Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akionyesha shehena na saruji mifuko 500 kwa ajili ya uzio wa Kituo cha Afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani |
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akiwa amebeba saruji ambayo itatumika kwenye ujenzi wa uzio wa kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani |
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa akizindua ujenzi wa uzio wa Kituo cha afya cha Mlandizi wilayani Kibaha mkoani Pwani |
Na John Gagarini, Kibaha
KITUO cha Afya cha Mlandizi kimeanza mchakato wa
kuelekea kuwa Hospitali ya wilaya kwa kuanza ujenzi wa uzio ambapo Mbunge wa
Jimbo la Kibaha
Vijijini wilayani Kibaha mkoani Pwani Hamoud Jumaa amewataka
wafadhili mbalimbali kujitokeza kusaidia ujenzi wa uzio huo ambao utagharimu kiasi
cha zaidi ya shilingi milioni 200.
Akizungumza na waandishi wa habari Mlandizi wakati
akizindua ujenzi huo mbunge huyo alisema kuwa wameanza kuboresha huduma
zinazotolewa kituoni hapo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa uzio huo ikiwa ni moja
ya vigezo vinavyotakiwa kufikia hadhi hiyo.
Jumaa alisema kuwa Kituo hicho cha afya ni tegemeo
kubwa kwa wakazi wa Jimbo hilo ambalo kwa sasa lina wakazi 70,000 na wilaya
jirani za Bagamoyo na miji ya Chalinze na Kibaha wanapata huduma hapo.
“Mpango huu nimeuanzisha kwa jitihada zangu binafsi
kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ambapo hadi sasa nimepata mifuko 500 ya
saruji, kokoto lori saba mchanga, mchanga na tani moja ya nondo ambavyo
vitasaidia katika ujenzi wa uzio huu tunaomba wadau wengine waendelee
kutusaidia,” alisema Jumaa.
Alisema kuwa kutokana na kituo hicho cha afya kuwa
tegemeo kubwa kwa wameona kuna haja ya kuwa Hospitali ya Wilaya ili waweze
kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi watakaokuwa wanapata huduma hapo.
“Tumekubaliana vitongoji 26 na madiwani sita watoe
240,000 huku mfuko wa jimbo ukitoa kiasi cha shilingi milioni 4 kwa ajili ya
tofali za uzio ambao utasaidia kuondoa uingiaji holela wa watu bila ya sababu
za msingi ndani ya eneo la Kituo cha afya,” alisema Jumaa.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Mlandizi Eufrasia
Kadala alisema kuwa wataungana na Mbunge huyo kuhakikisha wanafanikisha ujenzi
huo ili kuboresha kituo hicho cha afya.
Kadala alisema kuwa kutokana na kutokuwa na uzio
kumekuwa na mwingiliano wa watu kuingia kiholela hasa kutokana na kituo hicho
kuwa jirani na makazi ya watu.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mdogo wa
Mlandizi Tatu Jalala alisema kuwa waliupokea mkono mpango huo na kuupeleka kwa
jamii kwa lengo la kumuunga mkono mbunge wao.
Jalala alisema kuwa wanaendelea kuihamasisha jamii
ili iweze kuchangia ujenzi huo wa uzio ukamilike kwa wakati lengo likiwa ni
kufanikisha harakati za kuwa Hosptali ya wilaya.
Mwisho.