Friday, December 30, 2022

DOREFA YAFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA



DOREFA YAFANYA MKUTANO MKUU WA MWAKA 2022

Na Elizaberth Paulo, Dodoma.

VIONGOZI wa michezo na wanamichezo nchini wameaswa kupambania tasnia ya michezo ili iwe na thamani na kupewa kipaumbele kama tasnia zingine ili ichangiae katika ukuaji wa uchumi wa nchini kama nchi zilizowekeza kwenye michezo Duniani. 

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa michezo Nchini Ally Mayai Tembele wakati akizungumza na wadau wa soka kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa Chama Cha Mpira wa Miguu Dodoma(DOREFA).

Mkutano huo ulikuwa na lengo la kuweka wazi mambo yaliyofanywa na kamati tendaji tangu kuingia madarakani pamoja na changamoto zilizowakumba katika utendaji wao.

Mayai amesema kuwa ili tasnia hii ya michezo iendelee kukua ni wajibu wa kila mwanamichezo kuwajibika kwa nafasi yake katika kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na Umuhimu wa michezo ikiwa ni sehemu ya kuimarisha afya zetu hata uchumi wetu hii itasaidia kukua kwa tasnia hii bila kusahau kuwa na nidhamu kwa kila mmoja kumuheshimu mwenzake bila kujali cheo.

“Nawapongeza chama cha soka cha Mkoa wa dodoma kwa kuweza kufanya kazi bila kuwa na tofauti katika utendaji na hii itasaidia soka la Dodoma kuweza kukua kwa kasi kwani maendeleo bora huletwa na viongozi bora,"amesema Mayai

Ameongeza kwa kupongeza mkoa wa Dodoma kwa kuwa na programu ya vijana chini ya miaka 17 kwani itawasaidia vijana kukua kisoka na kuweza kuvumbua vipaji wakiwa bado na umri mdogo.

"Milango ya serikali ipo wazi kwa yeyote mwenye nia njema na tasnia hii na tunawakaribisha wadau wote kuweza kujitokeza kusapoti vipaji vya watoto wetu kwani kila mtu anaelewa mpira ni ajira kwa ajili ya kukuza uchumi na kuondokana na umasikini na kila mtu ameshuhudia namna ambavyo familia nyingi zimejikwamua kiuchumi kupitia michezo,"amesema Mayai.

Aidha ametoa rai kwa wadau wa mpira wa miguu kupambania haki za watoto katika kupata maeneo ya wazi ya watoto hao kufanyia mazoezi ya michezo yao ikiwa ni haki ya msingi ya mtoto na serikali imetoa maeneo ya wazi katika kila mtaa kwaajili ya michezo na shughuli zingine za kijamii.

“Ndugu zangu wanamichezo tuingie mitaaani kwenda kusaka vipaji, tukaelimishe jamii kuhusiana na haki za watoto wetu katika suala zima la michezo alafu kuna maeneo ya wazi ambayo hayatumiki kwa kazi zilizopangwa sasa hili nawaachia fuatilieni maeneo ya wazi kwaajili ya hiyo michezo alafu huko mitaani ndiko kwenye chimbuko la mpira wa miguu na hata historia ya watu wengi maarufu waliofanikiwa kwenye soka historia yao inaonyesha wametokea mitaani,"amesema Mayai

Kwa upande wake mwenyekiti wa Chama Cha Mpira wa Miguu Dodoma (DOREFA) Mohamed Aden amesema kuwa anawashukuru wadau wa soka jijini hapa kwa kuendelea kutoa maoni na ushauri ili kuhakikisha wanaboresha sekta ya michezo haswa mpira wa miguu jijini Dodoma.

Naye mwakilishi wa wanamichezo Jijini Dodoma amesema sekta ya michezo iko vizuri ila wanaiomba serikali chini ya Waziri wa Michezo Mohamed Mchengerwa kuwatatulia changamoto inayojitokeza ya mara kwa mara ya uwanja wa Jamhuri kufungiwa mara kadhaa kutokana na matumizi mengine ambayo ni tofauti na michezo hivyo kufanya wapenzi wa soka Jijini hapa kukosa burudani ya mpira wa miguu na kutumia viwanja vingine vilivyopo nje ya Dodoma.


No comments:

Post a Comment