Na John Gagarini, Bagamoyo
WANANCHI wa Kijiji cha
Msinune kata ya Kiwangwa wilayani Bagamoyo mkoani Pwani wameiomba serikali
kuwasaidia kujenga nyumba ya mganga ambaye anaishi kwenye chumba cha kuzalishia
kwenye zahanati ya kijiji hicho.
Akizungumza mbele ya mbunge wa Jimbo la Chalinze Said
Bwanamdogo wakati wa kikao cha Halamshauri ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya
Kiwangwa, mwenyekiti wa Kijiji hicho Kesi Hassan alisema mganga huyo inabidi afanye
hivyo kutokana na kukosa nyumba.
Hassan alisema kuwa mganga pamoja na muuguzi wanatumia
wanaishi humo kutokana na uhaba wa nyumba za watumishi katika kijiji hicho.
“Tunaiomba serikali na kwa kupitia kwako kutusaidia ujenzi wa
nyumba za watumishi kwani kutumia chumba kinyume na matumizi si sawa na
haipendezi mazingira ni magumu,” alisema Hassan.
Aidha alisema kuwa watumishi wengi hawana nyumba za kuishi
hivyo kuwapa wakati mgumu katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya
kuwahudumia wananchi.
“Suala la nyumba za watumishi ni changamoto ambayo inatukabili
hivyo ni vema kukawa na nguvu ya ziada kutoka juu ili kutusaidia watumishi wetu
waweze kukaa kwenye mazingira mazuri.
Kwa upande wake Bwanamdogo alisema kuwa suala hilo amelipata
na ataangalia jinsi gani ya kuweza kulifanyia kazi ili mganga huyo na watumishi
wengine waweze kuweza kuwa na nyumba.
Bwanamdogo aliwataka viongozi na wananchi kwenye vijiji vya
Jimbo hilo kujitolea kwa kutumia nguvu zao ili kuanzisha ujenzi wa nyumba za
watumishi na ofisi yake itachangia.
Mwisho.