Wednesday, July 26, 2023

WATAKIWA KUINGIA MIKATABA NA WAWEKEZAJI KWENYE ARDHI BADALA YA KUIUZA

NAIBU Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omar Kipanga amewataka wananchi wa Mafia wanaomiliki mashamba na viwanja vilivyopo karibu na ufukwe wa bahari kutokuyauza maeneo yao badala yake waingie ubia.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyopo kwenye Kata ya kirongwe Vijiji vya Banja na Jojo.

Kipanga alisema kuwa baadhi ya wananchi wa Mafia wamekuwa wakiuza maeneo yao kwa wanaowaita  wawekezaji ambao wanavutiwa na maeneo hayo.

"Wananchi wanapaswa kuyakodisha maeneo hayo au wangie mikataba kwa kugawana asilimia angalau nusu kwa nusu ili kupata faida zaidi kuliko kuyauza,"alisema Kipanga.

Alisema kuwa mashamba/viwanja ni vyao lakini kwa Sasa utaratibu mzuri wa kupata maendeleo ya ardhi yako sio kuuza bali ni kuingia ubia na wawekezaji.

"Acheni kabisa tabia hii siyo nzuri itafika hatua ardhi yote ya maeneo ya Pwani ya Mafia itakuwa inamilikiwa na wageni na wenyeji watakua hawana ardhi wakati ni sasa kila mmoja apate faida ya ardhi katika uwekezaji,"alisema Kipanga.

Aidha alisema kuwa Serikali ya Rais Samia na Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaboresha barabara za Mafia ni wazi maeneo hayo yanaenda kupanda thamani hivyo ni muhimu kuwawekea na kizazi cha baadae kupitia makubaliano kwenye ardhi.

JUMUIYA YA WAFANYABIASHARA TANZANIA (JWT) KUPAZA SAUTI

 

JUMUIYA ya Wafanyabiashara Tanzania (JWT) imejipanga kuhakikisha inakabili kero za wafanyabiashara na kupokea maoni na mapendekezo ya wafanyabiashara wote nchini na kuzifikisha sehemu husika.

Hayo yameyasema na Mwenyekiti wa wafanyabiashara Tanzania Hamis Livembe wakati wa mkutano wa wafanyabiashara mkoani Tanga.

Amewataka wafanyabiashara hao kuungana na kuwa na sauti ya pamoja katika kuhakikisha wanajenga jumuiya yao kwa kutetea masilahi ya biashara zao.

Livembe amesema kuwa umoja wa wafanyabiashara unasaidia katika kutatua kero na kuisaidia serikali katika kutatua changamoto za wafanyabiashara pamoja na kuundwa kwa sera bora ya biashara.

"Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ipo katika kusaidia na kutatua kero za wafanyabiashara kwa makundi siyo kwa mtu mmoja mmoja ndiyo maana waliunda kamati maalum ambayo lengo lake lilikuwa ni kukusanya na kuchakata na kuwasilisha kwa serikali," amesema Livembe.

Awali katibu wa JWT Mkoa wa Tanga Ismail Masod amesema kuwa hadi sasa bei ya vitenge imeshuka ambapo awali ilikuwa kati ya shilling milioni 200 na milioni 300 lakini kwa sasa ni shilingi milioni 60 kwa kontena ambayo hiyo ni kazi ya kamati iliyoundwa.

Masod amewataka wafanyabiashara wa Tanga watumie fursa ambazo serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imeziweka kwa kuagiza mizigo China kutokana na mfumo mzuri ambao serikali wameutengeneza.

Naye Mwenyekiti wa Kariakoo Martin Mbwana amesema kuwa serikali ipo pamoja na Jumuiya hiyo hivyo ametoa wito kwa wafanyabiashara watambue fursa na thamani ambayo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan ambayo ameitoa kwa wafanyabiashara hao.

Monday, July 24, 2023

URAIA WETU YAZINDULIWA

SHIRIKA la Maendeleo ya Vijana (YPC) la Kibaha Mkoani Pwani limeingia mkataba wa miaka mitatu na Shirika la The Civil Society (FCS) chini ya udhamini wa Jumuiya ya Ulaya (EU) wa kutoa elimu Utawala wa Kidemokrasia kupitia mradi wa Uraia Wetu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha Mkurugenzi wa YPC Israel Ilunde amesema kuwa mradi huo utatekelezwa kwenye mikoa minne ya Kanda ya Mashariki.

Ilunde amesema kuwa mradi huo una lengo la kuendeleza mazingira wezeshi kwa ajili ya utawala wa kidemokrasia nchini ambapo kwa kanda ya mashariki ni mikoa ya Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Morogoro.

Amesema kuwa mradi utawezesha majadiliano kati ya serikali na azaki kwa ajili ya uchechemuzi (ushawishi na utetezi) wa masuala wa kidemokrasia, maendeleo na kuboresha mahusiano na ushirikiano wa kikazi.

Aidha amesema kuwa mradi utatoa fursa wa azaki kujengewa uwezo kujiendesha kupitia shughuli zao ili kuwanufaisha wananchi wa kanda hiyo na Watanzania kwa ujumla.


Sunday, July 23, 2023

RC ATAKA WALIOCHOMA MOTO BONDE MZAKWE WASAKWE


MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama Mkoani Dodoma kuhakikisha vinawasaka na kuwabaini wote waliohusika na uchomaji moto katika Bonde la Mzakwe.

Senyamule ametoa agizo hilo leo Julai 21, 2023 mara baada ya kufika katika eneo hilo kujionea athari za uharibifu zilizosababishwa na moto ulioanza majira ya saa saba mchana.

Amesema asilimia 70 ya maji katika Jiji la Dodoma yanatoka katika bonde la Mzakwe na ni eneo la hifadhi hivyo ni muhumimu kukakikisha linalindwa na kuhifadhiwa kwa ustawi wa afya na mazingira ya watu wote.

Aidha, amewapongeza vijana wa JKT Makutupora walioshiriki katika zoezi la kuzima moto uliotokea hii leo tarehe katika Bonde la Mzakwe Jijini Dodoma. Senyamule amewapongeza kwa uzalendo walionyesha wa kudhibiti moto huo na kuzuia usilete madhara makubwa, amesema wameonyesha uzalendo mkubwa, uhodari na ushupavu.

 "Tumesikitishwa sana na moto huu kwa kuwa si kwamba umeathiri ikolojia ya eneo hili lakini pia umeharibu miundombinu ya Tanesco ikiwa ni pamoja na nguzo, hivyo kwanza nawapongeza vijana wetu kwa jitihada za kufanikisha kuzima moto huu na pili vyombo vyote vinavyohusika na uchunguzi vifanye kazi yake ili kubaini chanzo” Senyamule amesisitiza.

Amemuagiza Meneja wa Bonde la Wami Ruvu kuhakikisha kuwa wanachonga barabara maalum kwa lengo la kukinga moto katika bonde hilo ili athari za moto zisiwe kubwa pindi moto utokeapo.

Awali Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Dodoma Julishaeli Mfinanga amesema kuwa walipata taarifa kwa njia ya simu kupitia namba za dharura 114 na kuwahi eneo la tukio kwa haraka. Amesema moto umedhibitiwa na hakuna madhara makubwa na wanaendelea na doria kuhakikisha usalama katika eneo hilo.

Saturday, July 22, 2023

*UJUMBE KUTOKA KENYA WAJIFUNZA USIMAMIZI SEKTA YA MADINI*

Ujumbe kutoka Kenya ukiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Madini wa nchi hiyo Elijah Mwangi umefika nchini kujifunza kuhusu namna bora ya usimamizi wa Sekta ya Madini ambapo Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali ameupokea ujumbe huo.

Akizungumza katika kikao na ujumbe huo, Mahimbali amesema Tanzania ni sehemu salama ya uwekezaji kutokana na uongozi bora wa Serikali unaosimamiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo umepelekea kuifanya sekta hiyo kupata mafanikio makubwa.

Mahimbali amesema Wizara ya Madini ina Taasisi tano ambazo ni Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Taasisi ya Uwazi na Uwajibikaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) pamoja na Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) ambazo hutekeleza majukumu yake kwa ushirikiano.

Naye, Katibu Mkuu Wizara ya Madini kutoka Kenya Elijah Mwangi ameipongeza Wizara ya Madini kwa usimamizi bora wa sekta hiyo na kumuomba Mahimbali kuendelea kushirikiana katika nyanja mbalimbali ikiwemo tafiti na usimamizi wa biashara ya madini.

Katika kikao hicho mada mbalimbali zimewasilishwa ambapo Mtendaji Mkuu wa  GST Dkt. Mussa Budeba amewasilisha mada juu ya madini yapatikanayo Tanzania na aina za tafiti zilizokwisha fanyika. 

Dkt. Budeba amesema kwa sasa GST imejikita zaidi kwenye tafiti za madini ya kimkakati ambapo mpaka sasa Tanzania imefanyiwa tafiti za Kijiolojia kwa asilimia 96.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Ally Maganga amewasilisha mada juu ya shughuli za Tume ya Madini ikiwemo uwepo wa Masomo na Vituo vya Ununuzi wa Madini, Mfumo wa Leseni pamoja na shughuli za wachimbaji wadogo.

Mhandisi Maganga amesema   uwepo wa masoko na vituo vya kuuzia madini umesaidia kuongeza mapato ya Sekta ya Madini ambapo mchango wa sekta hiyo kwenye Pato la Taifa umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka ambapo kwa sasa umefikia asilimia 9.7 ikiwa lengo ni kufikia mchango wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.

Friday, July 21, 2023

MKE WA MBUNGE AWAPIGA TAFU WASANII.

 


KATIKA kuhakikisha sanaa inakuwa Wilayani Kibaha mke wa Mbunge wa Kibaha Mjini Selina Koka ametoa kiasi cha shilingi milioni 1.2 ili kuendeleza sanaa hiyo kupitia Chama Cha Waigizaji Wilayani Kibaha humo.


Mke huyo wa Mbunge huyo alitoa fedha hizo wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika Visiga Madafu wilayani humo.


Akikabidhi cheki ya fedha hizo aliwataka waigizaji hao kuzitumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na kukuza tasnia hiyo ya sanaa ambayo imekuwa na kuwa na maslahi mazuri.


Awali Rais wa chama hicho Dk Cynthia Henjewele alisema kuwa wasanii wanapaswa kuungana na kutumia fursa za mikopo kupitia mfuko wa utamaduni ambayo inatolewa kwa wasanii ambazo hazina riba.

MKE WA MBUNGE ACHANGIA MAMILIONI CHAMA CHA WAIGIZAJI KIBAHA

MKE wa Mbunge wa Kibaha Mjini Selina Koka ametoa kiasi cha shilingi milioni 1.2 kwa Chama Cha Waigizaji Wilayani Kibaha kwa ajili ya kuendeshea shughuli zao.

Koka alitoa fedha hizo wakati wa uzinduzi wa chama hicho uliofanyika Visiga Madafu wilayani humo.

Akikabidhi cheki ya fedha hizo aliwataka waigizaji hao kuzitumia fedha hizo kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao na kukuza tasnia hiyo ya sanaa ambayo imekuwa na kuwa na maslahi mazuri.

"Tumieni sanaa kwa ajili ya kuelimisha jamii, kuburudisha na kufundisha ili muwe sehemu ya maendeleo ya nchi na kujinufaisha wenyewe kwa wenyewe,"alisema Koka.

Awali Rais Sanaa za Maonyesho Tanzania Dk Cynthia Henjewele alisema kuwa wasanii wanapaswa kuungana na kutumia fursa za mikopo kupitia mfuko wa utamaduni ambayo inatolewa kwa wasanii ambazo hazina riba.

Henjewele alisema kuwa ili wasanii waweze kutambulika wanapaswa kujisajili ili watambulike kisheria ambapo wakijirasimisha watapata fursa mbalimbali.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kibaha Mjini Jumanne Kambi alimshukuru mke wa Mbunge kwa mchango wake wa kukuza sanaa kwenye Wilaya hiyo.

Kambi alisema kuwa kwa kuwa sasa wana ofisi na tayari wana wanachama 700 watahakikisha wanachama wao wanaingia mikataba yenye manufaa kwa wasanii tofauti na kipindi cha nyuma ambapo walikuwa wanadhulumiwa haki zao.