Wednesday, May 18, 2016

WAMKATAA MWENYEKITI WAMFUNGIA OFISI

Na Mwandishi Wetu, Kibaha
WAKAZI wa Mtaa wa Muheza kata ya Maili Moja wilayani Kibaha mkoani Pwani wamefunga ofisi ya mtaa huo kwa madai ya kuukata uongozi ambao wamesema haufanyi kazi kwa utaratibu uliowekwa ikiwa ni pamoja na kutofungua ofisi.
Wakizungumza na waandishi wa habari walisema kuwa uongozi huo tangu umechaguliwa umeshindwa kabisa kuwajibika hivyo kushindwa kuleta maendeleo kwa kipindi chote cha uongozi wao walipochaguliwa mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana.
Moja ya wakazi hao ambaye alijitambulisha kwa jina la Modestus Mpelembwa alisema kuwa uongozi huo chini ya mwenyekiti wake Maulid Kipilili umeshindwa kabisa hata kuitisha mikutano ya kisheria ambayo ndiyo sehemu ya wananchi kuweza kuchangia maendeleo na kujua kinachoendelea ndani ya mtaa huo.
“Wananchi wamefikia hatua ya kufunga mlaango wa ofisi kutokana na kuona kuwa hawana msaada wowote na uongozi ambapo hata kama unashida huwezi kusaidiwa kwani hakuna kiongozi hata mmoja anayeonekana zaidi ya kuonekana kwa matukio maalumu,” alisema Melembwa.
Mpelembwa alisema kuwa hata mapato ya mtaa hayaonekani licha ya kuwa mtaa huo ni moja ya mitaa ambayo ina maeneo makubwa ya ardhi ambayo yanauzwa kama viwanja kwa ajili ya makazi kutokana na eneo hilo kuanza kujengeka kwa sasa.
“Ofisi muda mwingi imefungwa kama una shida umpigie simu mwenyekiti na kama ni suala la mauziano ya viwanja ni huko huko na siyo ofisini kama taratibu zinavyosema hali ambayo inaonyesha kuwa hakuna uwazi wa fedha za asilimia zinazotakiwa kubaki kwenye mtaa kwa ajili ya shughuli za maenedeleo,” alisema Mpelembwa.
Naye Angela Mduma alisema kuwa uongozi huo haufai kuwaongoza kwani umeshindwa kukabili changamoto za wananchi ambao waliwachagua kwa ajili ya kutatua kero mbalimbali ikiw ani pamoja na ubovu wa barabara.
“Tuna chanagamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukosefu wa zahanati, shule ya msingi, maji pamoja na huduma nyingine za kijamii lakini endapo uongozi ungekuwa makini kupitia mikutano kama ingekuwa inafanyika tungeweka vipaumbele vya kuanza kuvifanyia kazi lakini uongozi hauna ushirikiano hakuna kilichofanyika hadi sasa,” alisema Mduma.
Mduma alisema kuwa kwa upande wa kinamama wanapata taabu hasa kwenye huduma za kiafya kliniki kwa wajawazito, kuwapeleka watoto wao kliniki na matibabu kwa ujumla kwao ni changamoto kubwa sana.
Naye Modestus Mapunda alisema kuwa mara ya mwisho mwenyekiti aliitisha mkutano wa mtaa lakini cha ajabu muda mfupi baadaye aliahirisha wakati tayari wananchi wameshajiandaa kwa mkutano hali ambayo ilisababisha wananchi kushikwa na hasira na kuifunga ofisi.
“Tunachotaka ni mkuu wa wilaya kuja hapa kwa ajili ya kujua kero zetu kwani uongozi umeshindwa kufanya kazi lakini cha kushangaza wajumbe kutakiwa kutofanya chochote na mwenyekiti na hawaruhusiwi kuingia ofisini hadi watakapoitwa,” alisema Mapunda.
Mwenyekiti wa mtaa huo Maulid Kipilili alisema kuwa hawezi kuongea chochote kwani anaongea na uongozi wa juu na pia suala hilo tayari amelipeleka polisi kulalamika wananchi hao kufunga ofisi ya mtaa.
Kwa upande wake diwani wa kata ya Maili Moja Ramadhan Lipwai alisema kuwa kufungwa kwa ofisi hiyo ni kinyume cha utaratibu kwani ile ni mali ya umma na wananchi wanapata huduma kupitia ofisi hiyo.
Lipwa alisema kuwa anafanya mawasiliano na viongozi mbalimbali ili kupata suluhu la tatizo hilo ili ofisi hiyo iweze kufunguliwa ili wananchi waweze kupata huduma kupitia ofisi hiyo ambayo imefungwa tangu Mei 15 baada ya mkutano wa mtaa kushindwa kufanyika.
Mwisho.  











   

Thursday, May 12, 2016

NOAH KUTOSAJILIWA KUBEBA ABIRIA BARABARA KUU

Na John Gagarini, Kibaha
MAGARI ya kusafirisha abiria aina ya Noah Hiace pamoja na pikipiki yamesababisha vifo vya watu 102 huku 246 wakijeruhiwa katika kipindi cha kuanzia 2015 hadi Machi 2016.
Kutokana na kukithiri kwa ajali za vyombo hivyo Mamlaka ya Udhibiti  wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) mkoa wa Pwani imesitisha utoaji wa lesseni mpya kwa magari aina ya Noah maarufu kwa jina la ‘Mchomoko’, na Hiace  kwenye barabara zote kuu ikiwamo barabara ya Morogoro.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Kibaha ofisa mfawidhi wa SUMATRA mkoa wa Pwani Nashon Iroga alisema kuwa kwa mujibu wa waraka walioupata kutoka makao makuu magari  hayo yote madogo  ya abiria yanayokwenda masafa  marefu kupitia barabara kuu hayatapewa leseni ya kubeba abiria.
“Barabara kuu kuna vyombo vikubwa vya  usafiri hivyo hayataruhusiwa kupata leseni mpya badala yake yaliyokwisha pata leseni yataendelea hadi hapo muongozo mwingine utakapo toka tena,” alisema Iroga.
Alisema kuwa agizo hilo limetolewa baada ya ongezeko kubwa la magari madogo ya kubeba abiria hasa magari  aina ya noah, kufanya safari ndefu huku baadhi  yakiwa yamebeba abiria na mizigo  bila kuangalia usalama wa abiria  na matokeo yake ni kusababisha ajali za mara kwa mara na msongamano katika barabara kuu.
“Ukiangalia kwa hali ya kawaida magari aina ya Noah yanabeba abiria wachache lakini ili wapate faida inabidi watoze viwango vikubwa vya nauli, kubeba abiria kuliko uwezo wake na kwenda mwendo kasi  ili wafanye safari nyingi na kupata faida, matokeo yake wanahatarisha usalama wa maisha ya abiria,” alisema Iroga.
Aidha alisema kuwa  magari hayo madogo yakiwamo Noah na Hiace yanayobeba abiria yatapewa lesseni mpya za kufanya biashara kutumia ruti za barabara  za ndani na sio barabara kuu.

Mwisho.

JESHI LA POLISI LAMSAKA MWANAFUNZI ALIYECHOMA BWENI


Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi Mkoani Pwani bado linaendelea kumtafuta mwanafunzi wa shule ya Sekondari ya Rafsanjani iliyopo Soga Tarafa ya Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani baada ya kuchoma bweni la wasichana la shule hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa mwanafunzi huyo ambaye hakuweza kufahamika alichoma bweni hilo juzi majira ya saa 4 usiku liitwalo Umoja.
Mushongi alisema kuwa hata hivyo tukio hilo halikuwa na madhara kwa wanafunzi zaidi ya kuharibu mali zilizokuwa kwenye bweni hilo ambazo hata hivyo thamani yake haikuweza kufahamika mara moja.
“Tunaendelea kumfuatilia mwanafunzi huyo ili tuweze kumjua na kumchukulia hatua za kisheria lakini hadi sasa bado hatujafanikiwa kumpata kwani aliandika kwenye sanduku la maoni juu ya dhamaira yake hiyo mbaya ya kuchoma bweni,” alisema Mushongi.
Alisema kuwa wanaendelea kuzifanyia kazi taarifa hizo ili waweze kumbaini mwanafunzi huyo ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi yake kwani kitendo alichokifanya ni cha hatari kwa maisha ya wanafunzi wenzake na mali.
“Tunatoa wito kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni wazingatie masomo na kuachana na vitendo visivyo kuwa na maadili kwani jeshi halitawavumilia wanafunzi ambao wanabainika kufanya vitendo viovu kwani tutawakamata na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria ikiwa ni pamoja na mahakamani,” alisema Mushongi.
Bweni hilo lilichomwa moto juzi na mwanafunzi huyo lakini hata hivyo kikosi cha zimamoto mkoa wa Pwani polisi pamoja na wananchi walifanikiwa kuzima moto huo na haukuweza kuleta madhara kwa wanafunzi.

Mwisho.

KIWANDA CHA TILES KUJENGWA MKURANGA


Na John Gagarini, Mkuranga
WAKAZI wa mkoa wa Pwani wametakiwa kuunga mkono mkakati wa serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dk John Magufuli ya kuhamasisha ujenzi wa viwanda na uwekezaji.
Akizungumza na wakazi wa vijiji vya Nyamato na Mkiu wilayani Mkuranga wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza vigae (Tiles) cha Goodwill Tanzania Ceramic mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema kuwa wananchi wananafasi kubwa ya kufanikisha nchi kuwa ya viwanda kwa kushirikiana na wamiliki wa viwanda.
Ndikilo alisema kuwa wananchi wanapaswa kuwapa ushirikiano wawekezaji wa viwanda ili waweze kufanya kazi bila ya kuhujumiwa kwani kuna baadhi ya watu wamekuwa wakihujumu miundombinu ya viwanda.
“Wawekezaji kama hawa wa viwanda mnapaswa kuwaunga mkono kwani manufaa ya uwepo wao ni mengi sana ikiwa ni pamoja na kupata ajira pamoja na nyie kuuza bidhaa zenu kwani biashara zitakuwa nyingi hivyo mtaweza kubadilisha maisha yenu lakini endapo mtawafanyia vitendo vya kuwakatisha tama wataondoka,” alisema Ndikilo.
Alisema kuwa kwa sasa mkoa wa Pwani ajenda yake ni kuhakikisha unakuwa mkoa wa viwanda na hilo linawezekana kwa kuwa na viwanda vingi vya kuzalisha bidhaa mbalimbali.
“Mkoa kwa sasa umeamua kujitangaza kiviwanda kwnai nafasi za uwekezaji bado zipo nyingi na lengo ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na uchumi wa kati na utainuka endapo kutakuwa na viwanda vingi mfano tu wilaya ya Mkuranga mmeanza kutekeleza kwa vitendo mkakati wa Rais wa kuwa na viwanda kwnai kwa sasa kuna viwanda 59,” alisema Ndikilo.
Aliwataka wakurugenzi na wakuu wa wilaya za mkoa huo kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kuhamasisha wageni na wazawa kujenga viwanda ili kuinua uchumi wa wananchi lakini wahakikishe wawekezaji wan je wanafuata taratibu za nchi kwa wafanyakazi kwa kuzingatia sheria za kazi.
Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa kiwanda hicho Yang Zhen alisema kuwa kiwanda hicho ni cha pekee kwani kitakuwa cha pili barani Afrika kwa ukubwa na cha kwanza Tanzania kwa uzalishaji wa vigae ambapo kwa siku kitakuwa kikizalisha meta 80,000 kwa siku.
Zhen alisema kuwa maradi huo una thamani ya dola za Kimarekani 100 na umegawanyika kwenye hatua mbili ambapo awamu hii ya kwanza itaisha mwishoni mwa mwaka huu huku ile ya pili ikiisha mwishoni mwa mwakani hivyo bidhaa hizo za vigae zitakuwa zikizalishwa hapahapa na siyo nje ya nchi.
Aidha alisema kuwa wanatarajia kujenga shule, kuwapatia maji, zahanati pamoja na kituo cha polisi ikiwa ni kama mchango wao kwa jamii inayozunguka kiwanda hicho ambapo mara kitakapokamilika kitaajiri watu 2,000 na kwa sasa kimetoa ajira kwa watu 200.
Mwisho.

Thursday, May 5, 2016

johngagariniblog: ACHINJA MKE NA MTOTO WAKE KISA WIVU WA MAPENZI

johngagariniblog: ACHINJA MKE NA MTOTO WAKE KISA WIVU WA MAPENZI: John Gagarini, Kibaha JESHI la Polisi mkoani Pwani linamshikilia Frowin Peter Mbwale (26) mkazi wa Kawe Jijini Dar es Salaam kwa tuhuma z...

WATAKA VYUO VYA KATI KUUNGANISHWA NA BODI YA MIKOPO

Na John Gagarini, Kibaha

SERIKALI na Bodi ya Mikopo Nchini (TCU) imeshauriwa kuviingiza kwenye mpango wa mikopo wanafunzi wanaosoma Vyuo vya Kati kama ilivyo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani Abdul Sharifu wakati mkutano wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Juu wa (CCM).

Sharifu alisema kuwa wanafunzi hao ni sawa na wale wa vyuo vikuu na wengine wanatoka kwenye mazingira magumu na wanahitaji mikopo ili waweze kupata elimu ya juu.

“Hali ya sasa ni ngumu na wazazi ni wale wale wanahitaji kupunguziwa mzigo wa kulipa ada ambazo ni kubwa hivyo tunaona kuwa kuna haja ya serikali kuviingiza na vyuo vya kati kwenye mpango wa kutoa mikopo kwa wanafunzi,” alisema Sharifu.

Alisema kuwa kwa kuwa nchi imeamua kuwekeza kwenye elimu kwa lengo la kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu bora hadi kufikia elimu ya juu ambayo ndiyo inaweza kumsaidia mtoto.

“Kwa sasa elimu ya juu ndiyo inayotakiwa tofauti na elimu ya kawaida ambayo si ya juu ambayo kwa sasa haina nafasi ya muhitimu kupata ajira hivyo kulazimisha watu wapate elimu ya juu,” alisema Sharifu.

Aidha alisema kuwa shirikisho hilo ni mboni ya chama na linafanya kazi kubwa ya kukijenga chama kwani hapo ni tanuru la kuandaa viongozi wa baadaye wa kukiongoza chama pamoja na nchi.

Kwa upande wake mwenyekiti wa CCM wilaya ya Kibaha Maulid Bundala  ambaye alimwakilisha mwenyekiti wa Mkoa Mwinshehe Mlao alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo alisema kuwa Shirikisho la Vyuo Vikuu la CCM linafanya kazi kubwa ya kukitetea chama.

Bundala alisema kuwa CCM imeleta ukombozi ndani ya nchi na ni chama kikongwe hivyo kwa wanavyuo waliojiunga na shirikisho hilo wako sehemu salama kwani mawazo yao yataleta manufaa kwa nchi.

Aidha alisema kuwa nchi kwa sasa ina hitaji kuongozwa na wasomi hivyo wasomi hawa wataleta mabadiliko na chama kiko tayari kubadilika na wao wananafasi ya kumshauri Rais na wao ndiyo watakaoliinua taifa.

Naye naibu katibu mkuu wa shirikisho hilo Siraji Madebe alisema kuwa shirikisho lao linakabilia na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na wancahama wake wale wa vyuo vya kati kutotambuliwa na Bodi ya Mikopo hivyo kutopata mikopo.

Madebe alisema kuwa licha ya changamoto mbalimbali lakini watahakikisha wanaendeleza umoja wao ili kufanikisha malengo ya kuanzishwa shirikisho hilo ambayo ni kuwaunganisha wasomi walio vyuo kuwa na umoja wao ili kukipigania chama.

Mwisho.

TANESCO KUWAUNGANISHIA UMEME WANA VIJIJI MRADI WA BILIONI 30

Na John Gagarini, Kisarawe

SHIRIKA la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Pwani kupitia mradi wa umeme vijijini (REA) unatarajia kusambaza umeme kwa wananchi 11,000 wenye thamani ya shilingi bilioni 30 kwenye vijiji 109 vya mkoa huo .

Kwa mujibu wa Mhandisi mkuu wa Mradi huo wa REA mkoa wa Pwani Leo Mwakatobe alisema mradi huo wa awamu ya pili utakamilika mwishoni mwa mwezi wa sita mwaka huu.

Mwakatobe alisema kuwa lengo kubwa kwa sasa ni kutekeleza agizo lililotolewa na serikali la kuhakikisha miradi hiyo ya umemem vijijini inawafiki wananchi wengi na kwa wakati uliopangwa.
“Tumeshaanza katika kutekeleza miradi hiyo katika maeneo ya Chalinze, Kisarawe na tutaendelea katika sehemu mbali mbali za Mkoa wetu wa Pwani na tunatarajia kufikia vijiji vipatavyo 109 vilivyopo katika Mkoa wetu,” alisema Madulu.   
Alisema kuwa kuwa mbali ya kuendelea kukutekeleza miradi hiyo hata hivyo wanakumbana na changamoto nyingi katika utekelezaji wa  wakati wanapotaka kupitisha miundomibu katika makazi ya watu.

“Baadhi ya watu wamekuwa hawataki kuridhia umeme kupita kwenye maeneo yao au kutaka fidia kubwa hali ambayo inasababisha kuwa na changamoto za hapa na pale lakini hata hivyo tunajitahidi kuwaelewe umuhimu wa miradi hiyo na kupata nishati hiyo ya umeme,” alisema Mwakatobe.

Kwa upande wake Meneja wa TANESCO Mkoa wa Pwani  Martin Madulu alisema kuwa kwa sasa wanatekeleza  agizo lililotolewa na serikali kuhakikisha wanawafikia wateja wao wote hususani wale wa vijijini  kwa lengo kuweza kuwaunganishia umeme kwa bei nafuu.

Madulu alisema kuwa watahakikisha wanafanya jitihada ili kuwafikia wateja wao ili waweze kuwa na nishati ya umeme katika maeneo mbai mbali hususan kwa wananchi wanaoishi katika maeneo ya vijijini.

Wakati huo huo wakazi zaidi wa 100 katika  kijiji cha  Nyeburu  Wilayani Kisarawe waliokuwa na tatizo  la upatikanaji wa nishati ya umeme na kuishi  katika giza  kwa kipindi cha muda mrefu kwa sasa wamenufaika baada ya  kuunganishiwa umeme kutokana na  kukamilika kwa mradi wa umeme vijijini (REA) awamu wa pili.

Baadhi ya wakazi hao walisema kwamba kukamilika kwa mradi huo kutaweza kuleta chachu kubwa ya kimaendeleo katika kijiji hicho kwani mwanzoni   walikuwa wanashindwa tutimiza malengo yao waliyojiwekea kutokana na kutokuwa na nishati hiyo ya umeme.

Mwisho.