Thursday, April 3, 2025

USSI ATAKA VIJANA KUCHANGAMKIA FURSA MIKOPO ASILIMIA 10 YA HALMASHAURI WAJIKWAMUE KIUCHUMI

VIJANA kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani wametakiwa kujiunga kwenye vikundi ili waweze kupata fedha za mikopo asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri ili wajikwamue kiuchumi.

Hayo yamesemwa na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Ismail Ussi alipotembelea kikundi cha The Dream kilichopo Mtaa wa Kilimahewa Kata ya Tangini.

Ussi amesema kuwa ili vijana waweze kujitegemea wanapaswa kuwa na shughuli za kufanya za kujiongezea kipato kwa kufanya shughuli za kiuchumi.

"Tuwapongeze vijana hawa kwa kuonyesha mfano mzuri kwa kukopa fedha ambazo matunda yake yanaonekana kwani fedha hizo za Halmashauri zimewanufaisha hivyo vibana wengine waige kikundi hichi,"amesema Ussi.

Akisoma risala mweka hazina wa kikundi hicho kinajishughulisha na utengenezaji wa Clips na Tambi  Neema Shao amesema kuwa walikopa kiasi cha shilingi milioni 15 kutoka Halmashauri Januari mwaka huu.

Shao amesema kuwa kikundi kinauwezo wa kuzalisha pakiti 600 na kwa mwezi pakiti 12,000 zenye thamani ya shilingi milioni 9.6 ambapo uzalishaji hufanyika kwa siku 20 kwa mwezi.

Amesema kuwa wanauwezo wa kupata faida ya shilingi milioni mbili ambapo hadi sasa wamesharejesha kiasi cha shilingi 625,000 na wameweza kununua Toyo ya kusambazia bidhaa zao ambapo zamani walikuwa wakikodisha pikipiki.


No comments:

Post a Comment