Na John Gagarini, Kibaha
BONDIA Zumba Kukwe wa Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani leo
anatarajiwa kushuka ulingoni kupambana na Baraka Nuhu wa Chalinze
wilayani Bagamoyo kwenye ukumbi wa Ndelema Inn uliopo Chalinze.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana mjini Kibaha Kukwe
maarufu kama Lazima Ukae au Mzee wa Uganda alisema kuwa amejiandaa
vema na pambano hilo na anatarajia kuibuka na ushindi kwenye pigano
hilo ambalo ni la kirafiki la uzito wa kati la raundi nane.
Mzee wa Uganda alisema kuwa tangu alivyotoka nchini Uganda Oktoba
kupambana na bondia Badru Lusambya ambapo alitoka sare, amekuwa kwenye
mazoezi makali chini ya mwalimu wake Gaudence Oyaga.
“Nimejiandaa vizuri na ninatarajia kufanya vema kwenye pambano hili
licha ya kwamba mpinzani wangu sijamfahamu vizuri lakini mashabiki
wangu wasiwe na wasiwasi kwani lazima niwakilishe vizuri na naamini
kuwa lazima akae,” alisema Mzee wa Uganda.
Aidha alisema kuwa mchezo alilocheza nchini Uganda umempa uzoefu
mkubwa kwani ameweza kupata mbinu mpya za kupigana na bondia huyo wa
Uganda ambaye anaishi nchini Uingereza, hivyo anaamini kuwa ushindi ni
lazima.
Mbali ya pambano hilo lililoandaliwa na Mama Ndelema Intertainmet na
Shumbili Promotion kutakuwa na mapambano mengine kati ya Mwaite Juma
na Adam Mustapha, Shani Jaribu na Dula Kiroba, Singa Angokile na Juma
Shumbili.
Mapambano mengine ni ati ya Osama Kaongwa na Mustapha Tozo, Alex Kado
na Juma Soja, Issa Mawe na Khalid Hongo, Ismail Tembo na Bodi
Kitongoji, Salehe Mkalekwa na Jumanne Mvuteni, mgeni wa pambano hilo
anatarajiwa kuwa diwani wa Bwiringu Nasir Karama.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment