Wednesday, January 31, 2024

DAWASA YATAKIWA KUPELEKA MAJI HOSP YA WILAYA LULANZI

HALMASHAURI ya Mji Kibaha imeitaka Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Kibaha kufanya utaratibu wa kupeleka maji kwenye Hospitali ya Wilaya ya Lulanzi ambapo ni miezi mitatu imepita tangu kutolewa hela kiasi cha milioni 60.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani Mwenyekiti wa Halmashauri Mussa Ndomba amesema kuwa fedha hizo zipo lakini wameshindwa kuzichukua.

Mussa amesema kuwa adha ya maji kwenye Hospitali ni kubwa sana kwa matumizi mbalimbali kwa wagonjwa wakiwemo mama wajawazito hali ni mbaya sana.

Akijibu hoja hiyo Meneja wa DAWASA Kibaha Alfa Ambokile amesema kuwa mradi huo tayari amesha andikia makao makuu juu ya fedha hizo kuchukuliwa.


Wednesday, January 17, 2024

WATUHUMIWA KUKUTWA NA NOTI BANDIA NA MASHINE YA KUZITENGENEZEA

WATU wanne wakazi wa Jijini Dar es Salaam wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Pwani kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia zenye thamani ya shilingi milioni 1.5.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi Mkoani humo ACP Pius Lutumo alisema kuwa watuhumiwa hao pia walikutwa na mtambo wa kutengeneza fedha hizo.

Lutumo alisema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya mchana huko Kijiji cha Msata Wilaya ya Kipolisi Chalinze 

Alisema kuwa chanzo cha fedha hizo kukamatwa ni taarifa iliyotolewa na raia mwema ambaye alitilia mashaka noti ya shilingi 10,000 aliyoipokea kwa ajili ya malipo kwa huduma ya kulala nyumba ya wageni.

"Katika upelelezi baada ya tukio hilo Polisi walifanikiwa kukamata mtambo wa kutengenezea fedha hizo bandia na zana nyingine kama kompyuta, kemikali mbalimbali za kutengenezea fedha bandia,"alisema Lutumo.

Aidha alisema kuwa mtambo huo ulikamatwa kwa moja ya watuhumiwa huko Goba Jijini Dar es Salaam na watuhumiwa walikutwa na noti za shilingi elfu 10,000 noti 155.

"Baada ya mtuhumiwa wa kwanza kukamatwa na noti hiyo bandia ya shilingi 10,000 aliwataja watuhumiwa wengine watatu wakiwa na bandia milioni 1.2 zikiwa noti za shilingi elfu tano na elfu mbili,"alisema Lutumo.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mbaraka Miraji (48), Zena Naringa (42) wakazi wa Buza, Masumbuko Kiyogoma mkazi wa Goba na Elias Wandiba (50) mkazi wa Kimara Suka Jijini Dar es Salaam.

Saturday, January 13, 2024

KATA YA MISUGUSUGU YAOMBA WADAU UKAMILISHWAJI JENGO LA WAZAZI

KATA ya Misugusugu Wilayani Kibaha Mkoani Pwani imeomba wadau mbalimbali kuwachangia kiasi cha shilingi milioni 39 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa jengo la mama na mtoto ili kuwaepusha wajawazito kujifungulia majumbani.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Diwani wa Kata hiyo Upendo Ngonyani kuwa wajawazito wengi wanajifungulia majumbani jambo ambalo ni la hatari kiafya.

Alisema kuwa Zahanati iliyopo haina huduma ya kujifungua licha ya kuwa na huduma nyingine za kitabibu isipokuwa za uzazi kutokana na kutokuwa na jengo la wazazi.

"Baada ya kuona changamoto ni kubwa ya akinamama kunifungua tulianzisha ujenzi kwa nguvu za wananchi kupitia wadau mbalimbali tumeweza kujenga jengo hilo la wazazi limeishia kwenye boma,"alisema Ngonyani.

Alisema kwa sasa wanaomba wadau ikiwemo Halmashauri kuwasaidia hatua iliyobaki ili jengo likamilike na kutoa huduma ambapo litanufaisha wananchi wa mitaa minne ya Vitendo, Karabaka, Misugusugu na Miomboni.

"Baadhi ya wajawazito hujifungulia nyumbani kutokana na kutokuwa na kipato wakihofia kwenda Hospitali kuwa gharama ni kubwa hivyo hujifungua kienyeji na wengine hukaa hadi siku ya mwisho ya kujifungua ndipo wanakwenda Hospitali,"alisema Ngonyani.

Aidha alisema wanapopata ujauzito huwa wanakwenda kliniki kwenye Zahanati ya Kata lakini inapofika muda wa kujifungua kwa wale wasio na uwezo hujifungulia nyumbani na kupeleka watoto kliniki kwa ajili ya chanjo mbalimbali.

"Kwa wale wenye uwezo inapofika muda wa kujifungua kwenye vituo vya afya Mkoani, Lulanzi au Mlandizi ambako ni mbali sana na hutumia gharama kubwa kwa usafiri ndiyo tukaona tujenge jengo hilo ili kuondoa changamoto hiyo,"alisema Ngonyani.

Alibainisha kuwa kuna madhara makubwa kwa wajawazito kujifungulia nyumbani kwani ni hatari ambapo mazazi au mtoto au wote wanaweza kupoteza maisha kwa kukosa huduma bora wakati wa kunifungua.

"Tunawapa elimu juu ya umuhimu wa kujifungulia Hospitali lakini wakati mwingine inakuwa vigumu kutokana na baadhi kuwa na kipato kidogo hivyo kushindwa kumudu gharama,"alisema Ngonyani.

Alizishukuru taasisi, wadau mbalimbali na wananchi kwa kujitolea hadi jengo hilo kufikia hapo na kuendelea kuwaomba waendelee kujitolea hadi litakapokamilika ili kunusuru maisha ya akinamama na watoto.

Mitaa hiyo minne ina jumla ya wakazi 8,000 na gharama za mwanzo za ujenzi wa jengi hilo la mama na mtoto limetumia zaidi ya shilingi milioni 20.

BUNGE SC KUCHUANA NA BUNGE LA WAWAKILISHI SC

Kombaini ya Wachezaji wa Bunge SC na BLW SC Katika picha ya pamoja na Waheshimiwa Maspika wa Bunge Mhe. Dkt Tulia Ackson na Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe Zubeir Ally Maulid Kabla ya mchezo wa Kombaini Hiyo na NMB. NMB waliibuka washindi kwa magoli 7-2. Leo Jumamosi tarehe 13.01.2024 Bunge SC itavaana na BLW Katika mchezo wa utangulizi kabla ya fainali ya Mapinduzi Cup

Friday, January 12, 2024

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE MKOA WA PWANI YATOA MISAADA KWA WAFUNGWA





KATIBU wa Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani Ndugu Omary Punzi ametuma salamu za Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Taifa Mhe.Paul Petro Kimiti na Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Taasisi Mhe.Mizengo Peter Pinda (Waziri Mkuu Mstaafu) kwa kutoa misaada mbalimbali kwa wafungwa.

Punzi amesema kuwa misaada hiyo ambayo imewalenga wafungwa imetolewa leo kwenye Gereza la Utete Wilaya ya Rufiji ikiwa inalenga kusherehekea miaka 60 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Tarehe 12.1.1964 .

 ametaja misaada iliyotolewa kuwa ni sabuni za unga na vipande, mafuta ya kupakaa, miswaki na dawa za meno pamoja na juisi katika .

Ndugu Omary Punzi aliwaomba wadau nchini wajitokeze kwa wingi kuwasaidia wafungwa Magereza kwa kutoa misaada mbalimbali kwani bado wanamahitaji mengi.

Kwa Upande wake Mkuu wa Magereza Utete Christopher Mwenda ambaye alipokea misaada hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Magereza Mkoa ameishukuru Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani kwa jinsi wanavyoendelea kuwatia moyo wafungwa siyo mara ya kwanza Taasisi hiyo kutoa misaada kwani mwaka jana walipokea katoni za sabuni boksi 50 za taulo za kike kwa ajili ya wafungwa wanawake

Aliomba wadau wajitokeze kwa wingi kuwasaidia wafungwa wanahitaji mahitaji mengi na Serikali haiwezi kufanya peke yake katika mahitaji.

Naye Monica Mbilla Mkuu wa idara ya Malezi ya Taasisi ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Mkoa wa Pwani amesema msaada mkubwa atakao wasaidia ni kuhakikisha wanapewa elimu na Msaada wa kisheria .

KATA PICHA YA NDEGE YAISHUKURU SERIKALI KUWAPATIA MILIONI 340 UJENZI MADARASA PICHA YA NDEGE SEKONDARI



KATA ya Picha ya Ndege imefanikiwa kuongeza madarasa 17 kwenye Shule ya Sekondari Picha ya Ndege ambayo awali ilikuwa na madarasa sita lakini kwa sasa ni madarasa 23 ambapo zimetumika kiasi cha shilingi milioni 340 kwa madarasa hayo yaliyoongezeka.

Hayo yalisemwa na Diwani wa Kata hiyo Karim Mtambo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi juu ya kuboreka kwa sekta ya elimu kulikofanywa na Serikali ya awamu ya sita.

Mtambo alisema kuwa ongezeko la madarasa hayo kumeondoa changamoto iliyokuwepo ya upungufu wa madarasa ambapo madarasa hayo pia yana viti vyake hivyo wanafunzi watasoma kwa raha bila ya usumbufu.

"Wakati tunaingia kwenye uongozi kulikuwa na boma la maabara mbili za Baiolojia na Kemia Serikali ilitoa milioni 60 kwa awamu ya kwanza na awamu ya ya pili ilitoa milioni 80 ambazo zimekamilisha maabara hizo ambapo bado ya Fizikia,"alisema Mtambo.

Alisema kuwa kuna baadhi ya changamoto zilizopo kwa sasa ni ukosefu wa jengo la Utawala kwaniwalimu imebidi watumie darasa moja kama ofisi kwa ajili ya shughuli zao ambapo walipeleka ombi Halmashauri ili kujengewa jengo la Utawala.

"Changamoto nyingine ni vyoo vya walimu ambapo imebidi watumie matundu ya vyoo vya wanafunzi moja kwa walimu wanawake na walimu wanaume na tumeongea na wazazi watoe tofali tano ili kuwajengea choo walimu kwani jambo ambalo siyo sawa,"alisema Mtambo.

Aidha alisema kulikuwa na changamoto ya maji ambapo walipewa milioni 10 na Halmashauri na kuvuta maji lakini bomba wanalotumia majo yanatoka kwa mgao lakini mradi wa Pangani ukikamilika maji yatapatikana muda wote.

Thursday, January 11, 2024

WATANZANIA WATAKIWA WAPANDE MITI KULINGANA NA UMRI WAO

WATANZANIA wametakiwa kuadhimisha siku za kumbukumbu zao za kuzaliwa kwa kupanda miti kutokana na umri wao ili kukabili mabadiliko ya tabianchi.

Hayo yalisemwa na Brigadia Jenerali Mstaatu Martin Kemwaga mwasisi wa kampeni ya Miti kwa Umri alipozungumza na gazeti hili kwa njia ya simu kuwa malengo yake ni kuifanya nchi kuwa ya kijani.

Kemwaga alisema kuwa kampeni hiyo ambayo alianza miaka mitano iliyopita ambapo ilizinduliwa na Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dk Jakaya Kikwete eneo la Msata Wilayani Bagamnoyo mkoani Pwani kwenye Hoteli ya Makmar ambayo yeye ni Mtendaji Mkuu.

"Namshukuru Rais Mstaafu Dk Kikwete kwa kutuzindulia kampeni yetu ambayo mimi na familia yangu, marafiki na vikundi mbalimbali huwa tunapanda miti kutokana na umri wetu na ningependa kila Mtanzania apande miti kutokana na umri wake,"alisema Kemwaga.

Alisema kuwa Watanzania waadhimishe siku zao za kuzaliwa kwa kupanda miti badala ya kutumia
gharama kubwa za kukumbuku za kukumbuka siku siku zao za kuzaliwa ambapo idadi ya Watanzania.

"Watu watumie maeneo ya taasisi za Umma kama vile kwenye Mashule, Hospitali, Zahanati, Polisi na vyuo na maeneo mbalimbali ya wazi ambapo miti ikipandwa kutasaidia hali ya hewa kuwa nzuri na kuondokoana na arhari za mabadiliko tabianchi,"alisema Kemwaga.

Aidha alisema kuwa Utamaduni huo warithishwe watoto ili wawe wanafanya hivyo ambapo ndani ya muda mnfupi nchi itakuwa na miti mingi na kukabili changamoto mbalimbali za hali ya hewa inayojitokeza
kutokana na ukosefu wa miti.

Aidha alisema kuwa katika eneo ambalo wamepanda miti wanaifuatilia ili kuhakikisha inakuwa na kama
mtu kapanda atakuwa anafuatilia mti alioupanda tofauti na baadhi ya taasisi zimekuwa zikipanda miti lakini hawaifuatili na kufa.

Monday, January 8, 2024

HALMASHAURI YAWATAKA WAVAMIZI SHAMBA LA MITAMBA KUONDOKA.

HALMASHAURI ya Mji Kibaha imewataka wavamizi waliovamia Shamba la Mitamba namba 34 kuondoa maendelezo waliyoyafanya kabla ya zoezi la kuwaondoa kufanyika ili wasipate hasara.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.

Munde amesema kuwa watu waliovamia walipewa ilani ya tarehe 22/11/2022 ya kuondoka kwenye eneo hilo lililopo Kata ya Pangani baada ya kamati maalumu kuundwa na waziri wa ardhi na kutoa majibu kuwa watu hao ni wavamizi kwani eneo hilo lina hati.

"Eneo hilo linamilikiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi na lina hati miliki ni sehemu ya eneo lenye ukubwa wa hekta 4,000 lilitwaliwa kisheria na wizara hiyo kwa kulipa fidia kwa wananchi 1,556 waliokuwa wakimiliki kiasili na kulipwa kwa awamu nne kati ya mwaka 1988 na 1991,"amesema Munde.

Amesema kuwa baada ya kulipa fidia na kumilikishwa kiwanja hicho chenye ukubwa wa hekta 1,037 wananchi walivamia na kuuza sehemu ya kiwanja na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kufanya ujenzi kinyume cha sheria.

"Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi wakati huo William Lukuvi alifanya mkutano Julai 15 mwaka 2021 na kuwataka wananchi waache kuvamia eneo hilo na kuuza na kuunda kamati ya wataalamu mbalimbali ikiongozwa na kamishna wa Polisi makao makuu Dodoma,"amesema Munde.

Aidha amesema kuwa baada ya maagizo ya mawaziri Halmashauri ya Mji Kibaha ilitoa ilani ya kwanza ya siku saba iliyotolewa 22/11/2022 kuwataka wavamizi hao kuondoka ili kuruhusu mpango wa uendelezaji wa kiwanja hicho.

"Pia Halmashauri ilipokea barua ya katibu mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi yenye kumbukumbu namba GA.16/200/01/75 ya Septemba 20 mwaka 2023 kwa ajili ya kupanga upya, kusimamia, kuwaondoa wavamizi wote na kupima kiwanja hicho.

Aliongeza kuwa kwa kuwa wananchi walishapewa ilani ya kuondoka mara mbili hivyo waondoe maendelezo yao kwani zoezi la kuwaondoa likianza hawatapata nafasi ya kuondoa mali zao.

Saturday, January 6, 2024

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE MKOA WA PWANI INATARAJIA KUJENGA KITUO WATOTO WANAOISHI KWENYE MAZINGIRA MAGUMU

TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoani Pwani inatarajia kujenga kituo cha kulea watoto waishio kwenye mazingira magumu kitakachogharimu kiasi cha shilingi milioni 150.

Hayo yamesemwa mjini Kibaha na Katibu wa Taasisi hiyo Omary Punzi alipokutana na wadau wanaoshirikiana nao katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Punzi amesema Taasisi hiyo imekuwa ikitoa misaada mbalimbali kwa watoto waishio kwenye mazingira magumu ambao wanasoma shule za msingi na sekondari, watu wenye uhitaji wakiwemo wafungwa na watu mbalimbali.

"Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere imekuwa ikitoa misaada kwa makundi kama hayo lakini baada ya kuona kuna changamoto ya watoto kuishi kwenye mazingira magumu mitaani tumeona kuna haja ya kujenga kituo kwa ajili ya watoto hao,"amesema Punzi.

Amesema kuwa kujengwa kwa kituo hicho kutaacha alama kwa Taasisi hiyo na wadau wanaoshirikiana nao katika kuihudumia jamii yenye uhitaji ambapo ni moja ya malengo Taasisi.

"Tunatarajia kujenga kituo hicho hapa Kibaha lengo likiwa ni kuihudumia jamii na kuenzi falsafa za Mwalimu Nyerere za kupambana na adui watatu umaskini, ujinga na maradhi,"amesema Punzi.

Aidha amesema kuwa watoto hao wakiwa hapo Taasisi itahakikisha watoto hao wanapata huduma muhimu za msingi ikiwani pamoja na elimu na matibabu ambazo ni falsafa za Mwalimu Nyerere,"alisema Punzi.

Ameomba wadau kushiriki kikamilifu wakati ujenzi utakapoanza ili malengo ya taasisi yafikiwe ya ujenzi wa kituo hicho ili kuwaondoa watoto hao kuishi mitaani badala yake waishi kwenye makazi maalumu.

Monday, January 1, 2024

TAASISI YA KUMBUKUMBU YA MWALIMU NYERERE PWANI YATOA VYETI VYA PONGEZI KWA WADAU








TAASISI ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Pwani imetoa vyeti vya shukrani kwa vyombo vya habari na wadau mbalimbali ambao ilishirikiana nao katika shughuli zake za maendeleo.

Akikabidhi vyeti hivyo hakimu mkazi mstaafu mkoa wa Pwani Stephen Mbungu amewataka waandishi wa habari na wadau kudumisha amani kwa kuzingatia maadili ya nchi.

Naye naibu katibu mkuu wa taasisi hiyo Neema Mkwachu alisema kuwa moja ya kazi zao ni kufundisha maadili kwa Watanzania ili nchi iendelee kuwa na amani.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dk Abdulsalaam Omar alisema kuwa wanashirikiana na taasisi na mashirika katika utoaji huduma ikiwa ni sehemu ya kuleta maendeleo.

Mwakilishi wa kamishna wa uhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Mathew Ntilicha aliwataka wananchi kulinda mazingira kwa kupanda miti na ufugaji wa nyuki.

Meneja wa Shirika la Ugavi la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Pwani Mhandisi Mahawa Mkaka alisema kuwa wataendelea kushirikiana na taasisi hiyo ili iendelee kuihudumia jamii.

Mwenyekiti wa (CCM) Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao alisema kuwa elimu inapaswa kutolewa kwa viongozi wakiwemo madiwani na viongozi wa umma kwani baadhi hawana maadili mazuri.

Mhamasishaji wa taasisi hiyo kitaifa Jirabi alisema kuwa lengo kuu ni kuwaunganisha Watanzania ili kujua falsafa za Nyerere ambaye alikuwa akipambana na adui watatu wa Taifa ambao ni Ujinga, Maradhi na Umaskini.

Kwa upande wake katibu wa taasisi hiyo Mkoani Pwani Omary Punzi alisema kuwa wamefanya hafla hiyo ikiwa ni sehemu ya kutoa shukrani kwa wadau mbalimbali ambao imeshirikiana nayo katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo.