Monday, November 25, 2013

VIZIWI WAHITAJI MSAADA WA VIFAA VYA MICHEZO

Na John Gagarini, Kibaha

TIMU ya Viziwi mkoani Pwani (PDSC) inatarajia kuingia kambini Desemba
20 mwaka huu kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha kujiandaa na
mashindano ya maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha katibu
wa timu hiyo Daudi Kulangwa alisema kuwa timu hiyo kwa sasa inaendelea
na mazoezi yake kwenye uwanja wa Kongowe wilayani Kibaha.

Kulangwa alisema kuwa mashindano hayo yatafanyika Januari 7 hadi 11
mwaka 2014 ambapo wao na Dar es Salaam wamealikwa watachuana na timu
wenyeji ambao ni Unguja na Pemba.

“Tunaendelea na mazoezi lakini changamoto yetu kubwa ni ukosefu wa
vifaa kama vile jezi ambapo tunacheza vifua wazi, hatuna viatu na
kujikuta wakicheza pekupeku na mipira,” alisema Kulangwa.

Alisema kuwa wanawaomba watu mbalimbali wakiwemo wabunge wa mkoa wa
Pwani wajitokeze kuwasaidia ili waweze kufanya vema.

“Maombi yetu tayari tumeyapeleka ofisi ya Mfuko wa Maendeleo ya
Wanawake (WAMA) pamoja na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani ambao
wameonyesha nia ya kutusaidia,” alisema Kulangwa.

Alibainisha kuwa mbali ya changamoto hizo wanaendelea na mazoezi chini
ya walimu wao Zuberi Boka na Philbert Mbwette na kuwataka watu
waitembelee timu yao na kuiunga mkono ili iweze kufanya vizuri kwenye
mashindano hayo.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment