Friday, March 15, 2024

TUENDELEE KUUNGANA KUKABILIANA NA MAAFA NCHINI” MKURUGENZI MSAIDIZI JANE

NA MWANDISHI WETU,DODOMA

Mkurugenzi Msaidizi Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bi. Jane Kikunya amesema Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau mbalimnali katika masuala ya uratibu wa maafa nchini ili kuendelea kuwa na stahimilivu na maafa. 

Ameyasema hayo wakati akifungua Warsha ya siku moja iliyowakutanisha wadau kutoka Serikalini, Makampuni ya simu, Taasisi zinazotoa Misaada ya kibinadamu kwa lengo la kujadili fursa na kutoa maoni kuhusu njia sahihi ya ujumuishaji wa teknolojia ya simu katika mifumo ya kutoa tahadhari ya Awali (Early Warning System – EWS) iliyofanyika tarehe 14 Machi, 2024 Jijini Dodoma.

Warsha hiyo ilihudhuriwa na wataalam kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Mifugo, Wizara ya Maji, Wizara ya Afya, Wizara ya Kilimo pamoja na Taasisi ikiwemo TCRA, TMA, REDCROSS, makampuni ya simu pamoja na Airtel, Vodacom, Tigo/Zanztel.

Aidha alitumia fursa hiyo kueleza majukumu ya msingi ya Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo ni kuratibu masuala ya menejimenti ya maafa nchini huku akiwaasa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali katika mzingo wa menejimenti ya maafa ikiwemo wa kuzuia, kujiandaa, kukabili pamoja kurejesha hali pindi maafa yanatokea.

“Tumienie warsha hii kwa matokeo chanya yaliyokusudiwa kwa kuongeza ujuzi na kushirikishana uzoefu katika masuala yanayohusu fursa mbalimbali kuhusu njia sahihi za kutumia teknolojia ya simu katika mifumo na kutoa taarifa za tahadhari za awali ili kuendelea kuwa na utayari katika kukabili maafa,” alieleza Bi. Jane

Aliongezea kuwa nchi ya Tanzania imekuwa ikikumbwa na maafa ya asili na yale yasiyo ya asili ikiwemo ya mafuriko, matetemeko ya ardhi, moto, maporomoko ya tope na mawe, ukame, upepo mkali, magonjwa ya milipuko kwa binadamu na wanyama hivyo warsha hiyo ni muhimu kwa kuzingatia umuhimu wa taarifa za tahadhari za awali ili kuendelea kujiandaa kisha kukabili kwa wakati na kupunguza madhara yanayoweza kutokea wakati wa maafa hayo.

Alifafanua kuwa, taarifa za awali zinaipa jamii uelewa wa hatua za awali za kuchukua kabla ya madhara ya maafa kuwa makubwa hivyo upo umuhimu wa kuendelea kuzijengea uwezo jamii juu ya matumizi sahihi ya taarifa hizo.

Awali aliwakumbusha kuendelea kupiga namba 190 endapo kunatokea majanga, maafa au dharura ili kupata msaada zaidi kupitia Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu.

WATAKIWA KUONDOKA KUEPUKA MAFURIKO MTO RUFIJI

SERIKALI imetoa taadhari kwa wananchi waliopo katika wilaya za Rufiji na Kibiti unakopita Mto Rufiji kuondoka ili kuepuka athari za mafuriko  baada ya milango ya mradi wa uzalishaji wa umeme wa bwana la Mwalimu Nyerere kufunguliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge baadhi ya mashamba ya wananchi yameathirika kwa kuzingirwa na maji.

Kunenge amesema, baada ya maji hayo kufunguliwa, maji hayo yalizingira mashamba na kuharibu baadhi ya mazao ya wananchi na kwamba kwa sasa bado wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari kubwa Iki kuthibiti maafa ikiwemo vifo visivyo vya lazima

"Bwawa Mwalimu Nyerere, limefurika kuliko matarajiyo yaliyo kuwepo,ambapo tulipokea taarifa kutoka wizarani na Shirika la umeme Tanzania Tanesco kwamba wanataka kufungua milango ya Bwawa ambapo tulitoa taarifa za tahadhari Kwa wananchi kuondoka maeneo hayo lakin baadhi hawakufanya hivyo hivyo nasisitiza waondoke katika maeneo hayo"amesema

Aidha amesema taarifa za kufunguliwa Kwa Bwawa hilo zitoleea kuanzia Machi Mosi mwaka hadi zoezi Hilo lilipofanyika  Machi 05, majira ya saa 9:00 alasiri ambapo kina cha maji kilichokuwepo ni mita za ujazo 
188.85 na kwamba mpaka sasa kimepungua na kifikia 183.45 baada ya kufunguliwa

Thursday, March 14, 2024

KATA YA TANGINI YAPATA MILIONI 120 KWA AJILI YA ZAHANATI

KATA ya Tangini Wilayani Kibaha imepata kiasi cha shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ambapo itakapokamilika itahudumia watu 20,146.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Diwani wa Kata ya Tangini Mfalme Kabuga amesema kuwa tayari fedha hizo zimetokana na mapato ya ndani.

Kabuga amesema kuwa ujenzi wa zahanati hiyo unatarajia kuanza wakati wowote kuanzia sasa na tayari eneo limepatikana eneo la mtaa wa Kilimahewa.

"Wananchi wa Kata hiyo wanapata huduma za kiafya kwenye Hospitali za Tumbi, Mkoani na Pangani ambapo hutumia gharama kubwa zinazofikia kiasi cha shilingi 4,000 hadi 6,000 za pikipiki kufika kwenye huduma za afya,"amesema Kabuga.

Amesema kuwa Zahanati hiyo itajengwa na serikali hadi kukamilika na itakapokamilika itawapunguzia gharama za usafiri na pia kuepuka kwenda moja kwa moja kwenye Hospitali kubwa ambapo gharama zinakuwa ni kubwa endapo hawajaanzia ngazi ya chini.

"Tunaishukuru serikali ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan na Mbunge wetu Silvestry Koka na Madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha ambao wametufanyia mambo makubwa katika kukabili changamoto za wananchi,"amesema Kabuga.

Ametaja mitaa itakayonufaika na zahanati hiyo kuwa ni Maili Moja B, Tangini, Kilimahewa, Machinjioni na Mtakuja na mtaa jirani wa Muheza toka Kata ya Maiili Moja.

ZINGATIENI MTINDO BORA WA MAISHA ILI KULINDA FIGO ZENU


Wakati Tanzania inaungana na mataifa mengine ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Figo Duniani leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH), Dkt. Alphonce Chandika, amewashauri wananchi kuzingatia mtindo bora wa maisha ili kulinda figo zao.

Dkt. Chandika, ametoa wito huo jijini Dodoma, akisema wananchi wanapaswa wafanye mazoezi kuzingatia mlo usioathiri moyo ili kuzilinda figo.

"Mtindo bora wa maisha unaozingatia milo isiyoathiri moyo utaisaidia kuzilinda figo," amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali.

Siku ya Figo Duniani mwaka huu inaadhimishwa ikiwa na kauli mbiu, 'Afya ya Figo kwa Wote pamoja na Upatikanaji Bora wa Matibabu.'

Dkt Chandika amesema wagonjwa 50 wenye tatizo la figo husafisha damu kwa siku katika Kitengo cha Kusafisha Damu katika Idara ya Magonjwa ya Figo katika BMH.

"Watu wenye tatizo la figo wanasafisha damu mara tatu (3) kwa wiki," ameongeza.

Dkt Chandika amesema mpaka sasa, BMH imeishafanya oparesheni za upandikizaji figo kwa watu 36 toka huduma hii ianze miaka sita (6) iliyopita.

Mwaka 2019, BMH ilikuwa Hospitali ya pili nchini kuanzisha huduma ya upandikizaji figo, lakini ndiyo Hospitali pekee kutoa huduma hiyo bila usaidizi wa Hospitali za nje.

CCWT YATANGAZA MUDA WA KUCHUKUA FOMU ZA UCHAGUZI


Na Wellu Mtaki, Dodoma.

Chama Cha Wafugaji Tanzania (CCWT) kimetangaza muda wa kuchukua fomu za kugombea nafasi za uongozi kwa wanachama wake wanaotaka kugombea huku wakibainisha kuwa malipo ya uchukuaji wa fomu hizo yanapaswa kufanyika kupitia akaunti ya tume ya uchaguzi na sio kwenye akaunti ya chama hicho.

Hayo yameelezwa leo Machi 12, 2024 Jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi ya CCWT Bw. Charles Lyuba alipokutana na waandishi wa habari katika ofisi ya chama hicho ambapo amesema kuwa lisiti za malipo zinapaswa kuambatanishwa katika fomu wakati wa kuzirejesha.

“Tangu mwaka jana tumeanza mchakato wa uchaguzi na hadi sasa tunaendelea na chaguzi za ngazi mbalimbali ikiwemo za wilaya, nawatangazia wafugaji na wanachama wote kuwa fomu za kugombea uongozi ndani ya chama chetu ngazi ya kanda na taifa zitaanza kutolewa Machi 13 - 25,2024 na mwanachama yeyote mwenye nia ya kugombea nafasi yeyote ya kanda anapaswa kuzingatia ratiba na kalenda nzima inayotolewa na tume,”amesema.

Amesema wanachama wao ni muhimu kuwa na taarifa sahihi zinazohusu uchaguzi ili kuepuka mikanganyiko na hasa wanapotoa ratiba isije kuonekana kuna watu wana ratiba zao binafsi.

“Hii ndio ratiba ya tume ya uchaguzi na sisi tunasema hiyo tarehe 13 kwa yaani kesho hadi tarehe hadi tarehe 25, Machi tunaanza kutoa hizo fomu za kanda sambamba na fomu za ngazi ya taifa,” amesema.

Aidha Bw. Lyuba amewasisitiza wagombea wote kufuata ratiba ya tume ipasavyo na kuchukua fomu kwa wakati kwa ngazi ya taifa uchaguzi utaanza Aprili 8,2024 utakao wahusisha viongozi wote wa wilaya na walaya ambayo haitakuwa imefanya uchaguzi wa ngazi haitaruhusiwa kufanya uchaguzi wa ngazi ya kanda pamoja na taifa kwasababu watakuwa hawajatimiza takwa la katiba ya wanachama hicho.

Kwa upande wake mjumbe wa tume ya uchaguzi George Kifuliko amewasisitiza wagombea na wanachama wote kuzingatia ratiba ili kuepusha vikwazo vitakavyojitokeza.

Wednesday, March 13, 2024

MADALALI WA KUPIGIA DEBE WAGOMBEA WATAKIWA KUACHA MARA MOJA



CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Kata ya Picha ya Ndege Wilayani Kibaha imewataka watu wanaojifanya madalali wa watu wanaotaka kugombea nafasi za uenyekiti wa serikali za mitaa waache kwani muda wa viongozi walio madarakani haujaisha.

Aidha kimewataka watu kuacha kuwasemea vibaya viongozi walioko madarakani kwani nikukiharibia chama kwani wanatokana na chama hicho.

Hayo yamesemwa na Katibu Mwenezi wa Kata ya Picha ya Ndege Said Namamba wakati wa ziara kwa mabalozi wa Kata hiyo.

Namamba amesema kuwa kuna baadhi ya watu wanajifanya wanawapigia debe baadhi ya watu wanaotaka kuwania nafasi za uongozi huku muda wa kuwania nafasi hizo ukiwa bado.

Naye Mjumbe Mkutano Mkuu kutoka Kata  Subira Said amesema kuwa wametumia fursa hiyo kuwafundisha mabalozi hao kujua wajibu na majukumu yao.

Said amesema kuwa pia wamewaelekeza namna ya kutunza kumbukumbu za wanachama na kuhifadhi taarifa mbalimbali za mashina yao na kutoa taarifa juu ya changamoto kwa balozi wanazoziongoza.

Kwa upande wake Katibu wa Hamasa wa Vijana wa Kata Lenatus Mkude amesema kuwa wao wanataka mabalozi wasikubali kupotoshwa na watu wanaotaka kuwatumia kuwapigia debe wakati muda haujafika.

Mkude amesema wao wanataka utaratibu wa chama ufuatwe ili mgombea atakayechaguliwa kupitia kura za maoni apeperushe bendera ya chama na siyo vinginevyo.


Tuesday, March 12, 2024

WAFANYABIASHARA WA DODOMA WAIOMBA SERIKALI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA BIASHARA





Na Anna Misungwi, Dodoma 

WAFANYABIASHARA wa Mkoa wa Dodoma waiomba serikali kurekebisha miundombinu ya soko la Machinga Complex pamoja  soko la Mavunde  lililopo Kata ya Chang'ombe ambapo kipindi cha mvua maji huingia na biashara kuharibika.

Hayo yamesemwa na wafanyabiashara wa masoko hayo Tarehe 11 Machi 2024 wakati wa ziara ya mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Hamis Livembe, kwenye ziara iliyolenga kupokea changamoto, kero na maoni ya wafanyabiashara.

Mmoja wa wafanyabiashara Abdalla Ramadhan amesema kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na miundombinu ya soko kwani maji yanaingia na hivyo kusababisha bidhaa kuharibika.

Ramadhan amesema kuwa pia wanaomba kushushwa kwa ushuru kutoka 1,000 na kuwa 500 kwenye kizimba kwenye soko la Machinga Complex ambapo kizimba kimoja kinaweka wafanyabiashara wawili kwani ushuru wanaolipa unasababisha kushuka kwa biashara zao.

"Wafanyabiashara kipato chetu kinashuka tunaimomba serikali itusaidie kwani kizimba kimoja tunakaa watu wawili na kila mtu kwenye kizimba analipa shilling 1,000 ambapo watu wawili ni shilling 2,000 tunaomba tupunguziwe tulipe shilling 500 kwa kila mtu,"amesema Ramadhan.

Amesema wanaiomba serikali kuacha kuwafungia vizimba kutokana na hali ya wafanyabiashara kudaiwa kulipia ushuru kwani kizimba kikifungwa husababisha kukosa mapato kwa wafanyabiashara na serikali kwa ujumla.

"Tunafungiwa vizimba sababu ya mtu kama hajalipa ushuru siku moja au mbili kitendo ambacho wengi wanashidwa kuja kugomboa maana unapofungiwa lazima uje utoe fedha ndo ufunguliwe tunaomba serikali itusaidie,"wamesema wafanyabiashara hao.

Kwa upande wake mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe amesema kuwa lengo la kuja ni kupokea changamoto, kero na maoni na changamoto ambazo zinaweza kutolewa majibu zinatolewa ufafanuzi na ambazo majibu hawana watazipeleka sehemu husika ili kuzitafutia ufumbuzi.

Livembe ametoa wito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wanakuwa wamoja katika kushughulikia matatizo kwa umoja.