Na John Gagarini,
Kibaha
HATIMAYE baada ya kilio cha muda mrefu cha abiria juu ya
madereva ambao wamekuwa wakiweka pombe za viroba kwenye chupa za maji na
kujifanya wanakunywa maji, kimesikika baada ya jeshi la polisi mkoani Pwani
kupata vipima ulevi 100.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha kamanda wa
kikosi cha usalama barabarani Nasoro Sisiwaya alisema kuwa vifaa hivyo
vitasaidia kukabiliana na madereva walevi ambao wamekuwa wakisababisha ajali
kutokana na ulevi.
Sisiwaya alisema kuwa kutokana na kero ya ulevi kuwa kubwa
kwa baadhi ya madereva wamekuja na njia hiyo ili kuwadhibiti madereva hao ambao
wamekuwa wakinywa pombe huku safari ikiendelea.
“Vifaa hivi vitatusaidia katika kukabiliana na madereva hao
ambao ni chanzo kikubwa cha ajali kwani hupoteza umakini wakati wa kuendesha na
kusababisha ajali ambazo zingeweza kuepukika,” alisema Sisiwaya.
Aidha alisema kuwa kitengo cha usalama barabarani kinaendelea
kukabiliana na changamoto za ajali kwa kuweka askari mbalimbali wakiwemo ambao
wanakuwa wamevaa kiraia ili kudhibiti madereva ambao wanakiuka sheria za
usalama barabarani.
“Tunamshukuru Mungu kuwa ajali zinaendelea kupungua kutokana
na udhibiti kuwa mkubwa ambapo kwa sasa makosa madogo yameongezeka ambayo
yanaashiria kupungua kwa ajali katika mkoa,” alisema Sisiwaya.
Aliongeza kuwa kwa sasa wanashirikiana na mamlaka ya
kudhibiti usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA) katika kuwakamata madereva
wanaovunja sheria ambapo mafanikio yameanza kuonekana kwani makosa makubwa ya
barabarani yamepungua kwa asilimia 26.
Aliwataka wananchi na abiria kutoa taarifa mbalimbali
kuhusiana na madereva ambao hawazingatii taratibu za uendeshaji wawapo
barabarani na wataendelea kufanya operesheni za mara kwa mara ili kuwabaini
madereva wazembe.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment