ILIKUWA mwaka 1996 majira ya asubuhi nilisikia wimbo wa Taifa kupitia Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD) wakati huo kwa sasa ni TBC Taifa jambo ambalo si la kawaida kwani unapopigwa wimbo huo basi kuna tukio kubwa la kitaifa ambapo Rais wa Awamu ya Tatu Benjamini Mkapa alitangaza kutokea tukio la ajali ya Mv Bukoba iliyotokea Mkoani Mwanza.
Wakati taarifa hiyo inatangazwa nilikuwa nikielekea shule ambapo nilikuwa nasoma Sekondari ambapo imepita miaka 29 tangu kutokea ajali hiyo mbaya ambayo iliacha simanzi kwa Watanzania na hata baadhi ya raia wa nchi mbalimbali.
Meli hiyo ya Mv Bukoba wakati ikisafiri ilibeba watu wa aina mbalimbali kuanzia wafanyabiashara, wataalamu, watu wa dini, rangi tofauti tofauti na rika tofauti ambao walikuwa wakitokea Bukoba Mkoani Kagera kwenda Mkoani Mwanza kwa shughuli zao za kawaida.
Ni takribani miaka 10 imepita tangu nimfahamu moja ya watu walionusurika kwenye ajali hiyo nikijaribu kumshawishi ili anisimulie mkasa huo bila ya mafanikio kwani alishindwa kutokana na huzuni kubwa aliyokuwanayo kutokana na tukio hilo ambalo hataweza kulisahau maishani mwake.
Baada ya kumshawishi kwa muda mrefu hatimaye alikubali na kunisimulia juu ya mkasa huo ambapo alifahamika kutokana na ajali hiyo kwa kunusurika kwa kupitia Mkungu wa ndizi ambao ndiyo uliookoa maisha yake kwa kuushikilia kwa zaidi ya masaa mawili.
Huyo si mwingine bali ni Happy Leopard ambaye kwa wakati ule alikuwa ni mtoto mdogo mwenye umri wa miaka (17) wakati ajali hiyo inatokea akiwa na dada yake ambaye kwa bahati mbaya alifariki dunia katika ajali hiyo.
Akielezea juu ya kilichotokea wakati wa ajali hiyo alisema kuwa yeye na dada yake Emiliana walikuwa wakiishi Singida ambapo dada yake alikuwa ni mtumishi wa Shirika la Bima Tanzania (NIC) walikwenda Bukoba ambapo ndiyo nyumbani kwao kwa ajili ya mazishi ya mama yao mzazi.
Leopard alisema kuwa baada ya mazishi ilibidi waondoke kwenda Mwanza kwa ajili ya kupeleka msiba Moshi ambako ni nyumbani kwa mama yao alikozaliwa.
"Nilipanda kwenye meli majira ya saa 1 jioni ambapo saa 3 safari ndipo ilipoanza nilipanda lakini sikuwa na furaha tulikata tiketi ya meli ya Mv Victoria lakini meli hiyo ilikuwa kwenye matengenezo na tukapanda meli ya Mv Bukoba,"alisema Leopard.
Alisema kuwa yeye na dada yake walikata siti za VIP na abiria walikuwa wengi ambapo baadhi ya abiria walikosa nafasi na kupanda magari kwenda kupanda kituo cha mbele cha Kemondo na kupanda na wengine waliachwa ambapo ndi ilikuwa nusura yao.
"Mimi na dada tulikuwa ndani lakini nilishindwa kulala kila wakati alikuwa akija na kuniangalia akashangaa kwanini silali ambapo dada alilala lakini sikulala ikabidi nitoke nje ambapo pembeni kulikuwa na kwaya ilikuwa ikiimba pia alikuja kuniangalia na kunipa khanga ili nijifunike kwani kulikuwa na baridi,"alisema Leopard.
Alisema kuwa ilipofika majira ya saa 10 alfajiri walipokuwa wakikaribia kufika Mwanza walipofika eneo linaloitwa Kisiwa cha Juma yalitokea mawimbi makubwa na sehemu hiyo ni muingiliano wa maji na kuna mawimbi makali ambapo inasemekana huwa ajali za meli hutokea mara kwa mara ambapo manahodha wazoefu huwa hawapiti hapo na kukwepa eneo hilo.
"Baada ya muda meli ilianza kuyumba na vyombo jikoni vilianza kuanguka askari walikuwa wakisafirisha fedha walianza kuwaambia abiria kaeni upande huu mmeelemea sehemu moja nendeni huku wakati huo tulianza kuona taa za Bugando kwa mbali kidogo meli ilianza kuyumba sasa watu wakawa wanakimbia hawajui la kufanya,"alisema Leopard.
"Tulianguka kama vile mtu anamwaga kitu dada alibaki kule kwenye chumba, nikifanikiwa kushika boya lakini kuna mtu alininyanganya nikazama chini nilipoibuka nikakutana na Mkungu wa ndizi ambao niliungangania hivyo nikawa naelea licha ya mawimbi ya maji kutupiga na niliona watu wengine hao wakiwa na maboya huku wakiomba msaada,"alisema Leopard.
Alisema kuwa kwa mbali aliona baadhi ya watu wakiwa kwenye ubavu wa meli wakiwa wamejishikilia huku kwenye maji kukiwa na maiti nyingi zikiwa zinapelekwa na maji na vitu mbalimbali ikiwa ni pamoja na maburungutu ya fedha na vifaa mbalimbali.
"Tukiwa ndani ya maji nilikuwa nauomba Mungu atusaidie ili tuweze kupona na niliamini dada yangu ni moja ya watu waliokuwa kwenye ubavu wa meli naye atapona lakini kumbe haikuwa hivyo kumbe yeye alibaki kule chumbani na hakuweza kutoka na alikuja kupatikana baada ya kuvunjwa vile vyumba tena siku chache kabla zoezi la kutafuta maiti kusitishwa,"alisema Leopard.
"Ilikuja boti ya wavuvi wakauliza mna hela ili tuwaokoe kama hamna hela basi wakaanza kuchukua fedha na vitu mbalimbali vya abiria wakaweka kwenye boti yao wakaondoka lakini jambo la kushukuru wakatokea wavuvi wengine wakiwa na mtumbwi wakatuokoa na kisha kutupeleka kwenye meli nyingine ambayo ilitokea Uganda wakatuchukua baadhi ya watu walikufa baada ya kuchoka kushikilia maboya kwani walikaa majini muda mrefu sana,"alisema Leopard.
Alisema kuwa meli hiyo ilivuja mafuta ambayo yaliingia kwenye maji na kutupiga hivyo yalituumiza machoni, puani na masikioni na tulipokuwa kwenye ile boti tuliookolewa watu watano, maji yalikuwa yanaingia ikabidi awe anayachota na kuyamwaga nje huku wale wenzake wakiwa wamelala hoi yeye akiwa kidogo ana nguvu.
Alisema kuwa anamshukuru Mungu na siku hiyo alivaa rozari ambayo alipewa na babu yake ambaye alikuwa padri na anaamini Mungu ndiye aliyemwokoa katika ajali hiyo mbaya ya majini kutokea nchini.
"Tangu tunatoka Singida kwenda Bukoba moyo wangu haukutaka kabisa kusafiri nilimkatalia dada hiyo safari hadi majirani zetu walinishawishi kusafiri ambapo aliogopa kupanda meli na majirani waliniambia kuwa kwani umeshawahi kusikia ajali ya meli walinibembeleza ikabidi niende,"alisema Leopard.
"Cha ajabu ile sehemu niliyookolewa alitokea nyoka mkubwa mweusi watu wakanionyesha baada ya kuokolewa wakasema huyo ndiye alikuwa mzimu wake ambapo kama angemuona angemuokoa niliwaambia nikiwa majini niliogopa zaidi mtu na siyo kitu kingine kwani yule aliyeninganganya boya alinifanya nione adui ni binadamu na siyo mnyama au kitu kingine,"alisema Leopard.
Alisema kuwa miaka zaidi ya 10 bila ya kupanda meli baada ya tukio hilo licha ya siku alipopatikana dada yake ilibidi apande kwenda kuzika na walimbembeleza sana apande alikubali lakini aliogopa sana meli akikumbuka tukio hilo na fedha zote za pole alizopewa alizipeleka kanisani kama sadaka kwani hakuona thamani ya kitu chochote kwa wakati huo na ndoto zake zote zikitoweka.
"Dada alikuwa na mipango ya kwenda Uingereza ambapo aliniahidi tungeenda naye na aliahidi angenisomesha kwani mimi nilikuwa mtoto wa mwisho na dada yangu alikuwa akinipenda tulipendana sana nilitamani angepona ili tuje tusimulie kuwa sisi ni mashujaa lakini haikuwa hivyo tukio hilo limeniumiza sana sitaweza kulisahau maishani mwangu,"alisema Leopard.