Na John Gagarini, Kibaha
JUMLA ya watu 12,500 kwenye
vijiji vinne kwenye Halmashauri ya wilaya ya Kibaha mkoani Pwani watanufaika na mradi wa kitaifa wa maji wa Wami – Chalinze
awamu ya pili wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni tatu.
Akizungumza na waandishi wa
habari ofisini kwake mjini Kibaha kuelezea mafanikio ya wilaya kwa kipindi cha
miaka saba iliyopita mkuu wa wilaya Halima Kihemba alisema kuwa mradi huo
utakamilika wakati wowote mwaka huu.
Kihemba alisema kuwa kwa
sasa mradi huo umefikia asilimia 35 ya utekelezaji wake na kuvitaja vijiji hivyo
kuwa ni Magindu, Lukenge, Gwata na Gumba.
“Mbali ya vijiji
vilivyotajwa hapo juu pia tunatarajia jumla ya vijiji 45 vitanufaika na mradi
mwingine ambao utasaidia kukabiliana na changamoto ya maji ambayo ni kubwa
kwenye wilaya,” alisema Kihemba.
Aidha alisema kuwa kwa
upande wa miradi hiyo yenye thamani ya zaidi ya shilingi zaidi ya bilioni mbili
itategemeana na upatikanaji wa fedha kutoka wadau mbalimbali.
Ameitaja miradi hiyo kuwa
ni mradi wa bomba Vikuruti, Boko Mnemela, Dutuni, bwawa la maji Mperamumbi
uchimbaji wa kisima kirefu chenye uwezo wa kutoa lita 36,000 za maji kwa saa.
“Miradi hiyo itakuwa katika
vijiji vya Lupunga, Mwabwito, Kisabi, Madimla, Disunyala na Makazi Mapya,”
alisema Kihemba.
Ameongeza kuwa kwa upande
wa Kibaha Mjini mitaa 15 ambayo ni Sofu, Muheza, Vikawe, Bondeni, Vikawe
Shuleni, Kidenge, Galagaza, Sagale, Mikongeni, Mwanalugali, Saeni, Jonugha, Zogawale
na Viziwaziwa miradi hii itakuwa na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.
Alibainisha kuwa changamoto
kubwa ni pamoja na kutegemea vyanzo vya maji vya ya juu ya ardhi, mabwawa, mito
ambayo hukauka wakati wa ukame na kusababisha shida ya maji hivyo kuweka
mikakati ya kuhamasisha jamii kutunza vyanzo vya maji, kuandaa andiko la miradi
ya maji ili kupata wafadhili na kutumia visima virefu kwa kuwa ni vyanzo vya
uhakika zaidi kulinganisha na mabwawa.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment