Na John Gagarini,Chalinze
WIZARA ya Biashara Viwanda na Uwekezaji imesema kuwa imeweka
mazingira mazuri ya uwekezaji na kuzitaka taasisi zinazohusika na uwekezaji
kutokuwa na ukiritimba.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Biashara Viwanda na Uwekezaji
Charles Mwijage kwenye Kitongoji cha Pingo Chalinze wakati akiweka jiwe la
Msingi kwenye kiwanda cha Vigae cha Twyford Ceramics Ltd.
Mwijage alisema kuwa uwekezaji kama huu unaendana na dhana ya
Rais Dk John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda ambapo itaongeza pato la
nchi na itazalisha ajira kwa wingi.
“Baadhi ya idara ambazo zinafanikisha uwekezaji ikiwa ni
pamoja na brela, idara ya uhamiaji, idara ya kazi, mamlaka ya mapato TRA,
wizara ya ardhi, shirika la viwango TBS, Baraza la Mazingira NEMC na nyinginezo
zinapaswa kufanya kazi kwa wepesi ili kufanikisha uwekezaji,” alisema Mwijage.
Alisema kuwa kati ya idara hizo baadhi zimekuwa zikifanya
vizuri lakini nyingine zimekuwa zikiwapa usumbufu mkubwa wawekezaji hali ambayo
inawakatisha tamaa.
“Kwa upande wa wizara yangu hakuna tatizo lolote lakini kuna
baadhi ya idara zimekuwa kero kubwa kwa wawekezaji kwa kuwa na ukiritimba usio
na sababu naomba kama kuna idara zinakuwa kikwazo niambieni ili tuwachukulie
hatua,” alisema Mwijage.
“Viwanda vikiwa vingi nchi itapata mapato makubwa kupitia
kodi ambazo zitalipwa kutokana na uuzwaji wa bidhaa zitakazokuwa zinazalishwa
viwandani,” alisema Mwijage.
Alisema kuwa nchi zilizofanikiwa kukuza uchumi wake kupitia
viwanda zimeweza kutoa ajira nyingi hasa kwa vijana kupitia sekta rasmi na
isiyo rasmi.
Kwa upande wake mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho Jack Feng
alisema kuwa kiwanda hicho asilimia 95 ya malighafi itakuwa inatoka hapa nchini
ambapo kigae kinatumia maligahafi zaidi ya 10.
Feng alisema kuwa mara kiwanda hicho kitakapokamilika Agosti
mwaka huu kitaweza kupunguza asilimia 30 ya uagizaji wa vigae toka nje ya nchi.
“Tunatarajia kuajiri wafanyakazi 2,000 moja kwa moja na 4,000
kazi za muda na gharama ya mradi huu ni dola milioni 56 sawa na bilioni 120
ambapo tunatarajia kuuza hadi nje ya nchi kama vile Zambia, Uganda, Rwanda na
Burundi,” alisema Feng.
Alisema kuwa wanaunga mkono nchi ya Tanzania kuwa na mpango
wa kuwa nchi ya viwanda na wao wanapenda kuwa mfano kwa wawekezaji.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa kituo cha uwekezaji
Cliford Tandari alisema kuwa uwekezaji wa kiwanda hicho ni wa mfano kwani
utavutia makampuni mengi.
Tandari alisema kuwa hadi sasa kituo chake kimeweza kutoa
wigo mkubwa katika kuandikisha miradi mbalimbali toka china na kufikia miradi
667 ambayo itazalisha ajira 83,141 kwa watanzania ambapo miradi 452 ni miradi
inayohusiana na sekta ya uzalishaji viwandani.
Naye mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema
kuwa kwa sasa mkoa huo umeweza kuwa na viwanda 264 huku vikubwa vikiwa ni
viwili.
Ndikilo alisema kuwa uwekezaji huo ni mkubwa na unatarajia
kukuza ajira kwa vijana wa mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.
Alisema kuwa mkoa wa Pwani bado una maeneo makubwa ya
uwekezaji na tayari kuna eneo lenye bukubwa wa hekari 5,000 linahitaji
mwekezaji na wameamua mkoa huo kuwa kituo cha uwekezaji.
Naye Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete
aliwapongeza wawekezaji hao kutoka nchi ya China na kusema kuwa Chalinze nayo
imejipanga kuwa sehemu ya uwekezaji ambapo kuna ujenzi wa viwanda mbalimbali.
Ridhiwani alisema kuwa changamoto kubwa inayokabiliwa
wananchi na wawekezaji ni ukosefu wa maji ambapo wamekuwa wakijitahidi
kuikabili lakini bado hawajafanikiwa kuidhibiti aliomba wawekezaji hao kutoa
ajira bila ya kuwabagua wenyeji.
Mwisho.
 |
No comments:
Post a Comment