Thursday, April 17, 2025

UJENZI WA MRADI WA MAJI PANGANI KIBAHA WAANZA

 

MAMLAKA ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imemkabidhi mkandarasi  eneo la mradi wa maji wa Pangani Wilayani Kibaha Mkoani Pwani utakaogharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.9.

Akizungumza na baadhi ya wananchi wa Mtaa wa Pangani Kaimu Mtendaji Mkuu wa Dawasa Mhandisi Ramadhani Mtindasi alisema kuwa mradi huo ni wa miezi 12.

Mtindasi alisema kuwa Mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni kampuni ya Shanxi Construction Engineering Corporation and Mineral Company ya China ambapo kutakuwa na hatua tatu za ujenzi wa pampu mbili, tenki la maji na usambazaji wa maji.

Alisema kuwa mradi huo utahusisha ujenzi wa matenki mawili ambapo pampu itakuwa na uwezo wa kuzalisha lita 250,000 kwa saa ambapo yatajengwa eneo la Shirika la Elimu Kibaha (KEC).

"Maji hayo yatatoka kwenye bomba kubwa la maji lililopo jirani na barabara ya Morogoro na yatapelekwa hadi Pangani kwenye tenki hilo litakalokuwa na uwezo wa ujazo wa lita milioni sita kwa mara moja,"alisema Mtindasi.

Aidha alisema kuwa ili kufanikisha ujenzi huo aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa mkandarasi anayetekeleza mradi huo ili asipate changamoto.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Shangwe Twamala alisema kuwa wanamshukuru Rais kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya kukabili changamoto ya maji kwenye Kata ya Pangani.

Twamala alisema kuwa ujenzi wa miundombinu ya maji itakuwa ni mkombozi kwa wananchi na kuwataka wawe walinzi wa mradi huo ambao ulipaswa kuanza tangu mwaka 2023 lakini ulichelewa.

Naye Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa anaomba mkandarasi atekeleze mradi huo kwa wakati ili wananchi wapate huduma hiyo muhimu.

Koka alisema kuwa changamoto hiyo ilikuwa ni kubwa sana na wabanchi walikuwa wakilalamika sana na ni kilio kikubwa ambacho sasa kinaenda kutatuliwa ambapo wananchi zaidi ya 83,000 watanufaika na mradi huo.

Diwani wa Kata ya Pangani Agustino Mdachi alisema kuwa wananchi walikuwa wanalia sana lakini sasa wanafutwa machozi kwa mradi huo kuanza.

Mdachi alisema kuwa mradi huo utakuwa mkombozi kwani mbali ya kuhudumia Kata ya Pangani pia Kata za Maili Moja na Picha ya Ndege zitanufaika na mradi huo

No comments:

Post a Comment