunzo ya watoto, haki za watoto, sheria za kazi, mazingira, na nyinginezo,"amesema Mlenga.

Amewataka wananchi wa Kibaha kukitumia kituo hicho ili waweze kusaidiwa pale wanapopata changamoto za kisheria na wasifumbie vitendo vya ukatili ndani ya jamii kwa kutoa taarifa.

Wednesday, May 1, 2024

WAHITIMU JKT KUJITOLEA WATAKIWA KUTANGULIZA UZALENDO

 




Na John Gagarini, Kibaha

VIJANA wanaohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakujitolea wametakiwa kutumia dhana ya uzalendo katika shuguli za ujenzi wa Taifa ili kuiletea nchi maendeleo.

Hayo yalisemwa Mlandizi na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John wakati wa kufunga mafunzo ya (JKT) ya kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT kwenye Kikosi cha Ruvu Kibaha.

John alisema kuwa Vijana hao wameandaliwa vema kulipambania Taifa hivyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao lazima watangulize uzalendo.

"Zingatieni mambo manne muhimu Utii, nidhamu, uhodari na uaminifu haya ndiyo mambo ya kuzingatia hapa ndipo mtakuwa mnafanya uzalendo ambayo ndiyo nguzo kuu ya mafunzo yenu,"alisema John.

Alisema kuwa pia wawe na uhodari kwenye jambo moja ambalo ni fani ili wawe mahiri kwani kuchanganya mambo mengi kwa wakati mmoja hawataweza kuwa mahiri.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Meja Jenerali Ibrahim Mhona alisema kuwa vijana hao wanapaswa kujilinda kiafya kwani suala la afya ni muhimu sana.

Mhona ambaye pia ni Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alisema kuwa mafunzo hayo ni ya kuwapatia stadi za maisha na baadaye watapata stadi za kazi ikiwa ni hatua ya pili baada ya hatua ya kwanza.

Alisema kuwa mafunzo hayo yamekuza moyo wa uzalendo ukakamavu na kutumia vizuri muda na hawajakosea kujiunga na mafunzo hayo ya kujitolea kwani maamuzi yao ni ya busara na kuwapongeza wazazi na walezi kwa kuwapeleka vijana wao kwenye mafunzo hayo.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa JKT Kanali Robert Kessy alisema kuwa wakati wa kutekeleza majukumu yao wahakikishe wanatatua changamoto bila kuvunja sheria na kuwa na nidhamu bila kusahau uhodari kwani Taifa limewekeza sehemu sahihi.

Kessy alisema kuwa vijana wanapaswa kujitolea kulitumikia Taifa na kumuenzi Baba wa Taifa ambaye aliasisi Jeshi hilo na wahakikishe wanaonyesha uzalendo kwa vitendo na weledi na wajiulize watalifanyia nini Taifa siyo Taifa kuwafanyia nini pia wahakikishe wanasimamia viapo vyao.

Awali Mkuu wa Kikosi cha Ruvu 832 KJ Kanali Peter Mnyani alisema kuwa mafunzo hayo ya awali ya kijeshi waliyoyapata vijana hao ni pamoja na ukakamavu ujasiri ambavyo wamefanya kwa vitendo.

Mnyani alisema kuwa mafunzo hayo yalikuwa ya muda wa miezi minne kati ya miezi 24 ya mkataba wao ambapo walijifunza utimamu wa mwili, usomaji ramani, uraia,  usalama na utambuzi na kwata za silaha ndogo ndogo.

Akisoma risala ya wahitimu wa mafunzo hayo Lulu Godfrey alisema kuwa Vijana wa Kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT walianza mafunzo hayo Desemba 2023.

Godfrey alisema kuwa kwenye mafunzo hayo walifundishwa mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja mbinu za ulinzi, ukakamavu, utii, ulinzi wa taifa ujasiri uvumilivu, na hawatatumia vibaya mafunzo hayo kinyume na malengo ya Taifa.

Jumla vijana 800 walijiunga na mafunzo hayo ambapo waliohitimu walikuwa 776 wavulana wakiwa 438 na wasichana walikuwa 338 na vijana 24 hawakumaliza mafunzo hayo na kwa kipindi cha miezi 20 watakuwa kwenye majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na malezi, uzalishaji mali na ulinzi.

 Mwisho.