Friday, March 8, 2024

WANAWAKE WATAKIWA KUWA NA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA

 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

WANAWAKE nchini wametakiwa kutambua suala la matumizi sahihi ya fedha ili kuweza kujiongezea kipato zaidi na kujikwamua kiuchumi.

Hayo yameelezwa na  Mkurugezi Msaidizi sehemu ya usimamizi Rasilimali watu Wizara ya fedha Bi, Faudhia Nombo wakati akimwakilisha katibu mkuu wizara ya fedha katika  maonesho ya banda la wizara hiyo  leo Machi 7  siku ya ufunguzi  wa maonyesho ya wanawake  kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani.

Nombo amesema wizara inaendelea kutoa Elimu kwa wanawake kujiandaa wakati wa kustafu kazi katika kipindi cha uzee pamoja na suala la kutunza fedha 

"Wizara haitokaa kimya ila itahakikisha inaendelea kutoa Elimu kwa wanawake ili pindi wanapostafu kazi wapate fedha za kujikimu kipindi chote cha uzee , wapo wanawake wanatumia fedha katika majukumu ambayo si sahihi na mwisho wa siku fedha hupotea na kuelekea mwisho mbaya uzeeni," amesema Nombo.

Aidha amesema kuwa wanawake wengi wanatamani kuingia katika vikoba ili kuweza kujikimu kiuchumi ila wanashidwa kutambua namna ya utunzaji wa fedha hivyo wizara imeona watoe mafunzo ya namna ya kutunza fedha katika maonesho ya siku ya wanawake Dunia.

Pia ametoa wito kwa wanawake wa Dodoma kutambua fursa zilizopo katika wizara hiyo na kutumia kiusahihi ili kufanikisha shughuli zao za kiuchumi.

KUNDO ATAKA VYOMBO VYA HABARI NCHINI KUANZISHA VIPINDI VYA KUHAMASISHA MILA NA DESTURI ZA WATANZANIA.

NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo amevitaka vyombo vya habari kuanzisha vipindi vinavyohamasisha mila na Destiri ya mtanzania ili kuwaelimisha vijana kuhusu tamaduni zao.

Mhandisi Kundo ametoa kauli hiyo Leo Februari 13,2024 Jijini Dodoma , alipomwakilisha Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya habari Mhe. Nape Nnauye, katika ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Vyombo vya Utangazaji Nchini ulioenda sambamba na kilele cha maadhimisho ya siku ya Utangazaji Duniani

“Ni muhimu sana kwenu TCRA kuliangalia suala hili kwa umakini mkubwa kwani Mkifanya hivi itawasaidia sana kufanya kazi kwa ufanisi,na Sisi kama Serikali tunawaahidi kuendeleza ushirikiano uliopo ili kuleta maendeleo kwa jamii, "amesema Mhandisi Kundo

Pia Mhandisi Kundo ameiagiza Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA),kuhakikisha inajitathmini Mara kwa Mara ili kujua ni wapi kuna mapungufu na kuweza kuyafanyia kazi mapungufu hayo.

Katika hatua nyingine Mhandisi Kundo amebainisha kuwa katika kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa Vyombo vya Habari vinatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuzingatia Maadili na kanuni za utoaji Habari kwa jamii kwa maslahi ya Taifa.

“Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa katika Taifa letu hivyo Ni muhimu kila mmoja kuzingatia taaluma na kutimiza majukumu yake kwa weledi mkubwa,amesisitiza Naibu Waziri

Aidha amewaasa Waandishi wa habari kuhakikisha wanazingatia usawa katika kuripoti matukio ya kampeni za Uchaguzi na matokeo Yake bila upendeleo

Kwa upande Wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania( TCRA )Jones Kilimbe amewataka watangazaji na waandishi wa habari kuzingatia Madili na kanuni ya kazi zao.

Amegusia pia uchaguzi  wa Serikali za mitaa kuwa,vyombo vya habari vina jukumu la kutoa elimu kwa wapiga kura ikiwa ni pamoja na kuhabarisha umma kuhusu mwenendo mzima wa kampeni bila upendeleo na kutoa ripoti sahihi za siku ya kupiga kura.

Amesema TCRA kama wadau wa Utangazaji watahakikisha wanakuwa bega kwa bega na vyombo vya Utangazaji kwa kuhakikisha wanatoa mwelekeo wa maudhui yenye ubora bila upotoshaji.

Thursday, February 29, 2024

BMH YAENDELEA KUPANDIKIZA BETRI KWENYE MOYO



Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) ya jijini Dodoma imefanya upandikiza betri kwenye moyo kwa watu watatu.

Upandikizaji wa betri kwenye moyo ambao kitaalamu unaitwa _pacemakers_  _implantation_ unafanyika kwa watu wenye matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo na kusababisha mapigo ya moyo kuwa chini ya kiwango kinachotakiwa kwa mtu wa kawaida ambayo ni 60-100 kwa dakika.Wengi wao huwa ni chini ya 40.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Moyo wa BMH, Daktari Bingwa wa Moyo, Happiness Kusima, amesema leo kuwa BMH imefikisha upandikizaji kwa watu 18 toka huduma ianzishwe mwaka 2021.

"Jana tumepandikiza watu watatu (3), leo tumepandikiza watu wawili," amesema Daktari huyo Bingwa wa Moyo.

Dkt Happiness amesema upandikizaji huu umefanyika kwenye kambi ya Madaktari Bingwa wa Moyo wa BMH kwa kujengewa uwezo na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) ya jijini Dar es Salaam.

ZEGERENI FC MABINGWA LIKUNJA CUP


TIMU ya soka ya Zegereni Fc imetwaa ubingwa wa Likunja Cup baada ya kuifunga Visiga Veterans kwa mabao 2-0

Mchezo huo ulifanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Zegereni ulihudhuriwa na mashabiki wengi licha ya mvua kubwa kunyesha.

Washindi walipata seti ya jezi na mpira mmoja huku mshindi wa pili akijinyakulia jezi seti moja ambapo zawadi hizo zilitolewa na Mwenyekiti wa CCM Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka.

Nyamka amesema kuwa michezo ni ajira hivyo mashindano hayo ni moja ya utekelezaji wa ilani ya CCM hivyo kuwataka wadau wa michezo kuandaa michezo mingi.

Amesema kuwa mbali ya michezo kuwa ajira pia ni afya hivyo wananchi washiriki michezo na wahakikishe wanadumisha ulinzi na kuwaondoa vijana kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

Naye mwandaaji wa mashindano hayo Rashid Likunja ambaye ni mwenyekiti wa serikali ua mtaa wa Zegereni amesema kuwa jumla ya timu 12 zilishiriki mashindano hayo.

Likunja amesema mashindano hayo kwa mwaka huu ni mwaka wa 10 kuyaandaa ambapo mwakani zawadi zitaongezwa ili kuleta msisimko.

Wednesday, February 28, 2024

Taasis ya Digital Agenda for Tanzania Initiatives yasisitiza haki ya faragha na ulinzi wa taarifa binafsi Nchini.*


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Wataalamu kutoka Taasisi ya Digital Agenda for Tanzania Initiative imekutanaa pamoja na wadau kutoka Wizara ya habari, mawasiliano na teknolojia ya habari  wamekutana Jijini Dodoma kujadiliana kuhusu utetezi wa haki kidigitali.

Lengo la kikao hicho ni kutoa matokeo ya ripoti mbili zilizofanywa na Taasisi ya Digital Agenda Tanzania Initiative kuhusu utambuzi Kwa kutumia taarifa za kibayometriki,usajili wa laini za simu unaofanywa na Makampuni ya simu nchini.

Tafiti  imebainisha kuwa makampuni  ya simu nchini licha ya kufanya vizuri katika kutoa huduma lakini bado kuna mapungufu  katika kulinda haki ya faragha na ulinzi wa taarifa binafsi zonazowahusu wateja wao.

Akibainisha mapungufu hayo mkurugenzi mtendaji wa taasisi hiyo Peter Mmbando amesema kuwa ulinzi wa data, uhuru wa kujieleza pamoja na uendeshaji wake vilibainika kuwa ni moja kati ya mapungufu ya mitandao hiyo.

Mmbando amesema kuwa, elimu zaidi Kwa wananchi inapaswa ku ndelea kutolewa ili kuhakikisha taarifa zao zinakuwa salama pamoja na kuhakikisha wanaepukana na makosa ya kimtandao ambayo yamekuwa yakifanyika.

Kwa upande wake  Mtaalamu wa ulinzi wa taarifa binafsi Nchini Tanzania,Mrisho Swetu ameitaka jamii kuamka na kuwa mstari wa mbele katika kulinda taarifa zao. Amesisitiza kuwa taarifa binafsi nyeti za kibayometriki mfano alama za vidole zina athari kubwa endapo zitatumika vibaya.

Pia ameendelea kuhimiza wadhibiti na wachakataji wa taarifa binafsi Nchini kuboresha viwango vya ulinzi wa taarifa binafsi pamoja  na kuendelea kutoa elimu ya ulinzi wa taarifa binafsi kwa mujibu wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi,2022. Wadhibiti na wachakataji wanapaswa kuheshimu haki ya faragha na hyo itasaidia kuongeza uaminifu na wateja wao.

Kwa upande wa Jamii amesema,wadau wa serikali na sekta binafsi waendelee kutoa elimu kwa umma kuhusu haki ya faragha na ulinzi wa taarifa binafsi.Jamii inapaswa kupewa elimu ya kutosha kuhusu ulinzi wa taarifa binafsi pamoja na haki zao kama haki ya kuomba kufutwa kwa taarifa zako,haki ya kurekebisha,haki ya kupata fidia pale itakapotokea misingi ya sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi imekiukwa.

Aidha,ameendelea kusema, mafunzo hayo wamelenga kuyafikia makundi yote katika jamii, mikoa yote ambapo kwa upande wa watu wenye ulemavu wa kuona na kusikia wapo kwenye mpango wa kukutana na wataalamu wa lugha ya alama ili  kujua elimu hiyo itawafikiaje jamii hiyo ya watu wenye ulemavu. 

"Lengo ni kuikumbusha jamii matumizi sahihi  ya taarifa  binafsi,kujua haki zao ,lakini ni muhimu wafahamu kuwa taarifa zao binafsi zikitumika vibaya zinaweza kuleta madhara,lakini wafahamu kuwa endapo kutatokea  uvunjifu wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi basi ni wapi wanaweza kupeleka malalamiko yao" amesema Mrisho Swetu 

Naye, Afisa Mwandamizi Tume ya Haki za binadamu za Utawara Saidi Zuberi amesema mafunzo hayo yatakwenda  kumasaidia mwananchi kuweza kulinda  taarifa zake na kutambua haki za faragha. 

Pia ametoa wito kwa watoa elimu wa tume ya ulinzi wa data kuwa na miongozo itayoweza kutoa elimu ya haki ya faragha katika jamii .

WATANZANIA WATAKIWA KUENZI FALSAFA ZA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE






WATANZANIA wametakiwa kuenzi falsafa za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za Ujamaa na Kujitegemea kwani siyo umaskini bali ni kuwafanya wananchi kuwa na umoja ili kujiletea maendeleo.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Taifa Paul Kimiti wakati wa Kongamano la Maadili lililofanyika kwenye Shirika la (TATC) Nyumbu Kibaha.

Kimiti alisema kuwa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alisema kuwa taasisi hiyo ilianzishwa ili kuyaenzi yale aliyoyafanya hasa katika kujitegemea.

"Sisi ambao tunajua alichokuwa akikitaka Nyerere kuhusu uzalendo na kujitegemea na kudumisha umoja na amani lazima tuwakumbushe viongozi na vijana ili wazingatie falsafa hizo ili kuleta maendeleo,"alisema Kimiti. 

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Kikosi cha Nyumbu na Mkurugenzi wa Nyumbu Kanali Charles Kalambo alisema Shirika hilo ambalo ni maono ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere limepata mafanikio ikiwa ni pamoja na kubuni gari aina ya Nyumbu.

Kalambo alisema kuwa wanamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kulipatia Shirika la Nyumbu fedha kwa ajili ya kufanya shughuli zake mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya kiufundi.

Naye Kanali Ngemela Lubinga katibu mkuu mstaafu (NEC-CCM) siasa na uhusiano wa kimataifa akifundisha somo la uzalendo, itifaki na uadilifu alisema kuwa viongozi wanapaswa kuwa na moyo wa kujituma kwani ndiyo msingi wa kujenga jamii bora na yenye uzalendo.

Lubinga alisema kuwa viongozi wanapaswa kuwa na uadilifu ili kujenga jamii bora pia wawe wabunifu, moyo wa kujituma ili kuleta maendeleo kwa wananchi na awajali ili kuwa na mipango ya pamoja.

Balozi Mstaafu Meja Jenerali Anselm Bahati alisema kuwa ili kuwa na usalama mahali pa kazi kwa wafanyakazi lazima wafanyakazi wapate mafunzo ya namna ya kujilinda na kujikinga.

Bahati alisema kuwa wafanyakazi wakiwa na mazingira salama watakuwa na uwezo wa kuzalisha pia maslahi yao kuangaliwa ili kuepukana na afya ya akili inayotokana na msongo wa mawazo.

Naibu Katibu Mkuu wa Taasisi hiyo Neema Mkwachu alisema malengo ni kutoa elimu kwa wanafunzi kuanzia ngazi ya shule za msingi hadi vyuo juu ya falsafa za Nyerere ikiwemo uzalendo wa nchi.

Mkwachu alisema kuwa pia ni kuwa na klabu za Mwalimu Nyerere ambazo zitakuwa zinatakuwa pia na uwezo wa kutunza mazingira ambayo ni moja ya vitu alivyohimiza Hayati Nyerere 

Katibu wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani Abdul Punzi alisema kuwa ili kuenzi falsafa za Nyerere kwa kufungua Klabu ya Mwalimu Nyerere Nyumbu.

Punzi alisema kuwa uzalendo unapaswa kuanzia chini kabisa ili wananchi watambue misingi mizuri iliyoasisiwa na Nyerere na kuifanya Tanzania kuwa na umoja na mshikamano ambapo kongamano hilo lilidhaminiwa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Benki ya CRDB na NSSF.


Monday, February 26, 2024

*HISTORIA YAANDIKWA; JNHPP YAINGIZA MEGAWATI 235 GRIDI YA TAIFA*

📌 *Serikali yatekeleza ahadi kabla ya siku tatu*

📌 *Megawati 235 nyingine kuingizwa Machi, 2024*

📌 *Uzinduzi rasmi kufanyika mwezi Machi mwaka huu*

📌 *Dkt. Biteko asema hakuna kulala; vyanzo vipya kutekelezwa*

📌 *Mkandarasi apongeza usimamizi wa Dkt.Biteko*

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa megawati  2,115  umeanza kazi na kuingiza  megawati 235 katika gridi ya Taifa kupitia mtambo Namba 9. 

Hatua hii ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali kuwa mtambo huo ungeanza kuzalisha umeme tarehe 25 Februari 2024, ahadi iliyotimizwa siku tatu kabla kuanzia tarehe 22 Februari 2024  mtambo huo ulipoanza uzalishaji.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 25 Februari 2024 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa baadhi ya wakuu wa vyombo vya Habari na Wahariri katika eneo la mradi wilayani Rufiji mkoani Pwani ambapo wahariri hao walipata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ikiwemo Bwawa la kuhifadhi maji yatakayozalisha umeme, Tuta Kuu na mitambo ya umeme.

Ameeleza kuwa, kuingia kwa megawati 235 kwenye Gridi ya Taifa  kumeboresha hali ya upatikanaji umeme nchini na kupunguza upungufu wa umeme kwa zaidi ya asilimia 85.

Ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere unaendelea na ifikapo mwezi  Machi 2024 megawati nyingine 235 zitaingia katika gridi kupitia mtambo namba 8 na kufanya JNHPP kuingiza megawati 470 kwenye gridi na hivyo kupelekea nchi kuwa na ziada ya umeme ya megawati 70.

Amesema utekelezaji wa mradi huo ni jitihada za Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye alikuta mradi huo ukiwa na aslimia 33 na sasa  mradi huo unafikia mwisho.

Amesema, Dkt. Samia anaijali nchi kwa dhati na sasa mipango yake ya maendeleo haiangalii kipindi cha sasa tu bali miaka 30 hadi 40 ijayo na ndio maana ameshaagiza uendelezaji wa vyanzo vipya vya umeme ikiwemo Gesi, Maji na Nishati Jadidifu inayojumuisha Jua, Upepo na Jotoardhi.

Dkt. Biteko pia amepongeza juhudi za Serikali ya  Awamu ya Tano chini ya Hayati, Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wa kutekeleza mradi huo ambao ulianza kutekelezwa mwaka 2018.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameeleza kuwa, utekelezaji wa JNHPP hauifanyi Wizara ya Nishati na Taasisi zake kubweteka na kutegemea umeme kutoka mradi huo pekee bali kasi ya utekelezaji wa miradi mingine mipya inaendelea ikiwemo mradi wa Rumakali (222MW), Ruhudji (358) na miradi ya Jotoardhi ya Ngozi na Kiejo-Mbaka pamoja na mradi wa umeme Jua wa Kishapu (150MW).

Kuhusu utunzaji wa mazingira, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Wahariri wa Vyombo vya Habari kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa utunzaji wa mazingira ambao ndio unasababisha mabwawa ya umeme kuwa na maji ya kutosheleza kuzalisha umeme na pia kutoa elimu kuhusu athari za kuharibu vyanzo vya maji vinavyopeleka maji pia katika mabwawa ya umeme.

Kwa wananchi wanaozunguka maeneo  yenye mitambo ya kuzalisha umeme, Dkt. Biteko amesisitizaTANESCO ihakikishe hawapati changamoto ya umeme kwani hao ndio walinzi wa maeneo hayo na mradi unapofika katika eneo lolote lazima ubadilishe hali ya wananchi katika eneo husika kwa namna mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa huduma za kijamii.

Dkt. Biteko ameipongeza TANESCO na  kampuni ya usimamizi wa mradi ya TECU kwa utekelezaji na usimamizi madhubuti wa mradi ambao umewezesha kuingiza megawati 235 kwenye gridi.

Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso amesema kuwa, ujazo wa maji unaohitajika katika Bwawa la umeme la JNHPP ni mita za ujazo bilioni 32.7 na sasa kuna mita za ujazo bilioni 28 hivyo bado mita nne tu Bwawa hilo kujaa kabisa.

Amesema kuwa, makadirio ni kuwa mita nne zilizobaki zitajaa mwezi huu kupitia usimamizi madhubuti wa Bonde la Maji la Rufiji.

Ametoa wito kwa wananchi kutunza vyanzo vya maji na kutofanya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji pia wasichepushe maji kiholela.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema kuwa, mradi huo ni muhimu katika kutekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Pwani kuwa Mkoa wa kimkakati kwa kujenga viwanda vingi zaidi ambavyo kufanya kwake kazi kunategemea nishati ya umeme ya uhakika.

Amesema kuwa, mahitaji ya umeme mkoani Pwani ni megawati 130 lakini bado hayatoshelezi mahitaji hivyo mradi wa JNHPP kupitia kituo cha umeme cha Chalinze kitawezesha Mkoa huo kupata umeme wa uhakika ambao utachochea wawekezaji wapya.

Ameongeza kuwa, kwa sasa Mkoa wa Pwani una viwanda 1,533 ambapo  katika Serikali ya Awamu ya Sita viwanda 30 vinajengwa huku 17 vikiwa ukingoni kumalizika hivyo mradi wa JNHPP ni muhimu katika kufanya viwanda hivyo kufanya uzalishaji.

Meneja Mradi kutoka kampuni zinazotekeleza mradi huo (Arab Contractors na Elsewedy Electric) Mohamed Zaky, amesema kuwa kampuni hiyo inaona fahari kufikia hatua hiyo ya uzalishaji na kwamba nia yao ni kutimiza ndoto ya Tanzania kuzalisha megawati 2115 kupitia mradi wa JNHPP.

Aidha, amempongeza Dkt. Doto Biteko kwa msukumo anaoutoa kwa wakandarasi hao ili kutekeleza mradi kwa wakati na pia kwa kuusimamia kwa karibu mradi husika.

Viongozi wengine walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ni  Mkuu wa Wilaya ya Rufiji, Meja Edward Gowele, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Mteule Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga,  Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Dkt. Rhimo Nyansaho na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.