Tuesday, February 11, 2025

WAANDIKISHAJI WASAIDIZI DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA HALMASHAURI YA MJI KIBAHA WAASWA





WAANDIKISHAJI wasaidizi wa zoezi la uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura Halmashauri ya Mji Kibaha wametakiwa kuwa waadilifu na waaminifu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dk Rogers Shemwelekwa alipokuwa akifunga mafunzo ya siku mbili kwa waandikishaji wasaidizi kwenye Halmashauri hiyo.

Shemwelekwa amesema kuwa waandikishaji hao wasaidizi wamepewa jukumu kubwa na wameaminiwa kwani zoezi hilo ni la Kitaifa hivyo wahakikishe wanalifanya kwa weledi ili kuepusha changamoto zinazoweza kujitokeza.

Amesema mafunzo hayo yawe chachu ya utendaji kazi wao kwenye zoezi la uboreshaji taarifa za wapiga kura na kuandikisha wapiga kura wapya litakuwa la siku saba kuanzia Februari 13 hadi 19.

Amewataka watumie lugha nzuri wakati wakiwahudumia wananchi ili iwe sehemu ya kuwavutia watu wengi wajitokeze kuboresha taarifa zao na kuandikisha wapiga kura wapya.

Jumla ya waandikishaji 262 wamepatiwa mafunzo hayo na kuna vituo 131 vitatumika kwenye zoezi hilo ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwaka huu.


Sunday, February 9, 2025

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA TAMISEMI YARIDHISHWA MIRADI YA ELIMU NA AFYA HALMASHAURI YA MJI KIBAHA





KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imekagua miradi ya ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kibaha iliyogharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.1.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha Catherine Saguti kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashari wakati akitoa taarifa juu ya ujenzi wa hospitali hiyo.

Dk Saguti amesema kuwa mapokezi ya fedha za mradi wa Ujenzi wa Hospitali na ununuzi wa vifaa tiba kutoka Serikali Kuu yalitolewa kwa awamu nne 
jumla ya shilingi bilioni 3.3 kwa ajli ya ujenzi na shilingi milioni 400  kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. 

"Fedha hizo zimepokelewa kwa awamu kuanzia mwaka wa fedha 2019/2020, 2020/2021, 2021/2022 na 2024/25 na jumla ya majengo ambayo yamejengwa hadi sasa ni 14 na majengo 11 yamekamilika na yanatumika huku majengo matatu yanaendelea na utekelezaji katika hatua ya
ukamilishaji,"amesema Saguti.

Amesema kuwa Halmashauri imechangia jumla ya shilingi milioni 446.7 kwa ajili ya ukamilishaji wa
miundombinu na majengo ambayo hayakukamilika kwa fedha za Serikali Kuu.

Pia kamati hiyo imetembelea ujenzi wa kituo cha afya cha Kata ya Pangani kilichogharimu kiasi cha shilingi milioni 914 huku Halmashauri ya Mji Kibaha ikichangia kiasi cha shilingi milioni 189 kutokana na mapato ya ndani.

Wabunge hao wa Kamati ya Tamisemi walitembelea mradi wa shule mpya ya sekondari ya Kata ya Tangini iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 528.9.

Ujenzi huo umetokana na mradi wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 398 wa kidato cha kwanza na cha pili wanawake 191 na wanaume 207.

Katika hatua nyingine kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Tamisemi pia ilitembelea ujenzi wa Shule ya Msingi Mtakuja Kata ya Pangani ambayo ina mfumo wa Kiingereza ambayo imegharimu kiasi cha shilingi milioni 309.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Zainab Katimba amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imewekeza fedha nyingi kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya na elimu.

Katimba amesema kuwa Serikali imewekeza kwenye miradi mingi ili kuwaletea wananchi huduma karibu na maendeleo ili kupunguza changamoto.

Amesema kuwa maagizo na maelekezo yaliyotolewa na kamati ili kuboresha miradi hiyo wataifanyia kazi ili iwe na ubora na kuwa na manufaa kwa wananchi.  

Akitoa majumuisho ya ziara ya Kamati Mwenyekiti wa kamati hiyo Justin Kamoga amesema wameridhishwa na ujenzi wa miradi hiyo kwani imejengwa kwa viwango vizuri.

Kamoga amesema licha ya miradi hiyo kujengwa vizuri lakini kuna baadhi ya changamoto ndogo ndogo ikiwa ni pamoja na kukamilisha baadhi ya maeneo yaliyobakia.

Friday, February 7, 2025

KITUO CHA AFYA VIGWAZA MBIONI KUKAMILIKA

KITUO cha afya cha Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoani Pwani kiko kwenye hatua za mwisho kukamilika ambapo kitatoa huduma mbalimbali zikiwemo za upasuaji hivyo kuwaondolea kero za akinamama za kujifungua.

Aidha serikali imetoa kiasi cha shilingi milioni 525 kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya kwenye Kata hiyo hivyo kuondoa changamoto hasa za mama wajawazito wakati wa kujifungua.
 
Diwani wa Kata ya Vigwaza Mussa Gama akizungumza Vigwaza wakati wa maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) amesema kwa sasa wananchi hususani wanawake waliokuwa wanashindwa kujifungulia kwenye Zahanati ya Vigwaza ambapo hawatapelekwa tena Mlandizi na Chalinze kupata huduma hizo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Lulu Rajabu kata ya Vigwaza amesema wanawake walikuwa wakikumbana na adha ya kutembea kilometa tisa na zaidi kipindi wanaposhindwa kujifungulia kwenye Zahanati.

Katika maadhimisho hayo wanachama wa CCM kutoka maeneo mbalimbali ya kata hiyo walioshiriki kupanda miti kwenye kituo hicho sambamba na kufanya harambee ya ujenzi wa ofisi ya chama ambapo zaidi ya milioni tatu zilichangwa 


Friday, January 31, 2025

TAKUKURU PWANI YAONGEZA MAPATO KUTOKA M 4.6 HADI M 12

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Pwani imefanikiwa kuongeza makusanyo kutoka kiasi cha shilingi milioni 4.6 hadi 12 kwa wiki kwenye kizuizi cha Maliasili cha Wilaya ya Kibiti.

Aidha kutokana na kuongezeka kwa mapato hayo kwa mwaka mmoja kupitia kizuizi hicho Maliasi watakuwa na uwezo wa kukusanya kiasi cha shilingi milioni 480 kwa mwaka.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Pwani Alli Sadiki alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake juu ya mafanikio yaliyopatikana kipindi cha miezi mitatu iliyopita kuanzia Oktoba hadi Disemba mwaka jana.

Sadiki amesema kuwa mafanikio ya makusanyo hayo yamefikiwa baada ya Takukuru kufanya uzuiaji katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato kwa kutumia mashine ya Pos.

"Uzuiaji huo ulikuja baada ya taasisi hiyo kutoridhishwa na ukusanyaji mapato kwani yalikuwa ni madogo kulingana na uwezo mkubwa wa kizuizi hicho,"amesema Sadiki.

Amesema kuwa Takukuru ilisimamia ukusanyaji kuanzia Novemba 5 mwaka 2024 hadi Novemba 11 mwaka huo kwa saa 24 na kufanikiwa kukusanya kiasi hicho cha shilingi milioni 12  badala ya shilingi milioni 4.6 kwa wiki moja.

Aidha amesema kuwa walibaini kuwa baadhi ya wakusanyaji ushuru walipewa fedha na wenye mizigo ili wasitozwe malipo ya serikali, baadhi ya magari hayakukaguliwa hivyo kukwepa kulipa ushuru, baadhi ya wakusanyaji kupewa mwanya ukadiriaji wa chini wa malipo.

Pia katika kipindi hicho walifanya ufuatiliaji wa miradi 52 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi bilioni 12 ambapo hakukuwa na mapungufu huku mingine ikiwa inaendelea na utekelezaji.

Ameongeza kuwa miradi hiyo ni ya sekta za afya, elimu, maji, barabara na katika uelimishaji umma wamefanya semina, mikutano ya hadhara, vipindi vya redio, kuimarisha klabu za wapinga rushwa na Takukuru Rafiki ambapo wamezifikia kata 11.

"Katika kipindi hicho Takukuru ilifungua kesi 24 mahakamani ambapo washitakiwa 13 wametiwa hatiani na tulipokea malalamiko 60 kati ya hayo 37 yalihusu rushwa na yanafanyiwa kazi yakiwa kwenye hatua mbalimbali,"amesema Sadiki.

Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa huo kuendelea kuunga mkono jitihada za mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwafichua wale wanaoshiriki vitendo vya rushwa.

Monday, January 27, 2025

KIBAHA SASA YAWA MANISPAA

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Dk Samia Suluhu Hassan kuipandisha hadhi Halmashauri ya Mji Kibaha kuwa Manispaa.

Koka ametoa shukrani hizo Mjini Kibaha wakati wa Mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kuunga mkono azimio la Mkutano Mkuu wa (CCM) Taifa kumpitisha Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea pekee wa kiti cha Urais kupitia chama hicho kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka huu na kumbukumbu ya kuzaliwa Rais.

Aidha Mbunge huyo amepongeza kuteuliwa Dk Hussein Mwinyi kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM Zanzibar na kuchaguliwa kwa Dk Emanuel Nchimbi kuwa Mgombea Mwenza na Steven Wasira kuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM.

Amesema kuwa hicho kilikuwa ni kilio chao kwa miaka mingi hivyo kupandishwa hadhi kwa Kibaha kutachochea maendeleo kwa wananchi kwani hata bajeti itakuwa ni kubwa na hata maslahi kwa watumishi wa umma.

Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mohamed Mchengerwa ametangaza rasmi hali ambayo ilizua furaha kubwa na amesema kuwa suala hilo ni jambo ambalo lililokuwa likisubiriwa kwa muda mrefu na sasa limekuwa.

Mchengerwa amesema kuwa kulikuwa hakuna sababu ya kutokuwa Manispaa lakini sasa wakati umefika na sasa Serikali imeridhia Mji wa Kibaha kuwa Manispaa ambapo ni makao makuu ya Mkoa wa Pwani.








Sunday, January 12, 2025

MANARA KUIUNGA MKONO SAMIA CUP KUTOA MILIONI 1

MDAU wa Mpira wa Miguu nchini Haji Manara ameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 1 kwa ajili ya mashindano ya Samia Cup  Wilayani Kibaha Mkoani Pwani ambayo yameandaliwa na Umoja wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Kibaha.

Manara alitoa ahadi hiyo kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mtongani  Mlandizi Kibaha wakati akizindua michuano hiyo ambayo itashirikisha timu 104 kutoka kwenye Kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha yakiwa na lengo la kuhamasisha wananchi wakiwemo vijana kujiandikisha na kushiriki kwenye uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

 

Alisema kuwa amevutiwa na vijana kuandaa mashindano kama hayo ambayo yanaunga mkono jitihada za Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuchangia kwenye michezo kwani ni sehemu ya kuleta maendeleo nchini.

 

“Kutokana na kitu kizuri mlichokiandaa nitaunga mkono na nitawapatia kiasi cha shilingi milioni 1 ili mfanikishe mashindano haya yafanyike kwa ufanisi mkubwa na kufikisha vizuri ujumbe wa vijana kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura litakalofanyika Februari na kushiriki uchaguzi mkuu,”alisema Manara.

 

Kwa upande wake katibu wa hamasa wa UVCCM Godfrey Mwafulilwa alisema kuwa lengo la mashindano hayo ni kuhamasisha watu kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la mpiga kura na kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa watu kuboresha taarifa zao.

 

Kwa kila kata watacheza hatua na kupata timu na kuingia hatua ya 16 bora ngazi Wilaya zawadi ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya guta la matairi matatu, mshindi wa pili atajinyakulia pikipiki na mshindi wa tatu atapata kiasi cha shilingi milioni 1.  

 

Mwafulilwa alisema kuwa kwenye mashindano hayo hakutakuwa na kiingilio na kila timu itapatiwa jezi na mipira miwili huku zawadi nyingine ni mchezaji bora kipa mfungaji kila mmoja atapata ngao na shilingi 50,000 na timu yenye nidhamu shilingi 100,000.


Naye mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Pwani COREFA Robert Munis alisema kuwa malengo yao ni kuhakikisha mpira Pwani unachezwa kwa kuzingatia taratibu na watashirikiana na wadau wanaoandaa mashindano mbalimbali lengo likiwa ni kuhakikisha vijana wanakuza vipaji vyao kwani soka ni ajira.

 

Munis alisema kuwa anawapongeza wadau hao kwa kuandaa mashindano hayo ambayo ni makubwa kwenye mkoa huo ambapo makubwa zidi ni yale yaliyoandaliwa na Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Omary Kipanga ambaye pia Mbunge wa Mafia.

 

Baadhi ya viongozi wa timu hizo waliwashukuru waandaaji wa mashindano hayo timu za Kujiandikisha na timu oresha taarifa zilitoka sare ya bao 1-1.

 

Mwisho.

VIJANA16 WENYE VIPAJI VYA SOKA KUWAKILISHA MKOA WA PWANI



VIJANA 16 wenye vipaji vya soka kutoka kwenye vituo vya Chama Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Pwani (COREFA) wenye umri wą miaka kati ya14 na 16 wamechaguliwa kwenda kwenye majiribio Mkoani Tanga baada ya kuchaguliwa na wataalamu wa soka kutoka Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Akizungumza na waandishiwa habari ofisini kwake Mwenyekiti wa Chama Cha Soka Mkoa wa Pwani (COREFA) Robert Munis alisema kuwa vijana hao wamepatikana kutoka vituo vya soka vya Wilaya za Mkoa huo baada ya kufanyiwa mchujo na Tff na baadaye Fifa wanakwenda Tanga na wakifuzu wataendelezwa na Fifa.

Munis alisema kuwa Wilaya zote zilishiriki mchujo huo isipokuwa wilaya ya Mafia ambapo wataalamu hao walishindwa kwenda kutokana na changamoto ya usafiri wa kufika huko.

"Tunaishukuru Fifa na Tff kwa kuwachukua vijana hao ambao ni wanafunzi kwa lengo la kuwaendeleza kwani itakuwa ni faida ya baadaye kwa nchi na itawasaidia vijana hao kuendeleza vipaji vyao na familia zao zitanufaika kwani kwa sasa mpira ni ajira kubwa sana,"alisema Munis.

Alisema kuwa hiyo ni bahati kwa vijana hao kikubwa wanachotakiwa ni kuonyes ha vipaji vyao na kwao hilo ni fanikio kubwa kupeleka vijana hao kuuwakilisha mkoa huo kwenye kituo cha Tff cha Mnyanjani cha kuendeleza vipaj vya vijana.

"Wazaz wao wanapaswa kuwahamasisha vijana wao washiriki michezo na waache dhana kuwa mtoto akishiriki michezo hatafanya vizuri darasani hiyo siyo kweli kwa ninichezo na michezo vinakwenda pamoja ambapo michezo inafanya akili inakaa vizuri hivyo kufanya vizuri kwenye masomo,"alisema Munis.

Naye mmojawapo wa watoto hao Tariq Mkenda alisemia kuwa wänamshukuru Mungu kwa kuwapatia näfasi hiyo na watahakikisha wanaonesha vipaji vyao ili wafanye vizuri na wachaguliwe na kwenda mbele zaidi waje kuitumikia nchi yao.

Rashid Said alisema kuwa wanaishukuru Corefa Tff na Fifa kwa kuona vipaji vyao na kuviboresha kwani itawasaidia waweze kuonyesha uwezo wao ili waje kuwa wachezaji bora watakaoleta mageuzi ya soka hapa nchini na kuwoamba wazazi nao wawaunge mkono kwa kuwapatia vifaa na muda wa kushiriki michezo.

Aziz Mwashambwa alisema kuwa wamefurahishwa sana na mpango huo wakuwa endeleza watotoili waendeleze vipaji vyao kwani hiyo itawasaidia kufika mbali kisoka na kuja kuwa wachezaji bora wa baadaye.

Mwashambwa alisema kuwa soka la kisasa linawekezwa kwa vijana na itakuwa ni nafasi nzuri ya kubadi soka la Tanzania na kufungua ukurasa mpya wa mpira wa Tanzania kwani mpango huo wa kuwa endeleza vijana ambapo uko kwenye mikoa 14 hapa nchini ambapo watoto hao watakutana huko.