Saturday, April 19, 2025

BALOZI MATINYI AAHIDI KUITANGAZA TANZANIA KIMATAIFA

BALOZI wa Tanzania nchini  Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, amesema kuwa atatumia uzoefu alioupata katika kazi yake ya  uandishi wa habari kutafuta taarifa na kung'amua mbinu za kuvutia watalii wengi kama ilivyo katika nchi hiyo ambayo inavutiwa na kutembelewa na watalii wengi.

"Nitakapofika katika nchi hizo tisa katika eneo langu la uwakilishi nitahakikisha ninatafuta na kujua ni mbinu gani wanazotumia kuvutia watalii kwani watalii wengi duniani huenda kwenye nchi hizo", alisema Mhe. Balozi Matinyi.

Alisema pia kuwa kwa kutumia uzoefu wake katika uandishi wa habari - fani ambayo hujenga tabia ya udadisi na mbinu za kutafuta taarifa za uwekezaji na pia tabia kulikamilisha jukumu la kazi baada ya kulichukua.

Balozi Matinyi alisema hayo  hivi karibuni katika mahojinao maalumu na kituo cha televisheni cha ZBC cha Zanzibar.

Alifafanua kwa kueleza kuwa diplomasia ya uchumi nchini ilianzishwa katika utawala wa awamu ya tatu ambapo ili kuujenga uchumi wetu baada ya kumaliza kuzisaidia nchi zingine za Afrika kupata uhuru.

"Hii ndiyo sababu viongozi wetu wakuu wanatusisitizia kwamba tunapokwenda nje ya nchi tukaifanyie kazi diplomasia ya uchumi," alidokeza Mhe. Balozi Matinyi.

"Nitakapofika katika nchi hizo tisa zilizoendelea kiuchumi, katika sekta ya uvuvi, kilimo katika viwanda vya mbolea na matrekta, utalii ambapo wanapokea watalii kati ya milioni 6 hadi 7 kwa mwaka wakitumia visiwa vingi na bahari kuvutia watalii, jukumu langu litakuwa kuhakikisha tunapata mbinu zao na Watanzania tunasonga mbele kiuchumi" alisema Mhe. Balozi Matinyi.

Aidha, akizungumzia namna atakakavyoiwakilisha  Zanzibar, alisema kuwa tayari ameshapata maelezo mbalimbali kutoka taasisi za uwekezaji, kama za uchumi wa buluu na utalii na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kujua namna ya kuielezea Zanzibar.

"Tuna nchi tisa katika eneo ninalokwenda wenye tabia ya kutaka kufahamu vyakula vya watu wengine; hivyo, nitawaeleza kwamba Zanzibar kuna viungo vya kipekee vyenye ladha nzuri."

Mhe.  Balozi Matinyi amezitaja nchi ambazo  atakuwa mwakilishi mbali ya Sweden kuwa Denmark, Finland, Norway, Iceland, Estonia, Latvia, Lithuania na Ukrane.

Akijibu swali kuhusu mgogoro wa nchi za Ukraine na Russia, Mhe. Balozi Matinyi alisema kuwa Tanzania inasimamia amani na hivyo inataka nchi zinapokwaruzana zitafute suluhu kwa mazungumzo na si kupigana vita.


Thursday, April 17, 2025

UJENZI WA MRADI WA MAJI PANGANI KIBAHA WAANZA

 

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imemkabidhi mkandarasi  eneo la mradi wa maji wa Pangani Wilayani Kibaha Mkoani Pwani utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.9.

Akizungumza na baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Pangani Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Ramadhani Mtindasi alisema kuwa mradi huo ni wa miezi 12.

Mtindasi alisema kuwa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni kampuni ya Shanxi Construction Engineering Corporation and Mineral Company ya China ambapo kutakuwa na hatua tatu za ujenzi wa pampu mbili, tenki la maji na usambazaji wa maji.

Alisema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa matenki mawili ambapo pampu itakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 250,000 kwa saa ambapo yatajengwa eneo la Shirika la Elimu Kibaha (KEC).

"Maji hayo yatatoka kwenye bomba kubwa la maji lililopo jirani na barabara ya Morogoro na yatapelekwa hadi Pangani kwenye tenki hilo litakalokuwa na uwezo wa ujazo wa lita milioni sita kwa mara moja,"alisema Mtindasi.

Aidha alisema kuwa ili kufanikisha ujenzi huo aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo ili asipate changamoto.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala alisema kuwa wanamshukuru Rais kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kukabili changamoto ya maji kwenye Kata ya Pangani.

Twamala alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya maji itakuwa ni mkombozi kwa wananchi na kuwataka wawe walinzi wa mradi huo ambao ulipaswa kuanza tangu mwaka 2023 lakini ulichelewa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa anaomba mkandarasi atekeleze mradi huo kwa wakati ili wananchi wapate huduma hiyo muhimu.

Koka alisema kuwa changamoto hiyo ilikuwa ni kubwa sana na wabanchi walikuwa wakilalamika sana na ni kilio kikubwa ambacho sasa kinaenda kutatuliwa ambapo wananchi zaidi ya 83,000 watanufaika na mradi huo.

Diwani wa Kata ya Pangani Agustino Mdachi alisema kuwa wananchi walikuwa wanalia sana lakini sasa wanafutwa machozi kwa mradi huo kuanza.

Mdachi alisema kuwa mradi huo utakuwa mkombozi kwani mbali ya kuhudumia Kata ya Pangani pia Kata za Maili Moja na Picha ya Ndege zitanufaika na mradi huo

Thursday, April 3, 2025

UJENZI KIWANGO CHA LAMI BARABARA YA PICHA YA NDEGE-BOKOMNEMELA UNARIDHISHA-MKIMBIZA MWENGE KITAIFA ISMAIL USSI

MWENGE wa Uhuru umeridhishwa na mradi wa ujenzi wa barabara ya Picha ya Ndege-Bomotimiza yenye urefu wa mita 550 kiwango cha lami wenye thamani ya shilingi milioni 760.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ussi akikagua barabara hiyo ambapo fedha hizo nikutoka serikali kuu kutokana na tozo ya mafuta amesema serikali inapenda wananchi wapate miundombinu mizuri.

Ussi amesema kuwa kutokana na mradi huo kuwa na ubora wananchi wanapaswa kuulinda na kuutunza ili ulete manufaa ya muda mrefu na kuufanyia usafi.

Amesema kuwa serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa kutengeneza miundombinu ambapo mradi huo umejengwa kwa viwango vinavyotakiwa kutokana na usimamizi mzuri.

"Rais Dk Samia Suluhu Hassan anapenda kuona miradi kama hii inakuwa na matokeo mazuri kwani ndiyo malengo ya serikali hivyo ulindeni mradi huu ambao una gharama kubwa,"amesema Ussi.

Kwa upande wake Mhandisi Samwel Ndoveni amesema kuwa mradi huo ulianza Oktoba mwaka 2023 na ulitegemewa kukamilika Aprili 2024 lakini muda uliongezwa na kukamilika Julai 2024 kutokana na mvua za elnino.

Ndoveni amesema kuwa mradi huo kwa sasa uko katika kipindi cha matazamio hadi Julai 2025 na kukabidhiwa rasmi na kuwa kiasi kilicholipwa hadi sasa ni shilingi milioni 696.9 sawa na asilimia 91.7.

Naye Mwentekiti wa Halmashauri ambaye ni Diwani wa Kata ya Sofu Mussa Ndomba amesema kuwa baravara hiyo ambayo inaanzia barabara ya Morogoro ina urefu wa kilometa saba ni muhimu sana.

Ndomba amesema kuwa barabara hiyo inapita kwenye maeneo ya Shule, Magereza na Hospitali na inaunganisha Kata tatu za Sofu, Picha ya Ndege na Bokomnemela ambapo zamani ilikuwa ni changamoto kubwa sana kwa wananchi wa maeneo hayo.


MWENGE WAZINDUA MRADI WA KISIMA CHA MAJI HOSPITALI YA TUMBI KUTOA LITA 10,000 KWA SAA

HOSPITALI ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani ya Tumbi imepata mradi wa kisima kirefu kinachohudumia watu 920 kwa siku ambapo kwa siku kina uwezo wa kuzalisha lita 10,000 kwa saa.

Hayo yamesemwa na ofisa uendeshaji na matengenezo Mhandisi Charles Stephen wa Dawasa Kibaha akitoa taarifa ya mradi wa kisima kirefu cha maji kwa kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Ismail Ussi amesema mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 45.9.

Stephen amesema kuwa mradi huo umefadhiliwa na taasisi ya Direct Aid Society  na lengo la mradi huo ni kupata chanzo mbadala cha maji ili kusaidia kupata huduma ya maji ya uhakika inapotokea changamoto.

"Hospitali inatumia lita 110,000 kwa siku ambapo awali ilikuwa inategemea chanzo kimoja tu cha Dawasa hivyo kwa sasa maji yatakuwa ya uhakika mara inapotokea changamoto Dawasa,"amesema Stephen.

Amesema mradi huo ulianza Julai mwaka 2024 na kukamilika Agosti 2024.

USSI ATAKA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA MIKOPO ASILIMIA 10 YA HALMASHAURI WAJIKWAMUE KIUCHUMI

VIJANA kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani wametakiwa kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata fedha za mikopo asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri ili wajikwamue kiuchumi.

Hayo yamesemwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ussi alipotembelea kikundi cha The Dream kilichopo Mtaa wa Kilimahewa Kata ya Tangini.

Ussi amesema kuwa ili vijana waweze kujitegemea wanapaswa kuwa na shughuli za kufanya za kujiongezea kipato kwa kufanya shughuli za kiuchumi.

"Tuwapongeze vijana hawa kwa kuonyesha mfano mzuri kwa kukopa fedha ambazo matunda yake yanaonekana kwani fedha hizo za Halmashauri zimewanufaisha hivyo vibana wengine waige kikundi hichi,"amesema Ussi.

Akisoma risala mweka hazina wa kikundi hicho kinajishughulisha na utengenezaji wa Clips na Tambi  Neema Shao amesema kuwa walikopa kiasi cha shilingi milioni 15 kutoka Halmashauri Januari mwaka huu.

Shao amesema kuwa kikundi kinauwezo wa kuzalisha pakiti 600 na kwa mwezi pakiti 12,000 zenye thamani ya shilingi milioni 9.6 ambapo uzalishaji hufanyika kwa siku 20 kwa mwezi.

Amesema kuwa wanauwezo wa kupata faida ya shilingi milioni mbili ambapo hadi sasa wamesharejesha kiasi cha shilingi 625,000 na wameweza kununua Toyo ya kusambazia bidhaa zao ambapo zamani walikuwa wakikodisha pikipiki.


KIONGOZI MBIO ZA MWENGE KITAIFA ISMAIL USSI APONGEZA UJENZI ZAHANATI KILIMAHEWA

MKIMBIZA mbio za Mwenge Kitaifa Ismail Ussi ameweka jiwe la msingi kwenye Zahanati ya Kilimahewa ambayo mara itakapokamilika itahudumia wananchi 68,371 wa Kata tatu.

Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ussi amesema kuwa ujenzi huo ni azma ya Rais anayoitaka ya kuwaondolea adha wananchi ya kupata huduma za afya mbali.

Ussi amesema kuwa anaipongeza Halmashauri na wananchi kwa kufanikisha ujenzi huo ambapo hadi kukamilika kwake unatarajia kutumia kiasi cha shilingi milioni 234.3.

"Tumeambiwa mara itakapokamilika wananchi hawatapata usumbufu kwenda mbali kupata huduma za afya watapata karibu hivyo kupata muda kufanya shughuli za maendeleo,"amesema Ussi

Akisoma taarifa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha Catherine Saguti amesema kuwa ujenzi wa Zahanati hiyo kwa sasa umefikia asilimia 61 ya ujenzi na mradi huo unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha wa 2025/2026.

Saguti amesema kuwa manufaa ni kwa Kata tatu za Tangini, Maili Moja na Pangani zenye jumla ya mitaa 16 ambapo wananchi wataondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.

Aidha amesema kuwa hadi sasa mradi huo umetumia kiasi cha shilingi milioni 108.3 huku wananchi wakichangia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni moja kwa kujaza kifusi.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka amesema anaishukuru serikali kuwapatia eneo hilo ambalo lilikuwa mali ya Wizara ya Mifugo na kupangiwa matumizi ya jamii.

Koka amesema kuwa afya ni kipaumbele kikubwa kwa wananchi kwani wakiwa na afya njema wataweza kujiletea maendeleo.


MWENGE WAWEKA JIWE LA MSINGI MRADI SHULE YA AWALI MSINGI YA MCHEPUO WA KIINGEREZA KATA YA SOFU

HALMASHAURI ya Mji Kibaha imetoa kiasi cha shilingi milioni 458.4 kwa ajili ya ujenzi wa shule ya awali na msingi ya Nyerere ya muundo wa Kiingereza iliyopo Mtaa wa Sofu na Kata ya Sofu.

Aidha hadi mradi huo utakapokamilika utatumia kiasi cha shilingi milioni 704.6 ikiwa ni mapato ya ndani ya Halmashauri.

Akisoma taarifa mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ismail Ussi, ofisa elimu awali na msingi Theresia Kyara amesema kuwa ujenzi huo uko hatua ta umaliziaji.

Kyara amesema kuwa ujenzi huo umehusisha vyumba tisa vya madarasa, matundu 17 ta vyoo, kichomea taka, jengo la utawala, ununuzi wa samani na madawati.

Amesema kuwa hadi sasa zimetumika kiasi cha shilingi milioni 297.7 kwa awamu ya kwanza huku awamu ya pili ikitumia milioni 157.1 na awamu ya tatu zitatumika kiasi cha shilingi milioni 89 na ujenzi umefikia asilimia 64.5

Kwa upande wake kiongozi huyo wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ussi amesema kuwa shule za msingi za mchepuo wa Kiingereza za serikali ni nzuri katika kuendeleza elimu kwa watoto.

Ussi amesema kuwa shule hizo ni nzuri kwani gharama zake ni nafuu hivyo mradi huo ni mkombozi kwa wanafnzi walioko kwenye maeneo jirani na shule hiyo.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye pia Diwani wa kata ya Sofu Mussa Ndomba amesema kuwa wananchi waliomba mradi huo ambapo na kupelekwa kwenye baraza la madiwani na kupitishwa.

Ndomba amesema hilo lilikuwa hitaji kubwa la wananchi wa Mtaa na Kata hiyo hivyo utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kwa watoto wao.

KIONGOZI MBIO ZA MWENGE ASIFU MRADI WA MAEGESHO YA MALORI YA MIZIGO

MBIO za Mwenge zimekagua eneo la mradi wa maegesho ya magari makubwa ambao utakapokamilika utaiingizia Halmashauri ya Mji Kibaha kiasi cha shilingi bilioni 3.3 kwa mwaka.

Akikagua na kupata taarifa kwenye mradi huo uliopo Kata ya Misugusugu kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ussi amesema kuwa hicho ni chanzo kizuri cha mapato kwa Halmashauri hiyo.

Ussi amesema kuwa mradi huo wa maegesho hayo ambayo yatakuwa ya kisasa yataifanya Halmashauri kuongeza mapato yake hivyo kuendelea kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

"Jambo ambalo ni zuri ni kulipa fidia na maendelezo kiasi kikichotengwa ni bilioni 1.8 kwa watu 23 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kimelipwa kwa watu 21 hii inaonyesha kuwa wananchi wanalipwa haki zao na hakuna mtu atakaye kosa haki yake,"amesema Ussi.

Kwa upande wake Mthamini wa Halmashsuri ya Mji Kibaha Patrick Kibwana amesema kuwa mradi huo utakuwa wa shilingi bilioni 23 ikiwa ni mapato ya ndani.

Amesema kuwa hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 317.8 bado hakijalipwa huku watu wawili wakiendelea na taratibu za kibenki.

Kibwana kuwa mradi utakuwa na nyumba za kulala wageni sehemu ya kuoshea magari kituo cha zimamoto mama lishe hoteli sehemu ya kutengeneza magari mifumo ya miundombinu ya gesi vyoo na mabafu kituo cha mafuta kituo cha polisi fremu za biashara huduma za afya ghala za kuhifadhia mizigo na mizani ya kupimia uzito.

Amesema kuwa mradi amesema kuwa mradi huo utatoa ajira kwa vijana 1,000 ambapo eneo hilo lina ukubwa wa hekari 18 na utaondoa msongamano wa malori kutoka Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amesema kuwa maegesho hayo yamejengwa jirani na eneo la viwanda la Zegereni hivyo huduma hiyo inahitajika sana.

John amesema kuwa mradi huo utakuwa ni sehemu ya kuzalisha ajira kwa wananchi hususani vijana kwenye Wilaya hiyo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano.

 



Wednesday, April 2, 2025

KIONGOZI MBIO ZA MWENGE WA UHURU KITAIFA AFURAHISHWA MRADI MAEGESHO YA HALMASHAURI YA MJI KIBAHA


MBIO za Mwenge zimekagua eneo la mradi wa maegesho ya magari makubwa ambao utakapokamilika utaiingizia Halmashauri ya Mji Kibaha kiasi cha shilingi bilioni 3.3 kwa mwaka.

Akikagua na kupata taarifa kwenye mradi huo uliopo Kata ya Misugusugu kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ussi amesema kuwa hicho ni chanzo kizuri cha mapato kwa Halmashauri hiyo.

Ussi amesema kuwa mradi huo wa maegesho hayo ambayo yatakuwa ya kisasa yataifanya Halmashauri kuongeza mapato yake hivyo kuendelea kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.

"Jambo ambalo ni zuri ni kulipa fidia na maendelezo kiasi kikichotengwa ni bilioni 1.8 kwa watu 23 ambapo kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kimelipwa kwa watu 21 hii inaonyesha kuwa wananchi wanalipwa haki zao na hakuna mtu atakaye kosa haki yake,"amesema Ussi.

Kwa upande wake Mthamini wa Halmashsuri ya Mji Kibaha Patrick Kibwana amesema kuwa mradi huo utakuwa wa shilingi bilioni 23 ikiwa ni mapato ya ndani.

Amesema kuwa hadi sasa kiasi cha shilingi milioni 317.8 bado hakijalipwa huku watu wawili wakiendelea na taratibu za kibenki.

Kibwana kuwa mradi utakuwa na nyumba za kulala wageni sehemu ya kuoshea magari kituo cha zimamoto mama lishe hoteli sehemu ya kutengeneza magari mifumo ya miundombinu ya gesi vyoo na mabafu kituo cha mafuta kituo cha polisi fremu za biashara huduma za afya ghala za kuhifadhia mizigo na mizani ya kupimia uzito.

Amesema kuwa mradi amesema kuwa mradi huo utatoa ajira kwa vijana 1,000 ambapo eneo hilo lina ukubwa wa hekari 18 na utaondoa msongamano wa malori kutoka Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson John amesema kuwa maegesho hayo yamejengwa jirani na eneo la viwanda la Zegereni hivyo huduma hiyo inahitajika sana.

John amesema kuwa mradi huo utakuwa ni sehemu ya kuzalisha ajira kwa wananchi hususani vijana kwenye Wilaya hiyo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano.

 

Tuesday, April 1, 2025

TAASISI YA BEGA KWA BEGA NA TANZANIA PWANI YACHANGIA DAMU CHUPA 19

TAASISI ya Bega kwa Bega na Tanzania Mkoani Pwani imechangia damu chupa 19 kwenye benki ya damu ajili ya wagonjwa wanaohudumiwa kwenye hospitali Wilayani Kibaha. 

Kiasi hicho cha damu kilipatikana wakati wa bonanza la kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki kwenye uzinduzi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa Mkoani Pwani 2025 lililofanyika kwenye uwanja wa Bwawani Kibaha.

Mratibu wa taasisi hiyo kitaifa Ruth Mateleka bonanza hilo limefanywa ili kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru zitakazofanyika leo kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha.

"Kazi yetu kubwa ni kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za kimaendeleo na kutaja kazi zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan na tunashukuru watu kujitolea damu ili kusaidia wagonjwa,"amesema Mateleka.

Kwa upande wake Zuhura Sekelela ambaye ni mratibu wa taasisi hiyo Mkoa wa Pwani alisema kuwa upatikanaji wa damu hiyo kutasaidia benki ya damu kuwa na damu ili kusaidia wagonjwa.

Sekelela alisema kuwa shughuli nyingine ambazo wanazifanya ni kupanda miti, kufanya usafi kwenye taasisi za umma ikiwa ni pamoja na shuleni, hoapitali na maeneo mbalimbali pamoja na kusaidia watoto waishio kwenye mazingira magumu.

Naye Mchungaji Josephine Mwalusama amesema kuwa yeye kama Mchungaji anamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuhimiza wanawake kushika nafasi za uongozi.

Mwalusama amesema kuwa Rais amefanya kazi kubwa na zinaonekana na ameshukuru Mwenge kuwashiwa Mkoani Pwani kwani utautangaza Mkoa na wajasiriamali watanufaika kwa kuwashwa mwenge huo wa uhuru.

Naye Mwenyekiti wa Vijana kutoka taasisi hiyo ya Bega kwa Bega na Tanzania Mkoa wa Pwani Athuman Lusambi  amesema kuwa wanawahamasisha vijana kushiriki kwenye Mwenge ili wawe wazalendo na nchi yao.