Tuesday, May 21, 2024
Saturday, May 18, 2024
JKT RUVU YAZINDUA BUSTANI YA WANYAMAPORI
MKUU wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amezindua bustani ya Wanyamapori ya Kikosi cha Jeshi cha Ruvu JKT (Wildlife).
John akizindua bustani hiyo iliyopo kwenye eneo la Kikosi cha 832 KJ Mlandizi Wilayani Kibaha Mkoani Pwani amewataka wananchi kujitokeza kwenda kuangalia wanyama ambao sasa wanapatikana karibu.
Amesema uwepo wa Mbuga hiyo mbali ya kuwapunguzia gharama wananchi wanaotaka kuangalia wanyama pia itaongeza mapato ya Kikosi hicho na serikali.
Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi hicho Kanali Peter Mnyani amesema kuwa wameanza na wanyama wachache lakini watawaongeza ili wawe wengi ambapo watakuwa na fursa ya kupiga picha na wanyama hao.
Mnyani amesema kuwa mwezi Juni wataongeza wanyama wakiwemo Simba ili kuongeza idadi ya wanyama na eneo hilo lina ukubwa wa hekari 70.
Amesema mbali ya kufuga wanyama hao pia wanatunza mazingira kutokana na eneo hilo kuwa na mazingira mazuri na ya asili.
Thursday, May 16, 2024
TUMEPANGA, TUMETEKELEZA, KUTEKELEZA: JAJI MKUU
Na Mwandishi Wetu , Dodoma
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewapongeza watumishi wote wa Mahakama kwa kuendelea kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano awamu ya pili pamoja na programu ya Maboresho ya Miaka Mitano, ambazo zinalenga pia kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025.
Mhe. Prof. Juma ametoa pongezi hizo kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Jaji Amidi wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija, leo tarehe 16 Mei, 2024 kwenye Baraza Kuu la Wafanyakazi linalofanyika kwenye Ukumbi wa PSSSF jijini hapa.
“Nina kila sababu ya kuwapongeza wafanyakazi wa Mahakama kutokana na kujituma kwenu kuhakikisha kuwa tunatekeleza kwa ufanisi mipango tuliyojiwekea. Tufahamu kuwa kupanga ni jambo moja na utekelezaji wa mipango ni jambo lingine, kwetu sisi tumepanga, tumetekeleza na tunaendelea kutekeleza,” amesema.
Jaji Mkuu ametoa rai kwa wafanyakazi wote kutokurudi nyuma katika jitihada za kimaboresho kwani Viongozi wa Mahakama wanatambua na kuheshimu mchango wa kila mmoja ambao ndiyo uliowezesha utekelezaji wa programu mbalimbali za kimaboresho.
Ametumia fursa hiyo kuwahimiza watumishi wote kuipokea mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inayotumiwa na Mahakama ya Tanzania ambayo siyo tu inawalenga wananchi na watumiaji wa huduma za Mahakama kwa kuwapa huduma kwa weledi, ufanisi, uwazi na kwa haraka lakini pia inalenga kuwaboreshea mazingira ya kufanya kazi za utoaji wa huduma.
Jaji Mkuu ametaja mfano wa Mfumo Mpya wa Usimamizi wa Mashauri (e-CMS) ambao una faida lukuki zinazolenga kurahisha utendaji kazi kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania.
Amesema kuwa, badala ya kupitia malundo ya majalada na karatasi kukusanya takwimu, Mfumo huu utakusanya takwimu na taarifa mbalimbali kwa njia ya elektroniki kwa usahihi.
Jaji Mkuu amesema kuwa takwimu zitasaidia kuona yaliyojificha, hivyo kusaidia katika utekelezaji wa mipango mbalimbali na kuboresha jukumu la utoaji haki.
“Mfumo huu utasaidia kupima utendaji wa kila mmoja wetu bila ubaguzi au uonevu kwa watumishi. Utaongeza tija, ufanisi na uono wa viwango vya utoaji wa huduma wa kila mtumiaji wa mfumo huu, kwa mfano Majaji, Wasajili, Mahakimu, Masjala za Mahakama, wadau wote wa Mahakama,” amesema.
Jaji Mkuu ametaja faida nyingine ni kupungua kwa watumishi kukutana na wadaawa uso kwa uso na kuondoa lawama za kimaadili kwa vile wadaawa na wananchi watapata fursa ya kuingia katika mfumo kutafuta taarifa bila kumuona mtumishi wa Mahakama.
“Hakutakuwa na nafasi ya mtumishi kudhaniwa kuwa kapokea rushwa ili atoe huduma. Mfumo huu pia utaboresha usimamizi na ukaguzi. Kwa mfano, Jaji au Hakimu Mfawidhi na Wasajili, wataweza kuona kila hatua ambayo shauri lolote linapitia na kufikia mbele ya Jaji au Hakimu, bila kuliita jalada au kuomba taarifa ya mashauri kutoka kwa aliye na jalada,” amesema.
Jaji Mkuu ametaja Mfumo mwingine wa Tafsiri na Unukuzi (Transcription and Translation Software -TTS) ambao umelenga kuwapunguzia watumishi, hususan Majaji na Mahakimu, mzigo mzito wa kuandika mienendo ya mashauri kwa kalamu ya mkono.
Ameeleza kuwa Mfumo huo unapokea sauti, uinakili hiyo sauti na kuiweka katika maandishi ya kiswahili na unao uwezo wa kutafsiri hayo maandishi kutoka lugha ya kiswahili hadi kiingereza na pia kutoka lugha ya kiingereza hadi kiswahili.
“Mfumo wa TTS tayari umefungwa na kuanza kutumika katika Mahakama 11, ikiwemo baadhi ya Mahakama Kuu (ambazo pia ni Masjala Ndogo za Mahakama ya Rufani),” Mhe. Prof. Juma amesma.
Amesisitiza kuwa, mfumo huo wa TTS utaongeza ufanisi katika uchukuaji wa mwenendo wa shauri kwa kumpunguzia Jaji au Hakimu mzigo wa kusikiliza na kuandika kwa wakati mmoja na kuharakisha kupatikana kwa mienendo ya mashauri kwa ajili ya kukata rufani.
TANZANIA YAADHIMISHA MIAKA 60 YA KIDIPLOMASIA KATI YAKE NA CHINA
- Filamu ya " Amazing Tanzania " yazinduliwa China
Na Mwandishi Wetu - Beijing
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeadhimisha Miaka 60 ya Kidiplomasia kati yake na China sambamba na uzinduzi wa mwaka wa Utalii na Utamaduni ulioambatana na uzinduzi rasmi wa filamu ya “Amazing Tanzania” Mei 15, 2024 jijini Beijing China.
Akizungumza katika Maadhimisho hayo Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amesema uhusiano kati ya China na Tanzania ulianza tangu kipindi cha Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Aidha,amesema mahusiano kati ya China na Tanzania ni thabiti chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping.
"Tunapoadhimisha miaka 60 ya uhusiano wetu na pia tunasherehekea mwaka wa utamaduni na utalii kama ilivyotangazwa na viongozi wetu mwaka 2022 katika ziara ya Kiserikali ya Rais Samia Suluhu alipotembelea nchini China" Mhe. Kairuki amesisitiza.
Katika hatua nyingine Waziri Kairuki ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais Samia na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ally Mwinyi pamoja na mwigizaji maarufu wa filamu kutoka China, Jin Dong kwa kushiriki katika uandaaji wa filamu hiyo.
Kufuatia uzinduzi wa filamu ya " Amazing Tanzania " Mhe. Kairuki amesema kuwa filamu hiyo itaonyesha vivutio vya utalii wa Tanzania kwa soko la utalii la China na kwamba Tanzania inatarajia kupokea watalii wengi kutoka nchini China baada ya uzinduzi huo.
Naye,Waziri wa Utamaduni na Utalii wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Sun Yeli amesema kuwa urafiki wa jadi kati ya China na Tanzania ulijengwa na viongozi wa kizazi cha zamani wa nchi hizo mbili na kwamba
tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia miaka 60 iliyopita China Tanzania imestahimili jaribio la mabadiliko ya mazingira ya kimataifa na kuimarika zaidi.
"Leo tunapokutana hapa kuzindua mwaka wa Utalii na Utamaduni wa Tanzania China natumai tutaifanya kuwa mwanzo mpya wa kuendeleza mabadilishano ya kitamaduni na ushirikiano wa Utalii ili kurahisisha ziara zetu za pande mbili, mabadilishano kati ya taasisi za kiutamaduni na sanaa na vile vile kampuni za utalii kuongeza usambazaji wa bidhaa za utalii." amesisitiza.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, wajumbe wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania akiwemo Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa, Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro,Waziri wa Vijana,Utamaduni na Michezo Zanzibar Mhe. Tabia Maulid Mwita pamoja na maafisa wa taasisi mbalimbali za sekta za umma na binafsi.
Wednesday, May 15, 2024
MAKUMBUSHO YA CHINA NA TANZANIA KUSHIRIKIANA
Wednesday, May 8, 2024
KUSIMAMA VIVUKONI NI AMRI SIO HIARI
Mkuu wa Dawati la elimu ya usalama barabarani Tanzania Kamishina Msaidizi wa Polisi, Michael Deceli amewataka madereva wa vyombo vya moto kuzingatia alama za barabarani ili kupunguza ajali kwa watumiaji wengine wa barabara.
Akizungumza Leo Mei, 08 baada ya kuhitimisha utoaji wa elimu ya uvukaji wa barabara kwenye vivuko vya waenda kwa miguu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani Deceli amesema kumekuwepo na baadhi ya madereva wa vyombo vya moto wakiwemo madereva wa serikali kutokusimama kwenye vivuko vya waenda kwa miguu na kupelekea ajali katika baadhi ya maeneo.
"Suala la kuheshimu alama za barabarani ni la kila dereva anayeendesha chombo cha moto, Sheria haijabagua madereva wa kuziheshimu alama hizo na wengine kutokuheshimu".
Kadhalika, Deceli amewataka madereva walioweka magari yao ving'ora pasipo kuwa na kibali cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuondoa mara moja na wale watakao kamatwa wakiwa hawana vibali hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Friday, May 3, 2024
KPC YAWATAKA WANANCHI KUTUMIA KITUO CHAO KUTATUA CHANGAMOTO ZA KISHERIA.