Sunday, April 21, 2013

RIZIWANI KUKABIDHI KOMBE


Na John Gagarini, Kibaha
RIZIWANI Kikwete kesho anatarajiwa kuwakabidhi kombe la ubingwa mabingwa wa mkoa wa Pwani wa daraja la tatu timu ya Kiluvya United.
Kwa mujibu wa ofisa habari wa chama cha soka mkaoni Pwani (COREFA) Victor Masangu alisema kuwa Riziwani ndiye atakayekuwa  mgeni rasmi kwenye sherehe za kuikabidhi kombe timu hiyo kwenye uwanja wa Ruvu Jkt Mlandizi wilayani Kibaha.
Alisema kuwa maandalizi ya sherehe hizo za kuwakabidhi ubingwa United zimekamilika na kinachosubiriwa ni muda ili kuikabidhi ubingwa timu hiyo.
“Ili kunogesha sherehe hizo mabingwa hao wa mkoa wanatarajiwa kucheza siku hiyo na timu ya vijana chini ya miaka 20 ya Ruvu Shooting kwa lengo la kusindikiza sherehe hizo,” alisema Masangu.
Aidha alisema kuwa timu hiyo iliweza kunyakua ubingwa wa mkoa kwa kuifunga timu ya Baga Friends magoli 3-0 mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha.
“Tunawapongeza viongozi, wachezaji, wanachama na wadau wa timu hiyo ya Kiluvya United kwa ushindi walioupata na tunawataka wajipange vizuri kwa ajili ya kuwakilisha mkoa kwenye ligi ya Kanda ambako watakutana na mabingwa wa mikoa mingine,” alisema Masangu.
Aliwataka wadau na mashabiki wa soka mkoa Pwani kujitokeza kuipongeza timu yao kwa kufanikiwa kuwa mabingwa ili kuwapa hamasa ya kujiandaa vema na mashindano ngazi ya Taifa.
Mwisho.

No comments:

Post a Comment