Monday, July 10, 2023

MHE.MASANJA AFANYA MKUTANO WA HADHARA SENGEREMA, AGUSA MAKUNDI MAALUM

 


MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja amekabidhi baiskeli tano zenye thamani ya shilingi milioni tatu kwa wananchi wenye ulemavu wa miguu Wilayani Sengerema na kuahidi kuwalipia bima ya afya, ikiwa ni mwendelezo  wa ziara yake ya kukutana na makundi maalum katika Jamii Mkoani Mwanza. 


Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika eneo la Stendi ya zamani Mhe. Masanja amesema Serikali ya Awamu Sita inayoongozwa na Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati ya kutatua changamoto za makundi maalum yasiyojiweza katika jamii hivyo msaada huo ni utekelezaji wa ilani ya CCM.


Mhe. Masanja amewaelekeza Madiwani na viongozi wengine wa Serikali kuibua wananchi wenye changamoto mbalimbali za ulemavu ili Serikali iwafikie na kuwasaidia.


"Kama kuna wananchi huko hawawezi kutembea wengine mmewaficha ndani, na kama kuna watoto wadogo hawawezi kwenda shule waleteni Serikali itawahudumia" Mhe. Masanja amesisitiza.


Aidha, Mhe. Masanja amewataka wananchi kuhakikisha wanaiunga mkono Serikali na kuipigia kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu unaokuja. 


Katika mkutano huo, Mhe. Masanja amesikiliza changamoto za baadhi ya wananchi kuhusu kero ya watumishi wa  maliasili kukamata baiskeli na pikipiki za wananchi, kero za maji, kero ya uhaba wa vifaa vya kujifungulia katika vituo vya afya,ardhi, uhaba wa walimu kero za  wafanyabiashara ndogondogo.


Mhe. Masanja ameahidi kuziwasilisha kero hizo katika Sekta husika na kufanyia kazi kero zinazohusu Sekta ya Maliasili na Utalii.

UWEKEZAJI BANDARI MANUFAA UCHUMI WA NCHI

Halmashauri kuu ya ccm Taifa ( NEC) imepokea na kujadili kwa kina taarifa ya makubaliano ya Uwekezaji na uendeshaji wa bandari na kuazimia kwamba Uwekezaji na uendeshaji wa bandari hiyo ni kwa manufaa ya uchumi wa Nchi pamoja na utekelezaji wa vitendo vya Ilani ya CCM ya Mwaka 2020 - 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma katibu wa Halmashauri kuu ya Ccm Itikadi na Uenezi Bi Sofia Mjema amesema halmashauri kuu ya Ccm imekutana Katika kikao Chake Cha kawaida chini ya mwenyekiti wa Ccm na RAIS wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasani.

Mjema amesema kikao hicho kimeazimia kwamba serikali iongeze kasi ya kutoa Elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo Katika makubaliano ya Uwekezaji na uendeshaji wa bandari.

Sunday, July 9, 2023

VYAMA VYA SOKA VYATAKIWA KUWA NA UTAWALA BORA





VYAMA vya Soka Nchini vimetakiwa kuzingatia utawala bora ili kuhakikisha sheria miongozo na taratibu za mpira zinafuatwa ili soka liweze kuimarika na kupata timu na wachezaji bora.

Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mkurugenzi  wa Sheria Habari na masoko kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Boniface Wambura wakati wa semina elekezi kwa Kamati Mbalimbali za Chama Cha Soka Wilaya ya Kibaha (KIBAFA).

Wambura alisema kuwa utawala bora kwenye mpira unasaidia kuhakikisha mpira unachezwa kwa kuzingatia taratibu za mpira zilizowekwa na chama husika.

"Utawala bora unaonyesha kila mtu anawajibika kwa nafasi yake pasipo kuingiliana kwenye majukumu yao ya kiutendaji,"alisema Wambura.

Alisema kuwa mpira una taratibu zake hivyo ili mpira uchezwe lazima sheria zake zifuatwe kwani tofauti na hapo klabu na nchi haitaweza kuwa na timu wala wachezaji wazuri.

"Kwa sasa mambo yamebadilika tofauti na zamani ambapo kulikuwa na migogoro mingi lakini kwa kuwa mambo yanaendeshwa kwa weledi na mpira umebadilika timu zimekuwa nzuri na wachezaji wana ubora,"alisema Wambura.

Aidha alisema kuwa mpira umekuwa na hadhi kutokana na kuwekwa mifumo mizuri ambapo kila mtu anafanya kazi kwa nafasi yake na huo ndiyo utawala bora.

Kwa upande wake mwenyekiti wa KIBAFA Robert Munis alisema kuwa lengo la kuandaa semina elekezi kwa kamati hizo ni kuwaelekeza viongozi kila mmoja kujua mamlaka yake.

Munis alisema kuwa moja ya changamoto zinazojitokeza ni baadhi ya viongozi kutofahamu majukumu yao hivyo kuwa na mwingiliano kiutendaji.

Awali katibu wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) Mohamed Masenga alisema kuwa wao wanasimamia wilaya ili kuhakikisha mipra unachezwa.

Masenga alisema kuwa wanakipongeza chama hicho kwa kuandaa semina hiyo na kuvitaka vyama hivyo kuandaa semina kama hizo ili kuwajengea uwezo viongozi.

Saturday, July 8, 2023

RAIS DK SAMIA SULUHU HASSAN MGENI RASMI MIAKA 60 YA JKT

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Amri jeshi mkuu  Mhe, Dkt,Samia Suluhu  Hasani anatarajiwa kuwa mgeni rasmi Katika maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la kujenga Taifa JKT.

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Mhe, Innocent Bashungwa wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

Mhe, Bashungwa amesema kilele Cha maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT kinatarajiwa kuadhimishwa rasmi julay 10 2023 Katika viwanja vya Jamuhuri jijini Dodoma ambapo wageni mbalimbali watashiriki kutoka ndani na nje ya Nchi.

Aidha amewaalika viongozi wote wa serikali, taasisi mbalimbali za umma na binafsi,watumishi,wananchi wa mkoa wa Dodoma na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kuhudhuria siku ya kilele Cha maadhimisho Hayo.

Hata hivyo Maadhimisho Hayo yanatarajiwa kuanza saa kumi na Mbili Asubuhi ambapo kutakuwa na maonyesho ya vifaa mbalimbali vya SUMA JKT, burudani za ngoma kutoka vikundi vya JKT na wasanii Mbalimbali.

MHE. MARY MASANJA AGUSA MAKUNDI MAALUM KWA KUYATEMBELEA NA KUTOA MISAADA MBALIMBALI


MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja ameanza kuyagusa makundi maalum yasiyojiweza kwa kutoa misaada itakayowasaidia kutatua changamoto zao wilayani Magu mkoani Mwanza .

Hatua hiyo ni moja ya utekelezaji wa majukumu yake na pia ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa UWT Taifa, Ndugu Mary Chatanda pamoja na Naibu wake Ndugu Zainabu Shomari ya kuwataka  viongozi wa Chama cha Mapinduzi kuwa mfano wa kuigwa kwa  kuyaangalia makundi maalum yasiyojiweza na kutoa misaada mbalimbali itakayowasaidia kutatua changamoto zao.

Katika kutekeleza agizo hilo Mhe.Masanja ametembea nyumba kwa nyumba na kutoa msaada wa baiskeli tano za walemavu wa miguu zenye thamani ya shilingi milioni 3.2, majiko matano ya gesi yenye thamani ya shilingi laki tatu, fedha taslimu laki moja na nusu kwa kila mhitaji pamoja na kuahidi kuwalipia bima ya afya watoto hao wenye ulemavu katika  Tarafa tatu za Wilaya ya Magu ambazo ni Sanjo,Itumbili na Kahangara.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhe. Masanja amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ni Serikali ya vitendo  na moja ya vitendo ni kutembelea kila jamii kuangalia changamoto za watoto, kinamama na vijana na kuzitatua.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali  ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu ni Serikali pekee na Rais pekee itayoweza kuwavusha watanzania kutoka uchumi wa chini mpaka juu.

Naye, Mericiana Faustine ambaye ni miongoni mwa wanufaika wa msaada huo ametumia fursa hiyo kutoa shukrani zake kwa  Rais Samia Suluhu Hassan huku akiahidi kuendelea kuiomba Serikali kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum na maeneo mengine

Kwa upande wake Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Magu, Loyce Mabula amewataka  Watanzania kumuunga mkono Rais Samia kwa kuwa na viongozi wanaojitolea kutatua matatizo ya watu wenye mahitaji maalum.

Diwani wa Viti Maalum, Mhe. Diana Philemon amemshukuru Mhe. Masanja kutoa misaada hiyo.

Friday, July 7, 2023

SENYAMULE AAGIZA WAZEMBE KUCHUKULIWA HATUA ZA KISHERIA


MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ametaka hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa watumishi wote ambao wamebainika kuhusika na vitendo vya ubadhirifu wa rasilimali au fedha za umma na kusababisha hoja za ukaguzi kwa uzembe.

 Akizungumza katika Kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Senyamule amekemea vikali tabia ya baadhi ya watumishi kutotimiza majukumu na wajibu wao wa msingi kwa makusudi hali inayopelekea kukithiri kwa hoja za ukaguzi zisizokuwa na majibu.

 "Kila mmoja atimize wajibu wake, hoja nyingi hapa zinatokana na uzembe wa baadhi ya watumishi kutotimiza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria, wanashindwa kuambatisha nyaraka za msingi zinazohitajika hali inayopelekea kukithiri wa hoja za ukaguzi. Senyamule ameonya.

Amesema ili Halmashauri hiyo kuondokana na hoja nyingi ni lazima Kamati ya Fedha kukutana kila mwezi na kuwa na agenda ya kudumu ya kujadili mwenendo wa namna ya kujibu hoja za Mkaguzi wa ndani na zile za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na kuchukua hatua stahiki pale inapobainika uzembe wa aina yoyote.

Senyamule pia, ametoa rai kwa madiwani hao kuhakikisha kuwa fedha zinapelekwa kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kuzingatia mgawanyo wa asilimia 40 na asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mujibu wa Sheria. Pia amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino Dkt. Semistatus Mashimba kuhakikisha mapato ya Serikali yanakusanywa kikamilifu na kudhibiti upotevu.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo ya mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022  kwa Halmashauri ya Chamwino, Bw. Chambi Ngelela Mkaguzi Mkuu wa Nje amesema Halmashauri hiyo ilipata hati inayoridhisha. 

"Halmashauri  ya Wilaya ya Chamwino ilikuwa na hoja 61 ambapo hoja 13 zimeweza kufungwa na kusalia na hoja 48 ambazo utekelezaji wake unaendelea." Amesema Bw. Ngelela.

Aidha Senyamule katika hatua nyingine amewataka Viongozi hao wa ngazi ya Wilaya kuendelea kutunza Mazingira na kuanza maandalizi ya kuoteshea vitalu vya miche ya miti kwa ajili ya  kupanda wakati wa msimu wa mvua unapokaribia ili kuwe na miche ya kutosha kwa kila Halmashauri kupanda miti milioni moja na laki tano kwa mwaka kwa mujibu wa maelekezo ya Serikali.

"Katika kuendelea kukijanisha Mkoa wetu na kutunza Mazingira tuanze mapema maandalizi ya kuandaa vitalu vya miche na kila wilaya iwe na Miche ya kutosha isiyopungua milioni moja na laki tano,"amesema Senyamule 

"Hapa nisisitize kuwa katika kila wilaya nitakayofanya ziara kuanzia mwezi wa nane nitakagua vitalu hivyo vilevile hakikisheni mnatenga maeneo kwa ajili ya kunufaika na biashara ya hewa Ukaa na kila Wilaya angalau iwe na maeneo matatu kama tulivyokubaliana hapo awali". Amesisitiza  Senyamule

Thursday, July 6, 2023

"ELIMISHENI WANAWAKE JUU YA FURSA ZA MIKOPO YA HALMASHAURI" MHE. MASANJA

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary  Masanja amewataka wana Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Mkoani Mwanza kuelimisha wanawake na vijana kuhusu fursa za mikopo ya Halmashauri ili waweze kujiinua kiuchumi. 

Mhe. Masanja ameyasema hayo jana katika Kikao cha Baraza la UWT Wilaya ya Nyamagana kilichofanyika katika Ofisi za CCM jijini Mwanza.

"Niwaombe wakinamama turudi chini tuwaelimishe wanawake wengine kuhusu mikopo hii ya Halmashauri na kuwasimamia kutekeleza miradi yao ili wajiinue kiuchumi" Mhe. Masanja alisisitiza. 

Aidha, Mhe. Masanja amewataka wakinamama wa UWT  kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi juu ya mafanikio ya Serikali kuhusu Utekelezaji wa Miradi mbalimbali ili kuhakikisha Chama kinapata ushindi katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaokuja. 

"Sasa tunaenda kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa tusilale wakinamama sisi ni wenye kura sisi ndio wa kuzitafuta kura usiku na mchana kuhakikisha chama chetu kinaibuka kinara" Mhe. Masanja ameongeza.

Amesema ni lazima kutembea kifua mbele kutokana  na miradi iliyotekelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kusisitiza kwamba anastahili kupewa maua yake.

Katika kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kutangaza utalii,Mhe. Masanja wajumbe wataanza kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii hapa nchini.

Mhe. Masanja anaendelea na ziara yake jijini Mwanza kwa ajili  ya kukutana na makundi mbalimbali ya kijamii yenye uhitaji maalum  ambayo yanajihusisha na biashara mbalimbali.