Wednesday, May 15, 2024

MAKUMBUSHO YA CHINA NA TANZANIA KUSHIRIKIANA




Na Mwandishi Wetu-Beijing 

Makumbusho ya Taifa  ya China na Tanzania zimekubaliana  kushirikiana katika kubadilishana uzoefu, teknolojia na kuwa na maonesho ya pamoja  kwa lengo  la kuhakikisha kuwa huduma za makumbusho zinakuwa na faida kwa pande zote mbili za nchi hizo.

Makubaliano hayo yamefikiwa katika mazungumzo kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la China, Gazo Zheng yaliyofanyika kwenye Makumbusho ya China jijini Beijing Mei 14,2024.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kairuki amesema kwa kuwa Makumbusho ya Taifa la China ina uzoefu wa miaka mingi, ni vyema ikashirikiana na Makumbusho ya Taifa la Tanzania katika dijitali ,kufanya tafiti, kuwa na Maonesho ya pamoja, kuonesha utamaduni na historia ya nchi zote mbili pamoja na kubadilishana uzoefu wa utaalamu katika kutunza na kuhifadhi mikusanyo.
Aidha, Mhe. Kairuki amesema kuwa Tanzania ingependa kujifunza namna ya  kuvutia kizazi cha vijana kinachokua ili kiwe na utamaduni wa kutembelea Makumbusho mbalimbali zilizopo nchini Tanzania.

Amesema  Serikali ya Tanzania kupitia ubalozi wake ulipo jijini Beijing nchini China utahakikisha unafuata taratibu zote za kuwepo kwa  Mkataba wa Makubaliano kati ya makumbusho hizo ili kurasimisha ushirikiano huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Zheng amesema Makumbusho ya Taifa la China iko tayari kushirikiana na Tanzania katika maeneo yote yaliyopendekezwa.

“Makumbusho ya Taifa la China ina uzoefu mkubwa na ina wataalamu zaidi ya mia moja hivyo ina furaha kushirikiana na Makumbusho ya Taifa la Tanzania hasa katika kuhifadhi mikusanyo, kufanya tafiti, kubadilishana uzoefu na namna ya kuvutia  vijana kuwa na utamaduni wa kutembelea makumbusho” amesema.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, wajumbe wa Kamati ya Rais ya Kuitangaza Tanzania akiwemo Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Fatma Mabrouk, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Anderson Mutatembwa pamoja na maafisa wa taasisi mbalimbali za sekta za umma.

Waziri Kairuki yuko nchini China kwa ajili ya kushiriki katika Maadhimisho ya Miaka 60 ya Kidiplomasia kati ya Tanzania na China pamoja na uzinduzi wa mwaka wa Utalii na Utamaduni na pia uzinduzi rasmi wa filamu ya “Amazing Tanzania” utakaofanyika Mei 15, 2024 jijini Beijing

Wednesday, May 8, 2024

KUSIMAMA VIVUKONI NI AMRI SIO HIARI

Mkuu wa Dawati la elimu ya usalama barabarani Tanzania Kamishina Msaidizi wa Polisi, Michael Deceli amewataka madereva wa vyombo vya moto kuzingatia alama za barabarani ili kupunguza ajali kwa watumiaji wengine wa barabara.

Akizungumza Leo Mei, 08 baada ya kuhitimisha utoaji wa elimu ya uvukaji wa barabara kwenye vivuko vya waenda kwa miguu kwa wanafunzi wa shule ya msingi Misugusugu Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani Deceli amesema kumekuwepo na baadhi ya madereva wa vyombo vya moto wakiwemo madereva wa serikali kutokusimama kwenye  vivuko vya waenda kwa miguu na kupelekea ajali katika baadhi ya maeneo.

"Suala la kuheshimu alama za barabarani ni la kila dereva anayeendesha  chombo cha moto, Sheria haijabagua madereva wa kuziheshimu alama hizo na wengine kutokuheshimu".

Kadhalika, Deceli amewataka madereva walioweka magari yao ving'ora pasipo kuwa na kibali cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuondoa mara moja na wale watakao kamatwa wakiwa hawana vibali hivyo watachukuliwa hatua za kisheria.

Friday, May 3, 2024

KPC YAWATAKA WANANCHI KUTUMIA KITUO CHAO KUTATUA CHANGAMOTO ZA KISHERIA.

 

WANANCHI wa Halmashauri ya Mji Kibaha wametakiwa kukitumia Kituo cha cha Msaada wa Kisheria (KPC) ili kutatua changamoto zinazohusiana na masuala ya kisheria ili kuokoa muda wa kwenda Mahakamani.


kimeendelea na utoaji elimu na msaada wa kisheria kwa makundi mbalimbali ili kuwajengea ufahamu wa sheria wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Akizingumza na waandishi wa habari Mjini Kibaha Mkurugenzi wa KPC Catherine Mlenga amesema kuwa baadhi ya masuala ya kisheria yanaweza kutatuliwa kituoni hapo kabla hawajayafikisha Mahakamani.

Mlenga amesema kuwa wananchi wanaweza kutatuliwa changamoto za kisheria na kuokoa muda ambao wangeutumia kwenda mahakamani na kufanya shughuli zao za maendeleo.

Aidha amesema kuwa wanatoa elimu pamoja na msaada kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali kupitia ustawi wa jamii pamoja na mahakama.

Amewataka wananchi wa Kibaha kukitumia kituo hicho ili waweze kusaidiwa pale wanapopata changamoto za kisheria na wasifumbie vitendo vya ukatili ndani ya jamii kwa kutoa taarifa.

Mwisho.

KPC YAENDELEA KUTOA MSAADA NA ELIMU YA KISHERIA KWA WANANCHI WA KIBAHA

KITUO cha Msaada wa Kisheria (KPC) kimeendelea na utoaji elimu na msaada wa kisheria kwa makundi mbalimbali ili kuwajengea ufahamu wa sheria wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha.

Akizingumza na waandishi wa habari baada ya kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa Shule mbalimbali Mkurugenzi wa KPC Catherine Mlenga amesema kuwa elimu hiyo ni kwa wananchi wote.

Mlenga amesema kuwa wanatoa elimu pamoja na msaada kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo serikali.

"Tunaishukuru serikali kwa kutupatia vibali ambavyo vinatuwezesha kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wananchi lengo likiwa ni kuwapa uelewa wa kujua sheria mbalimbali,"amesema Mlenga.

Amesema kuwa elimu ya sheria imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi ambapo baadhi wamepata uelewa na kuweza kutoa taarifa pale wanapoona kuna uvunjwaji wa sheria.

"Elimu tunayoitoa ni kuanzia kwa wanafunzi mashuleni, majumbani, masokoni, kwenye nyumba za ibada, kwenye mikutano na mikusanyiko mbalimbali ta kijamii,"amesema Mlenga.

Aidha amesema kuwa wanatoa msaada wa kisheria bure kwa watu wasiokuwa na uwezo hususani wanawake na watoto na kuwapigania hadi kupata haki zao.

"Sheria tunazowafundisha ni zote ikiwa ni pamoja na mirathi, ndoa, ardhi, matunzo ya watoto, haki za watoto, sheria za kazi, mazingira, na nyinginezo,"amesema Mlenga.

Amewataka wananchi wa Kibaha kukitumia kituo hicho ili waweze kusaidiwa pale wanapopata changamoto za kisheria na wasifumbie vitendo vya ukatili ndani ya jamii kwa kutoa taarifa.

Wednesday, May 1, 2024

WAHITIMU JKT KUJITOLEA WATAKIWA KUTANGULIZA UZALENDO

 




Na John Gagarini, Kibaha

VIJANA wanaohitimu mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wakujitolea wametakiwa kutumia dhana ya uzalendo katika shuguli za ujenzi wa Taifa ili kuiletea nchi maendeleo.

Hayo yalisemwa Mlandizi na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John wakati wa kufunga mafunzo ya (JKT) ya kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT kwenye Kikosi cha Ruvu Kibaha.

John alisema kuwa Vijana hao wameandaliwa vema kulipambania Taifa hivyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao lazima watangulize uzalendo.

"Zingatieni mambo manne muhimu Utii, nidhamu, uhodari na uaminifu haya ndiyo mambo ya kuzingatia hapa ndipo mtakuwa mnafanya uzalendo ambayo ndiyo nguzo kuu ya mafunzo yenu,"alisema John.

Alisema kuwa pia wawe na uhodari kwenye jambo moja ambalo ni fani ili wawe mahiri kwani kuchanganya mambo mengi kwa wakati mmoja hawataweza kuwa mahiri.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi Meja Jenerali Ibrahim Mhona alisema kuwa vijana hao wanapaswa kujilinda kiafya kwani suala la afya ni muhimu sana.

Mhona ambaye pia ni Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) alisema kuwa mafunzo hayo ni ya kuwapatia stadi za maisha na baadaye watapata stadi za kazi ikiwa ni hatua ya pili baada ya hatua ya kwanza.

Alisema kuwa mafunzo hayo yamekuza moyo wa uzalendo ukakamavu na kutumia vizuri muda na hawajakosea kujiunga na mafunzo hayo ya kujitolea kwani maamuzi yao ni ya busara na kuwapongeza wazazi na walezi kwa kuwapeleka vijana wao kwenye mafunzo hayo.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa JKT Kanali Robert Kessy alisema kuwa wakati wa kutekeleza majukumu yao wahakikishe wanatatua changamoto bila kuvunja sheria na kuwa na nidhamu bila kusahau uhodari kwani Taifa limewekeza sehemu sahihi.

Kessy alisema kuwa vijana wanapaswa kujitolea kulitumikia Taifa na kumuenzi Baba wa Taifa ambaye aliasisi Jeshi hilo na wahakikishe wanaonyesha uzalendo kwa vitendo na weledi na wajiulize watalifanyia nini Taifa siyo Taifa kuwafanyia nini pia wahakikishe wanasimamia viapo vyao.

Awali Mkuu wa Kikosi cha Ruvu 832 KJ Kanali Peter Mnyani alisema kuwa mafunzo hayo ya awali ya kijeshi waliyoyapata vijana hao ni pamoja na ukakamavu ujasiri ambavyo wamefanya kwa vitendo.

Mnyani alisema kuwa mafunzo hayo yalikuwa ya muda wa miezi minne kati ya miezi 24 ya mkataba wao ambapo walijifunza utimamu wa mwili, usomaji ramani, uraia,  usalama na utambuzi na kwata za silaha ndogo ndogo.

Akisoma risala ya wahitimu wa mafunzo hayo Lulu Godfrey alisema kuwa Vijana wa Kujitolea Operesheni Miaka 60 ya JKT walianza mafunzo hayo Desemba 2023.

Godfrey alisema kuwa kwenye mafunzo hayo walifundishwa mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja mbinu za ulinzi, ukakamavu, utii, ulinzi wa taifa ujasiri uvumilivu, na hawatatumia vibaya mafunzo hayo kinyume na malengo ya Taifa.

Jumla vijana 800 walijiunga na mafunzo hayo ambapo waliohitimu walikuwa 776 wavulana wakiwa 438 na wasichana walikuwa 338 na vijana 24 hawakumaliza mafunzo hayo na kwa kipindi cha miezi 20 watakuwa kwenye majukumu mbalimbali ikiwa ni pamoja na malezi, uzalishaji mali na ulinzi.

 Mwisho.

Tuesday, April 30, 2024

*BMH YAHUDHURIA UFUNGUZI WA MKUTANO WA 24 BARAZA LA MAWAZIRI* *SEKTA* *YA* *AFYA* *EAC*

Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imehudhuria ufunguzi wa Mkutano wa Kawaida wa 24 wa Baraza la Mawaziri la sekta ya Afya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Dar es Dar es Salaam. 

Mkutano huo wa siku tano, ulioanza leo tarehe 29 Aprili hadi Mei 3,  unafanyika kwa njia ya mseto (video na ana kwa ana) umeanza katika ngazi ya wataalam ukilenga kufanya tathimini ya utekelezaji wa maagizo na makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa 22 wa Baraza hiloa mbapo taarifa itawasilishwa katika Mkutano wa Makatibu Wakuu.

Mkutano utafuatiwa na ngazi ya Makatibu Wakuu tarehe 2 Aprili 2024, ambapo taarifa itawasilishwa, Makatibu na kuhitimishwa na Mkutano ngazi ya Mawaziri ukaofanyika Mei 3.

Mbali na kufanya tathimini ya utekelezaji wa maagizo na makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa 22 wa Baraza hilo, Mkutano huo utajadili agenda nyingine zinazotarajiwa ikiwemo Mkutano taarifa za Vikundi Kazi (Technical Working Group – TWG) sita (06) vya Sekta ya Afya na mapendekezo ya Tanzania ya kuanzisha Kituo cha Umahiri cha Upandikizaji Uloto na Sayansi ya Matibabu ya Magonjwa ya Damu chini ya Hospitali ya Benjamin Mkapa. 

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano huo, Mganga Mkuu wa Serikali wa Tanzania Prof. Tumaini Nagu, ametoa rai kwa wataalamu wa sekta ya Afya ya EAC kutoa michango itayosaidia Jumuiya kuimarisha miundombinu ya huduma ya afya ili kukabiliana na matishio ya kiafya kwa magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza.

“Tumekuja kujadili na kutoa suluhisho na majawabu yatakayotusaidia kukabili changamoto za kiafya katika Jumuiya yetu kwa kuzingatia ubunifu na weledi katika mifumo yetu ya afya huku tukiwa wamoja na wenye nguvu zaidi” amesema Prof. Nagu

Pro. Nagu amehimiza umuhimu wa Sekta ya Afya katika Jumuiya kuendelea kufanya kazi kwa ufanisi na umoja katika utekelezaji progamu mbalimbali za Afya ikiwemo miradi ya Sekta ya Afya na mikakati inayopangwa ili kufikia mafanikio yanayotarajiwa kwa wakati.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii katika Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Irene Isaka, ameeleza kuwa kupitia mkutano huo nchi wanachama watapata fursa ya kusikia taarifa zitakazowasilishwa na kila nchi ili kwa pamoja kuweza kuchangia na kushauri namna bora ya kusimamia na kutekeleza programu, miradi na miundombinu ya Afya katika Jumuiya.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umeongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu na wajumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ambapo imewakilishwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii Mhandisi Abdillah Mataka. 

Wengine kutoka Tanzania walioshiriki Mkutano huo ni pamoja na Wizara za Afya (Tanzania Bara na Zanzibar), Hospitali ya Benjamin Mkapa, Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TMDA), Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) Bohari ya Dawa (MSD), Maabara Kuu ya Taifa, Mpango wa Kitaifa wa Kudhibiti Malaria (NAMCP) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA).

Monday, April 29, 2024

MWENGE KUPITIA MIRADI YA TRILIONI 8.6

MWENGE wa Uhuru umeanza mbio zake Mkoani Pwani ukitokea Mkoani Morogoro ambapo utapitia miradi 126 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi trilioni 8.5.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge alipoupokea Mwenge huo eneo la Bwawani Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo, kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Adam Malima.

Kungenge alisema kuwa kati ya miradi hiyo 18 itawekewa mawe ya msingi 22 itazinduliwa 86 itakaguliwa.

"Miradi hiyo imefanikiwa kutokana na Rais kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ushirikiano kati ya viongozi, wananchi na wadau wa maendeleo katika kutafuta fedha hasa ikizingatiwa Pwani ni Mkoa wa kimkakati,"alisema Kunenge.

Kwa upande wake kiongozi wa mbio za Mwenge Godfrey Eliakim Mzava alisema kuwa wanapofika kwenye miradi ya maendeleo wakute taarifa sahihi za utekelezaji wa miradi ya maendeleo pia nyaraka zote za msingi zinazoeleza utekelezaji wa miradi iliyoyopo na wataalamu watoe maelezo ya kina na vifaa vya upimaji ubora wa miradi viwepo.

Mwisho.