Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo |
Baadhi ya wachezaji wa Kiluvya United inayoshiriki ligi daraja la kwanza wakimskiliza mkuu wa mkoa wa Pwani hayupo pichani walipomtembelea ofisini kwake mjini Kibaha |
Nahodha wa Timu ya Kiluvya United ya mkoani Pwani Ramadhan akishukuru baada ya kukabidhiwa fedha kwa ajili ya hamasa na mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo. |
Na John Gagarini, Kibaha
KUELEKEA mchezo wake wa ligi daraja la Kwanza leo dhidi ya
Ruvu kuwania kupanda Ligi Kuu unaotarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Filbert Bayi wilayani Kibaha
mkoa wa Pwani umeipatia timu ya Kiluvya United kiasi cha shilingi milioni mbili
kwa ajili ya hamasa ili waweze kushinda mchezo huo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi fedha hizo kwa viongozi wa
timu hiyo walioambatana na wachezaji ofisini kwake mjini Kibaha mkuu wa mkoa wa
Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa lengo ni kuhakikisha wanashinda
mchezo huo.
Ndikilo alisema kuwa viongozi wa timu hiyo walifika ofisini
kwake na kuomba msaada wa kuisaidia timu yao ili iweze kufanya vizuri kwenye
michezo yake mitano iliyosalia ya ligi hiyo na endapo watashinda watafanikiwa
kupanda Ligi Kuu ya Voda Com.
“Tuko pamoja na timu yetu ambayo inawakilisha mkoa na leo tunawakabidhi
fedha ambazo zimetolewa na wadau wa mkoa ili kufanikisha malengo ya kupanda
Ligi Kuu kwani uwezekano huo upo,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa wadau wanachotaka ni timu yao kushinda kwani imeonyesha
ina uwezo wa kufanya hivyo kutokana na uwezo inaounyesha wanaamini inaweza
kufanya vizuri na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya harakati zake za kiutaka
kupanda daraja ili kufikia Ligi Kuu ya Voda Com.
“Wadau wa soka wa mkoa wa Pwani wamejitolea fedha hizo kama
hamasa ya kufanya vyema kwenye mchezo wa leo ambao utakuwa na ushindani mkubwa
kwani timu hizo ziko kwenye nafasi nzuri ya kupanda Ligi Kuu ambapo Ruvu ndiyo
kinara wa kundi hilo na United wakiwa kwenye nafasi ya tatu,” alisema Ndikilo.
Aidha alisema kuwa mdau ambaye anataka kuipeleka timu ya
Kiluvya United nchi ya Ulaya ya Finland atafurahi kuona timu hiyo inashinda
mchezo huo na kutoa zawadi ya mwaka mpya kwa wadau wa mkoa wa Pwani.
Naye nahodha wa timu hiyo Ramadhan Ally alisema kuwa wao wkao
tayari kwa pambano hilo na watahakikisha wanapambana kwa nguvu zote ili wapate
ushindi na kujiweka vizuri kwenye harakati zao za kupanda daraja.
Ally alisema kuwa kutokana na kupewa fedha hizo zitawasaidia
kama morali kwao kwa ajili ya kupata ushindi huo ambao utakuwa muhimu ili
kuwapa raha watu wa mkoa wa Pwani.
Mwisho.