ReplyReply allForward |
Thursday, December 28, 2023
WATU WATATU WAMEFARIKI DUNIA BAADA YA GARI WALILOKUWA WAKISAFIRIA KULIGONGA GARI LINGINE KWA NYUMA
Saturday, December 16, 2023
ATFT KUENDELEZA VIPAJI KUPITIA KIPAJI BILA MIPAKA
KITUO cha kuendeleza vipaji Africa Talent Forum-TZ (ATFT) cha Mkoani Pwani imewakutanisha wasanii wa fani mbalimbali ili kujadili namna ya kuendeleza vipaji vya wasanii ili viweze kutoa ajira.
Wednesday, December 6, 2023
TPFNET CHALINZE WATOA MSAADA KITUO CHA WATOTO DOLPHINE.
Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mkoa wa Pwani, Disemba 05, 2023 wametoa msaada kwa watoto wenye uhitaji katika kituo cha Dolphine kilichopo Kijiji cha Kipera, Kitongoji cha Mwanabele Wilayani humo.
Akizungumza akiwa kituoni hapo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Sophia Lyidenge alisema jukumu la ulezi wa watoto wenye uhitaji na kuwatunza ni la jamii nzima hivyo wao wakiwa ni sehemu ya wazazi wameguswa katika siku 16 za maadhimisho ya kupinga ukatili wa Kijinsia kufikia kwa watoto hao wenye uhitaji na kuweza kutoa msaada wa vitu mbalimbali.
"Jamii inapaswa kutambua malezi ya watoto na kuwatunza na kuwatembelea mara kwa mara kujua changamoto walizonazo na kuzitafutia ufumbuzi watoto wenye uhitaji kwenye vituo vya malezi ni la watu wote na kufanya hivyo ni kuwapa faraja watoto walio kwenye vituo hivyo kuona jamii ina wajali na kuwathamini".Alisema Lyidenge.
Lyidenge amewapongeza wasimamizi wa kituo hicho kwa malezi ya watoto hao akiweka wazi kuwa jambo wanalolifanya la kuwalea watoto kwenye maadili mema ni kubwa sana mbele ya Mungu na la kupongezwa.
Amesema kuwa watoto hao endapo wangeachwa bila ulezi kwenye kituo hiki wangeweza kuwa katika makuzi mabaya hivyo kutumbukia kwenye makundi ya kihalifu na hivyo kupeleka Jamii kuwa na kizazi kisichokuwa na maadili.
Aidha, Lyidenge amewaasa watoto hao kuwa wasikivu kwa walezi wao na kutambua kuwa wao ni taifa la kesho akiwasisitiza kusoma kwa bidii ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za changamoto walizonazo kwa walezi wao bila woga ili ziweze kupatiwa ufumbuzi kwa wakati.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa jamii Bi. Linna Jackson Mlay ameahidi kuendeleza ushirikiano na walezi wa kituo hicho katika kutatua changamoto mbalimbali walizonazo.
Nae msimamizi wa kituo hicho Anna Munisi amelishukuru Jeshi la Polisi Wilaya ya Kipolisi Chalinze kwa msaada waliowapatia na kuomba wananchi wengine kuendelea kusaidia kituo hiko kwani uhitaji ni mkubwa katika maelezi ya watoto waliopo kituoni hapo.
Msaada uliotolewa na Jeshi la Polisi kituoni hapo ni unga wa sembe, mchele, sabuni, madaftari, kalamu na taulo za watoto.
Monday, December 4, 2023
TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE MKOA WA PWANI YAWATAKA WANAWAKE KUMUENZI BIBI TITI MOHAMED KWA KULETA MAENDELEO
Aidha amewataka kuunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwaletea maendeleo wananchi kwa kuwapatia fursa mbalimbali za kujiletea maendeleo.
TASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE MKOA WA PWANI YAWAPONGEZA WAANDAJI WA MAFUNZO YA IJUE KESHO YAKO KWA WANAWAKE MLANDIZI KIBAHA
Sunday, November 26, 2023
*KATENI UMEME KWA WADAIWA - DKT. BITEKO AIAGIZA TANESCO*
*📌Akemea vikali wahujumu wa miundombinu ya umeme, Asema Serikali iko kazini, Itawashughulikia*
*📌Ataka TANESCO kusikiliza na kujibu Wateja kwa haraka*
*📌Asisitiza utunzaji wa Mazingira*
Arusha
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukata umeme kwa wadaiwa wote wasiolipa gharama za kutumia umeme ambapo Shirika hilo linadai jumla ya Shilingi Bilioni 224 kutoka Taasisi mbalimbali za Serikali, Binafsi na waliohama na madeni kutoka mita za zamani za umeme kwenda za kisasa hali inayopelekea changamoto katika utekelezaji wa majukumu ya TANESCO.
Amesema hayo tarehe 26 Novemba 2023, wilayani Arumeru mkoani Arusha, wakati alipokagua kituo cha umeme cha Lemuguru mkoani Arusha ambacho ujenzi wake ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa njia kuu ya umeme ya msongo wa kV 400 kutoka Singida mpaka Namanga kuelekea Kenya ( Kenya- Tanzania Power Interconnection Project (KTPIP).
“Hapa Arusha tu, TANESCO anadai wateja wake shilingi bilioni 7.7, na mara nyingi wanaodaiwa si wanachi wadogowadogo bali Taasisi za Serikali na Wawekezaji wanaojiita wawekezaji wakubwa ambao ukiwakatia umeme wanakwambia unaua ajira, wepesi wa kujificha kwenye kisingizio cha kulipa kodi na ajira; TANESCO anahitahi fedha ili awekeze na kisha awapelekee umeme wananchi, TANESCO nawaambia kateni umeme kwa mtu yeyote mnayemdai ili mradi unamdai kwa haki.” Amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko pia ameagiza wadaiwa wote wa madeni ya bili za umeme wakalipe madeni hayo ili zipatikane fedha za kuwahudumia wananchi na ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushughulikia changamoto za umeme nchini kwa aina mbalimbali ikiwemo kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji umeme ukiwepo wa Julius Nyerere (MW 2115), ambao umefikia asilimia 94 ambapo amesema kuwa, Mkandarasi ameshafunga mashine mbili tayari kwa kuanza majaribio ya kuzalisha umeme.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amekemea vikali watu wote wanaohujumu miundombinu ya umeme akitolea mfano wizi wa shaba na mafuta ambapo kati ya tarehe 25 Novemba, 2023 na 26 Novemba, 2024 kuna matukio 14 katika Ukanda wa Pwani ya kuharibu au kuhujumu miundombinu ya umeme, ambapo ameeleza kuwa, Serikali itawashughulikia kwa kuendesha msako na watakapopatikana sheria itachukua mkondo wake.
Aidha, Dkt. Biteko ameitaka TANESCO kuwasikiliza na kuwapatia majibu kwa haraka wananchi wanaopiga simu kwenye Shirika hilo ili kupata huduma za umeme na mahali penye matatizo waambiwe, “huu utaratibu wa watu kupiga simu anaambiwa subiri, hii tumekubaliana kuwa haiwezekani ikaendelea na ndio maana nimewaambia kituo cha Huduma kwa Mteja tukiimarishe kutoka miito 65 na ziongezwe kufika 100 na zaidi.”
Dkt. Biteko ametaka Watanzania kulinda vyanzo vya maji ambavyo vinazalisha umeme, amesema vyanzo hivyo visipolindwa vitapelekea athari mbalimbali zikiwemo kwenye uzalishaji umeme, na pia ameitaka TANESCO kutokukaa nyuma katika masuala ya utunzaji wa mazingira bali washirikiane na Wizara inayoshughulika na suala la mazingira na NEMC ili wote kwa pamoja washirikiane kusimamia mazingira.
Kuhusu utekelezaji wa kituo hicho cha umeme cha Lemuguru kilichopo wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha, Dkt. Biteko amesema kuwa mradi huo ni mkubwa na unagharimu Dola za Marekani milioni 258.8 na kina faida mbalimbali ikiwemo kupelekea wananchi umeme usiokatika mara kwa mara na kituo kitaimarisha hali ya umeme mkoani Kilimanjaro na Arusha.
Dkt. Biteko vilevile ameipongeza TANESCO kwa hatua mbalimbali inazochukua ili kupunguza makali ya mgawo wa umeme pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuongeza kiwango cha Gesi Asilia kinachozalisha umeme.
Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa njia Kuu ya kusafirisha umeme wenye msongo wa Kilovoti 400 kutoka Singida hadi Namanga kuelekea Kenya, Msimamizi wa Mradi huo Mhandisi Peter Kigadye, amesema kukamilika kwa mradi huo kutasaidia kuongeza uwezo wa kusafirisha umeme kwenda mikoani na migodi ya uchimbaji madini na hivyo kuwezesha kufikia uwezo wa juu wa megawati 2000 katika kusafirisha umeme.
Amesema, utekelezaji wa mradi unahusisha vipengele Sita ikiwemo ujenzi wa njia 8 za laini ya kV 400/33 kutoka Kituo kipya cha kupoza umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kV 400 kutoka Singida hadi Namanga kupitia Arusha yenye urefu wa kilomita 414.3, Babati -Arusha kilomita 150, Arusha –Namanga, Kilomita 114.3 ambao umefikia asilimia 96.
Ameeleza mradi huo pia unahusisha, upanuzi wa vituo vya kupoza umeme ambao umefikia asilimia 98.72, mradi wa usambazaji umeme kwa vijiji vilivyopitiwa na mradi vijiji na ujenzi wa vituo vyq kupoza umeme vya Dodoma, Singida, ambavyo vimekamilika.
*DKT. BITEKO ATUNUKU VYETI KWA WAHITIMU 439 CHUO CHA MWEKA*
*📌Awataka kuchukia rushwa na kulinda Maliasili kwa Wivu Mkubwa*
*📌Apongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa usimamizi wa Sekta*
*Kilimanjaro*
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametunuku vyeti vya ngazi mbalimbali kwa wahitimu 439 wa Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori cha Mweka, mkoani Kilimanjaro ambapo amewaasa kuwa chochote watakachofanya kuchukia rushwa, kutojitajirisha katikati ya hali ngumu za wananchi na walinde maliasili za nchi kwa wivu mkubwa na kuwa walinzi wa wenzao.
Amesema hayo tarehe 25 Novemba, 2023 wakati alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Mahafali ya 59 ya Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Mweka, mkoani Kilimanjaro ambapo Mahafali hayo yameenda sambamba na Kilele cha Maadhimisho ya Miaka 60 ya Chuo hicho.
“Chuo hiki ni kiungo muhimu katika Sekta ya Maliasili na Utalii, kuanzishwa kwake kulitokana na tamko la Baba wa Taifa, Hayati, Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika Kongamano la Uhifadhi wam Wanyama Pori mwaka 1961, na kupitia tamko hilo alionesha dhamira na utayari wake wa kuifanya Afrika kuwalinda wanyama na mazingira yao kwa kizazi kilichopo na vizazi vijavyo, hivyo nyinyi ndio mnaoendeleza kazi lengo hilo la Baba wa Taifa.” Amesema Dkt. Biteko
Amesema kuwa, Chuo hicho pia ni kielelezo cha ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi nyingine duniani kwani Chuo hicho kinapata wanafunzi kutoka nchi mbalimbali duniani.
Amesema kuwa, Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua mchango wa Chuo hicho katika ukuaji wa Sekta ya Maliasili na Utalii nchini na hivyo ameahidi kuwa kama kuna changamoto zozote Serikali itazichukua na kuzifanyia kazi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kusimamia vyema sekta ya Maliasili na Utalii ambayo amesema kuwa ni kiungo kikubwa kwenye uchumi wa nchi kwani bila Sekta hiyo mapato na fedha zinazohitajika kuendeleza miradi mbalimbali zinaweza kuwa na changamoto ya upatikanaji.
Amesema, Utalii unachangia takribani asilimia 21 ya Pato la Taifa, na asilimia 25 ya fedha za kigeni, pia ni chanzo kikubwa cha ajira nchini kwani unachangia ajira milioni 1.5 na zaidi ya asilimia 11 ya ajira zote hapa nchini.
Dkt. Biteko aliongeza kuwa, asilimia 80 ya Utalii nchini unatokana na Wanyama pori, ambao wametokana na mazingira yetu tuliyoyahifadhi, mapori ya akiba, mapori tengefu, misitu pamoja na hifadhi za wanyama.
Katika Mahafali hayo wahitimu 439 walitunukiwa vyeti katika ngazi mbalimbali za masomo ikiwemo Shahada ya Uzamili ya Mipango na Usimamizi wa Utalii, Shahada ya Usimamizi wa Wanyamapori, Stashahada ya Juu ya Utalii wa Wanyamapori, Astashahada ya Usimamizi wa Wanyamapori na Cheti cha Msingi cha Usimamizi wa Wanyamapori.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na Viongozi mbalimbali akiwemo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu na Balozi wa Msumbiji nchini Tanzania, Ricardo Mtumbuida.