Wednesday, March 1, 2023

WATENDAJI KATA WAKABIDHIWA PIKIPIKI

HALMASHAURI ya wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani imewapatia Pikipiki watendaji wa Kata tano ili kuondoa changamoto ya kushindwa kuyafikia maeneo ambayo hayafikiki kirahisi.

Akikabidhi Pikipiki hizo kwa watendaji hao wa Kata katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Mbunge wa Kibaha Vijijini Michael Mwakamo amewataka watendaji kuzitumia pikipiki hizo kama ilivyokusudiwa na serikali na siyo kwenda kuzifanya boda boda.

Mwakamo amesema kuwa pikipiki hizo ni kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuondoa changamoto ya usafiri kwa watendaji kata ili kuwarahisishia majukumu yao. 

"Niwasihi watendaji waliopewa pikipiki leo mkazitumie kama ilivyokusudiwa na tusizikute zimebeba abiria mtaani maana siyo nia ya kukabidhiwa bali ni kutekeleza majukumu ya kazi zenu,"amesema Mwakamo.

Amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kuhakikisha wanawasaidia kwenye matengenezo na kuwawekea mafuta pikipiki hizo kwani ni vyombo vya kazi na wasivitumie kama vyombo binafsi. 

Awali Mwakamo aliishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi ya kutoa vitendea Kazi kwa watendaji wa ngazi zote Ili kurahisisha utendaji kazi kwa watumishi wa Umama.Kata zilizopokea pikipiki ni Soga, Magindu, Kwala, Gwata na Dutumi ambazo ni kata zilizopo pembezoni mwa Halmashauri.

WALIMU KUZAWADIWA VIWANJA



KATIKA kuhakikisha wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne hawapati sifuri Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amesema itatoa viwanja kwa walimu shule zao zitakazofanya vizuri.

Akizungumza kwenye kikao cha wadau wa elimu kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha kilichofanyika Kibaha alisema kuwa kuna changamoto katika ufuaulu na masomo ya Sayansi.

John alisema kuwa lengo ni kuondoa asilimia 50 ya wanafunzi ambao wanashindwa kuendelea na masomo kutokana na kutofanya vizuri kwenye mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne.

"Tutatoa viwanja kwa walimu ambao watafanya vizuri kwa kuongeza ufaulu ambapo tungetamani kusiwe na daraja sifuri na daraja la nne kwani madaraja haya yanawafanya wasiweze kuendelea na masomo tunataka angalau kuanzia daraja la tatu na kupanda juu,"alisema John.

Alisema kuwa mbali ya kutoa viwanja pia kutakuwa na motisha mbalimbali zitatolewa ikiwemo fedha taslimu kwa walimu watakaofanya vyema na mkazo utawekwa kwenye masomo ya Sayansi ambayo matokeo yake siyo mazuri.

"Pia tunataka Mwalimu anapaswa kuhakikisha mwanafunzi katika somo lake apate alama C na kama atashindwa kufikia hapo itabidi aulizwe changamoto ni nini,"alisema John.

Aliwataka wazazi na wadau wa elimu kushirikiana na shule ili kufanikisha kuondoa sifuri kwenye shule za sekondari zilizokwenye Halmashauri ya Mji Kibaha.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri Musa Ndomba alisema kuwa uongozi wa shule ukabili changamoto na siyo kulalamika hata kwa mambo yaliyo ndani ya uwezo wao.

Ndomba alisema kuwa watahakikisha mipango na mikakati iliyowekwa wanaitekeleza ili kuondoa matokeo mabaya kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya Sekondari ili kupata wasomi watakaoshiriki kwenye uchumi ikizingatiwa mkoa wa Pwani ni wa viwanda.

Awali ofisa Elimu Halmashauri ya Mji Kibaha Rosemary Msasi alisema kuwa ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne kwa kipindi cha miaka mitano 2018 hadi 2022 umeongezeka.

Msasi alisema kuwa ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 7.89 kwa kutoka asilimia 84.4 hadi asilimia 92.2 na ule wa kidato cha sita kutoka asilimia 99.4 hadi asilimia 100.9.

Baadhi ya walimu wakuu ambao shule zao zilifanya vizuri walisema kuwa kikubwa ni ushirikiano uliopo baina ya walimu wazazi na wanafunzi na Halmashauri.

Kikao hicho cha wadau baadhi ya walioshiriki ni pamoja na kamati ya usalama Wilaya, maofisa elimu wa Kata, watendaji wa kata, wakuu wa shule za msingi na sekondari.

Mwisho. 

Tuesday, February 28, 2023

IRUWASA YAONGOZA KUFUNGA MITA ZA MAJI KABLA YA MALIPO

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAMLAKA ya Maji na Usafi wa Mazingira Iringa (IRUWASA) imevunja rekodi kwa kuongoza nchini kwa kufunga mita 6,752 za malipo ya Maji Kabla ambazo zimekuwa suluhisho na kupunguza idadi ya wadaiwa sugu wa ankra za maji.

Akizungumza Jijini Dodoma Mkurugenzi Mtendaji wa IRUWASA, David Pallangyo amesema, Mamlaka hiyo iliyoanza daraja C hadi sasa ipo daraja A na inajitegemea gharama za matengenezo na uendeshaji na sehemu ya uwekezaji, imefanikiwa katika eneo la TEHAMA kwa kufunga mita za malipo kabla kwa wateja hao.

Pallangyo amesema kuwa kutokana na kufunga mita za malipo kabla kwa viongozi wa serikali na taasisi mbalimbali, kumepunguza ongezeko la madeni ya watumiaji maji bila kulipa na kubaki deni la shilingi bilioni mbili ambalo wadaiwa wengi ni watu wa kawaida.

Amesema kuwa mamlaka hiyo pia imevuka lengo la Sera ya Maji ya 2002 na Ilani ya CCM ya kutoa huduma ya usambazaji maji kwa mji wa Iringa na maeneo ya pembezoni kwa kuunganisha wateja 40,459 sawa na asiimia 97 ya wakazi ambazo ni zaidi ya asilimia 95 zinazoelekezwa kwenye sera na Ilani.

Aidha amesema kuwa katika mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia IRUWASA inakusudia kutekeleza mradi mkubwa wa uboreshaji huduma ya majisafi na majitaka katika manispaa ya Iringa, miji ya Kilolo pamoja na baadhi ya vijiji kando ya bomba la maji litakapopita.

"Mradi huu unalenga kuanzisha chanzo kipya katika mto Mtitu uliopo Wilaya ya Kilolo utaongeza upatianaji wa maji ya kutosha kwa miaka 20 ijayo na utaongeza utoaji wa majitaka zaidi ya asilimia 30 ya wakazi wa Iringa kutoka asilimia 6.8 za sasa,"amesema Pallangyo.

Ameongeza kuwa mradi huo utekelezwa kwa ushirikiano wa serikali kupitia mkopo wenye masharti nafuu kutoka serikali ya Korea wa dola za Kimarekani milioni 88.4 utaanza kutekelezwa Mei 2023 na ujenzi utaanza Aprili 2024 na utakamilika 2027.

Amesisitiza kuwa mradi utakapokamilika huduma za maji safi na salama kwa miji ya Iringa, Kilolo na Ilula zitafikia asiimia 100 kwa saa 24 kwa siku saba.

Jumla ya wananchi 456,010 watanufaika na huduma ya majisafi hadi mwaka 2045, huku wananchi 141,543 watanufaika na huduma ya uondoaji majitaka na Watanzania 6,455 watanufaika na kazi za mikataba na utachangia uchumi na ustawi wa jamii. 


Thursday, February 23, 2023

MAMLAKA YA SERIKALI MTANDAO KUONGEZA UWEZO WA MAWASILIANO


Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MAMLAKA ya serikali Mtandao (eGA) imepanga kupanua uwezo wa Mtandao wa mawasiliano serikalini ( Government Network) na kuufikisha wilaya zote nchini Ili kurahisisha utekelezaji wa jitihada za serikali Mtandao na kuwafikishia huduma wananchi wote popote walipo.

Hayo yamesemwa na Mkurugezi mkuu wa mamlaka ya serikali mtandao Mhandisi Benedict Ndomba wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa mamlaka hiyo.

Ndomba amesema kuwa mfumo wa ubadilishaji taarifa serikalini imewezesha zaidi ya taasisi 50 kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo na amezitaka taasisi za umma ambazo hazijaunganishwa katika mfumo huo ziunganishwe Ili ziweze kubadilishana taarifa na taasisi nyingine pale inapohitajika.

"Jumla ya taasisi 200 zinatumia mfumo wa ofisi Mtandao kwa ajili ya kurahisisha utendaji kazi katika taasisi za umma pia umesaidia kupunguza matumizi ya karatasi kutunza mazingira na kuokoa fedha za serikali,"alisema Ndomba.

Serikali mtandao ni matumizi ya Teknolojia ya habari na mawasiliano ( TEHAMA) Katika utendaji kazi wa taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa wananchi wenye lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi Katika taasisi ya umma pamoja na kuboresha utoaji huduma kwa umma Ili huduma hizo zipatikane kwa urahisi haraka na gharama nafuu. 

WASIOENDELEZA ARDHI KUNYANGANYWA

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete amezitaka Serikali za Vijiji kuorodhesha majina ya wawekezaji ambao wamehodhi ardhi bila kuiendeleza ili irudishwe kwa ajili ya matumizi mengine.

Aliyasema hayo alipokuwa kwenye ziara ya kwenye Kata ya Lugoba Halmashauri ya Chalinze kuzungumza na wananchi kutatua kero na changamoto kwenye Jimbo la Chalinze ambapo yeye ndiyo Mbunge wa Jimbo hilo.

Ridhiwani alisema kuwa maeneo mengi aliyopita kikiwemo Kijiji cha Makombe  kumekuwa na malalamiko mengi toka kwa wananchi juu ya baadhi ya maeneo yaliyoombwa na wawekezaji hayajaendelezwa na kuwa mapori.

"Vijiji na Vitongoji orodhesheni majina ya wawekezaji wote walio katika maeneo yenu ambao hawajaendeleza ardhi waliyoiomba kufanya uwekezaji lakini wameiacha bila kuiendeleza kwani huo siyo utaratibu ni vema wakanyanganywa na kupewa watu wengine ili kuyatumia kuleta maendeleo,"alisema Ridhiwani.

Alisema kama kuna maeneo mnaona yametelekezwa na wawekezaji wasipate shida wanachotakiwa viongozi kupitia mikutano mikuu ni kutoa hoja na kuandikwa muhutasari kisha upelekwe Halmashauri na kupelekwa Wizarani ili kubadilishwa matumizi na kurudishwa Kijijini na kupangiwa shughuli nyingine.

"Tena kuna baadhi ya wawekezaji wanapokwenda kuomba maeneo wanatoa ahadi nyingi kuwa wakipewa watasaidia huduma za jamii au kutoa ajira kwa Vijana wa eneo husika lakini hawafanyi hivyo ni vema wakaachia ardhi waliyopewa,"alisema Ridhiwani.

Naye Diwani wa Lugoba Rehema Mwene alisema kuwa Kijiji cha Makombe kinakabiliwa na changamoto ya ubovu wa barabara, ukosefu wa maji, uchakavu wa Zahanati na baadhi ya maeneo kukosa umeme.

Mwene alisema kuwa changamoto nyingine ni baadhi ya wawekezaji kuchukua maeneo na kutoyaendeleza hivyo kufanya kuwe na mapori makubwa ambayo yanahatarisha usalama wa watu.

Kwa upande wake kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Makombe Godfrey Nyange akisoma risala ya Kijiji alisema kuwa kuna migogoro ya mipaka baina ya Kijiji hicho na Vijiji vya Kinzagu na Mindutulieni.

Nyange alisema kuwa changamoto nyingine ni wanufaika wa Mfuko ya Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuondolewa kwenye mfumo na wengine kutolipwa fedha zao za kila mwezi. Naibu Waziri alitembelea Vijiji vya Makombe, Mindutulieni na Lunga kwenye Kata ya Lugoba.



TANESCO KUONGEZA UZALISHAJI UMEME


Na Mwandishi Wetu Dodoma

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) linatarajia kuzalisha megawati 5,000 kupitia miradi mbalimbali ifikapo kwa mwaka 2025 hivyo kuongeza uzalishaji umeme kupitia gridi ya Taifa.

Hayo yamesemwa na kaimu Mkurugezi wa huduma kwa wateja wa shirika la umeme Tanzania ( TANESCO) Martin Mwambene wakati akielezea utekelezaji wa shughuli mbalimbali ya shirika hilo na uelekeo wake kwa mwaka wa 2023 .

Mwambene amesema kuwa kwa sasa shirika hilo lina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 1,820 wakati mitambo iliyopo ina uwezo wa kuzalisha megawati 1,300 pekee. 

Amesema kuwa TANESCO kwa kutambua matatizo ya umeme yaliyopo nchini imekuja na mradi wa Gridi Imara ambapo katika bajeti ya mwaka huu imetengewa shilingi bilioni 500 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wake.

"Katika mradi wa Grid Imara utajumuisha ununuzi wa mashine umba 6000, mita 700,000 za umeme, nguzo 380,000 ununuzi na ufungaji wa nyaya zenye urefu wa km 40,000, ujenzi wa njia za kusafirisha umeme mkubwa takribani kilomita 948 na ujenzi wa vituo 14 vya kupooza umeme,"amesema Mwambene. 

Aidha amezungumzia pia maendeleo ya ujenzi katika Bwawa la Mwalimu NYerere kuwa upo katika asilimia 88 na zoezi la uwekaji maji limefikia mita za ujazo 133 kutoka usawa wa bahari

TCU KUTHIBITI UBORA


Na Mwandishi Wetu Dodoma

TUME ya vyuo vikuu Tanzania (TCU) imeendelea kuimarisha mifumo yake ya uthibiti ubora na mifumo ya ndani ya vyuo vikuu Ili kuhakikisha vinaendana na mwelekeo wa nchi pamoja na kuandaa na kuratibu mafunzo kwa viongozi wahadhiri na maofisa wa vyuo vikuu vya umma na binafsi hapa nchini kwa lengo la kuwajengea uwezo katika usimamizi wa uendeshaji wa taasisi zao.

Hayo yamesemwa na katibu mtendaji tume ya vyuo vikuu Tanzania Prof. Charles Kihampa wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za tume hiyo kwa kipindi Cha Miaka miwili ya uongozi wa serikali ya awamu ya sita.

Kihampa amesema kuwa Katika kuhakiki ubora tume imeimarisha mifumo yake ya ushauri na ukaguzi wa mara kwa mara wa kawaida na wa kushtukiza kwa mujibu wa Sheria na utaratibu zilizopo kwa lengo la kuhakikisha kuwa Elimu itolewayo na vyuo vikuu hapa nchini inakidhi viwango vya ubora kikanda, kitaifa na kimataifa.

Amesema kuwa nafasi za masomo Katika vyuo vya Elimu ya juu Katika program za shahada ya kwanza zimeongezeka kutoka 157,770 Mwaka 2020/2021 Hadi 172,168 Mwaka 2022/2023 sawa na ongezeko la nafasi 14,398 ya asilimia 9.1.

Aidha amesema mwaka 2022/2023 serikali imetenga kiasi Cha shilingi bilion 6.4 kupitia mradi wa Elimu ya juu kwa mageuzi ya kiuchumi ( higher Education for Economic Transformation- HEET) kwa ajili ya kuimarisha uthibiti ubora na uhuishaji wa mitaala ya vyuo vikuu ambapo zaidi ya mitaala 300 ya vyuo hivyo vinafanyiwa mapitio Ili kuhuishwa kwa kizingatia maoni ya wadau mbalimbal