Sunday, March 19, 2023

RIDHIWANI KIKWETE AFUNGUA VYOO VILIVYOJENGWA NA IFM CHARITY




MBUNGE wa Chalinze ameshiriki sherehe yaMiaka 10 ya Taasisi ya Ifm Charity kwa kufungua Vyoo vilivyojengwa na Taasisi hiyo na kula chakula nao katika kituo cha kulelea Watoto Yatima cha Hope-Miono, Chalinze. Mh. Mbunge amewashukuru wanachuo hao kwa kujali wenye uhitaji #10IFMSO

Saturday, March 18, 2023

KANUNI UASALAMA MIGODINI

WACHIMBAJI WA MADINI WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI ZA USALAMA MIGODINI

SERIKALI imewataka Wachimbaji wa Madini kuzingatia Kanuni za Usalama na kufuata Sheria na Taratibu za Uchimbaji ili kuepusha ajali katika maeneo ya uchimbaji.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa Machi 17, 2023 alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji katika eneo la ajali ya wachimbaji wadogo waliofunikwa na kifusi na kufariki eneo la Igando Kata ya Magenge Tarafa ya Butundwe Mkoani Geita.

Dkt. Kiruswa, ameiagiza Tume ya Madini kutoa elimu ya Sheria ya Madini hususan elimu ya usalama kwa wachimbaji wanaozunguka maeneo ya uchimbaji katika kipindi cha mvua na kuchukua tahadhari.

"Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inatoa pole kwa wananchi waliopoteza ndugu na marafiki katika ajali hii. Tunawataka wachimbaji mzingatie sheria zilizowekwa na Serikali ili mfanye shughuli zenu kwa tija," amesema Dkt. Kiruswa.

Aidha, amewataka wachimbaji katika eneo hilo kushirikiana na Serikali na mkoa kuchukua hatua kwa wachimbaji wote watakaobainika kukaidi maelekezo ya Serikali kwa wote wanaofanya uchimbaji kwenye maeneo yaliyokatazwa.

Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt. Abdulrahman Mwanga amewataka wachimbaji katika maeneo yenye uwekezaji kutoa ushirikiano kwa watu wenye leseni ya madini ili wafanye shughuli zao bila usumbufu. Amewataka pia kuzingatia usalama katika kazi zao.

Naye, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita Mhandisi Martin Shija amemuelezea Dkt. Kiruswa kuwa, hatua mbalimbali zilichukuliwa kabla na baada ya ajali. Amesema mmiliki wa leseni na Serikali ya kijiji waliweka walinzi shirikishi kwenye eneo hilo ili kuzuia uchimbaji haramu na kuepusha madhara.

"Baada ya ajali tumeimarisha ulinzi katika eneo hilo, tumeendelea kufanya kaguzi mara kwa mara ili kubaini kama kazi zinaendelea na kuchukua hatua pale dosari inapojitokeza,"amesema Mhandisi Shija.

Naye, mwekezaji wa eneo hilo lenye leseni ya utafiti Abdul Stanslaus amesema katika eneo hilo ameendelea kuwa na mahusiano mazuri na jamii katika eneo hilo. Ameomba Serikali kuendelea kutoa elimu kuhusu Sheria ya Madini ili wachimbaji wanaozunguka maeneo ya uchimbaji kuwa na uelewa mkubwa.

Naibu Waziri amefanya ziara baada ya wachimbaji wadogo 8 kufariki tarehe 10 Machi, 2023 baada ya kutokea ajali ya wachimbaji kukutwa na maji ndani ya mashimo wakiwa wanaendelea na shughuli za uchimbaji.

Thursday, March 16, 2023

KAMATI YA NISHATI NA MADINI YAIPONGEZA SERIKALI KUIPATIA GST MASHINE ZA UTAFITI WA MADINI NCHINI

 

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI YAIPONGEZA SERIKALI KWA KUIPATIA GST MASHINE ZA KISASA ZA UTAFITI WA MADINI NCHINI

Na Mwandishi Wetu Dodoma

KAMATI ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Serikali Awamu ya Sita kwa kuipatia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) vifaa na mashine za kisasa kwa ajili kuongeza wigo wa  utafiti wa madini nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na makamu  mwenyekiti wa Kamati hiyo Judith Kapinga mbunge wa viti maalum wakati akiongea na vyombo vya habari mapema baada ya kukamilisha ziara hiyo.

Ziara hiyo ya kutembelea maabara za GST kwa ajili ya kujionea utekelezaji wa majukumu ya GST , Mhe.  Mbunge Judith Kapinga aliipongeza serikali kwa kuwekeza mashine za kisasa katika kufanya uchunguzi, utambuzi na unjenjuaji wa madini mbalimbali.

"Kwa kweli niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita kwa juhudi inazofanya katika kuiwekeza  taasisi yetu ya GST kwa kuipatia mashine mbalimbali za uchunguzi , utambuzi na uchenjuaji wa madini " alisema Kapinga

Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Songwe Philipo Mulugo  ambaye pia ni mjumbe wa Kamati hiyo alishauri  kuwa katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2023/2024  GST iongezewe nguvu zaidi ya kibajeti ili kuweza kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi.

Kabla ya ziara hiyo kuanza, Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba aliwakaribisha wajumbe wa Kamati na kuwashukuru kwa mchango wao mkubwa wanaotoa katika kusimamia GST katika kutekeleza majukumu yake. 

"Ninashukuru sana Kamati hii kwa usimamizi wake nzuri ambao umeendelea kuifanya GST kuboreka zaidi katika  utoaji wa huduma zake,"Alisema Dkt. Budeba.

Mapema baada ya utambulisho huo Dkt. Budeba alimkaribisha Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa kwa ajili ya kuanza ziara hiyo ambapo Dkt. Kiruswa aliishukuru Kamati kwa namna mnavyoendelea kuishauri na kuisimamia Wizara ya Madini kwa ufanisi mkubwa. 

"Sisi tunafarijika sana kwa namna mnavyotusimamia Wizara  na Taasisi zake na tunawakaribisha GST muweze kujione mlichokisoma kwenye taarifa zetu". Aliongeza Dkt. Kiruswa

Katika ziara hiyo wajumbe wa Kamati hiyo walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali juu ya utekelezaji wa majukumu ya GST hasa juu ya  uchunguzi wa sampuli za madini katika maabara ya GST.

Wednesday, March 15, 2023

67 WAKAMATWA NA VITU MBALIMBALI


JESHI la Polisi Mkoani Pwani linawashikilia watu 67 kutokana na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja na tuhuma ya kukutwa na silaha moja aina ya gobore.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani (ACP) Pius Lutumo alisema kuwa watu hao walikamatwa kwenye misako na opereseheni zilizofanywa katika kipindi cha wiki mbili Machi Mosi hadi Machi 14.

Lutumo alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na tuhuma za makosa mbalimbali ambapo watapelekwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

"Lengo la misako hiyo ni kuzuia uhalifu ambapo tunawashukuru wananchi kwa ushirikiano ili kufanikisha kukabiliana na uhalifu,"alisema Lutumo.

Alitaja baadhi ya vitu vingine vilivyokamatwa ni pamoja na bhangi viroba vitatu, puli 102 na kete 789 na pombe ya moshi lita 143 na mtambo mmoja wa kutengenezea pombe hiyo.

"Vitu vingine ni pikipiki 10 ambazo zina usajili wa aina tofauti isipokuwa pikipiki tatu ambazo hazina usajili na watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani mara upelelezi utakapokamilika,"alisema Lutumo.

Aidha alisema kuwa Polisi inatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kuhusiana na taarifa za uhalifu na wahalifu ili kuendelea kuufanya mkoa kuwa shwari.

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria



MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Florent Kyombo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama na Naibu Waziri wake Mhe. Ridhiwani Kikwete wakimkabidhi fedha mlengwa wa TASAF Wilayani Uyui Bi. Amina Abdallah zilizochangwa na Wajumbe wa Kamati hiyo kumuwezesha mlengwa huyo kukamilisha ujenzi wa nyumba aliyoanza kuijenga kutokana na ruzuku ya TASAF anayoipata.

Monday, March 13, 2023

TASAC YAKANUSHA TAARIFA KWENYE MITANDAO YA KIJAMII

Na Mwandishi Wetu Dodoma

SHIRIKA la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limekanusha Taarifa zilizokua zikisambaa hivi karibuni kwenye mitandao ya kijamii hususan Twitter na Instagram kuhusu mikataba ya mafunzo ya kazi kwa vijana zaidi ya 400 ilivunjwa bila kufuata utaratibu ikiwa imebaki mwaka mmoja kuisha kwa mikataba hiyo.

Akizungumza na Wandishi wa habari Jijini Dodoma Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania(TASAC) Kaimu Abdi Mkeyenge amesema taarifa zilizozidi kusambaa ni pamoja na vijana kufanya kazi bila bima ya afya na kwamba ilitoa rushwa kwa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) katika mashauri ya kazi yaliyofunguliwa na vijana hao ili haki isitendeke.

Mkeyenge amesema kuwa mwezi Julai, 2022 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya mabadiliko ya Sheria ya Uwakala wa Meli Tanzania kwa kufuta majukumu ya kipekee ya uwakala wa meli, uhakiki wa mizigo, udhibiti wa nyaraka na kupunguza wigo wa jukumu la kufanya uwakala wa forodha katika bidhaa zilizokuwa zinagombolewa na kuondoshwa na TASAC.

"TASAC ilikuwa ikitekeleza majukumu hayo kupitia vijana waliokuwa wameajiriwa moja kwa moja pamoja na waliokuwa wakifanya mafunzo ya kazi lakini kufuatia mabadiliko hayo Agosti 11 mwaka 2022 TASAC ilivunja mikataba ya mafunzo ya kazi kwa jumla ya vijana 209 waliokuwa wakifanya kazi za uhakiki wa shehena na si zaidi ya 400 kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii,"amesema Mkeyenge.

Amesema kuwa vijana hao waliandikiwa barua kuwa mikataba yao haitahuishwa tena ifikapo tarehe 30 Agosti, 2022 kutokana na merekebisho ya Sheria ambayo yamesababisha baadhi ya majukumu ya TASAC kufutwa na kuhamia sekta binafsi.

 "Kwa mujibu wa masharti ya mikataba, TASAC ilikuwa inawapa mkataba ya miezi mitatu na kuongeza muda kila ilipoonekana inafaa kutokana na utendaji kazi wa mtu,"amesema Mkeyenge. 

Aidha, mikataba ilikuwa imeainisha utaratibu wa namna ya kuvunja mikataba ya mafunzo kazi na ndiyo utaratibu uliotumika kuvunja mikataba hiyo.

"Kwa kuwa vijana wanaolalamika walikuwa kwenye mafunzo kazi na siyo waajiriwa wa moja kwa moja, TASAC kama taasisi nyingine yoyote ya Serikali haina wajibu wa kuwakatia bima ya afya vijana inaowachukua kwa mafunzo kazini kwani stahiki zao zimeainishwa kwenye Muongozo wa Kitaifa wa Mafunzo Kazini uliotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu,"amesema Mkeyenge.

Ameongeza kuwa TASAC ni taasisi ya Serikali inayosimamiwa na Sheria, Kanuni na Miongozo ya Serikali, hivyo basi mashauri yake kisheria yanasimamiwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ikiwa ni pamoja na shauri hilo na kuwahakikishia TASAC haijatoa na haiwezi kutoa rushwa yoyote kwa CMA ili kuzuia haki isitendeke kama ilivyoripotiwa katika mitandao ya kijamii.

"Kati ya vijana 209 waliofutiwa mikataba yao, ni vijana 41 tu ambao hawakuridhika na maamuzi hayo na Vijana 32 kati ya vijana 41, shauri lao lilifutwa na CMA kwa kuwa liliwasilishwa nje ya muda, hivyo ni vijana 9 tu ambao shauri lao dhidi ya TASAC lilipokelewa na lipo katika Tume ya Usuluhisi na Uamuzi vijana 168 waliobaki hawakupinga uamuzi wa TASAC wa kuvunja mikataba yao kutokana na mabadiliko ya Sheria ambayo yalikuwa ni nje ya uwezo wa Shirika,"amesema Mkeyenge.

Amebainisha kuwa suala hilo lipo kwenye chombo cha maamuzi kisheria na TASAC haipaswi kulizungumzia shauri hilo lakini ilionekana ni busara kulitolea ufafanuzi wa kilichofanyika kwa upande wa TASAC na kuacha hatua za maamuzi zinazoendelea kuchukua mkondo wake.

"TASAC kama Shirika la Umma linatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayotolewa na Serikali, hivyo linatoa wito kwa Umma kuwa na subira wakati Tume inapoyafanyia kazi mashauri hayo,"amesema Mkeyenge.

WCF YALIPA FIDIA KWA WAFANYAKAZI BILIONI 49.4

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umefanikiwa kulipa fidia ya shilingi bilioni 49.4 kwa wafanyakazi wanaoumia kuugua ama kufariki kazini 10,454 tangu kuanzishwa kwake mnamo mwaka 2015. 

Takwimu hizo zimetolewa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo Dkt. John Mduma wakati akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mfuko mbele ya Waandishi wa Habari mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO.

Dkt.Mduma amesema kwamba Serikali kupitia WCF imeleta mageuzi makubwa nchini kwani kabla ya kuanzishwa kwa mfuko malipo ya fidia nchini kwa mwaka mzima yalikuwa chini ya shilingi milioni 200 lakini baada ya kuanzishwa kwa malipo yanaongezeka mwaka hadi mwaka.  

“Hadi kufikia Juni 30 mwaka 2022 WCF imelipa mafao yenye thamani ya shilingi bilioni 44.6 kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko kubwa kwa kulinganisha na kipindi cha kabla ya kuanza kwa mfuko kwa hesabu zisizokaguliwa katika kipindi cha Julai 2022 hadi Desemba 2022 WCF ililipa mafao ya jumla ya shilingi bilioni 6.1 kwa wanufaika 1,004 na hivyo kufanya wanufaika wa Mfuko toka kuanzishwa kwake kufikia 10,454 ambao wamelipwa jumla ya shilingi Bilioni 49.4.” alisema Dkt. Mduma.

Amesema kuwa Mfuko huo umekuwa ukilipa malipo endelevu (pensheni) kwa wanufaika ambapo kwa mwezi Juni 2022, wanufaika 1,114 walilipwa kiasi cha shilingi milioni 231.3 kwa mwezi huo.

Akizungumzia kuhusu Kusajili Waajiri Tanzania Bara amesema kuwa kwa taarifa zisizokaguliwa, hadi kufikia mwezi Februari 2023, WCF ilikuwa imesajili jumla ya waajiri 29,978 ambapo amefafanua kuwa ongezeko kubwa la waajiri kujisajili na Mfuko katika kipindi cha awamu ya sita ni kutokana na hatua za makusudi za Serikali kuweka vivutio vya kufanya biashara na kuondoa vikwazo vilivyokuwepo ikiwa ni pamoja na kupunguza viwango vya uchangiaji na kutoa msamaha wa riba.

Aidha katika upande wa uwekezaji hadi kufikia Juni 30 mwaka 2022, Mfuko umekusanya jumla ya shilingi bilioni 241.4 toka kwenye mapato yatokanayo na uwekezaji ambapo kwa takwimu za hivi karibuni, WCF ilitengeneza shilingi bilioni 69.8 katika mwaka wa fedha 2020/2021 na shilingi bilioni 74.2 katika mwaka wa fedha 2021/2022. 

Ameongeza kuwa jumla ya mali za Mfuko hadi Juni 30 mwaka 2022 ni shilingi bilioni 545.1 ambapo asilimia 89.7 ya uwekezaji wa Mfuko upo kwenye Hati fungani za Serikali.