Na John Gagarini,
Kibaha
TIMU ya soka ya Simba
imetakiwa isimtafute mchawi kutokana na matokeo mabaya inayoyapata uwanjani
kwani hali hiyo inatoka na usajili ambao haukuwa mzuri kwa kutosajili wachezaji
wenye uzoefu.
Wachezaji wengi
waliosajiliwa ni wale ambao wanahitaji uzoefu wa muda mrefu kabla ya kutegemewa
na timu ya Simba ambayo ni timu kubwa hapa nchini.
Akizungumza na gazeti
hili msemaji wa Tawi la Simba wilayani Kibaha mkoani Pwani lililopo Kwa Mfipa
maarufu kama “Simba Tishio” Fahim Lardhi alisema kuwa wachezaji waliyopo wengi
ni chipukizi ambao walipaswa kuwa na wachezaji wenye uzoefu.
“Timu ni nzuri lakini
wachezaji wengi ni chipukizi na hawana uzoefu wa michezo mikubwa kama hii ya
ligi kuu ambayo ni ngumu na inahitaji uzoefu mkubwa ambapo wachezaji hawa
wanashindwa kumudu dakika 90 za mchezo,” alisema Lardhi.
Lardhi alisema kuwa
hakuna haja ya kumtafuta mchawi na kutuhumiana kuwa kuna kundi fulani
linahujumu timu hiyo si kweli kwani hali halisi inaonekana kuwa wachezaji wa
Simba wengi hawawezi kumudu mikimikiki ya ligi.
“Hakuna cha Simba
Ukawa wala nini bali timu yetu inashindwa kuhimili vishindo ni dhahiri kuwa
kamati ya Usajili msimu huu imesajili timu ya Vijana wadogo wengi ambao
walitakiwa kusaidiana na wachezaji wenye uzoefu,” alisema Lardhi.
Aidha alisema kwa
upande wa kocha hawezi kulaumiwa kwani uwezo wake ni mzuri na timu aliikuta
hata hivyo amejitahidi kuhakikisha timu inacheza vizuri tatizo ni kukosa
wachezaji wazoefu.
Alibainisha kuwa huu
ni msimu wan ne timu ya Simba haiku vizuri wanaifanya kama timu ya majaribio
ligi kuu ni ngumu na inahitaji wachezaji wenye uzoefu mkubwa hivyo viongozi
wasitoe lawama zozote.
Mwisho.
Na John Gagarini,
Kibaha
TIMU ya
soka ya Kiluvya United ya Mkoani Pwani imefanikiwa kupanda daraja la kwanza baada
ya kutoka sare ya goli 1- 1 na timu ya Mshikamano ya Jijini Dar es Salaam
kwenye mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Ruvu JKT Mlandizi wilayani Kibaha.
Kiluvya
United imefanikiwa kupanda licha ya kuwa bado ina michezo miwili mkononi kwenye
mashindano ya ligi daraja la Pili Taifa ilianza mbio zake za kuwania
kupanda daraja tangu mwaka jana.
Katika mchezo
wa huo ulioifanya timu hiyo kupanda hadi daraja la Kwanza kutoka la pili ulishuhudiwa
na mashabiki wengi toka timu hizo mbili ulikuwa na ushindani mkubwa na kufanya
kuwa na mvuto uliowafanya mashabiki kupata burudani ya nguvu.
Mashabiki
wa United walifurahia matokeo hayo ambayo yameipandisha timu hiyo ya mkoa wa
Pwani ambayo imepania msimu ujao kupanda ligi kuu ya Voda Com ili kuungana na
timu za Ruvu Shooting na Ruvu Stars.
Akizungumza
na waandishi wa habari baada ya mchezo kwisha kocha mkuu wa United Yahaya Issa alisema
kuwa kwa kwa sasa kikosi chake kina jumla ya pointi 20 na kwamba kimebakiza
michezo miwili, Mshikamo ikiwa na pointi 13 ikifuatiwa na Abajalo ikiwa na
pointi 12 zote za Jijini Dar es Salaam.
‘Ndugu waandishi
kwanza kabisa napenda kumshukuru mungu kwa timu yangu kupanda daraja la kwanza
na hii yote nikutokana na juhudi za wachezaji na uongozi mzima wa United pamoja
na mwamko wa mashabiki wa Pwani ndiyo waliofanikisha kupanda daraja,” alisema
Issa.
Issa alisema
kuwa kwa sasa wao ndiyo vinara kwa pointi 20 na bado wana michezo miwili dhidi
ya Abajalo na Cosmo hivyo hakuna timu yoyote ambayo itaweza kufikia pointi zao
hata kama wakishinda michezo yote.
Naye Mkrugenzi
wa timu hiyo ya United Edward Mgogo “Eddo Master” alisema kwamba ndoto yao
kubwa ni kuhakikisha timu hiyo inafika mbali ili kuweza kushiriki katika ligi
kuu ya Tanzaania Bara.
Aidha
alitoa wito kwa wadau mbali mbali na mashabiki wa Mkoa wa Pwani kuiunga mkono
timu yao ili kuweza kutimiza azama yao ya kuweza kufika mabli na hatimaye
katika siku zijazo iweze kushiriki hata michuano mbali mbali ya Kimataifa.
Kikosi
hicho ambacho kwa sasa kimeacha gumzo ya hali ya juu kutokana na wachezaji wake
kuonyesha kandanda la aina yake siku ya jumamosi kinatarajia kushuka dimbani
kumenyana na timu ya Abajalo katika nyasi za uwanja wa Karume Jijiji Dar es
Salaam ikiwa kama kumalizia michezo yake miwili ya mzunguko wa mwisho.
Mwisho.
Na John
Gagarini, Kibaha
SHIRIKA
la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Pwani limepata hasara ya zaidi ya
shilingi milioni 12 ikiwa ni pamoja na wateja wake kujiwekea nguzo kinyemela na
kujiunganishia nyaya za umeme zenye urefu wa mita 2000.
Shirika hilo
liliweza kubaini kuwa kuna baadhi ya wateja wake ambao wameamua kujiunganishia
umeme kwa kujiwekea nguzo pamoja na nyaya za umeme zenye urefu huo kinyume cha
utaratibu.
Hayo yalisemwa
na ofisa Usalama wa TANESCO Mkoa wa Pwani Henry Byarugaba na kusema kuwa tukio
hilo la kuhujumu miundombinu hiyo limetokea katika eneo la Matumbi
Wilayani Bagamoyo.
“Shirika
iliweza kubaini kuna baadhi ya wateja wake ambao wameamua kujiwekea nguzo
kinyemela pamoja na nyaya za umeme zenye urefu wa mita 2000 bila ya TANESCO
ambao ndiyo waunganishaji wa umeme kufahamu jambo ambalo ni kinyume cha sheria,”
alisema Byarugaba.
Byarugaba
alisema kuwa Shirika limepata hasara kuwaba kutokana na kuwakuta wateja wawili
kujiunganishia nguzo saba bila ya TANESCO kufahamu kwani mbali ya hujuma hiyo
pia ni hatari sana maana miundombinu hiyo inahujumiwa na watu wachache hivyo
hawataweza kuvumilia hali hiyo.
“Baada
ya kukuta nguzo hizo zimewekwa hatua ambazo tulizichukua ni kuziondoa nguzo
zote saba kwani hazikuwa zimezingatia taratibu katika uwekaji wa miundombinu
hiyo hivyo hazikuwa halali kuwepo katika eneo hilo,” alisema Byarugaba.
Aidha alisema
kuwa kubainika kuwepo kwa nguzo hizo ni kutokana na juhudi za makusudi ambazo
zinafanywa na wafanyakazi wa Shirika hasa nyakati za usiku na mchana ili kuweza
kuangalia miundombinu yake na kuwabaini wateja ambao wamekuwa wakivunja sheria
kwa kujiunganishia nguzo wenyewe.
“Hivi
kweli jamani mtu anafanya maamuzi ya kuamua kuhujumu miundombinu yetu bila ya
woga wowote ule hii ni hatari sana na ndio maana sisi jukumu letu ni
kuhakikisha miundombinu yetu inakuwa katika hali ya usalama, na siyo wateja wetu
kujichukulia maamuzi wao wenyewe bila ya kuwaona wahusika kutoka,”alisema Byarugaba.
Ofisa usalama
huyo wa TANESCO alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa hali hiyo wameshapeleka
taarifa polisi ili kuweza kuwasaka watuhumiwa wote ambao wamehusika katika
tukio hilo la kujiunganishia nguzo na nyaya kiholela ili waweze kuchukuliwa
hatua kali za kisheria.
Alibainisha
kuwa kwa sasa bado wanendelea kufanya uchunguzi wa kina ili waweze
kuwafahamu ni watu gani ambao wamehusika katika zoezi hilo la kuwawekea wateja
hao nguzo na nyaya bila ya uongozi wa Shirika kufahamu lolote juu ya
tukio hilo.
Mwisho.