SERIKALI imetoa zaidi ya shilingi bilioni 44 kuwezesha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) Mkoa wa Pwani ili kutekeleza miradi ya kunusuru kaya maskini katika kipindi cha miaka mitano 2020/2025.Aidha jumla ya vikundi 1,601 vyenye wanachama 16,495 kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) vikiwa na mtaji wa kiasi cha shilingi milioni 330.
Hayo yalisemwa Mjini Kibaha na Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Pwani Roseline Kimaro wakati wa kikao kazi cha mwaka cha Utekelezaji wa (TASAF III – Awamu ya Pili).
Kimaro alisema kuwa fedha hizo ni za ruzuku kwa walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kupitia miradi ya Afya na Elimu, miradi hii ni miradi ya ajira za muda, mitaji kwa ajili ya biashara ndogo ndogo.
Alisema kuwa vikundi hivyo vina jumla ya wanawake 14,568 ambapo idadi hiyo ni hadi kufikia Juni 2025 ambapo vimeanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
"Vikundi hivyo kupitia wanachama wake vinafanya miradi ikiwemo ile ya kilimo, ufugaji, biashara ndogondogo, ushonaji, usindikaji wa bidhaa na ufumaji,"alisema Kimaro.
Alisema kuwa Mkoa ulitekeleza miradi ya maendeleo katika sekta za afya na elimu katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati, wodi, mabweni na nyumba za watumishi.
"Haya ni mafanikio yaliyopatikana nani ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, viongozi wa jamii na wanufaika wenyewe,"alisema Kimaro.
Aliongeza kuwa mpango huo unatarajiwa kuendelea kuleta mabadiliko chanya na kuchochea maendeleo endelevu ya Mkoa wa Pwani kwa kuboresha maisha ya wananchi.

No comments:
Post a Comment