Sunday, May 28, 2023

RC KUNENGE KUIPA KIPAUMBELE MICHEZO

MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema Mkoa utatoa kipaumbele kwenye michezo kwani ni moja ya ajira zenye utajiri mkubwa duniani.

Kunenge ameyasema hayo wakati akifunga michezo ya Umoja wa Michezo Taaluma Sanaa kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) mkoa wa Pwani kwenye viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Tumbi.

Alisema kuwa miongoni mwa matajiri wakubwa duniani wanatokana na michezo hivyo ni sehemu ya kutoa ajira kwa watu wakiwemo vijana.

"Mkoa utaunga mkono kwa kuifanya sekta ya michezo kuwa kipaumbele kwa kutoa fursa mbalimbali zinazohusiana na michezo,"alisema Kunenge.

Aidha alisema kuwa ili nchi iweze kuwa na vipaji na wachezaji wazuri lazima michezo ianzie chini kabisa kama nchi ilivyoweka utaratibu wa michezo hiyo kwani washiriki ni watoto wadogo hivyo kuwajengea kujiamini.

"Michezo inakuza uchumi pia ni ajira na ni afya hivyo lazima iwezeshwe kwa kuwajengea vijana mazingira mazuri ya kuendeleza vipaji vyao,"alisema Kunenge.

Alisema kuwa michezo ya mwaka huu imebeba kauli mbiu ya Miundombinu ya elimu na taaluma nchini ni chachu ya maendeleo ya sanaa na Michezo. 

Aliwataka wanamichezo hao kudumisha nidhamu ili kuuletea mkoa ushindi.Jumla ya wanamichezo kutoka Halmashauri tisa zilichuana kwenye michezo mbalimbali. 

Friday, May 26, 2023

DK SAMIA AGAWA ARDHI HEKARI 5,520 KWA WANANCHI

Hayo yamesemwa leo Mei, 26 2023 na Mhe David Silinde (Mb.) Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wakati wa makabidhiano ya ardhi  iliyokuwa sehemu ya Ranchi ya Ruvu kwenda kwa Wananchi wa Wilaya ya Bagamoyo na Kibaha ambapo pande zote zimeridhia.

Ameeleza uamuzi huo wa  Serikali ni kuwawezesha Wananchi kupata Ardhi kwa ajili ya Shughuli za kilimo, Mifugo na shughuli zingine za kijamii.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika Ukumbi wa Ranchi ya NARCO Ruvu ukishuhudiwa na Viongozi wa Wilaya,Tarafa, Kata, Vijiji na Viongozi wa Wakulima na Wafugaji na wawakilishi wa Wananchi kutoka Vijiji 10. 

Akipongeza uamuzi huo Mhe Kunenge Mkuu wa Mkoa wa Pwani  amewaagiza Viongozi wa Mkoa na Wilaya kutimiza wajibu wao wa kusimamia kupanga matumizi ya Ardhi hiyo na kuwataka Wananchi kuheshimu Sheria na kwamba wasivamie tena eneo hilo la Serikali.

MIAKA 30 YA MISA TANZANIA


Na Wellu Mtaki, Dodoma

MSEMAJI  Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amefungua Maadhimisho ya Miaka 30 ya Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara Tawi la Tanzania (MISA Tanzania) na akiwasisitiza waandishi wa habari kuzingatia maadili ya uandishi wa habari.

Msigwa amesisitiza hilo leo Mei 25,2023 Jijini Dodoma wakati akimwakilisha Naibu waziri wa Habari, Mawasiliano na Tekonolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya MISA.

Amesema serikali inaendelea kuboresha mazingira ya vyombo vya habari huku akisisitiza kuwa tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani hakuna chombo kilichofungiwa na vilivyokuwa vimefungiwa vimefunguliwa.

Aidha amesema katika kipindi hiki mafunzo au semina kwa waandishi zinahitajika hivyo kuiomba Misa Tanzania na wadau wengine kuwapatia mafunzo mbalimbali waandishi wa habari.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISA Tanzania, Salome Kitomari amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayofanya ya kuwatumikia Watanzania, lakini zaidi kwa namna amechukua hatua kadhaa zilizowezesha waandishi wa habari kutekeleza majukumu yao kwa kuondoa vikwazo vingi.

Kitomari amesema MISA Tanzania imepita kwenye safari ya miaka 30 yenye milima na mabonde na kutokana na mambo yote hayo ameupongeza uongozi, sekretarieti na wanachama wa MISA Tanzania kwa kushikamana mpaka kufikia hatua hiyo.

Sanjari na hayo ameongeza kuwa mafanikio mengine ni pamoja na kutoa mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa waandishi wa habari, Kuwezesha uanzishwaji wa vyombo vingine vya habari zikiwamo Radio za Kijamii na kufanya marekebisho kwenye sheria mbalimbali tangu Sheria ya Magazeti, Sheria ya Huduma za Habari, Sheria ya Haki ya Taarifa na nyinginezo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Misa Tanzania, Elizabeth Riziki amesema Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Jangwa la Sahara,Tawi la Tanzania (MISA Tanzania), inaadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993 baada ya kikao cha wanahabari waliokutana Windhoek, Namibia kujadili mambo mbalimbali yaliyokuwa yanaukabili Ukanda wa Nchi za Kusini.

MISA ina matawi tisa katika nchi za Zambia, Msumbiji, Malawi, Lesotho, Botswana, Namibia, Angola, Tanzania na Zimbabwe ambako ndiyo makao makuu ya matawi yote.

Amefafanua kuwa katika mkutano huo wa siku mbili wadau watajadiliana kuhusu kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia na namna ambavyo umma unahusishwa kwenye uhuru wa kujieleza na upatikanaji wa taarifa lakini pia watajadili changamoto zilizopo kwenye sekta ya habari na kuweka mkakati wa kuzitatua ikiwamo namna ya kuboresha maisha ya waandishi wa habari.

Pia amesema Majadiliano hayo yana lengo la kuongeza ukaribu na ushirikiano baina ya waandishi wa habari na Jamii, pia kuibua hoja zitakazowaleta pamoja Jamii na waandishi wa habari katika kuwa na mpango kazi wa utekelezaji ili kuhakikisha kila mwanajamii anatumia vizuri nafasi ya uhuru wa kujieleza kupitia vyombo vya habari kwaajili ya maendeleo endelevu.

Ikumbukwe kuwa Misa Tanzania inaadhimisha miaka 30 huku kauli mbiu ikiwa ni "Uhuru wa Kujieleza Msingi wa Haki Zote kwa Maendeleo Endelevu.

Thursday, May 25, 2023

SHULE ZA SEKONDARI TUMBI NA MWANALUGALI ZAPOKEA MILIONI 300

SHULE ya Sekondari ya Tumbi imepokea kiasi cha shilingi milioni 200 kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ya shule.

Aidha Shule ya Sekondari ya Mwanalugali imepokea kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa bwalo la chakula.

6,052 WATAMBULIWA MTAA WA LUMUMBA WALIOVAMIA SHAMBA LA MITAMBA

MTAA wa Lumumba Halmashauri ya Mji Kibaha utambuzi wa wananchi waliovamia eneo imefanyika na kukamilika na jumla ya wananchi 6,052 wametambuliwa.

Hayo yalisemwa na Hamis Shomari ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya mipango miji na mazingira na diwani wa Kata ya Kongowe aliyasema hayo kwenye kikao cha kawaida kipindi cha robo tatu Januari-Machi cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Alisema kazi ya utambuzi wa wananchi waliovamia eneo imefanyika na kukamilika na kazi ua uandaaji michoro nane yenye jumla ya viwanja 7,264 imekamilika.

"Maandalizi ya upimaji katika mtaa wa Lumumba yamekamilika na kazi ya upimaji wa viwanja na matarajio ni kupima viwanja 7,264 ambapo itakamilika ndani ya miezi miwili,"alisema Shomari.


HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAFANYA UTAMBUZI WA WALIOVAMIA ENEO MTAA WA MKOMBOZI

HALMASHAURI ya Mji Kibaha imefanya utambuzi wa wananchi waliovamia maeneo kwenye Mtaa wa Mkombozi ambapo 4,509 wametambuliwa.

Hayo yalisemwa na Hamis Shomari ambaye ni Mwenyekiti wa kamati ya mipango miji na mazingira na diwani wa Kata ya Kongowe aliyasema hayo kwenye kikao cha kawaida kipindi cha robo tatu Januari-Machi cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Shomari alisema kuwa watu hao wametambuliwa ili kupimiwa viwanja 6,250 kwenye michoro 22 ambayo imeandaliwa na kuidhinishwa. 

"Kazi ya upimaji wa viwanja 6,300 imefanyika na kuwasilishwa kwa ajili ya uidhinishwaji wa ramani kwa mpima ardhi wa mkoa na jumla ya viwanja 3,950 vimeidhinishwa,"alisema Shomari.

Alisema kuwa uuzaji wa viwanja katika mtaa umeanza Machi 24 ambapo wananchi walijulishwa kwa njia ya matangazo na mkutano wa hadhara ambapo hadi Aprili jumla ya ankara ya viwanja 168 vyenye thamani ya shilingi milioni 129.2 zimetolewa.

HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAKUSANYA MABILIONI

HALMASHAURI ya Mji Kibaha imekusanya kiasi cha shilingi bilioni 3.5 sawa na asilimia 78 ya makisio ya mwaka 2022/2023 ikiwa ni mapato ya ndani ambapo ilikadiria kukusanya shilingi bilioni 4.5.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Selina Wilson wakati wa kikao cha baraza la madiwani kwa kipindi cha robo tatu Januari hadi Machi.

Wilson alisema kuwa makusanyo hayo ni kuanzia Julai 2022 hadi Machi 2023 ambapo kwa upande wa vyanzo fungwa makisio ilikuwa ni shilingi milioni 506.7.

"Na kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai 2022 mpaka Machi 2023 kiasi cha shilingi milioni 587.8 kimekusanywa sawa na asilimia 116 ya makisio ya mwaka,"alisema Wilson.