Tuesday, April 1, 2025

TAASISI YA BEGA KWA BEGA NA TANZANIA PWANI YACHANGIA DAMU CHUPA 19

TAASISI ya Bega kwa Bega na Tanzania Mkoani Pwani imechangia damu chupa 19 kwenye benki ya damu ajili ya wagonjwa wanaohudumiwa kwenye hospitali Wilayani Kibaha. 

Kiasi hicho cha damu kilipatikana wakati wa bonanza la kuhamasisha wananchi kujitokeza kushiriki kwenye uzinduzi wa mbio za Mwenge wa uhuru Kitaifa Mkoani Pwani 2025 lililofanyika kwenye uwanja wa Bwawani Kibaha.

Mratibu wa taasisi hiyo kitaifa Ruth Mateleka bonanza hilo limefanywa ili kuhamasisha wananchi kushiriki uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru zitakazofanyika leo kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha.

"Kazi yetu kubwa ni kuhamasisha wananchi kushiriki shughuli za kimaendeleo na kutaja kazi zilizofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan na tunashukuru watu kujitolea damu ili kusaidia wagonjwa,"amesema Mateleka.

Kwa upande wake Zuhura Sekelela ambaye ni mratibu wa taasisi hiyo Mkoa wa Pwani alisema kuwa upatikanaji wa damu hiyo kutasaidia benki ya damu kuwa na damu ili kusaidia wagonjwa.

Sekelela alisema kuwa shughuli nyingine ambazo wanazifanya ni kupanda miti, kufanya usafi kwenye taasisi za umma ikiwa ni pamoja na shuleni, hoapitali na maeneo mbalimbali pamoja na kusaidia watoto waishio kwenye mazingira magumu.

Naye Mchungaji Josephine Mwalusama amesema kuwa yeye kama Mchungaji anamshukuru Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuhimiza wanawake kushika nafasi za uongozi.

Mwalusama amesema kuwa Rais amefanya kazi kubwa na zinaonekana na ameshukuru Mwenge kuwashiwa Mkoani Pwani kwani utautangaza Mkoa na wajasiriamali watanufaika kwa kuwashwa mwenge huo wa uhuru.

Naye Mwenyekiti wa Vijana kutoka taasisi hiyo ya Bega kwa Bega na Tanzania Mkoa wa Pwani Athuman Lusambi  amesema kuwa wanawahamasisha vijana kushiriki kwenye Mwenge ili wawe wazalendo na nchi yao.

No comments:

Post a Comment