Tuesday, April 9, 2024

*WMAs ZATAKIWA KUWA NA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA*

 

Serikali imewataka viongozi wa Jumuiya za Hifadhi Wanyamapori (WMAs) kuzingatia matumizi sahihi ya fedha  ili kuwanufaisha wananchi wa vijiji wanachama   pia kuzingatia mikataba inayoingiwa na WMAs hizo  kwa maslahi ya Taifa.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) ametoa kauli hiyo  leo Aprili 8,2024 Jijini Dodoma wakati wakati wa kikao cha viongozi wa Jumuiya hizo pamoja  na baadhi ya maofisa wanyamapori wa wilaya kuhusu changamoto za usimamizi wa maeneo ya WMAs nchini.

Amesema rasilimali fedha ni lazima  zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa ikiwa ni pamoja na kuendeleza miradi ya maendeleo ya vijiji kwa kuwashirikisha wananchi wa vijiji hivyo. 

 “Ni lazima muweke mkazo katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na uwazi na matumizi sahihi ya fedha pamoja na  utoaji wa taarifa kwa wanufaika kwenye vijiji husika, msipofanya hivyo uongozi utageuka shubiri mtakapofanyiwa ukaguzi” Mhe. Kairuki alisisitiza.

Amesema kuwa katika kipindi cha Mwaka wa fedha  2022/2023 Serikali imetoa mgao wa takribani bilioni 9.6 ambazo Serikali  inaamini zimetumika kwa mujibu wa Kanuni za WMAs ambazo zinaelekeza kuwa sehemu ya fedha hizo zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo ya vijiji. 

Amesema kupitia kanuni hizo za uanzishaji na uendelezaji wa maeneo ya hifadhi kwa sasa kuna jumla ya WMAs 22 zilizodhinishwa na kupata haki ya matumizi ya rasilimali za wanyamapori lakini kuna nyingine 16 ambazo ziko kwenye mchakato wa kuanzishwa.

Aidha, ametumia fursa hiyo kuzishukuru WMAs kwa mchango wao katika kusaidia  kukuza uchumi kwa mtu mmoja mmoja na katika jamii  pamoja na kusaidia katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika jamii na vijiji wanachama.

“Hii imejidhirishisha katika Sekta ya uwindaji wa Kitalii na utalii wa picha ambapo tumeshuhudia umekuwa chachu ya uchumi  kwa vijiji wanachama ambao wanaunda jumuiya zetu” Mhe. Kairuki amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Kairuki alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Wadau wa uhifadhi imeendelea na jitihada mbalimbali za kuhakikisha Jumuiya zinaendelea kuimarika ikiwa ni pamoja na kuwajengea uwezo viongozi wa WMAs kwa lengo la kuimarisha utawala na usimamizi wa maeneo hayo na kuwezesha mafunzo kwa Askari wa Wanyamapori wa Vijiji (VGS) ambapo takribani VGS 540 wamepata mafunzo katika Chuo cha Wanyamapori Likuyuseka – Maganga.

Pia amesema Serikali imewezesha upatikanaji wa vitendea kazi ikiwemo magari ya doria kwa baadhi ya Jumuiya kama Mbarangandu na Nalika, Vilevile, Jumuiya zimewezeshwa vifaa vya uwandani kama vile mahema, GPS, kamera, sare za Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) na vifaa vya ofisini kama kompyuta katika Jumuiya za MBOMIPA, WAGA na UMEMARUWA.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Kamishna CP Benedict Wakulyamba, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Dkt. Fortunata Msoffe ,Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA,wawakilishi wa Makamishna Uhifadhi wa TANAPA, NCAA na TFS, Wakuu wa Idara na Taasisi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Maafisa Wanyamapori wa Wilaya, Wadau wa Wizara ya Maliasili na Utalii na  Viongozi wa Jumuiya za Wanyamapori.

Sunday, April 7, 2024

WASICHANA WATAKIWA KUWA MABALOZI KUPINGA VITENDO VYA UKATILI


Kamati ya Kupinga Ukatili wa kijinsia iliyo chini ya Wanawake na Samia imewataka wasichana ( Mabinti ) kuhakikisha wanakuwa viongozi wa kujiongoza wenyewe ili kuhakikisha wanapingana na suala zima la ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri Ili kukomboa jamii inayokumbana na suala la unyanyasaji wa Mabinti na wanawake.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa kamati ya ukatili wa kijinsia mkoa wa Dodoma  Grace Ringo wakati wa mafunzo ya utoaji  wa elimu katika chuo Mipango  chini ya uongozi wa Binti Makini kuhusu kupinga unyanyasaji kwa wanawake.

Amesema yapo mambo ambayo mwanamke wanakutana nayo kama Ulawiti, kupigwa , pamoja na kukosa haki ambazo zinamfanya mwanamke akashidwa kujiamini katika nafasi yake na kupelekea anguko  la uchumi katika jamii hata familia hivyo niwaombe Mabinti ambao mmepata elimu leo muhakikishe mnasaidia jamii

Kwa upande wake Mjumbe wa kamati ya ukatili wa kijinsia Mkoa wa Dodoma Irene Sanga amewasihi Mabinti kutumia mitandao kwa ajiri ya kuwaingizia kipato na sio kutumia mitandao kwa kufanya mambo maovu huku akiwasisitiza wawe na nidhamu Katika jamii ya leo

"Wapo Mabinti ambao wanatumia mitandao kwa kuangalia vitu visivyofaha na kupelekea Vijana kualibika kwa kuiga mambo ambayo kwa nafasi na umri bado na kulazimisha kufanya vitu kama rushwa za ngono," amesema Sanga.

Naye Mjumbe wa kamati ya kupinga ukatili chini ya ofisi ya Mkoa wa Dodoma  Rhoda Denis amewataka wasichana kuzingatia kujithamini na kujitambua  Ili kujikomboa katika maisha ya jamii ya leo.

"Wapo wanawake wanapigwa na waume zao sababu kukosa kujitambua ila kama utajua thamani yako utaweza kufika sehem ambayo utaweza kupata msaada," amesema Rhoda

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Binti Makini Chuo Cha Mipango Dodoma Swaumu Rajabu amewahimiza wanawake kujitokeza kugombania nafasi mbalimbali za uongozi kwani wanawake tunanafasi kubwa sana katika jamii leo hivyo tuwe mstari wa mbele kuwasihi na wengine unaowaona wanaweza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika nchi yetu .

 Aidha amesema kuwa chuo Cha mipango kinaenda kufanyika uchaguzi wa viongozi wa serikali ya wanafunzi ikiwemo nafasi mbalimbali kama Rais wa chuo Cha mipango, wabunge pamoja nafasi nyingine hivyo amewaomba Binti Makini wote wenye sifa wajitokeze wakagombee nafasi hizo.

Ikumbukwe kuwa kamati ya Kupinga Ukatili wa kijinsia iliyochini ya wanawake na Samia inaendelea kufanya mafunzo ya utoaji wa elimu kwa wanawake na wanaume ili kuhakikisha elimu hii inawafikia wengi ili kutengeneza Taifa lenye nguvu kazi na lenye Maadili ikiwa na kauli mbiu IPELEKE DODOMA DUNIANI NA DUNIA  ILETE  DODOMA

Saturday, April 6, 2024

MTAA WA KWAMFIPA WAANZA UJENZI WA SEKONDARI

MTAA wa Kwamfipa Kata ya Kibaha Mkoani Pwani umeishukuru serikali kwa kuwapatia kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ambayo utawapunguzia changamoto wanafunzi wa Mtaa huo wanaotembea umbali wa Kilometa nane kwenda Shule ya Sekondari ya Simbani.

Hayo yamesemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kibaha Mohamed Muanda alipotembelea kuangalia maendeleo ya ujenzi huo kwani ni ukombozi kwa wanafunzi wanaotoka kwenye Mtaa huo.

Muanda amesema kuwa hicho kilikuwa kilio cha wananchi wa Mtaa huo pamoja na Mtaa wa Mwendapole ambapo Mitaa hiyo miwili ina jumla ya shule tatu za Msingi ambapo wanafunzi wote husoma Shule hiyo ya Simbani ambayo ni ya Kata.

Kwa upande wake Mjumbe wa Serikali ya Mtaa huo Jumanne Mwinshehe amesema kuwa wananchi walijitolea kwa kufanya usafi kabla ya ujenzi kuanza huo ukiwa ni mchango wa wananchi na wataangalia fedha za Halmashauri zitaishia wapi ili wananchi wachangie ambapo ujenzi huo uko hatua ya msingi.

Naye Christina Sabai wanafunzi wanakwenda Sekondari mbali na kwa watoto wa kike ambao hukumbana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kurubuniwa na waendesha pikipiki na kuhatarisha masomo yao kwa kupata ujauzito.

Aidha fundi wa ujenzi wa mradi huo wa Shule hiyo Juma Mabula amesema watatumia siku 75 kukamilisha ujenzi huo kwani vifaa vyote viko hivyo wanaamini watakamilisha kwa muda uliopangwa ili wanafunzi waanze kusoma.

Friday, April 5, 2024

TAASISI YA KUMUOMBEA RAIS NA WASAIDIZI WAKE YAFANYA MAOMBI KUIOMBEA SERIKALI

 

Na Wellu Mtaki, Dodoma

Taasisi ya kumuombea Rais  na wasaidizi wake imefanya maombi ya kuombea viongozi wa serikali akiwemo Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Spika wa Wabunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Tulia Akson pamoja na Mawaziri na Wabunge. 

Katibu Mkuu wa taasisi hiyo Angelina Malembeka akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya maombi hayo amesema lengo ni kuwaombea ili waongoze kwa hekima.

Malembeka amesema kuwa anaamini taasisi hiyo itaweza kusaidia mambo mengi yasiyofaa yasipate nafasi na malengo ya taasisi ni kumuombea Rais  na wasaidizi wake pamoja na wataalamu mbalimbali wanaofanya shughuli za jamiii ndani ya nchi.

"Katika utekelezaji wa miradi mbalimbali na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) mambo yanaenda vinzuri ila wao wanafanya kazi ya kuombea Ili kuhakikisha utekelezaji unaenda vizuri zaidi,"amesema Malembeka.

Alisema wanaona mambo yanaenda vizuri katika miradi mbalimbali na utekelezaji wa ilani ya CCM na kazi yao ni kuombea viongozi wawe na ujasiri, nguvu na kuwapa matumaini na ikumbukwe kuwa suala hili la kuombea Rais na wasaidizi wake ni suala la muendelezo na kazi yake ni kujenga Taifa lenye hofu ya Mungu.

Aidha amesema kuwa idadi ya wanachama ni zaidi ya wanachama 600 lakini walioshiriki maombi hayo walikuwa ni 208 ambapo wengine hawakuhudhuria kutokana na sababu mbalimbali.


 

Thursday, April 4, 2024

MKUU WA MKOA DODOMA ROSEMARY SENYAMULE AKAGUA MIRADI YA MAENDELEO

Ziara ya kikazi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, imeendelea Wilayani Kondoa April 3/ 2024 ambapo amefanya ukaguzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa wilayani humo ikiwemo Ujenzi wa Wodi ya wazazi, jengo la Mochwari na jengo la upasuaji katika hospitali ya wilaya ya kondoa.

Aidha amekagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari  ya wasichana Kondoa pamoja ukaguzi wa nyumba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya kondoa mji ambapo ujenzi unaendelea na unatarajia kukamilika muda wowote kwani umefika hatua za umaliziaji ( Finishing).

Hatahivyo Mhe. Senyamule ameendelea kuwahimiza watumishi wa sekta ya afya kuendelea kutunza mazingira yanayozunguka katika vituo vyao ili kuendelea kuweka mazingira safi na ya kuvutia siku zote ikiwemo kupanda miti kwa mpangilio unaofaa.

SIDO YAWATAMBUA WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUZALISHA BIDHAA BORA KUKUZA UCHUMI

KATIBU Tawala Mkoa wa Pwani Rashid Mchatta amewataka wajasiriamali  watakiwa kuzingatia uzalishaji wa bidhaa zao kitaalam ili kukuza uchumi wa mkoa huo.

Mchatta ameyasema hayo wakati akikabidhi vyeti vya kwa wajasiriamali wenye viwanda vidogo na vidogo kabisa wa mkoa huo ambao wametambuliwa na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) Mkoa wa Pwani.

Amesema kuwa wajasiamali hao wanapaswa kuzingatia ubora na viwango pia kushirikiana na taasisi zinazothibitisha viwango vya bidhaa ili ipate soko ndani na nje ya nchi.

Aidha ameipongeza SIDO kwa jitihada za kuwawezesha wajasiriamali ambapo Mkoa huo una jumla ya viwanda 1,533 vikubwa 122 vya kati 120 vidogo 274 na vidogo sana 1,117.

Naye Meneja wa SIDO Mkoa wa Pwani Beata Minga amesema kuwa unatambua jitihada za wajasiriamali ambao wameanzisha viwanda ambavyo vitaongeza ajira na kuongeza pato la mwananchi mkoa na Taifa.

Minga amesema kuwa vyeti hivyo vya kuwatambua vitawasaidia pale wanapohitaji kutambuliwa na taasisi nyingine ambazo ni za uwezeshaji na zoezi hilo litakuwa endelevu ambapo jumla ya wajasiriamali 65 wametambuliwa 

Wednesday, April 3, 2024

*MTOTO* *ATOLEWA* *SARAFU KOONI*

Wataalamu katika Idara ya ENT ya Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) wamefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto mdogo kwa siku sita.

Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo wa BMH, Emmerenceana Mahulu, amesema BMH imempokea  mtoto huyo wa miaka miwili siku ya Alhamisi ya tarehe 26, Machi.

"Tumefanikiwa kuitoa sarafu iliyokuwa imekwama kwenye koo la mtoto kwa siku sita kwa kutumia kifaa tiba kinachoitwa _esophagoscopy_," amesema Daktari huyo Bingwa ambaye pia Kaimu Mkuu wa Idara ya ENT ya BMH.

Dkt Mahulu amefafanua kuwa sehemu ya koo ilipokuwa imekwama sarafu  ilisabisha uvimbe, akiongeza kuwa ilikuwa imeacha uwazi kidogo ambayo ilikuwa ikiruhusu vimiminika kama uji, maji juisi kupita.

"Mtoto anaendelea vizuri baada ya matibabu na anaweza kula vizuri kwa sasa. Tumeishamruhusu na tutamuona tena baada ya wiki moja ili kuona maendeleo yake," amesema. 

Kwa mujibu wa mama wa mtoto, Juliana Yuda, mkazi wa kijiji cha Mkoka, Kongwa, Dodoma, mtoto wake, ambaye alitoka kucheza na wenzake siku ya Jumamosi ya  tarehe 20, Machi, alirudi nyumbani muda wa mchana akiwa analia.

"Mtoto alikuwa hawezi kula kwa muda wa siku sita, alikuwa anashindia uji, juisi na maji tu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya Siku ya Alhamisi," anasema.

Anaongeza kuwa Alhamisi ya tarehe 26, Machi alimpeleka mtoto Hospitali ya Wilaya ya Kongwa ambapo alipewa rufaa kuja BMH baada ya kupigwa picha ya x-ray na kubaini sarafu imekwama kwenye koo.