Tuesday, November 5, 2013

WAFA KWA MATUKIO TOFAUTI

Na John Gagarini, Kibaha

Jeshi la Polisi Mkoani Pwani linamshikilia Zaina Selemani umri miaka 14 mkazi wa Kitongoji cha Janga tarafa ya Mlandizi Wilaya ya Kibaha kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wake aitwaye Mariam Stamili mwenye miezi tisa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishina Msaidizi Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo alitenda kosa hilo mnamo tarehe 21/10/2013 majira ya saa 00:00 usiku kwa kumnywesha vitu vinavyosadikiwa kuwa ni sumu ya panya huko Kata ya Janga mtoto wake huyo.
Kamanda Matei ameongeza kuwa kifo cha mtoto huyo hapo awali ilidaiwa kuwa kilitokana na kusumbuliwa na maradhi ya degedege hali iliyopelekea familia yake na majirani kuamini hivyo na kupelekea taratibu zingine za mazishi kufanyika.
Kamanda Matei ameongeza kuwa siku ya tukio, baada ya mzazi wa mtoto huyo kununua sumu hiyo alimnyeshwa mtoto wake na baada ya kuona hali yake imebadilika na kuwa mbaya alimpigia simu mume wake Stamili Shabani umri miaka 21 na kumweleza kuwa mtoto wao anasumbuliwa na ugonjwa wa degedege hivyo wampeleke kwa mganga wa kienyeji.
Ameongeza kuwa baada ya mume wake kurejea nyumbani walimchukua motto huyo na kumpeleka kwa mganga huko Kijiji cha Disunyara ambapo marehemu alianza kupatiwa matibabu lakini hata hivyo kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya walimchukua mtoto huyo na kwenda nae kituo cha afya Mlandizi ambapo alipoteza maisha siku ya tarehe 21/102013 majira ya saa 00:00 usiku.
Baada ya kutokea kwa kifo hicho mwili wa marehemu ulichukuliwa na ndugu zake na kuzikwa majira ya saa 17:00 jioni huko Kijiji cha Kilangalanga, lakini hata hivyo baada ya kumalizika kwa mazishi hayo mtuhumiwa wa mauaji hayo usiku wa kuamkia tarehe 23/10/2013  alianza kulia na kumwambia mume wake huyo kuwa mtoto wao hakufa kwa ugonjwa wa degedege ila alikuwa amemnywesha sumu hivyo kumuomba amsamehe.
Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma dhidi yake mara baada ya upelelezi kukamilika.
Katika tukio jingine mnamo tarehe 03/11/2013, majira ya saa za 6.30 usiku huko Kijiji cha Mindutulieni Kata ya Talawanda Tarafa ya Chalinze (W) Bagamoyo (M) Pwani. Said Mbena miaka 30, mbena, mkulima mkazi wa Kijiji cha Mindutulieni aliuawa kwa kupigwa na fimbo sehemu mbalimbali za mwili na Machocho Matei miaka 35, mmasai, mfugaji, mkazi wa Kijiji cha Mindutulieni baada ya kutokea ugomvi kati yao wakiwa kwenye sherehe za ngoma za kienyeji nyumbani kwa Asha Rashid. Mtuhumiwa baada ya kukamatwa akiwa njiani kupelekwa katika ofisi ya Kijiji cha Mindutulieni kabla ya kufikishwa katika ofisi hiyo aliuawa na wananchi waliojichukulia sheria mkononi. Miili ya marehemu ya marehemu imehifadhiwa katika ofisi ya Kijiji hicho ikisubiri kufanyiwa uchunguzi na Daktari.
Aidha mnamo tarehe 02/11/2013, majira ya saa za 9.00 usiku huko Kitongoji cha Mlandizi Kati Kata ya Mlandizi Tarafa ya Mlandizi Wilaya ya Kibaha (M) Pwani. Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina moja la Kingstone umri kati ya miaka 30-35, mkulima mkazi wa Mlandizi aliuawa na mtu / watu wasiofahamika kwa kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu ya mguu wa kushoto kwenye maungio ya goti, hali iliyosababisha damu nyingi kuvuja na kusababisha kifo chake. Mwili wa marehemu umehifadhiwa chumba cha maiti Hospitali ya Tumbi Kibaha ukisubiri kufanyiwa uchunguzi na Daktari / kutambuliwa na ndugu.
Kadhalika Kamanda Matei ameeleza kuwa mnamo tarehe 02/11/2013, majira ya saa za 4.00 asubuhi huko Kijiji cha Kazimzumbwi Kata ya Kisarawe Tarafa ya Sungwi barabara ya Dar es Salaam - Kisarawe (W) Kisarawe (M) Pwani. Gari Na. T.762 BSB aina ya Noah likiendeshwa na Dereva asiyefahamika akitokea Dar es Salaam kwenda Msanga aligongana uso kwa uso na pikipiki Na. T.219 BUM aina Fekon iliyokuwa ikiendeshwa na Sixbert Ngatunga miaka 36, mkazi wa Kazimzumbwi akitokea Kisanga kwenda Kazimzumbwi. Katika ajali hiyo dereva wa pikipiki alifariki dunia papo hapo. Mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na Daktari na kukabidhiwa ndugu kwa mazishi. Chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva wa Gari Na. T.762 BSB aina ya Noah.
 
 

No comments:

Post a Comment