Thursday, August 3, 2023

WANNE WAFA AJALINI PWANI

MKURUGENZI wa benki ya APSA Nechi Msuya (45- 50) mkazi wa Dar es Salaam na watu wengine watatu wamefariki dunia baada ya gari walilokuwa wakisafiria kuligonga gari lingine uso kwa uso.

Akizungumza na waandishi wa habari wa ofisini kwake Kamanda wa polisi mkoani Pwani ACP Pius Lutumo alisema watu hao walifariki papo hapo.

Lutumo alisema kuwa ajali hiyo ilitokea Agosti 3 mwaka huu majira ya saa 2.30 kijiji cha Mapatano Kata ya Mbwewe wilaya ya kipolisi chalinze.

Alisema kuwa marehemu alikuwa akiendesha gari aina ya Toyota Prado lenye namba za usajili T 104 CBU likitoka Dar es Salaam kwenda Same mkoani Kilimanjaro.

"Gari lake liligongana na lori lenye namba T 881 DWU na tela namba T 888 DWU aina ya Scania likitoka Arusha kwenda Dar es Salaam likiendeshwa na Philipo Mtisi (43) mkazi wa Mafinga,"alisema Lutumo.

Aliwataja watu wengine waliokufa kuwa ni Dayana Mgeta (40-45) mfanyabiashara, Nora Msuya (40-45) mwalimu wa chuo kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam na abiria wa kike ambaye jina lake bado halijafahamika (30-35).

Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa Prado kuhama upande wake wa kushoto wa barabara kwenda upande wa kulia kisha kugongana uso kwa uso na lori hilo.

Aidha alisema kuwa miili ya marehemu imehifadhiwa kwenye zahanati ya Lugoba kwa uchunguzi na kusubiri ndugu kwa ajili ya mazishi baada ya uchunguzi.

"Tunawashauri watumiaji wa barabara wakiwemo wale wanaotumia vyombo vya moto kuwa makini ili kupunguza ajali ambazo zinazuilika,"alisema Lutumo.

Monday, July 31, 2023

MAKONGAMANO YA NANE NANE KUWA NA TIJA


Na Manase Madelemu, Dodoma 

MKUU wa mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamle amesema kuwa tofauti na maonesha ya miaka iliyopita ya nane nane mwaka huu 2023 yatahusisha matukio muhimu na makongamano yanayoongeza wigo wa uzalishaji bora.

Senyamule amesema hayo leo julai 31,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Maadhimisho ya nane nane mwaka kikanda.

Amesema kutakuwa na makongamano ya tasnia ya alizeti,kongamano la zao la mtama ambapo mikoa ya Dodoma na singida ilikabidhiwa jukumu la kuzalisha alizeti Kwa wingi ili kupunguza nakisi ya mafuta ya kula nchini na hivyo kuokoa fedha za kigeni.

Aidha ameongeza kuwa kutakuwepo na siku maalumu ya uhamasishaji uzalishaji kuku wa kienyeji hasa katika mkoa wa Singida unafahamika katika mikoa mbalimbali hapa nchini hadi kufikia watu kuwaita kuku wa Singida 

Pia Senyamule amesema kuwa Katika maonesho ya mwaka huu kutakuwa na huduma za Afya na matibabu ya kibingwa zitakazotolewa na madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa na huduma hizi zitatolewa bure.

Kauli mbiu ya maonesha na sherehe za nane nane kitaifa Kwa mwaka 2023 ni Vijana na wanawake ni Msingi Imara wa Mifumo Endelevu ya Chakula"na kauli mbiu kikanda Kilimo ni Biashara, Biashara ni Uwekezaji.

Saturday, July 29, 2023

PINDA KUZINDUA MAONYESHO NANE NANE KANDA YA MASHARIKI

 

WAZIRI Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maonyesho ya wakulima nane nane Kanda ya Mashariki Mkoani Morogoro Agosti Mosi mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa maonyesho hayo yanashirikisha mikoa minne ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro.

Kunenge amesema kuwa hadi sasa tayari washiriki 589 wamejiandikisha kushiriki maonyesho hayo ambapo ni ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo washiriki walikuwa 476.

Amesema kuwa maonyesho hayo ni ya 30 tangu kufanyika kwa kanda hiyo ya Mashariki ambapo kauli mbiu inasema Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula.

Aidha amesema kuwa wakulima na wananchi wanakaribishwa kujitokeza kwa wingi ili kujifunza teknolojia za kisasa kwenye sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi.

Friday, July 28, 2023

WAZIRI MKUU MSTAAFU PINDA MGENI RASMI NANE NANE KANDA YA MASHARIKI

WAZIRI Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maonyesho ya wakulima nane nane Kanda ya Mashariki Mkoani Morogoro Agosti Mosi mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Kibaha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa maonyesho hayo yanashirikisha mikoa minne ya Pwani, Dar es Salaam, Tanga na Morogoro.

Kunenge amesema kuwa hadi sasa tayari washiriki 589 wamejiandikisha kushiriki maonyesho hayo ambapo ni ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na mwaka jana ambapo washiriki walikuwa 476.

Amesema kuwa maonyesho hayo ni ya 30 tangu kufanyika kwa kanda hiyo ya Mashariki ambapo kauli mbiu inasema Vijana na Wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula.

Aidha amesema kuwa wakulima na wananchi wanakaribishwa kujitokeza kwa wingi ili kujifunza teknolojia za kisasa kwenye sekta za kilimo, ufugaji na uvuvi.

TASAC KUNUNUA BOTI ZA UOKOZI ZIWA VICTORIA

SHIRIKA la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) limesema limejipanga kununua boti tatu za uokozi katika Ziwa Victoria ambazo zitakwenda kusaidia kutatua changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza pindi ajali zinapotokea

Hayo yamesemwa jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw.Kaimu Abdi Mkenyenge wakati  akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2023/2024 .

Amesema  katika boti hizo tatu zitakazonunuliwa mbili zitakuwa ni za mwendonkasi kwaajili ya ukokozi na Moja itakuwa kwaajili ya kubebea majeruhi na wagonjwa (Ambulance) .

“Boti hizi tatu zitatumika kufanya uokozi katika ajali ambazo zimekuwa zikitokea katika Ziwa Victoria ambapo mbili zitakuwa ni za meendo kasi na Moja itatumika kama ambulance kwa ajili ya majeruhi”amesema

Aidha amesema TASAC  imeendelea kuimarisha udhibiti huduma za usafiri majini, na kuhakikisha kuna ushindani sawia miongoni mwa watoa huduma.

Amesema kuwa linafanya ufuatiliaji, tathmini na kutoa maelekezo kuhusu utekelezaji wa vigezo na viwango vya ubora wa huduma (performance standards and Benchmarks) kwa watoa huduma za bandari na usafiri majini.

“Tunaendelea kuratibu maombi ya tozo za usafiri wa meli katika Maziwa (Victoria na Nyasa) na kuhakikisha viwango vya tozo vinavyotumika haviathiri ushindani wa kibiashara;

“Lakini pia zoezi la urasimishaji wa bandari bubu Tanzania bara ambapo bandari bubu kumi na tatu (13) zilizowasilishwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kwa ajili ya urasimishaji zilikaguliwa na kufanyiwa tathmini ya kina kwa kushirikiana na TPA, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Baraza la Usimamizi wa Mazingira (NEMC)”amesema Mkeyenge

Kadhalika amesema  bandari bubu kumi zilionekana kukidhi vigezo hivyo na kupendekezwa kwa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi) (WUU-U) kwa ajili ya kurasimishwa kwa mujibu wa sheria

“waendeshaji wa zilizokuwa bandari bubu binafsi tano (05) za Mwanza ambazo ni miongoni mwa zilizokuwa bandari bubu ishirini (20) zilizorasimishwa kupitia Tangazo la Serikali (GN) namba 293/2022 wamepewa leseni za uendeshaji huku TPA wakielekezwa kusimamia kwa karibu bandari kumi na tano (15) zilizobakia.

Akizungumzia kuhusu Kuboresha usalama, ulinzi kwa usafiri majini na kudhibiti uchafuzi wa mazingira baharini utokanao na meli amesema Shirika limetimiza lengo hilo la kimkakati kwa  kuendelea kusimamia usalama wa vyombo vya usafiri majini kwa kufanya ukaguzi wa meli kubwa na vyombo vidogo vya majini.

“Shirika lilifanya kaguzi za usalama kwa meli kubwa zibebazo tani 50 au zaidi ili kuhakikisha kuwa ni salama na zinaendeshwa na mabaharia wenye sifa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Mwanza, Kagera, Kigoma na Mbeya ambapo katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Juni, 2023, Shirika lilifanya jumla ya kaguzi za meli kubwa 288 ambapo kaguzi 165 zilikuwa za meli za kigeni na kaguzi 123 zilikuwa meli za ndani.”amesema

Kuhusu uratibu Shughuli za Utafutaji na Uokoaji Majini amesema Kituo cha Utafutaji na Uokoaji Majini kilichopo Dar es Salaam kinachoratibiwa na TASAC kiliendelea kufanya shughuli zake  katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Juni, 2023 ambapo kituo kilipokea taarifa 4 za ajali zilizohusisha vyombo vya majini ambazo zilitokea katika eneo la maji ya Tanzania.

Katika ajali hizo  jumla ya watu 61 walihusika ambapo watu 58 sawa na 95% waliokolewa na watu 3 sawa na 5% walipoteza maisha.

Naye  Mkurugenzi wa Idara ya Habari -Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa amesema Serikali inataka kushirikiana na sekta binafsi kuendesha Bandari, mikataba nwatakaoendesha bado haijasainiwa.

“Sasa hivi ndio wataalamu wako mezani kuzungumza kuhusu mikataba, muda na gharama lakini hakuna bandari iliyouzwa, wataalamu watakapokamilisha majadiliano tutaangalia maslahi yetu yako wapi na maoni yanayotolewa na Watanzania yatazingatia Serikali iko macho wakati wote kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa”amesema Msigwa.

Thursday, July 27, 2023

MRADI MKUBWA WA KILIMO CHA VANNILA WAZINDULIWA DODOMA UNAKWENDA KUGHARIMU ZAIDI YA BIL 30 ZA KITANZANIA.

 


KAMPUNI ya Vanilla international Limited imezindua Mradi wa kilimo cha Vanilla Mkoani Dodoma Vanilla village Dodoma katika Kitongoji cha Zamahero Kata ya Mayamaya Wilaya ya Bahi.

Uzinduzi huo umeambatana na utoaji Elimu kwa wananchi wa eneo hilo kuhusu kilimo cha Vanilla ambao umefanyika Julai 22 2023 katika shamba la kitalu (green House)kubwa ya kilimo hicho inayotumia njia za kisasa.

Mkurugenzi Mtendaji na muasisi wa makampuni ya Vanilla international Limited ,Simon Mkondya amesema shamba kitalu lipo kilomita 40 kutoka katikati  ya JIJI la Dodoma barabara kuu ya kwenda Arusha lenye ukubwa wa hekta 125.

Mkondya amesema uwekezaji huo unakuja baada ya mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia kilimo hicho katika kisiwa cha Zanzibar.

JWT YAVUTIWA UTALII UWEKEZAJI YAWATAKA WAFANYABIASHARA WAKAWEKEZE

 

KATIKA kuunga mkono jitihihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kutangaza utalii Jumuiya ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) Mkoa wa Pwani imetembelea vivutio vya utalii na kutambua fursa za uwekezaji zilizopo Wilayani Bagamoyo.

Akizungumza mara baada ya kutembelea vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji mwenyekiti wa Jwt Abdala Ndauka alisema kuwa baada ya ziara hiyo wameweza kutambua fursa mbalimbali kupitia utalii.

Ndauka alisema kuwa fursa kwa wafanyabiashara ni nyingi sana kwenye utalii pamoja na fursa nyingine kwenye sekta mbalimbali zikiwemo za utoaji huduma.

Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Majid Mhina alisema kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni maeneo mengi yanamilikiwa na watu binafsi.

Naye ofisa biashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo Magdalena Kitilla alisema kuwa kuhusu uwekezaji wametenga eneo lenye ukubwa wa hekta 9,800 ambalo linahitaji wawekezaji.

Kitilla alisema kuwa sekta ya utalii ina fursa nyingi ambapo kwenye sekta ya uvuvi kupitia uchumi wa buluu bado haujatumika ipasavyo ambapo kuna ufugaji wa vizimba baharini kunakofanyika ufugaji wa majongoo bahari ambapo ni mwekezaji ni mmoja tu.

Moja ya wafanyabiashara Fihiri Msangi alisema kuwa ziara hiyo wamejifunza mambo mengi ambayo watayafanyia kazi ili waangalie namna ya kuweza kuwekeza.

Msangi alisema kuwa fursa hizo watazitumia vizuri ili kuinua uchumi wa Mkoa huo ambao unategemea uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali na pia unauwekezaji mkubwa wa viwanda.