Thursday, June 15, 2023
SERIKALI NA MAPAMBANO DHIDI YA MAGUGU MAJI
RC KUNENGE AZINDUA M-MAMA
MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge leo Juni 15, 2023 amezindua Mpango wa Usafiri wa Dharura kwa Mama Wajawazito, Wanawake waliojifungua na Watoto Wachanga ujulikanao kama M-Mama.
Akizindua Mpango huo katika Ukumbi wa Baraza la wakunga na uuguzi Kibaha, Hafla iliyohudhuriwa na Viongozi wote wa Mkoa huo Kunenge amesema:- M -Mama ni Mpango ambao Mhe Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameanzisha ili kuokoa maisha ya Mama na Mtoto. Hivyo amewataka Viongozi wote wa Mkoa Kuweka kipaumbele na kuhakisha inafanikiwa.
Ameeleza mpango huo unaendea sambamba na lishe, Kuhudhuria kliniki na wakati wa kujifungua kuwahi kituo cha afya kwa wamama Wajawazito na Watoto."Mpango huo ni mnyororo wa thamani wa uzazi" Ameeleza Kunenge.
Amewataka Viongozi wote wa Mkoa wa kuhakikisha M Mama inafanikiwa. "Suala hili liingizwe kwenye viashiria vya upimaji utendaji kazi wa Watumishi kila mmoja kwenye eneo lake ambapo kila mtu atapimwa navyo" amesema Kunenge.
DKT.JAFFO ATOA KONGOLE KWA WADAU WA MAZINGIRA
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amepongeza wadau kwa juhudi za kuhifadhi mazingira na kuonesha nia ya kufanya Biashara ya Kaboni nchini.
Amesema hayo alipokutana na Meneja wa Shirika linalohudumia wakimbizi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) la Denmark Bi. Jo Povey katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma leo Juni 14, 2023.
Dkt. Jafo amesema Serikali inatambua juhudi za wadau hao ambao wanafanya shughuli za kuhifadhi mazingira kwa kupanda miti katika kambi za wakimbizi zilizopo mkoani Kigoma na wananchi wanaozunguka kambi hizo.
Amesema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Raia sasa inaendelea kuzifanyia kazi Kanuni na Mwongozo wa Biashara ya Kaboni ili wananchi wanufaike na biashara hiyo.
Waziri Jafo amesema changamoto ya ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa ni ni kubwa katika maeneo mbalimbali hapa nchini hali inayochangia uharibifu wa mazingira na ukame na kusababisha upungufu wa maji na chakula.
Hivyo, amewashukuru wadau hao kwa kuonesha nia ya kuwekeza katika nishati mbadala ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza kasi ya ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
“Tunafurahi tunapoona wadau kama ninyi mnashiriki kikamilifu katika kulinda mazingira na tunaona juhudi zenu zE kupanda miti, kutuletea nishati mbadala na kuona namna ya kusaidia katika uwekezaji wa hewa ya ukaa na kwqa upande wetu kama Serikali tunaendelea kuhamisha wananchi wahifadhi mazingira,"amesema.
Kwa upande wake Meneja wa shirika hilo Bi. Jo amesema kipaumbele chao tangu mwaka 2021 ni kushirikiana na Serikali katika suala la upandaji wa miti ili kuhifadhi mazingira.
Amesema kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) pamoja na Halmashauri ya Kibondo mkoani Kigoma wanapanda miti katika kambi za wakimbizi na maeneo ya jirani ili kurudisha hali ya mazingira iliyokuwepo awali.
“Kukiwa na mkusanyiko wa watu hususan wakimbizi wakikaa katika eneo moja lazima wawe na mahitaji kama ya kupikia na lazima wakate miti kwa ajili ya kuni kwa hiyo ni lazima kupanda tena miti, hivyo tumeona tufanye uhifadhi,“ amesema Bi. Jo
Naye Meneja wa masuala ya uchumi wa shiriki hilo Bw. Alfred Magehema amesema kuwa kwa sasa wanatekelekeza mradi wa mkaa mbadala ambao unasambazwa katika kambi za wakimbizi.
Amesema katika kambi ya Nduta zinazalilishwa tani zaidi ya mbili kwa siku ambazo zinasaidia matumizi ya kila siku ya wakimbizi hivyo kusaidia kupunguza ukataji ovyo wa miti.
Pia, amepongeza Serikali ya Tanzania kwa kulipa uzito suala la Biashara ya Kaboni hatua ambayo inasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira huku akisema shirika linatoa hamasa ya kuhifadhi misitu.
BMH YAPANDIKIZA UUME KWA MARA YA KWANZA NCHINI
HOSPITALI ya Benjamin Mkapa (BMH)kwa kushirikiana na chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo nchini (TAUS) pamoja na dkt. Bingwa kutoka Ufaransa kwa mara ya kwanza wamefanya upasuaji wa kupandikiza uume kwa watu wawili ambao uume ulishindwa kufanya kazi kutokana na magonjwa mbalimbali.
Akizungumza baada ya kukamilisha upasuaji Dkt. Remidius Rugakingira daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa mkojo na wanaume kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa amesema kuwa upasuaji huu umefanyika kwa mara ya kwanza nchini.
“Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanya upasuaji wa aina hii kilichofanyika hapa ni kuweka vipandikizi maalumu vitakavyo wezesha uume kurudi katika hali yake upasuaji huu tumeshirikiana na chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo pamoja na daktari bingwa wa mfumo wa mkojo kutoka Ufaransa na tumefanikiwa katika hilo,” alieleza Dkt. Rugakingira
Dkt. Rugakingira aliendelea kwa kusema kuwa huu ni wito kwamba Hospitali ya Benjamin Mkapa inajali afya ya wanaume na upasuaji kama huu unaweza kufanyika Tanzania.
Kwa upande wake Dkt. Liuba Nyamsogolo ambae ni kiongozi wa chama cha madaktari bingwa wa upasuaji wa mfumo wa mkojo (TAUS) amesema kuwa wamefikia hatua hii kutokana na uwepo wa watu wengi wenye matatizo ya nguvu za kiume nchini na Afrika kwa ujumla.
“Moja wapo ya dhumuni ya TAUS ni kuendeleza wataalam nchini kwa kushirikiana ma wataalam kutoka nje ili kuleta teknolojia inayopatikana duniani nchini Tanzania na kutibu magonjwa kama haya kwa wale wenye matatizo,” alisema Dkt. Nyamsogolo.
Msemaji wa BMH Bw. Jeremiah Mbwambo ameeleza "Hospitali ya BMH imekua Hospitali ya kwanza nchini kufanya upasuaji wa kuweka vipandikizi kwenye uume kwa wagonjwa wenye matatizo ya nguvu za kiume, serikali ya awamu ya sita imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika Hospitali ya Benjamin Mkapa kwa kuiwezesha teknolojia za kisasa za matibabu ili kuwapatia matibabu thabiti wananchi"
Wednesday, June 14, 2023
*DKT. BITEKO ASISITIZA JENGO JIPYA MADINI KUKAMILIKA KWA WAKATI*
MKANDARASI wa Jengo Jipya la Wizara ya Madini Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ametakiwa kuongeza kasi ili kukamilisha jengo hilo kwa wakati.
Rai hiyo, imetolewa leo Juni 13, 2023 na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa jengo hilo linaloendelea kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Hadi kukamilika kwake Jengo hilo litagharimu shilingi bilioni 22.8 na linatarajiwa kukabidhiwa ifikapo mwezi Septemba, 2023.
Wengine walioshiriki katika ziara hiyo ni pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Naibu Katibu Mkuu Msafiri Mbibo, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania ( GST) Dkt. Mussa Budeba, Kaimu Katibu Mtendaji wa TEITI Joseph Kumburu na watumishi wa Wizara ya Madini.
Tuesday, June 13, 2023
SENYAMULE AAGIZA CHEMBA KUJIPANGA UPYA
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema hajaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Shule Mpya ya Msingi katika Kijiji cha Magungu Kata ya Mpendo Wilaya ya Chemba na kukemea vikali uongozi wa Kijiji kukusanya fedha kwa wananchi bila kufuata utaratibu.
Senyamule ameyasema hayo leo tarehe 13/06/2023 mara baada ya kufanya ziara yakukagua utekelezaji wa miradi ya boost katika Wilaya ya Chemba.
"Sijaona dhamira ya dhati katika ukamilishaji wa mradi huu kwa muda tuliokubaliana wa tarehe 30/6/2023, tumekubaliana sote kuwa miradi hii ikamilike kwa wakati lakini leo nimesikitishwa sana hatua hii ya ujenzi ambao uko katika hatua za awali" Senyamule amefafanua
Amesema hayuko tayari kuona dhamira njema ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea wananchi maendeleo hususan katika nyanja ya elimu haifikiwi kutokana na watu wachache kutotimiza wajibu wao.
"Katika mradi huu Chemba hamjafika hata asilimia 20 na mna siku 18 zimesalia, fedha zilitolewa kwa wakati mmoja nchi nzima, Wilaya nyingine za Mkoa wa Dodoma wako katika hatua za upauji, siko tayati kumuangusha Mhe. Rais, ujenzi ufanyike mchana na usiku" Senyamule ameagiza.
Katika hatua nyingine Mhe. Senyamule amekemea vikali utaratibu unaotumiwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Magungu Bw. Bernard Kapaya kuchangisha fedha wananchi bila kibali cha Mkuu wa Wilaya.
“Naomba kuwakumbusha kuwa Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya, vyumba vya madarasa ya awali na msingi, nyumba za walimu na ujenzi wa Vyoo. Wananchi wasishurutishwe kuchangia fedha, wachangie kwa hiari yao wenyewe na utaratibu ufuatwe ikiwa ni pamoja na kuambatanisha muhtasari wa mkutano wa Serikali ya Kijiji na barua iliyopitishwa kwa Mkurugenzi kwenda kwa Mkuu wa Wilaya. Ni kinyume kuchangisha fedha bila kufuata utaratibu huo” Senyamule ameonya
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chemba Bw. Gerald Mongella amesema kumekuwa na ucheweshaji kutokana na kusuasua kwa mchango wa nguvu za wananchi hali iliyopelekea ucheleweshaji wa upatikanaji wa madini.
Mkoa wa Dodoma kupitia mradi wa Boost umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10.6 kwa ajili ujenzi wa Shule mpya 16, vyumba vya madarasa ya msingi 163, madarasa ya awali 16, ujenzi wa vyoo 106, nyumba za walimu 03 na darasa 01 la elimu maalumu. Wilaya ya Chemba imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.3.
Katika ziara yake Mhe. Senyamule amekagua maendeleo ya ujenzi wa Shule mpya ya Magungu, Ujenzi madarasa katika Shule ya Msingi Birise, ujenzi wa madarasa Lahoda na Ujenzi wa shule mpya Handa ‘B’.
Saturday, June 10, 2023
PWANI BINGWA VIWANDA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dkt Samia Suluhu Hassan ameutaja Mkoa wa Pwani kuwa bingwa viwanda nchini.
Rais Dkt. Samia ametoa kauli hiyo Juni 9, 2023 wakati akiwatambulisha Wakuu wa Mikoa waliohudhuria kwenye mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu jijini Dar es Saalam.
Katika Mkutano huo Rais amewataka wakuu wa mikoa nchini kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya kuvutia wawekezaji na kwamba ataandaa tuzo kwa ajili ya mkoa kinara wa ukusanyaji mapato.
Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda 1522 kati ya hivyo vikubwa ni 117 na 120 vya kati.