Monday, March 31, 2025

NMB KUTUMIA ZAIDI YA BILIONI 6 MIRADI YA MAENDELEO

BENKI ya inatarajia kutumia kiasi cha shilingi bilioni 6.4 kwa ajili ya kuchangia shughuli za maendeleo kwa mwaka wa 2025.

Hayo yalisemwa na Meneja wa benki hiyo Kanda ya Dar es Salaam ambaye aliwakilishwa na meneja wa tawi la Mlandizi Wilayani Kibaha William Marwa wakati wa Kongamano la Vijana juu ya umuhimu wa kushiriki mbio za mwenge mkoa wa Pwani 2025.

Alisema vijana wanapaswa kujua historia ya mbio za mwenge wa uhuru na fursa zilizopo kupitia mwenge ambao ni alama ya mshikamano wa kuleta maendeleo ya nchi.

"Tangu mwenge umeanza mbio zake kwa sasa ni miaka 61 na pia tunakumbuka kifo cha mwasisi wa Taifa letu miaka 26 iliyopita lazima tumjue kwani aliifanyia nchi hii mambo makubwa,"alisema Marwa. 

Akizungumzia benki hiyo ambayo ni kubwa kuliko zote nchini imekuwa ikichangia maendeleo na ni chachu kwa kuchangia kwenye sekta ya afya, elimu na kutoa mkono wa pole kwa wananchi wanaopata majanga.

"Benki imekuwa ikirudisha sehemu ya faida kwa kuchangia suala la maendeleo kupitia sekta mbalimbali kwani wao ni sehemu ya wateja kwani ina matawi wilaya zote nchini,"alisema Marwa.

Alisema kuwa benki hiyo ina matawi 241 Atm 720 mawakala 50,000 na wateja milioni 8.7 kote nchini na bado inaendelea kuboresha huduma zake kimtandao.

Sunday, March 30, 2025

WAZIRI MKUU MAJALIWA AUPIGIA DEBE UWANJA WA SHIRIKA LA ELIMU KIBAHA KUTUMIWA NA TIMU ZA CHAN NA AFCON

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameupigia debe uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha kutumiwa na Timu za Taifa zitakazokuwa zinajiaandaa na michuano ya  CHAN na AFCON kwa ajili ya mazoezi.

Majaliwa aliyasema hayo alipotembelea kuukagua uwanja huo ambao utatumika kwenye usinduzi wa mbio za mwenge 2025.

Majaliwa alisema kuwa jana alifanya ukaguzi wa viwanja vitatu viyakavyotumika kwa ajili hiyo ambavyo ni vichache.

"Tanzania tumepata uenyeji wa mashindano hayo mawili ambayo ni makubwa hivyo lazima tuwe na viwanja vingi kwa ajili ya mazoezi na hichi kikiboreshwa kinaweza kutumika,"alisema Majaliwa.

Alisema kuwa wataangalia uwezekano wa uwanja huo kutumiwa kwa ajili ya mazoezi na tutaongea na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kama watakikubali itabidi kitumike.

"Kiwanja hichi kikiimarishwa vizuri kinaweza kutumika kwa ajili hata ya ligi kuu ni uwanja mzuri unahitaji maboresho kidogo tu kwani hata taa zipo kwa kweli hapa ni pazuri,"alisema Majaliwa.

Aidha alisema hayo ni matunda ya uwekezaji kwenye sekta ya michezo ambapo Rais Dk Samia Suluhu Hassan ameamua kuwekeza kwenye michezo.

"Kwa vijana wa Halaiki msiishie hapa endeleeni na mazoezi hii iwe ni sehemu ya kuanzia kwa wale watakaocheza mpira wa miguu, pete, riadha na michezo mingine ili muendeleze vipaji vyenu isiwe hapa ndiyo mwisho,"alisema Majaliwa.



WAZIRI MKUU MAJALIWA ARIDHISHWA MAANDALIZI UZINDUZI WA MWENGE WA UHURU PWANI 2025

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kuangalia maandalizi ya uwanja utakaotumika kuzindua mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2025 mkoani Pwani.

Majaliwa alitembelea uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha kuangalia maandalizi ya uzinduzi huo na kuridhishwa na maandalizi hayo na kutaka wakamilishe sehemu ambazo bado hazijakamilika.

Alisema kuwa ameridhishwa na maandalizi hayo ambapo pia alitumia muda huo kutembelea watoto wa halaiki na kusema amefurahishwa na jinsi walivyokuwa na hamasa ya uzinduzi huo.

"Nawapongeza kwa maandalizi mnayoendelea nayo nimeridhishwa kamilisheni sehemu zilizosalia ili kukamilisha mapema,"alisema Majaliwa.

Alisema kuwa amefurahishwa kuona viongozi wakiwemo mawaziri na makatibu wakuu wakiwa mstari wa mbele kuhakikisha maandalizi yanakuwa mazuri.

"Alikeni hata mikoa ya jirani Dar es Salaam, Morogoro na Tanga na watu mbalimbali kwani hili ni jambo la kitaifa shirikisheni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili hamasa iwe kubwa,"alisema Majaliwa 

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete maandalizi yako vizuri ila baadhi ya maeneo ikiwemo katikati ya uwanja ndiyo kunahitaji marekebisho kidogo.

Kikwete alisema kuwa mialiko kwa wageni mbalimbali imetolewa ikiwa ni pamoja na wakuu wa mikoa, wakurugenzi na watu wengine ili kushiriki uzinduzi huo.


Friday, March 28, 2025

VIJANA WAFUNDISHWE UMUHIMU WA MBIO ZA MWENGE

TAASISI mbalimbali nchini zimetakiwa kuwajengea uwezo vijana juu ya umuhimu wa mbio za Mwenge wa Uhuru katika kujenga uzalendo na uwajibikaji katika usimamizi wa shughuli za maendeleo na kutambua fursa za kiuchumi.

Hayo yamesemwa na Skauti Mkuu Nchini na Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta wakati Kongamano la Vijana juu ya umuhimu wa kushiriki Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025.

Mchatta amesema kuwa vijana wanapaswa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa namna ambavyo mtaelekezwa na viongozi katika maeneo wanayoishi.

"Tukifanya hivyo tutaupata ujumbe wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa ufasaha ili muweze kushuhudia kwa vitendo yale yote mtakayojifunza katika Kongamano hili,"amesema Mchatta.

Amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa kundi la vijana katika kuleta mageuzi ya Kijamii na Kiuchumi kutokana na ari, nguvu na ubunifu walionao. 

"Kwa kutambua hilo serikali kwa kushirikiana na wadau imekuwa ikitoa kipaumbele kwa vijana kupata elimu na makuzi bora kuwapa fursa ya kupata mikopo ya asilimia 10 kupitia Halmashauri na Programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (Build Better Tomorrow – BBT) 

Amesema kuwa Mwenge wa Uhuru Mwaka 2025 utazinduliwa mkoa wa Pwani kitendo ambacho kinaonesha nia njema ya Dk Samia Suluhu Hassani Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuendeleza na kuenzi kwa vitendo yale yote aliyoturithisha Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Rais wa Kwanza wa Tanzania. 

Kwa upande wake mratibu wa Kongamano hilo Omary Punzi amesema kuwa ili vijana waweze kufikia mafanikio ya kimaendeleo lazima wazingatie falsafa za Mwalimu Nyerere alizotumia wakati wa kuwashwa Mwenge wa Uhuru.

Punzi amesema moja ya falsafa za Mwenge wa Uhuru ni kuwafanya watu wawe na uzalendo kwa kujitoa kwa ajili ya nchi yao na kutokomeza maadui watatu ujinga umaskini na maradhi. 

Mbio za Mwenge wa Uhuru zitazinduliwa katika viwanja vya Shirika  la Elimu Kibaha Mkoani Pwani na Mgeni rasmi atakuwa Dk Philip Isdor Mpango Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

mwisho.


Wednesday, March 26, 2025

MAKAMU WA RAIS DK MPANGO KUZINDUA MBIO ZA MWENGE KITAIFA PWANI

MAKAMU wa Rais Dk Philip Isdor Mpango atazindua mbio za Mwenge kitaifa Mkoani Pwani Aprili 2 mwaka huu kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Ridhiwani Kikwete akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya juu ya uzinduzi huo amesema kuwa maandalizi ya uzinduzi yanaenda vizuri.

Kikwete amesema kuwa tayari Makamu wa Rais ameshathibitisha kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo wa mbio za  Mwenge kwa mwaka 2025.

"Kwa vitu vilivyobakia niwaombe mhakikishe vinafika kwa wakati ili kila kitu kiwe kwenye sehemu yake na bado tutaendelea kuangalia maandalizi ili siku hiyo mambo yawe mazuri,"amesema Kikwete.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa maandalizi yako vizuri ambapo hadi Machi 29 mambo mengi yatakuwa yamekamilika.

Kunenge amesema kuwa huduma zote zitapatikana kuanzia suala la afya, vyoo, maji, taa kubwa, umeme ambapo kutakuwa na jenereta endapo umeme utakatika.

Amewataka wananchi wa Mkoa huo na mikoa jirani na Watanzania kwa ujumla kujitokeza siku hiyo ili kuweka historia ya Pwani kuzindua mbio za Mwenge Kitaifa.

Tuesday, March 25, 2025

JK AWASILISHA UJUMBE MAALUMU KWA RAIS WA SENEGAL KUTOKA KWA RAIS SAMIA

Mhe. Rais Mstaafu  Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amewasilisha  ujumbe maalumu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenda kwa Rais wa Jamhuri ya Senegal, Mhe. Bassirou Diomaye Faye jijini Dakar.

Katika mazungumzo  yao ya kirafiki,  Rais Mstaafu alieleza dhamira ya dhati ya Rais Samia na Serikali anayoiongoza ya kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia, kiuchumi na kijamii kati ya Tanzania na Senegal.

Pamoja na masuala ya ushirikiano wa kiserikali, Rais Mstaafu pia alisisitiza umuhimu wa kukuza uhusiano baina ya wananchi wa mataifa haya mawili kupitia sekta za elimu, biashara, utalii, na maendeleo ya vijana na wanawake.

Ziara hii ni sehemu ya juhudi endelevu za Tanzania kuimarisha uhusiano wa kimataifa na mataifa ya Afrika Magharibi, huku ikiweka msisitizo kwa diplomasia ya uchumi na ushirikiano wa watu kwa watu.

MAANDALIZI UWASHWAJI MWENGE WA UHURU KITAIFA PWANI MBIONI KUKAMILIKA



MAANDALIZI ya Uzinduzi wa mbio za Mwenge Kitaifa yamefikia asilimia 96 ambapo Mwenge huo utawashwa Wilayani Kibaha Mkoani Pwani Aprili 2 Mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha (KEC) Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema kuwa maandalizi yanaenda vizuri.

Kunenge amesema kuwa kwa sasa zimebaki siku sita ambapo Mwenge utazinduliwa Aprili 2 na utatembelea kwenye Halmashauri tisa za mkoa huo kwa kuanza na Halmashauri ya Mji Kibaha utakapoanzia.

"Uwanja umekamilika yamebaki maeneo machache ambapo hadi leo sehemu kubwa itakuwa imekamilika na kubaki mambo madogo madogo,"amesema Kunenge.

Amesema kuwa majukwaa yamekamilika na matarajio ni kuwa na watu 16,000 ambapo miundombinu ya maji, sehemu ya magari kukaa tayari, taa, mifumo ya majitaka na ulinzi viko tayari.

Thursday, March 20, 2025

TANROADS YATOA UFAFANUZI LORI LILILOZIDISHA UZITO MIZANI YA VIGWAZA.

WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) imetoa ufafanuzi juu ya taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ya lori la mizigo lililokamatwa kwenye mizani ya Vigwaza kuwa taratibu za kulikamata lori hilo ulifuatwa.

Aidha gari hilo lilipigwa faini hiyo kwa kuzingatia sheria ya udhibiti wa uzito barabarani ya Afrika Mashariki ya mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018.

Akizingumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za mizani hiyo ya Vigwaza Mtaalamu wa Kitengo cha Mizani Tanroads Makao Makuu Vicent Tarmo amesema kuwa gari hilo lilizidisha uzito zaidi ya tani moja.

Tarmo amesema kuwa gari hilo lenye namba za usajili T 137 DLR na tela namba T 567 CUR lilikuwa limetokea nchini Congo likiwa limebeba madini ya Shaba ambapo uwezo wake ni kubeba tani 48 lakini lilikutwa likiwa na uzito tani 48.1.

"Kutokana na kuzidisha uzito huo gari hilo lilitakiwa kulipiwa faini ya shilingi 900,000 ikiwa ni adhabu ya kuzidisha uzito halisi lakini dereva huyo alisema kuwa amezidishiwa uzito hivyo kupinga faini hiyo,"amesema Tarmo.

Amesema kuwa sheria inataka magari yote yenye uzito kuanzia tani 3 na nusu lazima yapime uzito ili kuepusha uharibifu wa barabara hivyo kutokana na gari hilo kuzidisha uzito alipaswa kulipa faini hiyo.

"Dereva huyo amesema kuwa amepita mizani mbalimbali uzito haukuzidi hivyo kwa nini hapa uzidi lakini kwa mujibu wa sheria alipaswa kulipa na siyo kukaidi kulipa,"amesema Tarmo.

Amesema kuwa gari hilo lilipita hapo Machi 13 ambapo kwa siku hiyo yalipimwa mwagari 819 ambapo saba yalibainika kuzidisha uzito ambapo mengine yalilipa na kuendelea safari lakini gari hilo dereva wake aligoma kulipa akidai amezidishiwa uzito.

"Mzani huu ni automatiki lakini yeye alitaka uzito  urudiwe kupimwa jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu ambapo hupaswa kupunguza na kulipa uliizidi na kupima tena na siyo kupima upya,"amesema Tarmo.

Ameongeza kuwa uzito unaweza kuzidi kutokana na sababu kadhaa ikiwa ni pamoja na kuongeza mafuta, abiria na busta endapo zitakuwa na hitilafu ambapo hata walipofuatilia mizani nchini Zambia uzito ulikuwa na mabadiliko ikionekana kuzidi.

"Dereva baada ya kuona hizo tofauti alipaswa kuangalia mfumo wa gari lake kwani kutokana na baadhi ya changamoto kama hizo uzito unaweza kuongezeka,"amesema Tarmo.

Kwa upande wake Meneja wa Tanroads Mkoa wa Pwani Baraka Mwambage amesema kuwa kama kunatokea changamoto yoyote kuna taratibu za kufuata ili kuweza kupata haki zao na si kutumia mitandao kutoa malalamiko yao.

Mwambage amesema kuwa malalamiko yanaweza kupelekwa ofisini au kama wana wasiwasi wanaweza kupeleka kwenye vyombo vingine ikiwa ni pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kama sehemu ya kujua ukweli zaidi.

Hivi karibuni zilisambaa habari kupitia mitandao ya kijamii ambapo picha mjongeo ilimuonyesha dereva mmoja akilalamikia mizani ya Vigwaza kuwa imezidisha uzito.

TCRA KUSHIRIKIANA NA TBN KUSADIA KUZALISHA MAUDHUI YENYE TIJA

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeahidi kufanyakazi na Mtandao wa Wana Blogu Tanzania (TBN) pamoja na vyama vingine vya waandishi wa habari ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao.

Kauli hiyo imetolewa leo tarehe  19 Machi 2025 Jijini Dar es Salaam na Meneja wa Huduma za Utangazaji wa TCRA, Mhandisi Andrew Kisaka, alipokutana na ujumbe wa TBN ofisini kwake, katika kikao cha kujadiliana changamoto mbalimbali zinazowakabili Bloga nchini.

“Sisi huwa tunapenda kufanya kazi na vyama ambavyo vinawakilisha mahitaji na matakwa ya wanachama wao, badala ya kufanyakazi na mwaandishi mmoja mmoja…tunafurahi sana kufanyakazi na waandishi kupitia vyama vyao,” amesema Mhandisi Kisaka.

Mhandisi Kisaka amesema kuwa TCRA imefurahi kukutana na TBN kwa kuwa wanafahamu kuwa Bloga wanasehemu kubwa sana kwenye maudhui ya ndani, na hata kwenye usajili wa TCRA Bloga wanachukua nafasi kubwa sana katika maudhui ya mtandaoni.

“Kwa hiyo TBN mtakuwa silaha moja wapo nzuri sana yakutuwezesha sisi kama Mamlaka ya Mawasiliano nchini, tunao simamia utangazaji pamoja na maudhui ya mtandaoni kuwa karibu na nyinyi na kuhakikisha maudhui ya mtandaoni yanaleta tija na maendeleo kwa wananchi,” amesema Mhandisi Kisaka.

Friday, March 14, 2025

RAIS MSTAAFU DK KIKWETE AFANYA ZIARA NCHINI JAPAN KUIMARISHA USHIRIKIANO KATI YA BODI YA SHIRIKA LA ELIMU LA KIMATAIFA (GPE) NA JAPAN


Rais mstaafu, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akiwa  Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Elimu la Kimataifa (GPE), yupo Tokyo nchini Japan kwa ziara maalum yenye lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya GPE na serikali ya Japan katika kutatua changamoto za elimu ya msingi katika nchi zinazoendelea.

Katika siku yake ya kwanza Tokyo, Dkt. Kikwete amefanya mazungumzo na Waziri wa Fedha wa Japan, Mhe. Shin-ichi Yokohama, pamoja na Naibu wake, Mhe. Atsushi Mimura. 

Mazungumzo hayo yalijikita katika ushirikiano wa kifedha ili kusaidia miradi ya elimu inayosimamiwa na GPE, ikiwemo upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wa nchi zinazoendelea.

Baada ya mazungumzo hayo, Rais Mstaafu Kikwete alikutana na Bw. Akihiko Tanaka, Rais wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Japan (JICA). 

Shirika hili limekuwa na mchango mkubwa katika miradi ya maendeleo barani Afrika, na mazungumzo yalihusu namna JICA inaweza kusaidia jitihada za GPE katika kukuza elimu bora.

Dkt. Kikwete pia alikutana na Bw. Yohei Sasakawa, Mwenyekiti wa Taasisi ya Nippon. Bw. Sasakawa, mwenye umri wa miaka 86, ni mtu mashuhuri wa kusaidia miradi ya kijamii duniani. 

Katika mazungumzo yao, waligusia nafasi ya sekta binafsi katika kusaidia elimu, hasa kupitia taasisi zisizo za kiserikali. Vilevile, Bw. Sasakawa alishangaza dunia baada ya kufanikisha kupanda Mlima Kilimanjaro tarehe 12 Februari 2024, kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 85 ya kuzaliwa kwake – hatua inayothibitisha kuwa umri si kikwazo kwa ndoto kubwa.

Katika siku zinazofuata, Rais Mstaafu Kikwete anatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Mhe. T. Miyaji, pamoja na wabunge wa Bunge la Japan, ambapo ajenda kuu itakuwa nafasi ya elimu na teknolojia katika maendeleo ya jamii.

Pia, atashiriki mijadala maalum kuhusu elimu na teknolojia, kufanya mahojiano na vyombo vya habari, pamoja na kukutana na Mhe. Tetsuro Yano, Rais wa Taasisi ya AFRECO, ambayo inahusika na kukuza ushirikiano kati ya Japan na Afrika.

Ziara hii ni sehemu ya juhudi endelevu za Dkt. Kikwete katika kuboresha mifumo ya elimu duniani, hasa katika nchi zinazoendelea. 

Japan ni mshirika muhimu wa maendeleo ya elimu barani Afrika, na ushirikiano huu unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha watoto wengi zaidi wanapata fursa ya elimu bora.

 


Thursday, March 13, 2025

KIWANDA CHA KEDS CHATOA MSAADA KWA WANAWAKE

KIWANDA cha kuzalisha sabuni cha Keds Tanzania Company Ltd cha Kibaha Mkoani Pwani kimetoa misaada ya sabuni kwa wanawake wa Mtaa wa Lulanzi ambao uko jirani na kiwanda hicho ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe ya siku ya wanawake Duniani.

Akizungumza kiwandani hapo mara baada ya kukabidhi msaada hiyo Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bob Cheng amesema kuwa wanaungana na jamii katika kusaidia wanawake ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe hizo.

Cheng amesema kuwa wamewapatia misaada hiyo ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wa wanawake ambao ni mkubwa katika kuleta maendeleo kwenye jamii.

"Kiwanda kinaungana na wanawake katika maadhimisho haya hivyo tumeona turudishe kwa jamii ikiwa ni katika ushirikiano na wananchi katika kuleta maendeleo,"amesema Cheng.

Amesema kuwa kiwanda kitaendelea kushirikiana na jamii katika masuala mbalimbali ya maendeleo hususani kwa wananchi walio jirani na kiwanda na wananchi wote kwa ujumla.

Akishukuru kwa msaada huo wa sabuni za unga na vipande Jasmini Issa amesema kuwa wanashukuru kwa msaada huo kwani utawasaidia katika matumizi ya kila siku.

Issa amesema kuwa msaada huo umeonyesha jinsi kiwanda hicho kinavyoshirikiana na jamii katika suala zima la maendeleo ambapo wamekuwa wakisaidia miradi mbalimbali inayohusu wananchi.

Naye Meri Mkwizu amesema kuwa sabuni ni muhimu sana kwa familia na ni moja ya vitu muhimu katika mahitaji kwenye familia na hutumika muda wote.

Mkwizu amesema kuwa sabuni ina bajeti kubwa kutokana na matumizi yake ikiwa ni pamoja na kufulia nguo, kuoshea vyombo, kuogea na kufanyia usafi wa aina mbalimbali ambapo jumla ya wanawake 89 walipewa msaada huo.

KEDS KUENDELEA KUZALISHA BIDHAA BORA

KIWANDA cha Keds Tanzania Company Ltd kimesema kitaendelea kuzalisha bidhaa zenye ubora na bei nafuu kulingana na hali ya soko.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mkurugenzi wa kiwanda hicho Bob Cheng alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Cheng amesema kuwa katika utengenezaji wa bidhaa zao wanazingatia ubora ili kuendelea kuwa na soko kwa kuwapatia wananchi kitu kilicho bora.

"Malengo ya kuanzishwa kiwanda ni kukuza uchumi wa wananchi kwa kutoa ajira kwa watu wengi pia kutengeneza bidhaa bora zinzokubalika,"amesema Cheng.

Amesema kuwa malengo yao ni kutengeneza bidhaa nyingine lakini kwa sasa wanafanya kwanza utafiti ili kujua ni bidhaa gani watakayoizalisha.

"Kiwanda kinajihusisha na uzalishaji wa sabuni za unga, vipande, pampasi na pedi za akinamama na kinashirikiana na serikali kwa kufuata taratibu zote za kisheria,"amesema Cheng.

Aidha amesema kuwa kiwanda kinashirikiana na jamii kwa kurudisha kwa jamii kwa kusaidia kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kwenye sekta za elimu, afya, barabara na sekta mbalimbali.

"Kuhusu maji yanayotoka kiwandani hayana athari zozote za kiafya na kimazingira ambapo hata wafanyakazi wetu wanaishi jirani na kiwanda ni asilimia 60 hivyo hayana tatizo lolote,"amesema Cheng.

Kiwanda hicho kinauza bidhaa zake kote nchini pamoja na nchi za jirani baadhi zikiwa ni Uganda, Kenya na Malawi.







TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA (THBUB) YATEMBELEA VIWANDA PWANI

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imefanya ziara kutembelea viwanda kuangalia uzingatiwaji wa haki za binadamu ili zisivunjwe

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Kamishna wa Tume Nyanda Shuli wakati wa ziara ya kutembelea viwanda ili kufanya uchunguzi kujua kama kuna changamoto za uvunjifu wa haki.

Shuli amesema kuwa baadhi ya viwanda vimekuwa vikilalamikiwa kuvunja haki za binadamu kwa unyanyasaji wa wafanyakazi, uchafuzi taka maji na haki mbalimbali.

"Lengo la ziara ni kuangalia hali ya haki za binadamu na uzingatiwaji wa misingi ya utawala bora kuangalia usalama wa mazingira ya kazi na uzingatiaji wa viwango vya ajira,"amesema Shuli.

Amesema kuwa malalamiko waliyoyapokea watayafanyia kazi na kutoa majibu jambo kubwa ni kuona haki inatendeka ili kuondokana na uvunjifu wa haki za binadamu.

Kwa upande wake Bob Cheng ambaye ni Mkurugenzi wa kiwanda cha Keds Tanzania Company Ltd kinachojihusisha na uzalishaji wa sabuni za unga, vipande, pampasi na pedi za akinamama.

Cheng amesema kuwa kiwanda chao kinazingatia masuala ya haki za binadamu na lengo lake ni kukuza uchumi wa wananchi na hata maji ya kiwanda hicho hayana madhara ambapo asilimia 60 ya wafanyakazi wanaishi eneo jirani na kiwanda hivyo kama kungekuwa na changamoto yoyote wangefahamu.

Amesema kuwa wanafanya utafiti ili kuongeza bidhaa na uzalishaji wenye kuzingatia ubora na bei ambayo inaendana na soko.

Aidha kamishna aliambatana na Taasisi za Serikali ambazo ni OSHA, NEMC na Maofisa kutoka Ofisi ya RAS (Ofisa biashara, Ofisa Kazi na Ofisa Maendeleo ya jamii) kwa lengo la kuleta ufanisi katika ziara hiyo.


Wednesday, March 12, 2025

TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA (THBUB) INAFANYA ZIARA KWENYE VIWANDA MKOANI PWANI KUANGALIA UZINGATIWAJI WA HAKI ZA BINADAMU

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imefanya ziara kutembelea viwanda kuangalia uzingatiwaji wa haki za binadamu ili zisivunjwe.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Kamishna wa Tume Nyanda Shuli wakati wa ziara ya kutembelea viwanda ili kufanya uchunguzi kujua kama kuna changamoto za uvunjifu wa haki.

Shuli amesema kuwa baadhi ya viwanda vimekuwa vikilalamikiwa kuvunja haki za binadamu kwa unyanyasaji wa wafanyakazi, uchafuzi taka maji na haki mbalimbali.

"Lengo la ziara ni kuangalia hali ya haki za binadamu na uzingatiwaji wa misingi ya utawala bora kuangalia usalama wa mazingira ya kazi na uzingatiaji wa viwango vya ajira,"amesema Shuli.

Amesema kuwa malalamiko waliyoyapokea watayafanyia kazi na kutoa majibu jambo kubwa ni kuona haki inatendeka ili kuondokana na uvunjifu wa haki za binadamu.

Kwa upande wake Bob Cheng ambaye ni Mkurugenzi wa kiwanda cha Keds Tanzania Company Ltd kinachojihusisha na uzalishaji wa sabuni za unga, vipande, pampasi na pedi za akinamama.

Cheng amesema kuwa kiwanda chao kinazingatia masuala ya haki za binadamu na lengo lake ni kukuza uchumi wa wananchi na hata maji ya kiwanda hicho hayana madhara ambapo asilimia 60 ya wafanyakazi wanaishi eneo jirani na kiwanda.

Amesema kuwa wanafanya utafiti ili kuongeza bidhaa na uzalishaji wenye kuzingatia ubora na bei ambayo inaendana na soko 

Aidha kamishna aliambatana na Taasisi za Serikali ambazo ni OSHA, NEMC na Maofisa kutoka Ofisi ya RAS (Ofisa biashara, Ofisa Kazi na Ofisa Maendeleo ya jamii) kwa lengo la kuleta ufanisi katika ziara hiyo.


Wednesday, March 5, 2025

DOWEICARE YATOA YATOA MSAADA WA FEDHA UJENZI WA DARAJA LULANZI


KIWANDA cha Doweicare cha Kibaha Mkoani Pwani kimetoa fedha kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa daraja la Mtaa wa Lulanzi-Matunda ili kuboresha barabara ya mtaa huo.

Akikabidhi fedha hizo kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bob Chen amesema kuwa wameamua kutoa fedha hizo ili kukabili changamoto za jamii.

Amesema kuwa Kiwanda chao kimekuwa kikitoa misaada mbalimbali kwenye jamii ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii kama sehemu ya huduma za jamii ambapo fedha hizo ni asilimia 57.5 ya fedha za mradi huo.

"Tunashirikiana na jamii kwenye masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja elimu, afya, barabara na masuala yanayohusu jamii,"amesema Chen.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Thobias Shilole amesema kuwa wanakishukuru kiwanda hicho kwa msaada walioutoa utasaidia sana ujenzi wa daraja hilo.

Shilole amesema wananchi wamekuwa wakijitolea fedha kwa ajili ya ujenzi huo hivyo hiyo itakuwa imewaongezea nguvu kwenye kuanza ujenzi wa daraja ili kupunguza changamoto kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo.

Amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kuchangia ujenzi huo ili upunguze changamoto kwa watu wakiwemo wanafunzi wakati wakienda na kurudi shule.


WATAALAMU UDSM WAKUTANA NA VIONGOZI TBN

Wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), wamekutana na baadhi ya viongozi na wajumbe wa Tanzania Bloggers Network (TBN) kwa mahojiano maalum yenye lengo chanya la kukusanya maoni yao ili kuimarisha masuala ya blogging, nchini.

Hatua hiyo ya kukusanya maoni imekuja kufuatia wataalamu hao kuagizwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ambayo ipo katika utafiti maalum kwa nia ya dhati kuboresha Sera na kanuni zake mbalimbali katika eneo hilo la majukwaa ya mtandaoni.

Kikao hicho kimefanyika kwa mafanikio katika ofisi za TBN zilizopo kwa Aziz Ali, Temeke, watafiti hao wamechukua maoni ya TBN Makao Makuu, wakisema pia watafika katika Ofisi za Kanda za TBN.

Akizungumza Katibu Mkuu wa TBN Khadija Kalili amesema TCRA imefanya uamuzi sahihi kukutana na wadau wake kwa kupitia wataalamu hao kwani maoni yao yatawapa picha halisi juu ya tasnia ya habari na blogging kwa ujumla wake.

Amesema kilio kikubwa cha wana TBN ni gharama za usajili na tozo ya leseni kiasi ni kikubwa ambacho kwa uhalisia wengi bado hawamudu kulipia.

Amesema hali hiyo imefanya idadi kubwa ya wana TBN kushindwa kumudu kuendesha mitandao yao kutoka 300+ waliokuwapo kwanza hadi kufikia 100+ tu wanaoweza kulipia na kwa kusuasua.

Ameshauri pia TCRA kuendeleza utamaduni wa kukutana na wadau wake ikiwamo kwa mafunzo ya kuwaimarisha uwezo wao pamoja na kuangazia athari za gharama za bando za mtandao na vifaa.

Amesema ikiwa sekta ya blogging ndani ya tasnia ya habari ikisimamiwa vizuri kwa ushirikiano wa karibu na TCRA ni wazi kwamba Tanzania itanufaika na maudhui bora na yenye viwango ambayo yatasaidia kulinda maadili ya jamii yetu.

TBN yenye wanachama 300 waliopo wanaendesha mitandao kwa kusuasua kutokana na ada na tozo.

Watalaam hao walionesha kushangazwa na kuwapo kwa Chama Cha Bloggers chenye usajili kamili na wanachama zaidi ya 300, na pia wakaelewa bloggers ni tofauti na jumuiya zingine za waandishi wa mitandao ambao hawana blogs.

Wataalamu hao ni pamoja na Prof. Siasa Mzenzi, Dkt. Patrokil Kanje , Dkt. Said Suluo.

Wengine ni Mjata Daffa , Ally Mshana na Viongozi na wajumbe wa TBN, wakiongozwa na Katibu Mtendaji Khadija Kalili , Beda Msimbe na Rahel Pallangyo.



Mwisho

DOWEI CARE YATOA MSAADA WA FEDHA UJENZI WA DARAJA LULANZI

KIWANDA cha Dowei Care cha Kibaha Mkoani Pwani kimetoa fedha kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa daraja la Mtaa wa Lulanzi-Matunda ili kuboresha barabara ya mtaa huo.

Akikabidhi fedha hizo kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Mkurugenzi wa Kiwanda hicho Bob Chaing amesema kuwa wameamua kutoa fedha hizo ili kukabili changamoto za jamii.

Amesema kuwa Kiwanda chao kimekuwa kikitoa misaada mbalimbali kwenye jamii ikiwa ni sehemu ya kurudisha kwa jamii kama sehemu ya huduma za jamii ambapo fedha hizo ni zaidi ya asilimia 60 ya fedha za mradi huo.

"Tunashirikiana na jamii kwenye masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja elimu, afya, barabara na masuala yanayohusu jamii,"amesema Chaing.

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Lulanzi Thobias Shilole amesema kuwa wanakishukuru kiwanda hicho kwa msaada walioutoa utasaidia sana ujenzi wa daraja hilo.

Shilole amesema wananchi wamekuwa wakijitolea fedha kwa ajili ya ujenzi huo hivyo hiyo itakuwa imewaongezea nguvu kwenye kuanza ujenzi wa daraja ili kupunguza changamoto kwa wananchi wanaotumia barabara hiyo.

Amewataka wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kuchangia ujenzi huo ili upunguze changamoto kwa watu wakiwemo wanafunzi wakati wakienda na kurudi shule.


Monday, March 3, 2025

VYAMA SITA RAFIKI KUSINI MWA AFRIKA VISIYUMBISHWE VISIMAMIE SHABAHA YA KUWALETEA WANANCHI MAENDELEO

VYAMA vya Ukombozi Kusini mwa Afrika vimetakiwa vibadili mbinu za kuongoza na visikubali kuyumbishwa na mabadiliko ya dunia na kuacha shabaha ya kuziongoza nchi zao.

Hayo yalisemwa jana kwenye Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Mjini Kibaha na Makamu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Steven Wassira wakati akifungua mafunzo kwa viongozi wa vyama hivyo.

Wassira alisema kuwa baadhi ya nchi duniani havipendi kuona vyama hivyo vinaongoza wao wanaona demokrasia ni kuviondoa vyama hivyo madarakani.

"Mabadikiko ni mengi duniani lakini yasivitoe vyama vyetu kwenye shabaha yake ya msingi ambayo ni maisha bora na mazuri kwa wananchi huu ndiyo msingi wa vyama hivi,"alisema Wassira.

Alisema kuwa hiyo ndiyo misingi iliyowekwa na waasisi wa mataifa hayo ambayo yalipigania Uhuru wa nchi zao na kuacha misingi imara ambayo inapaswa kufuatwa.

Kwa upande wake Katibu wa masuala ya siasa uhusiano wa kimataifa na Halmashauri Kuu ya CCM NEC Rabia Hamidu alisema kuwa nchi hizo zinapaswa kuonyesha umoja wao ili kuzisaidia nchi za Afrika.

Naye Naibu Mkurugenzi wa idara ya masuala ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na idara ya kimataifa ya kamati kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na mkuu wa ujumbe wa IDPC Zhang Yanhong alisema kuwa ni jambo zuri kwa ushirikiano wa vyama hivyo sita na CPC.

Naye Mkuu wa Shule ya Mwalimu Julius Nyerere Profesa Marcelina Chijoriga alisema wanatoa mafunzo kwa viongozi wa vyama vya siasa, taasisi za umma na serikali pamoja na taasisi za watu binafsi.

SERA YA TAIFA YA MAENDELEO YA VIJANA 2007 YAENDELEA KUNADIWA

Leo tarehe 3.3.2025 Ndugu Omary Abdul Punzi Mwanadiplomasia na Mratibu wa Makongamano ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana Mwaka 2007 toleo la Mwaka 2024 katika kamati ya Vijana Wazalendo waliopewa kibali Maalumu na Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu 

Kwa ajili ya Kuinadi na kuineza Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana 

Amemtembelea Mheshiwimiwa Godfrey Eliakimu Mzanva Mkuu wa Wilaya ya Moshi kwa ajili ya kumpongeza kwa Kuaminiwa na Mheshiwimiwa Dk Samia Suluhu Hasani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya.

Unakumbuka kuwa Mheshiwimiwa Godfrey Eliakimu Mzanva ni miongoni mwa wakimbiza mwenge mwaka 2024 waliofanya vizuri katika kuendesha Makongamano ya vijana.

Aidha mazungumzo hayo yalitoa mwafaka wa Kuandaa Kongamano la Vijana Kuhusu Umuhimu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Ambalo litajikita zaidi kuelezea historia ya Tanzania, Itifaki, Maadili na Uzalendo kwa Vijana,Madhara ya matumizi ya madawa ya kulevya, utunzaji wa Mazingira na Fursa zinatopatikana Wilaya ya Moshi Mkoa wa Kilimanjaro