Na John Gagarini Kibaha
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi vyakula vya sikukuu ya Christmas na mwaka mpya makundi maalumu ili nao washerehekee kama walivyo watoto wanaoishi na wazazi.
Akimwakilisha Rais kukabidhi katika kituo cha kulelea watoto wanaoishi kwenye Mazingira magumu cha Makao ya Malezi Madina kilichopo Mtaa wa Vikawe kata ya Pangani Wilaya ya Kibaha Mkuu wa mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge alisema kituo hicho kinawakilisha vituo 37 vilivyopo mkoa mzima.
Kunenge alisema kuwa Rais kwa kutambua makundi maalum ametoa zawadi hizo ili watoto hao washeherekee kama watakavyosheherekea wengine ambao wanaishi kwa furaha na familia zao.
"Nimekuja hapa kumwakilisha Rais wetu amewaletea zawadi pamoja na salamu za sikukuu ya Christmas na mwisho wa mwaka ambapo amewaletea mbuzi wawili, mchele kilo 60, maharage kilo 40, mafuta lita 20, juisi na viungo mbalimbali,"alisema Kunenge.
Alisema kuwa wadau wa maendeleo na wenye uwezo kujenga tabia ya kujitolea kwa vituo vya watoto wenye mahitaji ambapo vitu vilivyotolewa ni pamoja na vitoweo ,mchele , maharage,mafuta ya kupikia ,vinywaji na viungo vingine mbalimbali vya kupikia.
Kwa upande wao watoto wa Makao ya Madina Zainab Athuman na Jumanne Manzi walimshukuru Mungu kwa kumwezesha Rais kupata na kuweza kuwapa zawadi hizo.
Naye Mlezi wa watoto Makao Malezi ya Madina Fatma Abdilai alisema kuwa wananchi waendelee kumuombea Rais Samia kwa mengi anayofanya nchini na kutekeleza ilani kwa kutambua makundi maalum.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kibaha Mjini Mwajuma Nyamka alimshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk Samia kwa kuitendea haki ilani ya Chama na kujali watoto .
Mkoa huo una jumla ya makao ya malezi 37 yenye jumla ya watoto 1,301 na kituo hicho cha Madina kina watoto 30.
Mwisho
No comments:
Post a Comment