UNYENYEKEVU KWA WAJASIRIAMALI NI MSINGI WA BIASHARA-MAVUNDE
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
NAIBU Waziri wa Kilimo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini amewaasa wajasirimali wadogo wadogo kujifunza unyenyekevu pindi wanapokuwa katika shughuli zao.
Mavunde ameyasema hayo katika ziara aliyoifanya pamoja na wajasirimali (Mama Lishe ) Mkoani Dodoma walipotembelea katika mashamba ya Waziri Mkuu Mstaafu Peter Pinda na kuishukuru familia hiyo kwa ukarimu wao.
Ziara hiyo ya kusherehekea maadhimisho ya Miaka 61 ya Uhuru wa Tanganyika na ambapo Naibu Waziri Mavunde aliitumia siku hiyo kwa kusaidia kuwaongezea mama lishe ujuzi katika ujasiriamali wao.
"Lipo jambo la kujifunza kwa sisi viongozi na kwenu nyie mliofika hapa tujifunze unyenyekevu jamani ukiagalia Waziri Mkuu Mstaafu Pinda kwa nafasi alizozishika lakini leo amekubali nimekuja na mama lishe na akakubali kututembeza shamba lote kwahiyo hapa ndipo tunajifunza Unyenyekevu,"alisema Mavunde.
Alisema kuwa ukiwa kiongozi ukiona watu hawaji kwako hata kuomba maji ujue unashida kwani kiongozi maana yake ni kupokea watu hivyo Pinda na familia yake wana mioyo ya kipekee na ukarimu mkubwa sana.
Aidha Mavunde ametumia ziara Hiyo kutangaza January kufanyika kongamano kubwa la siku ya MWANAMKE DODOMA JIJI ili kutathimi makubaliano ya mwaka mzima yalipofikia.
" Mimi nimejiitolea kulilea hili kundi ili nione mafanikio yao kila mmoja kwa nafasi yake nataka nione wanapiga hatua kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine Serikali ya CCM chini ya uongozi wa Rais Dk Samia imefanya kazi kubwa ya kuendeleza Dodoma inakuwa makao makuu fursa zipo nyingi nataka nione akina mama wa Dodoma wakichangamkia hizi fursa,"alisema Mavunde.
"Siyafanyi haya ili mnichague kuwa mbunge wenu, Sifanyi siasa nafanya haya kwasababu niliomba dhamana ya kuwa kiongozi nina wajibu wa kuwasaidia watu wangu,"alisema Mavunde.
Naye Waziri mkuu Mstaafu Mizengo Peter Pinda amewasihi kushirikiana kuifanya Dodoma kuwa ya Kijani kwani kila mtu mmoja akipanda mti itakua na mwonekano mzuri hiyo hudhihirishwa baada ya mvua kunyesha Dodoma inakuwa na muonekano mzuri.
Pinda alisema kuwa washirikiane katika kupanda miti ili kuifanya Dodoma ipendeze kwani mji ukiwa na kijani kingi ni mji unaovutia sana na kitu kingine yeye huwa anapenda kusema mjasiri wa mali na siyo mjasiriamali kwani ukishakua mjasiri wa mali utakuwa mbali kimaendeleo.
Alimwomba Mavunde amshirikishe kwenye hilo kongamano litakalofanyika Januari ili aweze kuhamasisha washiriki hao kupanda miti.
Nao baadhi ya wajasirimali waliozungumza kwa nyakati tofauti wametoa shukrani zao kwa Mavunde kwani hakuna mbunge aliyeifanya tukio kama hilo kwa kuwakutanisha na kuwapeleka katika mashamba ya Pinda kwani wamejifunza vitu vingi na kuahidi kwenda kufanyia kazi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment